NJAMA....

                                    
SURA YA NNE
FUNUNU   
"Samahani binti tunaomba kumuona Meneja", nilimwambia mwandishi mahsusi wa Meneja wa Bandari.

"Sijui nyinyi ni akina nani?", aliuliza msichana huyu aliyeonekana amechoka choka.

"Mwambie ni Willy Gamba na wateja wake kutoka gazeti la Afrika".

Meneja wa Bandari tulikuwa tunafahamiana kikazi, hasa kutokana na shughuli zingine tulizokuwa tunazifanya katika kampuni yetu ya Afrika Internation Agencies.

Yule msichana alizungumza na bosi wake kwa simu, alipomaliza alinyanyuka na kutufungulia mlango tukaingia ndani. Tulimkuta Issack Mlingi ambaye ndiye Meneja wa Bandari aliyehusika na tukio hili akionyesha hali ya kuchoka sana. Nafikiri hii ilitokana na bughudha alizopata toka kwa polisi na watu wengine wanaohusika na upelelezi wa tukio hili. Macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba.

"Karibuni ndani", alisema huku akinyanyuka ili tusalimiane.

"Samahani ndugu Mlingi, naamini una shughuli nyingi sana", nilimuomba radhi.

"Si kitu Gamba, karibuni".

"Hawa ni wateja wangu Sherriff na Veronika kutoka gazeti la Afrika ambalo kampuni yangu ni wakala wake, na jamani huyu ni Issack Mlingi, Meneja wa Bandari", walipeana mikono kisha wote tukavuta viti tukakaa.

"Ndugu Mlingi ni imani yangu kuwa umeisha ulizwa maswali mengi juu ya tukio hili lililotokea hapa bandarini. Lakini naamini hatutakuwa tumekuhangaisha kama tutakuuliza maswali. Kama nilivyokwisha kwambia hawa waandishi wa gazeti la Afrika na ni waandishi pekee walioruhusiwa kuingia hapa nchini kuandika juu ya tukio hili, naamini unajua msimamo wa gazeti la Afrika. Hata hivyo tutakuuliza maswali kidogo tu kusudi tusikuchoshe sana".

"Hebu nipeni vitambulisho vyenu niviangalie", aliomba.

Sherriff na Veronika walimpa vitambulisho, akaviangalia na aliporidhika akavirudisha.

"Haya ulizeni maswali yenu, maana ikiendelea hivi naweza kupata wazimu", alisema huku akitoa tabasamu la uchovu.

"Tumesoma maelezo yako uliyotoa polisi, ila tumekuja hapa kukuuliza maswali machache juu ya mambo ambayo hatukuwa tumeyaelewa vizuri", alisema Sherriff.

"Ulieleza kuwa ulipata simu kutoka kwa Jones Mantare ambaye umezoea sana sauti yake, kiasi kwamba huwezi kuikosea ukiisikia. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, Mantare anasema hakuwa amekupigia simu kwani alikuwa na mkutano na Mwenyekiti wa Kamati na Mwenyekiti amethibitisha kuwa ni kweli walikuwa wote toka saa tisa hadi saa kumi na moja. Baada ya kupata maelezo hayo bado unaweza kusema kuwa sauti ile ni sawa kabisa na ya Mantare?".

"Kwa sababu wakati ule nilikuwa sina wasiwasi kuwa kuna jambo baya roho yangu iliridhika kuwa ni Mantare. Lakini sasa kwa sababu Mantare anasema hakupiga simu, ndipo nakumbuka kuwa nilimwuliza kama ana mafua, maana kwa mbali alikuwa akizungumzia puani, na yeye alijibu kweli mafua yalikuwa yamemkaba sana. Lakini maelezo mengine, mathalani ambayo huwa tunataniana na Jonas, yalikuwa yote sawa. Kusema kweli inawezekana kabisa alikuwa mtu mwingine anayemfahamu sana, lazima niseme sana maana isingekuwa hili jambo la mafua bado ningeendelea kung'ang'ania alikuwa Jones. Lakini Jones amekuja hapa hana mafua hata kidogo kwa siku nyingi".

"Hebu fikiria tena kidogo juu ya sura na sauti au umbile na tabia ya huyu mtu aliyekuwa akijiita Meja Paul Liboi, unaweza kuwa na uhakika kabisa kuwa mtu huyu ni mzalendo wa Tanzania?", Veronika aliuliza.

Ndugu Mlingi alisita kidogo kujibu swali hili na uso wake ukakunjamana kidogo. Baada ya kufikiri sana akasema.

"Nafikiri anaweza asiwe mzalendo".

Wote tukamwangalia.

"Kwanini unafikiri hivyo?", mimi nilimuuliza.

"Wazo hili lilikuwa halijaingia kichwani mwangu, lakini sasa baada ya kuuliza swali hili inawezekana mtu huyu asiwe mtanzania maana kwanza kiswahili chake hakikuwa kimenyooka na alipenda sana kuchanganya na kiingereza. Mimi nilimfikiria kuwa huenda ni Mjaruo, lakini alikuwa hajang'oa meno. Vile vile alikuwa na haraka haraka na maneno ya mkato mkato. Nikifiri sana hakuna na ile hali ya kirafiki waliyonayo watanzania wengine wengi. Lakini kwa sababu nilijuwa ni mwanajeshi nikafikiri ndio sababu aikuwa na tabia ya namna hiyo".

"Una jambo jingine ambalo huenda sasa unafikiri halikuwa lakawaida juu ya tukio lolote baada ya kujuwa watu hawa walikuwa majahiri?".

"Nafikiri nimeshasema yote, ila tu huenda kitu kimoja, sijui kama kinahusika ama vipi".

"Ehe, kitu gani".

"Baada ya kuzungumza na huyo anayejiita Jones Mantare, simu za jengo hili hazikufanya kazi tena. Tulipowaeleza Posta kesho yake, walikuja mafundi na kusema waya inayounganisha jengo hili na waya zinazokwenda Posta ilikuwa imekatika kwa kuangukiwa na mti. Sasa nilianza kuona picha kidogo ya tukio hili. Nilijua mara moja kuwa watu waliokuwa wameshughulikia tukio hili ni watu wenye kujua ujasusi wa hali ya juu; kwani walihakikisha kuwa kila hatua wanayoichukua na nyayo zake wanazifuta ili asiwepo mtu wa kuzifuatiia".

TUjikuta tumeridhishwa sana na safari yetu ya bandarini hivyo tukaona tuondoke.

"Asante sana ndugu Mlingi, kama tukihitaji mambo zaidi tutakuona tena, na kama utakumbuka kitu cochote kinachoweza kutusaidia nipigie simu. Nafikiri simu yangu unayo?", nilimuuliza.

"Ndio ninayo", alijibu.

"Na tahadhali usizungumze ovyo juu ya tukio hili, maana si tukio zuri", nilimwonya.

"Bila shaka nitajitahidi".

Tuliagana nae, tukaondoka kuelekea mjini.

Nilijaribu nilivyoweza kuangalia kama naweza kumwona Eddy na mwenzake, lakini wapi hakika vijana walikuwa wanafanya kazi nzuri sana, maana kama mimi Willy sikuweza kuwatambua basi hakuna mtu mwingine tena, si kama najisifu ila huo ndio ukweli, mtu akitaka kunitafuta mimi basi ajiweke sawa, la sivyo shauri lake.

"Kamara kama ulivyomjua alikuwa mtu wa namna gani, unafiri anaweza kwa njia yoyote akawa kajiingiza katika jambo hili?", nilimuuliza Sherriff huku tukiwa tumesimama kungojea kuingia barabara ya site drive, tukutokea bandarini.

"Mimi nakuhakikishia komredi kuwa Kamara alikuwa hawezi kufanya jambo kama hilo, ni lazima tu iko namna ambayo alishambuliwa na kunyang'anywa karatasi hizo, alinihakikishia Sherriff.

"Oke, naona sasa twende kwenye ofisi ya kamati ya Ukombozi ya OAU", nilimweleza huku nageuza gari kuingia site drive na kuelekea kwenye ofisi ya kamati.

Tulipofika kwenye mapokezi ya ofisi hii ya kamati na kumkuta msichana mmoja akizungumza kwenye simu, ikatubidi tumsubiri kidogo amalize kuzungumza, niliangalia saa yangu ilikuwa yapata saa sita na dakika tano.

"Samani jamani, sijui niwasaidie nini", msichana alituuliza.

"Bila samahani binti, sisi tunaomba kumwona Jones Mantare", nilijibu.

"Mna ahadi naye?", binti aliuliza.

"Hapa, lakini nafikiri ukimwambia Willy Gamba wa AIA na wageni toka gazeti la Afrika, ambao wanataka kumwona, anaweza kutuona", nilimweleza.

"Msubiri basi", huyo msichana alijibu kisha akainua simu na kuanza kuzungumza na ofisi ya Mantare. Jones Mantare alikuwa ananifahamu, maana nilikuwa nimehakikisha kuwa nafahamiana karibu na kila mtu katika ofisi hii ya kamati, yeye alikuwa akinifahamu kama mfanyabiashara, maana ndivyo nilivyojulishwa kwake. Tokea hapo tulikuwa tunaonana mara kwa mara sehemu za starehe na kujenga uelewano wa kutosha, hivyo nilihisi kuwa asingeweza kunikatalia nisimuone, ingawa nilijuwa atakuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida. Baada ya kuzungumza kwa muda kwenye simu msichana alitwambia.

"Mnaweza kwenda kumwona, ofisi yake ipo mwisho wa ujia mkono wa kulia".

"Asante sana binti", nilimjibu.

Tulimwacha tukaelekea alikotuelekeza. Tulibisha mlango pale tulipokuwa tumeelekezwa.

"Karibu", tulisikia sauti ya msichana ikitoka ndani. Nilifungua mlango tukaingia na tujikuta katika ofisi kubwa ya mwandishi mahsusi wa Mantare.

"Habari zako bibie", nilimsalimia kwa niaba ya mwenzangu.

"Nzuri, ni Gamba na wenzake nafikiri?", aliuliza.

"Hasa", nilijibu.

"Ingieni moja kwa moja anawasubiri", alisema huku akisimama na kutufungulia mlango wa bosi wake. Tulipoingia tu Mantare alisimama.

"Ahaa ndugu Willy, karibuni".

"Asante, asante Jones".

"Nafikiri niwajulishe, huyu ni ndugu Jones Mantare, ofisa katika kamati hii ya ukombozi, na hawa ni komredi Ahmedi Sherriff na komredi Veronika Amadu. Ni waandishi wa habari wa gazeti la "AFRIKA".

Walipeana mikono kwa mara nyingine.

"Ehe, mlitaka kuniona, sijui niwasaidie nini?", aliuliza.

"Hawa makomredi ni wateja wangu, kampuni yangu ndio wakala wa gazeti la Afrika hapa nchini. Hasa kitu kilichotueta hapa ni kutokana na tukio hili la juzi. Nafikiri unaelewa msimamo wa gazeti la Afrika katika ukombozi, na kutokana na msimamo huo wameiomba serikali kama wanaweza kuandika habari za kuaminika juu ya tukio hili. Ni wasiwasi wao kuwa magazeti mengi ya kibeberu yataandika habari za kupotosha, na wao wako hapa ili waweze kueleza jumuia ya ulimwengu ukweli mtupu. Kwa hiyo tutashukuru sana ukiweza kutusaidia katika kujibu maswali machache. Hatutataka kupoteza muda wako kutueleza mengi, maana nakala ya maelezo yako tumeipata toka polisi. Hivi ni nia yetu uweze kutufafanulia katika sehemu ambazo hazieleweki katika tukio hili".

Niliona kule kutaja nakala ya maelezo yake kutoka polisi kulimtoa wasiwasi aliokuwa ameuonyesha usoni mwake. Niliona macho ya Veronika yakiwaka kuonyesha kuwa nilivyoeleza nimeeleza vizuri sana na Sherriff alitingisha kichwa kuonyesha kuwa niliyoyasema ni sawa kabisa.

"Sawa ndugu Willy, nitakuwa tayari kuwajibu mwaswali yenu, kusema kweli kama ulivyosema, radio za kibeberu zimekwisha tangaza uongo ili kuridhisha maslahi yao. Kwa jinsi hii tutakuwa radhi kuona ukweli unaandikwa na gazeti hili. Haya sijui mna maswali gani?".

"Inasemekana kuwa hayati Kamara Franki ndiye alikuwa anashughulikia suala hili la silaha. Na amekutwa ameuawa. Nafikiria hizi karatasi zilitokatokaje mikononi mwa marehemu na kuingia mikononi mwa hawa majahiri?. Maana kutokana na maelezo ya Polisi ofisi yenu hii haikuvunjwa mahali popote", Sherriff aliuliza.

"Sawa kabisa?, kutokana na maelezo ya mwandishi mahsusi wa marehemu, anasema ya kwamba?, wakati marehemu anatoka ofisini alimweleza aweke zile karatasi za kuchukulia silaha ndani ya mkoba wake, kwa sababu alikuwa anategemea kwenda kwenye kikosi cha Jeshi kinachoshughulikia silaha za wapigania uhuru kesho yake, kabla hajaja ofisini. Kwa hiyo, jibu kwa swali lako ni kwamba watu hawa walimnyang'anya marehemu karatasi hizo na ndio sababu wamemuua."

"Watu hawa unafikiri walijuajuaje kuwa marehemu atakuwa na karatasi hizi ndani ya mkoba wake?", Veronika aliuliza.

"Hapo ndipo hata sisi tumekwama".

"Huyu mwandishi mahsusi wa marehemu yupo", nilimuuliza.

"Ndio yupo".

"Unaweza kumwita tukazungumza nae kidogo?".

"Hali yake si nzuri sana, bado ana mshituko kwa ajili ya marehemu. Unajua mnapofanya kazi kwa uhusiano ulio karibu na mtu mnakuwa na urafiki wa hali ya juu sana. Hata hivyo nitajaribu kuwaitieni".

Alishika simu na kuzungumza na mwandishi wake. Wakati tukimsubiri Veronika alimuuliza tena. "Ofisa wa kule bandarini Ndugu Mlingi anasema mtu aliyempigia simu alikuwa na sauti kama yako, mathalani mambo mnayotaniana yalikuwa vile vile, unaweza kufikiri mtu yeyote hapa ofisini au hata nje anayeweza kuigiza sauti yako kiasi hicho?".

"Ni imani yangu kuwa mtu kukuigiza kiasi hicho lazima awe mtu aliyekuzoea, na mtu aliyekusikia ukizungumza mara kwa mara, hasa na huyu ndugu Mlingi".

"Kuesema kweli, nimefikiria kweli juu ya mtu huyu mpaka nimechoka, nitazidi kumfikiria kama wazo likinijia nitakupigia simu."

Mara mlango ulifunguliwa akaingia msichana mrefu mwembamba mwenye nywele nyingi. Kama unapenda wasichana warefu na wembamba, basi hapa pana msichana wa namna hiyo, jina lake Margreth. Ni mzuri kiasi chake.

"Karibu Margreth", Mantare alimkaribisha, wote tukasimama akatujulisha kwake. Mwandishi mahsusi alileta kiti kingine na Margreth akaketi.

"Samahani Margreth", hawa ndugu wana maswali kidogo ya kukuuliza," Mantare alimwambia.

Margreth hakujibu kiti bali alituangalia tu.

"Samahani sana binti, sisi wote yunaelewa hali uliyonayo, ila imetubidi tukuone tuweze kuzungumza nawe huenda utatusaidia kutatua huu mkasa uliompata bosi wako", nilimwelezea.

"Niko tayari kuwaelezea chochote kama kitasidia kuwapata watu waliomuua bosi wangu." Magreth alijibu huku machozi yakimlengalenga.

"Jaribu kukumbuka, nilimwambia, "wakati marehemu anakueleza uweke zile karatasi za kuchukulia silaha kulikuwa na mtu mwingine yeyote?".

Alikaa kimya kwa muda kisha akajibu, "Hapana", harafu kama amegutuka akasema, "Ndio nakumbuka sasa, alikuwepo tarishi wetu wa hapa ofisini".

Nikasikia kengere ya tahadhari inalia kichwani mwangu. Wote tulitazamana.

"Tarishi huyu yuko hapa?", niliuliza.

"Hapana, ni mgonjwa anaumwa na ameandikiwa kulala siku tano', Margreth alijibu.

"Toka lini?".

"Toka tarehe nne".

"Yaani siku ambayo ilibainika kuwa silaha zimeibiwa na bosi wako ameuawa?".

"Ndio".

"Yaani atakuwa kazini tarehe tisa".

"Ndio".

"Una uhakika kabisa alikuwepo?".

"Ndio".

Habari kama hizi mimi ndizo huwa zinanitibua, maana wakati kifo kinatokea haafu kinatokea kitu kingine chenye uhusiano wa karibu namna hii, basi hapo ndipo huwa naanza kujumulisha moja kwa moja na kupata mbili.

Nilimgeukia Mantare na kumwuliza, "Huyu tarishi ndiye alikuwa tarishi wa ofisi nzima?".

"Ndio'.

"Anaitwa nani?".

"Anaitwa George Kiki".

"Mmekuwa naye muda gari?".

"Yapata miezi sita sasa".

"Ni MTANZANIA!".

"Hapana ni mkimbizi kutoka Afrika Kusini, aliletwa kwenye ofisi yetu na chama cha wapigania uhuru cha Afrika Kusini kilichopo hapa mjini cha SANP. Ili tumsaidie. Alipokuja hapa alitupa maelezo yake na kuonekana ni kati ya vijana walioanzisha maandamano ya kitongoji cha Soweto huko Afrika Kusini. Alieleza kuwa yeye alipata mwanya wa kutoroka gerezani ndipo akakimbia na kuweza kufika hapa baada ya safari ndefu ya taabu. Kwa vile alikuwa hana kisomo cha kutosha jinsi yeye alivyojieleza tuliamua kumpa kazi ya utarishi ili kumsaidia. Kusema kweli amekuwa kijana mwenye bidii sana, na anapendwa na kila mfanyakazi wa hapa, hasa kwa nidhamu yake, na utekelezaji wa kazi yake".

"Kwa hivi alikuwa na fursa ya kuingia ndani ya ofisi ya mtu yeyote wakati waowote ili kuchukua mafaili na mambo kama hayo?".

"Hasa ndivyo ilivyokuwa".

"Anaishi wapi?".

"Anaishi huko Kinondoni sehemu za Hananasifu Estate katika nyumba za shirika la nyumba".

"Nyumba yenyewe unaijuwa?".

"Mimi nimewahi kufika kwake; tumewahi kumpeleka na marehemu", alisema Margret huku tena machozi yakimlengalenga.

"Samahani Mantare, sijui unaweza kumruhusu Margret akatuelekeza kwa Ndugu Kiki?".

"Bila wasiwasi mnaweza kwenda nae".

Niliwaangalia wenzangu nikaona wameridhika na maswali na majibu ya hapa, hivyo kwa niaba yao nikamshukuru ndugu Mantare.

"Ikiwa tutahitaji jambo lolote tutarudi tena au tutapiga simu. Na wewe ukipata jambo lolote usisite kutufahamisha".

"Hamna tabu, nitafurahi kuwasaidia".

Tuliagana tukaondoka kuelekea Kinondoni.

ITAENDEEA....

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU