Majeshi ya Amin yalivyopewa mkongoto na JWTZ

                       Aliyekuwa Kiongozi wa Kijeshi wa Uganda Hayati Nduli Iddi Amin Dadaa
                                      Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
SEHEMU YA PILI
Amin alitoa amri kuwa watu wote wanaopinga utawala wake, wapigwe risasi hadhalani, katika kutekeleza moja ya ndoto zake alizodai kuwa ni mazungumzo baina yake na Mwenyezi Mungu, aliwafukuza kutoka Uganda, Waasia wote waliokuwa na pasi za kusafiria za Uingereza na kuwanyanganya mali zao zote.

Baada ya shutuma nyingi za uongo dhidi ya Tanzania, mnamo tarehe 30 )ktoba 1978 Idi Amin aliyaamuru majeshi yake kuvuka mpaka na kulivamia eneo la Tanzania, ambapo watanzania zaidi ya 10,000 wasiokuwa na hatia yaliangamizwa na eneo la kilomita za mraba 1850 zilichukuliwa na majeshi ya Uganda.

Majeshi hayo ya Amin yalilikalia eneo la mto Kagera sehemu ya kyaka na kufanya vitendo vya kinyama kwa kuua wananchi wa mkoa wa Ziwa Magharibi hovyo, kuchoma nyumba, viwanda, kupora mali nyingi na kuzipeleka Uganda.

Katika kutekeleza uhalifu wao, majeshi hayo ya uvamizi yalivunja daraja la Mto Kagera lililoko eneo la Kyaka, na kufanya usafri katika eneo hilo kuwa mgumu, na kutangaza rasmi kuwa atalitawala eneo hilo kijeshi kama ilivyo nchini Uganda na kumteua Mkuu wa wilaya hiyo mpya.

Wakati wananchi wa Kagera wakikabiliwa na maafa ya vifo na njaa, baadhi ya vikosi vya majeshi ya uhaini vya Idi Amin Dadaa vilirejea Uganda na kusherehekea ushindi bandia vilivyoupata dhidi ya Tanzania, wakijigamba kuwa walitumia dakika 25 tu kuliteka eneo lote la Kagera.

Katika kambi zao mbali mbali nchini Uganda, vikosi hivyo vya uvamizi vilipewa vinywaji mbali mbali na vyakula kama viburudisho kushangilia ushenzi na unyama walioufanya dhidi ya Tanzania, Hospitali za Bukoba na nyingine zilizoko Kaskazini mwa Tanzania, zilifanya kazi kubwa ya kuhudumia majeruhi kutokana na ukatili wa askari wa Idi Amin.

Mfanyakazi mmoja wa kiwanda cha sukari Kagera, anaeleza jinsi alivyookolewa na majeshi shupavu ya Tanzania, baada ya kupigwa na kuporwa sh. 900 na wanajeshi wa Uganda, baada ya kuteswa kwa muda mrefu.

Moja ya vikosi vilivyoongoza kufanya uvamizi katika ardhi ya Tanzania, kilikuwa kikosi cha marine, katika sherehe zilizofanywa na kikosi hicho, Idi Amin binafsi alihudhuria na kueleza kufurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Kamanda wa kikosi hicho, ambaye alibebwa juu.

Akitoa pongezi kwa kikosi hicho, Idi Amin aliwaeleza wapiganaji hao kuwa amefika kikosini hapo kwa ajili ya kuwapongeza rasmi kwa kazi nzuri na ngumu waliyofanya ya kuishambulia Tanzania.

"Mimi nakuja hapa personal kupiga asante sana kwenu, kwa sababu mlifanya kazi ya nguvu sana, kwani sehemu mliyokuwa mnapigana ilikuwa ngumu sana tofauti na Bataliani zingine zote, lakini nyie mkiwa katika kombania moja bila Bataliani, mliweza kupigana na Bataliani tatu mzima, mpaka mnafungua njia kutoka Mtukula, mnaingia nayo mpaka kyaka, kwenda kuongeza nguvu mahali ambapo walikuwa Difcot", alikaririwa Amin akisema. 

Katika majigambo yake, Idi Amin anawaeleza wapiganaji wake kuwa aliamini hakuna kikosi cha Tanzania kinachoweza kuwarudisha nyuma, lakini alifurahi sana kuona wapiganaji wake wote wanarudi nyuma na kupata jereha kidogo kwa sababu walifanya kazi ngumu sana.

"Mpaka sasa Tanzania nakwisha nyamaza kimya, na mimi najua bado kidogo, Komandingi Ofisa ataletea mimi bendera ya Tanzania, yeye atampa kwangu, halafu hii bendera itakwenda kwa Kamandingi Force," anatamba Idi Amin na kuwapa molali wapiganaji wake kwa kusema WAPIGANAJI MOTO, nao wakijibu MOTO.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU