NJAMA


KUTOKANA NA MAOMBI YA WASOMAJI WETU WAPENDWA, TUTAENDELEA KUWALETEA NA HADITHI HII YA KUSISIMUA KUTOKA KITABU CHA NJAMA, KILICHOANDIKWA NA MWANA MAPINDUZI, A.E MUSIBA. SASA ENDELEA

NAONANA NA CHIFU
Ndege ilitua kwenye uwanja wa ndege wa mjini Dar es Salaam kiasi cha saa moja na nusu asubuhi. Nilipita harakaharaka katika sehemu za afya, uhamiaji na ushuru wa forodha, kisha nikachukua teksi iliyonipeleka moja kwa moja katika ofisi yangu ya 'Afrika International Agencies', iliyoko mtaa wa Independence karibu na ofisi kuu za shirika la Bima la Taifa.

"Hallo bosi, umerudi!", Rose mfanyakazi wetu sehemu ya mapokezi alisema.

"Naam nimepata ujumbe wa teleksi kutoka kwa Marcelina kuwa mama anakufa".

"Na kweli nenda ofisi kwako mwandishi wako mahususi alikuwa na wasi wasi maana huko juu wanakuulizia kila baada ya dakika kumi. Ama kweli huko juu kuna kitu kikubwa kinawawasha".

Nilielekea ofisini kwangu, nilipofika nikafungua mlango wa mwandishi wangu mahsusi, Linda.

Oh, Mungu wangu, afadhali umefika, kidogo nipate wazimu maana huko juu hawanipi nafasi hata ya kupumua. Naulizwa kila wakati kwanini hujafika, utafikiri mimi ndiye nakufuga".

"Poa sasa nimefika mwenyewe. Vipi shughuli hapa?".

"Mambo shwali, isipokuwa toka juzi kuna jambo limeharibika, maana jana nzima ofisi inawaka moto. Chifu huko juu ametingwa na mambo. Na afadhali uende sasa hivi, mimi nawajulisha kuwa uko kwenye lifti unaelekea ofisini kwake".

"Yaa fanya hivyo".

Niliacha mzigo wangu kwa Linda, nikaelekea ofisini kwa Chifu ambaye ofisi yake ilikuwa orofa ya tatu, na sisi tulikuwa chini katika jengo hilo hilo.

Nilifungua mlango bila kubisha hodi. Nikaingia ndani ya ofisi ya mwandishi mahsusi wa Chifu.

"Ooh, Mungu wangu! Afadhali umekuja!", Maselina alisema kwa moyo wa furaha.

"Hujambo lakini?".

"Sijambo ila wasiwasi ni juu yako tu. Pole sana, nafikiri tumekukatishia likizo murua kabisa".

"Wacha kusema. Tayari nilikuwa nimeshapata kipande cha msichana. Nilipopata ujumbe wako kidogo nipate ugonjwa wa moyo. Je kuna nini huku kinacholeta wasiwasi hivi?".

"Atakueleza mwenyewe kinachompandisha damu yake. Nakwambia amekuwa anakuhitaji kwa haraka sana, hata hivi anaona umechelewa. hivi sasa nilikuwa nataka kutuma teleksi nyingine".

"Mama yangu mzazi! mtafikiri nina roketi yangu mwenyewe!".

"Ngoja nimwambie kwamba umefika. Akifungua mlango kisha atukute tunapga soga sijui atafanya nini. Huenda atapasuka!".

"Mwache apasuke! Mnafikiri kunikatisha likizo yangu nilijisikiaje. Utadhani moyo wangu umetengenezwa kwa chuma, na wake kwa udongo".

"Kamwambie mwenyewe hayo huko ndani", Maselina alijibu akimwemwesa huku akiinua simu.

Huyu Maselina tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu kiasi ya kwamba uelewano wetu hauwezi kuelezeka kwa maneno. Huenda siku moja nitapata maneno ya kueleza, ila tu kwa leo naweza kusema ni rafiki yangu mkubwa.

"Chifu, namba moja yuko hapa", Maselina alitamka katika simu.

Nambari moja, ndivyo nilikuwa najulikana kikazi. Katika kazi yetu sisi hutumia namba, mimi nilikuwa namba moja hivyo unaweza mwenyewe kuchekecha ukajuwa kwa nini. Mimi Willy si mtu wa majivuno. Watu wengi, hasa wakubwa wa serikali walinijua kwa hii namba yangu. Wengi walikuwa hawajui namba moja ni Willy Gamba, ila kwa watu wachache sana. Hii ilinipa fursa hata nyumbani Dar es Salaam nijulikane kama mfanyabiashara wa kawaida tu, na si Willy Gamba ambaye ni namba moja katika Idara ya Usalama, Tanzania.

Maselina aliweka simu chini.

"Nenda ndani mara moja".

Nilifungua mlango, na nikamkuta Chifu akitembea toka kona moja ya chumba hadi kona nyingine. Kwa mtu ninayemfahamu nikajua hapo alipo alikuwa na matatizo makubwa sana yaliyomsakama rohoni mwake.

"Kaa chini namba moja', Chifu aliamru.

Chifu anaponiita kwa namba yangu ya kazi ujue kuna jambo kubwa.

nilivuta kiti nikaa, yeye akazidi kutembea kona hadi kona nyingine, hatimaye akasimama nyuma ya kiti chake.

"Nashukuru kwa kufika kwako mapema, namba moja ndio sababu nakutegemea sana".

"Asante", nilijibu halafu nikaendelea.

"Mbona hivi, nini kinakuwasha?".

Alichukuwa mtemba uliokuwa mezani, akafungua mkebe wa tumbaku akaijaza, kisha akawasha na kuanza kupuliza. Alipuliza mara mbili, halafu akazungusha kiti chake ambacho kinazunguka kwenye tendegu, akaketi.

"Kina jambo kubwa limetokea!".

Aliweka mtemba wake mezani na kuweka mikono yake kwenye mezani.

Akaniangalia machoni, huku macho yake yakionesha ukali wake.

Akili yangu ikiwa tayari kusikiliza jambo hili huku moyo ukinidunda.

Utanisikiliza, utauliza maswali baadaye".

Sawa".

"Nafikiri nitaanza toka mwanzo. Ingawaje mambo mengine unayajua, nitayarudia tu kwa ajili ya umuhimu wa habari yenyewe ilivyo, unaonaje?".

"Utakavyoona wewe Chifu".

"Unajua nchi yetu inalea vyama vingi vya wapigania uhuru. Kama vile vyama vya wapigania uhuru toka Zimbabwe, Afrika Kusini n.k. Pamoja n a kulea vyama hivi tunawapatia vijana wao ya kijeshi. Kwa vile mafunzo mengi yanapatikana hapa na makao makuu ya vyama hivi yapo hapa, basi silaha zao vile vile zinapitia hapa na sisi tunazipokea toka nchi rafiki na kuwapa wanaohusika.

"Hapa tuna vyama viwili vya wapigania uhuru katika Afrika kusini. Vyama hivi ni 'The Peoples liberetion Front, of South Afrika (PLF)" kinachoongozwa na Ndugu Cecil Chimalamo na South Afrika National Party (SANP) kinachoongozwa na Ndugu Ray Simbuche. Miezi sita iliyopita Ndugu Cecil Chimalamo wa PLF alikwenda Urusi ambako alioba msaada wa silaha na akaahidiwa kupewa silaha hizo ambazo zingepelekwa Dar es Salaam mnamo muda wa miezi sita.

"Wiki iliyopita Ubalozi wa Urusi wa hapa mjini ulipata karatasi za maelezo ya silaha hizi ambazo tayari zilikuwa zimeshapakiwa kwenye meli siku nyingi na zilikuwa njiani kuwasili Dar es Salaam. Na makaratasi haya yalisema meli hiyo itawasili mjini hapa mnamo wiki hii'.

"Basi yalipofika, ubalozi uliyashughulikia kikamilifu kwa upande wake, kisha ukayapitisha kwenye kamati ya ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), maana kamati hii ndiyo inashughulikia mambo haya kama unavyofahamu. Kamati nayo ilianza kuzishughulikia karatasi hizi mpaka zikawa tayari, wakawa sasa wanangoja meli kufika. Habari kutoka kwenye Wakala wa Meli zilieleza kuwa meli hiyo itaingia bandarini Dar es Salaam tarehe tatu mwezi huu ambayo ilikuwa juzi ile".

"Baada ya kupata habari hizi kamati ilipanga pamoja na ofisi ya mambo ya silaha za wapigania uhuru pia na maofisa wa bandari wanaohusika kuwa mizigo hiyo ipakuliwe usiku wa tarehe nne yaani juzi kuamkia jana. Kwa sababu karatasi zote zilikuwa zimekamilika na sehemu zote zikiwa na habari kamili, pande zote zilikaa zikisubiri silaha hizo mnamo siku hiyo kama ulivyopangwa".

Chifu alichukua mtemba wake tena akavuta kidogo kisha akauweka juu ya meza.

"Nafikiri umenielewa mpaka hapo?".

"Wakati huo mpango hii yote ya kupakua mizigo hii, ofisi ya PLF ilikuwa ikishirikishwa?", niliuliza.

"Ndio, kwa sababu huwa wanaelezwa mambo yote yanavyokwenda, hivyo huwa wana habari kamili ya mambo yote. Naweza kuendelea?".

"Unaweza".

"Sasa jambo la kushangaza likatokea juzi. Maofisa wa ofisi ya jshi la ulinzi inayoshughulikia silaha za wapigania uhuru walikwenda kwenye ofisi ya kamati ya ukombozi juzi mnamo saa nne ili kuchukua karatasi hizo za mizigo, wapate kijitayarisha kwa upakuaji wa mizigo hiyo wakati wa usiku. Walipofika kwenye ofisi hii wakakuta ofisa anayehusika hajafika kazini. Ikabidi wamwone ofisa wa juu katika ofisi hiyo kumweleza umuhimu uliopo wa kuandaa kupakua silaha hizo usiku.

"Huyu ofisa wa juu katika ofisi hii ya kamati naye alisema kuwa alikuwa ameshangazwa kwanini ofisa huyo alikuwa hajafika kazini. Hivyo wote kwa ujumla wakaondoka kuelekea nyumbani kwa ofisa huyo kuona kama anaumwa aweze kuwaelekeza wapi walipoziweka karatasi hizo. Huyu ofisa alikuwa akikaa sehemu za Upanga, Barabara ya Umoja wa mataifa, nyumba namba 1168".

"Walipofika nyumbani kwa ofisa huyo walimkuta mfanyakazi wake akiwa nje. Walipomuuliza kama wenye nyumba wapo aliwajibu kuwa yeye hakai hapo ila huwa anakuja kila asubuhi lakini alipofika asubuhi hii alikuta milango yote ya kuingilia ndani ya nyumba imefungwa.  Hivyo mpaka muda huo alikuwa anasubiri kwani alifikiri wametoka. Ofisa huyo alikuwa anakaa yeye pamoja na mke wake na walikuwa bado hawajapata watoto. Ofisa mmoja wa jeshi alikwenda kuangalia gereji akakuta gari la ofisa huyu lipo na lilikuwa bado halijatoka. Kitu hiki kilimtia mashaka akawaeleza wenzake na akashauri wajaribu kuingia ndani ya nyumba huenda walikuwa bado wamo ndani. Kwani kama kutoka wangekuwa wametoka na gari lao, walikubaliane wavunje mlango wa kuingilia ndani".

Chifu alinyamaza kidogo akainua macho yake kuniangalia.

"Walishtushwa kwa kumkuta ofisa huyu amepigwa risasi amekufa sebuleni, huku akiwa amevalia vizuri kabisa kuonyesha kuwa alikuwa anatoka matembezini. Halafu ukumbini walimkuta mke wa ofisa huyo naye amepigwa risasi amekufa huku akiwa amevalia nguo za kulia. Haapo hapo wakanyanyua simu na kutoa ripoti ya vifo hivi kituo cha polisi Oysterbay ambacho hakikuchelewa kutuma maofisa wao kwenye nyumba hiyo. Baada ya polisi kufika, maofisa hao wa jeshi na ofisa kutoka kamati ya ukombozi ilibidi warudi upesi kwenye ofisi ya kamati, maana vifo hivi vilileta wasiwasi".

Wakati wote huu akieleza, mimi nilikuwa kimya kabisa na akili yangu ilichemka niliposikia habari hizi za mauaji.

"Halafu ikawaje?".

"Walirudi ofisi za kamati upesi upesi, na kuanza kutafuta makaratasi haya ya mizigo kila mahali ofisini hapa, lakini hawakuona kitu. Hapo ndipo jasho lilipowatoka. Jambo hili liliwapa wasiwasi zaidi ikabidi wakimbilie bandarini kutoa habari kwa maofisa wa bandari kuwa karatasi zimepotea".

Chifu macho yake yaliwaka nikajua karibu anasema kitu cha kustua.

"Walipofika katika ofisi za bandari, ofisa anayehusika na habari hizi, walipomweleza kuwa makaratasi yamepotea, alishangaa sana, ndipo mwishoni akawaeleza kuwa silaha zilikuwa zimeisha chukuliwa usiku uliokuwa umepita na wanajeshi waliovalia nguo za jeshi la ulinzi na wakiwa na karatasi zote za kuchukulia silaha, zikiwa kamili kabisa. Walikuwa wamefika na magari ya jeshi la wananchi, hata akawatolea namba za magari. Kundi hili lililochukua silaha liliongozwa na mtui aliyevalia nguo za cheo cha meja. Kusikia hivi kundi lote lililofika kwenye ofisi ya bandari lilichoka kabisa.

"Lakini si walikuwa wamekubaliana na ofisi ya bandari kuwa watapakua usiku wa juzi kuamkia jana, ilikuwaje yeye akaruhusu mizigo ipakuliwe usiku wa juzi ile kuamkia juzi?".

"Huko ndiko nakuja kufafanua. Ofisa wa bandari alieleza kuwa mnamo terehe tatu mwezi huu ambayo ni juzi ile kiasi cha saa kumi alipata simu toka ofisi ya Kamati ya Ukombozi. Simu hii ilikuwa inatoka kwa ofisa wa juu katika Kamati ya Ukombozi anayeshughulikia mambo ya silaha, Ndugu Jones Mantare. Ambaye ndiye aligundua maiti ya ofisa huyo wa kamati akiwa pamoja na wanajeshi. Yeye anasema sauti ya Jones Mantare anaifahamu maana ameshughulika naye siku nyingi, na sauti hii aliyoisikia kwenye simu ilikuwa kama ya Mantare hivyo akaamini kuwa anazungumza na Mantare".

"Simu hiyo ilieleza kwamba, kwa ajili ya usalama ratiba ya upakuaji silaha imebadilika, kwa hiyo silaha zilikuwa zipakuliwe siku hiyo hiyo kuanzia saa mbili za usiku kwani silaha zilikuwa nyingi. Hivyo akasema amtegemee meja mmoja wa jeshi kwa jina la Paul Liboi, atakuja pamoja na askari wa jeshi la wananchi kutoka kwenye ofisi inayoshughulikia silaha za wapigania uhuru ambaye atashughulikia kazi hiyo. Kwa hiyo, anasema alimwomba aiweke hiyo meli tayari kwa kupakuliwa saa mbili usiku. Yeye alikubali bila masharti maana kazi ya silaha ni muhimu".

"Na mnamo saa kumi na nusu wakati akishughulika na kutoa amri ya meli hiyo kupewa nafasi kwenye geti alipata mgeni mwingine. Mgeni huyu alijitambulisha kwa jina la Andrew Mwambina ofisa usalama toka kamati ya ukombozi ya OAU. Alitoa kitambulisho chake na ofisa huyu wa bandari alivyokiona kilionekana halali maana ameshawahi kuona vitambulisho vya watu hawa. Mtu huyu alimwuliza kama amepata habari kuwa upakuaji umebadilishwa na ilibidi silaha zipakuliwe usiku huo saa mbili. Yeye alikubali kuwa amepata ujumbe na muda huo alikuwa anashughulikia jambo hilo. Ofisa huyo wa usalama alimwaga na kumwambia yeye na wenzake watakuwepo kikazi kama kawaida, akaondoka".

"Kwa taarifa yako. Namba moja maafisa watatu wa usalama wa Kamati ya Ukombozi ambao walipangiwa kufanya kazi bandarini tangu ilipofahamika kuwa meli hiyo inaingia walikuwa wameuawa na maiti zao zilikutwa sehemu ya Shimo la Udongo jana jioni".

Chifu alitua kidogo kupuliza mtemba wake.

"Taarifa ya ofisa wa bandari iliendelea kusema kuwa ilipofika saa mbili kamili za usiku magari manne ya jeshi tani kumi na mbili kila moja yaliingia. Na mtu aliyejitambulisha kama Meja Paul Liboi alifika ofisini kwake akiwa amevalia kijeshi na cheo chake kwenye mabega. Yeye alisema amekuja kushughulikia upakuaji wa silaha na kwamba aliamini ameshapewa habari na kamati ya Ukombizi mapema, na akatoa karatasi za kupokelea mizigo ya silaha ambazo zilikuwa sawa".

"Yeye alimjibu kwamba alishapata habari na mipango yote ilikuwa tayari, hivyo baada ya kumaliza shughuli za makaratasi alitoka na Meja huyu na kuwaelekeza meli ilipokuwa tayari kwa upakuzi. Aliendelea kueleza kuwa magari haya manne yalikuwa na askari wengi waliovalia kijeshi. Hivyo silaha zilianza kupakuliwa saa tatu na kufikia saa kumi alfajiri gari la mwisho liliondoka. Silaha zilikuwa nyingi sana za kisasa na za hali ya juu. Nafikiri umenielewa mpaka hapo".

"Ndio nimekuelewa".   

"Sasa kitu cha kutia huzuni ni kwamba silaha hizi zimepotea hazijulikani zilipo. Na wala watu na magari yaliyochukuwa silaha hizi hayajulikani yalipo mpaka  dakika hii tunapozungumza. Idara ya polisi imejaribu kutafuta lakini mpaka sasa hawana hata fununu. Huu ni wizi wa silaha uliopandwa barabara na kwa serikali yetu hii ni "KASHFA", kwa taarifa yako habari hizi zimevunja na zimeshatangazwa na nchi za Magharibi pamoja na Afrika Kusini juu ya tukio hili. Na tayari nchi adui za Tanzania zimeanza kuropoka ovyo ili kulichafua jina la nchi hii".

"Mimi ninadhani hizi ni hila na Njama za mabeberu, wapinga mapinduzi wa mapambano Kusini mwa Afrika. Nia yao ya kufanya hivi ni kutaka mambo matu. Nia yao ya kwanza ni kuhujumu, kuchukua silaha hizi kusudi zisiwafikie wapigania uhuru ambao mapambano yao huko Kusini mwa Afrika sasa yanapamba moto, maana silaha hizi zilikuwa za kisasa na zingalifika kwenye uwanja wa mapambano wanajua wangepata cha mtemakuni. Kwa hiyo hizi ni njama za kuhakikisha kuwa silaha hazifiki kwenye uwanja wa mapambano".

"Pili, wanataka kulipaka matope jina la Tanzania kwa vile Tanzania imeamua kuongoza ukombozi kusini mwa Afrika sasa ina maadui wengi sana, na maadui hawa wameanza kulipaka matope jina la Tanzania na kusema kuwa Tanzania huzitumia hizi silaha kwa majeshi yake. Wendawazimu wengine wameendelea kusema eti Tanzania kwa muda  mrefu imekuwa inatumia misaada inayotolewa kwa faida yake!".

"Hivi hili jambo si geni. Nia yao ya tatu ni kutaka kuzikatisha tamaa nchi rafiki zinazotoa misaada kwa wapigania uhuru, zisizidi kufanya hivyo, kwa kufikilia kuwa wanapoteza mali zao kwa kufanya kazi ambazo wao hawakuzipangia. Kwa hiyo, namba moja unaona hali ya hatari nchi yetu ilimo".

"Lo! ni hali mbaya sana. sasa sisi tunatakiwa kufanya nini?".

"Jambo hili sasa linashughulikiwa na Idara ya polisi na ofisi ya usalama. Upelelezi wao bado unaendelea na ni mkali sana. Katika usiku wa kuamkia jana serikali imeamua sisi lazima tulishughulikie jambo hili. Maana inaamini wizi huu uliofanywa ni wa kimataifa, hivi polisi hawakuzoea kupambana na hali kama hii. Kwa hiyo ingawake wao wataendelea na shughuri zao, sisi itabidi tujishughulishe kikamilifu juu ya jambo hili maana ni kima chetu polisi wameagizwa kuleta nakala ya ripoti zao zote za upelelezi wanaoufanya. Hii itafanya kupata habari nyingine ambazo zitatusaidia sana".

"Serikali inataka jambo hili litatuliwe haraka kusudi tuweze kuwafichua hao maadui zetu wanaotaka kutupaka matope, maana itabidi tuionyeshe jumuia ya ulimwengu jinsi maadui zetu wanavyojaribu kutupiga vita kwa ajili ya msimamo wetu thabiti katika ukombozi wa Afrika. Na hatuwezi kufichua ukweli wa jambo hili mpaka hapo tutakapowakamata hawa waliofanya kitendo hiki. Kwa hiyo kazi yetu sasa ni moja tu, nayo ni kuwakamata watu hawa. Na wewe namba moja umepewa jukumu hili kubwa la kulinda hadhi ya nchi yako, Tanzania. Una maswali?".

"Nipe muda kidogo nifikiri".

Nikasimama na muda huu kwa ajili ya mafikara niliyokuwa nayo nilianza kutembeatembea toka kona hadi kona ya chumba kama nilivyomkuta Chifu akifanya. Ilionekana Chifu alijisikia nafuu baada ya kutua mzigo huu kwangu ikawa zamu yangu kubanwa na mawazo ya tukio hili.

"Hizi habari zimevujaje?".

Niliuliza hukU bado natembeatembea nimeinamisha kichwa chini.

"Naamini, maharamia hao hao ndio wamezitoa ili wafanikishe moja ya shabaha zao. Yaani kuivunjia Tanzania hadhi".

Mara moja nikawakumbuka Sherrif na Veronika nikajuwa lazima habari hizi zilikuwa zimeshafika ofisi za gazeti la Afrika na Sherrif alikuwa anakuja Dar es Salaam ili kuja kuchunguza na kuandika juu ya tukio hili. Katika mipango yangu iliyokuwa inapita kichwani nilipata pointi moja ya kunisaidia.

"Huyu Jonas Mantare anasemaje juu ya tukio hili?".

"Baada ya kupata maelezo ya ofisi ya bandari, mara moja polisi walimkamata Jonas Mantare kwa kusaidia polisi katika uchunguzi, yeye alipoulizwa kama yeye ndiye aliyepiga simu, alikataa kabisa, na kukataa kwake kumedhihilishwa na Mwenyekiti wa kamati ya ukombozi kuwa Mantare alikuwa ofisini mwake toka saa tisa mpaka saa kumi na moja siku hiyo wakifanyakazi pamoja na wala hawakutoka hata dakika moja katika muda wa masaa hayo mawili".

"Kwa hiyo kutokana na usemi wa ofisa wa bandari, kuna mtu mwingine aliyeiga sauti ya Mantare. Hii ina maana mtu huyu amemzoea".

Nikarudi na kuketi kwenye kiti kwani akili zilianza kufanya kazi. Kwa mara ya kwanza nilitoa paketi yangu ya sigara nilizokuwa nimenunua katika ndege, nikaanza kuvuta.

"Bila ya shaka", Chifu alijibu.

"Ofisa huyo aliyeuawa anaitwa nani?".

"Anaitwa Kamara Frank, yeye ni mwenyeji wa Sierra Leon".

Unaona sasa mambo yanavyokuwa huyu mtu alikuwa rafiki ya Sherrif kama unakumbuka.

"Daktari anafikilia Frank na mkewe walikufa saa ngapi?".

"Daktari anakadilia kuwa walikufa kati ya saa sita na saa nane usiku. Na inavyoonekana ni kuwa kuna wakati alikuwa amefungwa kamba, maana alama zinaonekana kwenye mikono na miguu".

"Sasa Chifu kuna jambo moja ambalo lazima tuelewane. Tangu nimeanza kazi hii nimekuwa nikifanya kazi zangu nje ya Tanzania. Hapa nyumbani najulikana kama mfanyabiashara tu. Lakini kama nikianza shughuli hii lazima nitajulikana hasa mimi ndiye nani. Unasemaje?".

"Nani anajali", alifoka Chifu kwa sauti ya juu. "Kitu ninachotaka mimi ni kuona jambo hili linatekelezwa na washenzi hawa wamekamatwa. Kama itabidi ujulikane potelea mbali!".

"Lakini Chifu..."

"Hamna cha lakini hii ni amri ya serikali na serikali inataka matokeo juu ya suala hili na mapema iwezekanavyo".

Nilijuwa kuwa kweli iko kazi kama kweli Chifu kakubali mimi nitambulike kirahisi hivi nilikaa nikaanza kufiri jinsi ninavyoweza kufanya upelelezi wa tukio hili bila kutambuliwa maana mimi sikuwa nataka kabisa nijulikane kama mimi ni mpelelezi hapa nyumbani. Kwani watu wengi Tanzania wanajuwa wana mpelelezi mashuhuri, kiasi cha kujitapa  mitaani lakini hawajui kuwa ni mimi Willy Gamba. Na hivi ndivyo nataka, vinginevyo kila nitakapokuwa napita nitakuwa nafuatwa na kundi la wapenzi.

"Najuwa waandishi wa habari toka nchi za nje watakuwa na shauku kubwa kuja kuandika habari hizi. Kuna msimamo gani?".

"Haturuhusu waandishi wowote toka nje. wamezuiliwa mpaka hapo tutakapojuwa msimamo kamili wa jambo hili. La sivyo watakuja kuzidi kuchafua mambo hapa. hatutawaruhusu kabisa idara ya uhamiaji imeshaelezea na imeshatoa amri kwa vituo vyake, na jambo hili limeanza kutekelezwa. Asubuhi hii nchi za Magharibi zimelalamika kusikia haturuhusu waandishi wa habari toka nje.

Nilichukua nafasi hii kumweleza Chifu juu ya kukutana kwangu na Veronika Sherrif. Nikaendelea kumweleza kila kitu juu ya kuja kwao hapa.

"Hivyo nahisi gazeti la "Afrika" linawatuma waje kwa ajili ya tukio hili. Ni lazima wameishapata habari".

"Hawataruhusiwa kuingia".

"Mimi naomba hawa waruhusiwe kwa sababu nafikiria kuwatumia katika shughuri hii".

"Haiwezekani, watakuja tifua mambo tu, sitaki kuona waandishi wa habari toka nje!", Chifu alifoka huku akionyesha hasira.

"Sasa Chifu, ni lazima tuelewane, hili jukumu umenipa mimi. Na inabidi mimi mwenyewe nipange ninavyoona, jinsi nitakavyoweza kulitatua tatizo hili, na kama sasa hatuwezi kukubaliana, sijui shughuli itawezekanaje?".

Chifu alinyamaza kwa muda mrefu.

"Hebu ni majina kamili ya watu hao".

Nikampa. Akainua simu, akazungumza na Maselina.

"Hebu angalia kwenye mafaili ya waandishi wa habari hasa waandishi wa gazeti la "Afrika", angalia kama kuna faili zozote za majina ya Veronika Hamadu na Ahmed Sherrif wote kutoka Sierra Leon".

Akaweka simu chini, tukasubiri katika ukimya. Baada ya kitambo kidogo Maselina alifungua mlango akaingia na mafaili mawili, akampa Chifu. Chifu alipoinama kuyafungua kusoma,
Maselina alinikonyeza na kufua mlango, akatoka nje.

Chifu alisoma faili la kwanza, alipomaliza akanitupia. Lilikuwa faili ya Ahmed Sherrif. Na mimi nilianza kulipitia kwa makini sana nilipomaliza kulisoma Chifu alikuwa nae amemaliza kusoma faili la Veronika Hamadu, akanitupia. Nilisoma faili la Veronika kwa makini vile vile, lilikuwa na habari zilizonifanya nitabasamu mara kwa mara mpaka nilipomaliza. Nilikuta Chifu ameegemea kwenye kiti chake akaniangalia kwa makini.

"Oke, wataruhusiwa kuingia, inaonekana wanaweza kuwa wa manufaa kwako. Sijui unataka kuwatumiaje, kama hutajari kunieleza".

Baada ya kuwa nimesoma mafaili ya watu nilikata shauri namna ya kushughulika nao. Hivyo nilionelea juu ya mipango yangu maana huyu mzee kichwa chake kinafanyakazi. Kama akiona kuna kitu chochote hakifai atanikosoa mara moja. Waliompa kazi hii ni dhahiri walichagua mtu hasa anayefaa. Sidhani kuna mtu wa uwezo kama wake katika kuongoza kazi hii katika nchi hii. Yeye hiki ni kipaji alichopewa na Mungu. Na maendeleo yote ya idara hii ya upelelezi yamefanikishwa na uongozi wake ulio thabiti na wa busara.

"Mimi bado nahitaji kufanya upelelezi katika tukio hili, kujulikana kuwa mimi ni mpelelezi kwa watu wengi. Hivyo nimepanga kuwa kampuni yetu Afrikan International Agencies itakuwa wakala wa gazeti la Afrika. Kwa kufanya hivyo kampuni hiyo itawapokea hawa waandishi wa gazeti hilo kama wageni wake kwa sababu mimi najulikana kama meneja mkuu wa kampuni hivyo nitaandamana nao katika kutafuta habari zao nikiwa kama mwenyeji wao na kwa vile nafahamika hapa Dar es Salaam, nitawaongoza na wakati huo huo nitakuwa nafanya upelelezi wangu. Kwa kufanya huvi nitaweza kushughulika bila kutambuliwa kuwa mimi ni nani na ninafanya nini. Mpango kamili nitapanga na nitakueleza".

Alikaa kimya kutafakari mpango wangu.

"Vizuri sana, namba moja, akili yako inafanyakazi. Nimeishaona shughuli yote itakavyokuwa kwa urefu. Mpango wako ni mzuri, endelea nao. Unafikiri hawa waandishi watafika saa ngapi".

"Si zaidi ya usiku wa leo".

"Oke nitapeleka habari sasa hivi watu hawa waruhusiwe kuingia. Wewe nenda sasa ukapumzike maana najua haujalala tengeneza mpango wako wote wa upelelezi huo, na uniletee kesho asubuhi. Lakini kumbuka kazi hii ni kubwa na ya haraka, hivyo msaada wowote utakaoutaka utapewa. Ofisi yote imeweka kando kazi nyingine mpaka tutakapoona mwisho wa kazi hii. Mungu akusaidie kama amnavyo amekusaidia siku zote. Nina imani na wewe Willy. Najua utafanikiwa. Kwa heri Willy mpaka baadaye, kapumzike".

Chifu anapoanza kuniita Willy ujuwe kuna kitu kimemfurahisha hasira na wasiwasi wake umepungua. Na anakuwa na imani kuwa kazi itafanyika.

"Asante", nilijibu.

Niliangalia saa yangu. Ilikuwa saa saba za mchana mkutano huo ulikuwa umechukua muda mrefu sana. Nilimwaga Chifu nikamwahidi kumletea nakala ya mpango wangu wa operesheni hii asubuhi.

Nilifungua mlango nikaingia ofisini kwa Macelina.

"Kazi kubwa unayo, pole sana Willy".

"Nitafanyaje Macelina, mimi mwenyewe nilikubali kazi hii sasa siwezi kurudi nyuma. Na vile vile kwa sababu tukio hili linahusu wapigania uhuru, niko tayari kabisa kwa lolote. Wewe mwenyewe unajuwa moyo wangu ulivyo juu ya ndugu zetu wanaoteswa huko Kusini mwa Afrika".

"Naelewa Willy, naelewa sana roho yako ilivyo juu ya ukombozi wa Afrika Kusini. Vijana wote wa Kiafrika wangekuwa na roho kama yako sasa hivi kungekuwa hakuna ukoloni Afrika".

"Asante kwa kunipa moyo".

"Usiwe na wasiwasi, naamini mungu atakusaidia kama siku zote, maana wewe unatetea wanyonge wanaoonewa. Hata hivyo tukio hili n hatari kuliko mengine yote. Pole sana".

"Asante tena Maselina. Vipi huendi kula mchana?. Twende nikakununulie chakula cha mchana".

"Ngoja nimwage Chifu".

Maselina aaliingia ndani, alipotoka akasema ameruhusiwa muda wa saa moja tu saa nane ilimbidi awe kazini.

"Yeye haendi kula?".

"Ana vitafunio vyake humo ofisini, ndio hatoki tena. Huyu mzee kazi itamwua".

"Shauri yake. Yeye ameshaula kidogo si kama sisi. Miaka sitini ni miaka mingi.

Maselina alichukua mkoba wake tukaondoka.

                             

                                       III
Niliingia ofisini kwangu mnamo saa nane baada ya kupata chakula kitamu na Maselina.

"Linda nipeleke Colt Motors nikachukue gari langu".

"Hamna taabu bosi, twende zetu", Linda alijibu huku akichukua mkoba wake. Gari langu ni aina ya Colt GallantCoupe hivyo kila nikisafiri huwa naliacha kwenye kampuni yao.

"Vipi bosi, naona umeitwa shauri ya wizi wa silaha wa majuzi", Linda alinidadisi.

Huyu katibu wangu mahsusi alikuwa amefanya kazi nasi kwa muda wa miaka minne na mwaka huu alifikia kiasi cha kuaminika sana na kupewa nafasi ya kuwa katibu mahsusi wa Namba Moja.ambacho ni cheo cha juu sana. Kwa upande wa makatibu mahsusi yeye alikuwa amejipatia nafasi ya pili ya kuaminika baada ya Maselina. Alikuwa msichana mwenye akili nyingi, na alikuwa mzuri wa urubi. Alikuwa na kila sifa anazostahili katibu mahsusi kwa mpelelezi wa hali kama yangu. Nilimpenda kwa jitihada zake za kazi na nilimtegemea bila wasiwasi.

"Ndio Linda, matatizo kila wakati hutokea wakati niko katika kilelel cha maraha, sijui mkosi gani huu.

"Mimi huwa naamini huwa unapata raha fulani katika pilika pilika zako, maana kila ukimaliza shughuli fulani huwa nakuona katika hali ya furaha sana".

"Hiyo inatokana na kumaliza kazi yangu katika hali ya kuridhisha".

"Unafikiri watu hawa wameiba hizi silaha kusudi wazitumie kupindua serikali?", Linda aliuliza.

"La hasha, wanajua  hawawezi kabisa kupindua serikali, maana wananchi wote wa nchi hii wamejidhatiti katika ulinzi. Mimi nafikiri wana sababu nyingine, na sababu hii nitaipata katika muda si mrefu".

Saa nane hii magari yalikuwa mengi maana watu wengi walikuwa wanarudi makazini. Hivyo barabara hii ya Pugu ilikuwa na msongamano wa magari. Linda alitumia ujuzi wake wote ili kujipenyezapenyeza tuweze kufika upesi.

"Lazima nikupeleke upesi bosi maana najua una bonge la usingizi".

"Ndio sababu sikuchukii Linda, maana huwa ndiye mtu unayenionea huruma, wewe na Maselina, wengine wote wanafikiri mimi nimetengenezwa kwa chuma".

"Hata mimi lazima niungame kuwa huwa vile vile nafikiri wewe si binadamu wa kawaida maana mambo unayofanya nashindwa hata kueleza".

"Taa kwenye barabara hii zimezidi, hapa na pale taa, nadhani ndizo zinazosababisha msongamano wa magari", Linda alilalamika wakati tukiwa tumesimamishwa kwenye taa za usalama barabarani za karibu na Shirika la Usagaji na ofisi za Tazara..

"Hata mimi nafikiri hivyo hivyo. Nafikiri barabara hii ingefanywa barabara muhimu, na magari yote yatakiwe kwenda kasi, tuseme si chini ya kilomita themanini kwa saa. Hii ingesaidia watu kufika kazini haraka au wasafri wanaosafiri kwa ndege wasingekuwa na wasiwasi wa kuchelewa kama ilivyo hivi sasa".

Tulipoingia Colt Motors tulimkuta meneja ndio anarudi kipindi cha alasiri.

"Mbona umerudi haraka nawe ulisema utarudi baada ya wiki tatu?," meneja wa karakana aliniuliza.

"Nilipata habari kuwa mama anaumwa ikabidi nirudi haraka sana".

"Oh pole sana, kuna kitu chochote tunaweza kusaidia?".

"Asante sana, nimemwona; anapata matibabu ya kutosha huko hospitali ya Muhimbili".

"Kama utahitaji msaada wakati wowote usisite kusema".

"Asante, nitakumbuka", nilijibu.

Tulikuwa tumejenga uhusiano mzuri wa kibiashara na kampuni hii. Nilifuatana na Linda mpaka kwenye gari lake nikachukua mfuko wangu.

"Linda itabidi umwambie Godwin aweke watu wa kuaminika sana kwa usiku wa leo maana nategemea wageni. Akipata habari zozote anieleze moja kwa moja nyumbani, mimi sitakwenda mbali leo. Nitatoka kidogo saa mbili hivi na nitakuwa Palm Beach Hoteli kwa chakula cha jioni, lakini baada ya chakula nitarudi nyumbani.

"Usiwe na sahaka, yote yatatekelezwa kama ulivyotaka".

Tuliagana mimi nikaingia ndani ya gari langu na kuelekea nyumbani kwangu Upanga.

                           
                                          IV
Wakati nilipokuwa nimeondoka, kwa kujua kwamba nitakaa nje karibu mwezi mzima, nilikuwa nimemweleza mfanyakazi wangu naye achukue likizo. Alikuwa amekwenda Morogoro.

Nilipofika nyumbani kwangu, nyumba ambayo iko barabara ya Upanga karibu na Hoteli ya Plm Beach, nilimkuta mlinzi niliyekuwa nimemwajiri kwa muda kutoka kampuni ya ulinzi.

"Hapa salama", niliuliza.

"Salama tu, Mzee", alijibu.

"Nimerudi, hivyo sidhani kama nitakuhitaji tena. Nitawapigia simu ofisini kwako, hivyo unaweza kuondoka.

"Asante sana Mzee", alijibu huku akiondoka.

Niliweka gari langu gereji, nikafungua mlango wa nyumba, nikaingia ndani. Nyumba ilikuwa shwali kabisa.

Nilipomaliza kuoga ilikuwa saa kumi kamili za mchana, nilijibwaga kitandani nikalala na kupata usingizi moja kwa moja. Nilipoamuka ilikuwa saa moja na nusu. Hivyo nilivaa nguo nikanawa uso na kuelekea Palm Beach Hoteli. Kwa sababu Palm Beach ni karibu na nyumbani kwangu nilitembea kwa miguu. Na nilipoingia Palm Beach niliagiza chakula nikaomba nipewe haraka kwa sababu mimi najulikana kwenye Hoteli hii, nilishughulikiwa haraka sana.

Nilikula chakula changu upesi upesi na kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani nilivaa nguo za kulalia na kuingia kitandani. Kwa vile nilikuwa na usingizi mzito nilikuwa nasikia uchovu tena nilijua huu ndio ulikuwa usiku wangu wa kulala, maana siku zifuatazo nilijua kulala kwangu kutakuwa haba kweli. Usingizi ulinichukua mara tu baada ya kujitupa kitandani.

Niliamswa na mlio wa kengere ya simu. Nilipoangalia saa yangu ilikuwa inasema yapata saa nane.

Niliinua simu.

"Hallo Gamba hapa".

"Hallo bosi habari za kulala?".

"Lo Linda vipi?, bado uko ofisini".

"Nilijua kazi uliyoagiza inaweza kuwa ya maana hivyo nilionelea niishughulikie mwenyewe".

"Oh, mtoto wewe, wacha kufanya hivyo wewe bado mdogo unahitaji usingizi wako, tuachie sisi mambo hayo".

"Ni lazima nianze kujikomaza, vinginevyo sitaweza kulingana na shughuli zako, maana nimejifunza toka kwa Maselina ambaye anaweza kukaa siku mbili bila kulala kama kuna kazi inayobidi kufanyika kiasi hicho. Hivyo na mimi lazima nijizoeze muda huo ufikapo nisiuone mgumu".

"Haya mama, nafikiri una sababu ya maana. Haya leta ujumbe, naamini hukunipigia kunielezea uko ofisini mpaka saa hizi".

"La hasha, kuna wageni wako wawili wameingia hapa mjini wameniambie nikupashe habari zao. Ahmed Sherrif amefikia New Afrika Hoteli na Veronika Amadu amefikia Kilimanjaro Hoteli. wanasema kama inawezekana uwapigie simu sasa hivi".

"Asante nitafanya hivyo. Sasa wewe nenda ukalale. Mpigie Juma aje aendelee na kazi maana nitakuhitaji kwa kazi kesho asubuhi".

"Haya bosi nitafanya hivyo".

"Kwa heri, kalale salama mtoto wewe".

"Asante", alijibu na kukata simu.

Niliinua simu tena na kupiga New Afrika.

"Hallo New Afrika Hoteli habari yako ndugu?".

"Nzuri".

"Nipe mapokezi".

"Oke".

"Hallo mapokezi hapa".

"Nina mgeni wangu hapa ameingia usiku huu anaitwa Ahmed Sherrif naomba kuzungumza naye".

"Subiri bado yuko hapa mapokezi".

"Willy hapa habari ya safari?".

"Ohoo Willy, ofisi yako inafanya kazi vizuri sana tayari umeshapata habari?".

"Ndio, mmefika salama?".

"Ndio salama, salimini".

"Tulifikiri hatutaruhusiwa kuingia kama waandishi wengine wanavyorudishwa uwanja wa ndege wasiingie Tanzania. Lakini sisi tumeruhusiwa ni ajabu sana".

"Usijali tutazungumza kesho".

"Oke tuonane hapa Hotelini saa nne maana nina usingizi tele hapa niliposimama".

"Oke, tutaonana saa hizo, lala salama".

"Asante sana Willy".

Nilikata simu kisha nikapiga Kilimanjaro Hoteli.

"Hallo Kilimanjaro hapa".

"Habari yako ndugu?".

Nilimsalimia Opareta.

"Nzuri".

"Nina mgeni wangu amefikia Hotelini kwenu hapo nafikiri bado yuko mapokezi anaitwa Veronika Amadu".

"Subiri amepelekwa sasa hivi chumbani kweke".

"Hallo", nilisikia sauti ya Veronika.

"Hallo binti hujambo?".

"Hallo Willy, hujambo mpenzi?".

"Sijambo mie, pole na safari".

"Asante nimepoa".

"Najua umechoka nilitaka kujua tu kama umfika salama".

"Nimefika salama. Njoo unione saa tatu hivi kesho nitakuwa nimeisha amka".

"Uko chumba gani?".

"Niko orofa ya pili 208".

"Oke binti, tutaonana asubuhi".

"Ukifika gonga mara mbili haraka haraka, halafu ya tatu subiri kidogo halafu gonga nitajua ni wewe".

"Asante nitafanya hivyo".

"Kwa heri mpenzi, tutaonana asubuhi".

"Asante, kwa heri".

Niliweka simu chini nikalala ili nipumzike tayari kwa shughuli za asubuhi.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU