Benki ya Afrika Tanzania kufungua tawi jipya Mtibwa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Rais mstaafu wa Awamu ya tatu, Bw. Benjamin Wiliam Mkapa leo amezindua tawi jipya la Benki ya Afrika Tanzania lililoko Mtibwa mkoani Morogoro, likiwa tawi la 17 hapa nchini.

Hii ni moja ya matawi matatu yaliyofunguliwa mwaka huu ambapo tawi hili lipo ndani ya  kiwanda cha Sukari cha Mtibwa Sugar Estates Company katika eneo la Madizini.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa idara, huduma za wateja za reja reja wa benki hiyo, Bi. Mwanahiba Mzee alisema uzinduzi wa tawi hilo unaashiria nia waliyonayo katika kuhudumia watanzania.

“Uzinduzi huu unaeleza nia yetu ya kutoa bora huduma za kibenki hapa nchini,” alisema.

Alisema wananchi wa Mtibwa na maeneo ya jirani sasa watakua na fursa ya kupata huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo na kuwahimiza kutumia fursa hiyo kwa maendeleo yao nay a taifa kwa ujumla.

“Kwa niaba ya benki, nawahimiza wakaazi wa Mtibwa kutumia vizuri fursa hiyo,” alisema na kuongeza kwamba benki hiyo itaendelea kufungua matawi zaidi hapa nchini kuunga mkono juhudi za serikali za maendeleo.

Tangu ianze shughuli zake hapa nchini, benki hii imekua ikijitahidi kujitanua kwa kuanzisha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua matawi mapya.

Hadi sasa ina matawi kumi jijini Dar es Salaam pamoja na mengine sita katika mikoa ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya na Arusha.

Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast, Mali, Niger na Senegal.  Nyingine ni Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda.

Pia kuna matawi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU