NJAMA

SURA YA TANO
TWATOANA JASHO

Niliongeza gari moto ili wasije kunipotea. walikata kulia wakaingia mtaa wa Railway, nilipoingia mimi mtaa huu wao walikuwa wamefika kwenye mzunguko wa 'Clock Tower' na kuingia mtaa wa Nkurumah.

Kwenye mtaa huu wa Nkurumah niliwakaribia kabisa, nikiwa nimeacha gari mbili tu kati yangu na wao. Niliona mmoja katika gari lao akitoa kichwa nje na kuangalia nyuma, nadhani wanadhani nitawafuata na gari langu ambalo wanalijua sana. Lakini hawajui Willy ni mtu wa namna gani. Wakati huo nilikuwa naendesha gari aina ya Fiat 132 GLS, na si Colt Gallant Sports kama ambavyo walikuwa wanafikiria.

Walikwenda moja kwa moja na kushika barabara ya Pugu. Walipofika kwenye njia panda ya barabara ya chang'ombe na Pugu, walikata kushoto na kuingia barabara ya Chang'ombe. Saa hizi magari hayakuwa mengi hivyo kila gari lilikwenda kasi. Nilikuwa na bahati kuwa magari yale mawili yaliyokuwa kati yangu na wao nayo yalikata na kuingia barabara hiyo hiyo kuzidi kunificha.

Walipofika kwenye sehemu ambayo barabara ya Mbozi inagongana na Chang'ombe walikata kulia na kufuata barabara hiyo. hizi gari mbili mbele yangu zilionyesha kuwa zilikuwa zinaendelea na barabara ya Chang'ombe. Nilipunguza mwendo ili wasije wajanitambua. Mara nilisikia wanapiga honi ya namna ya pekee kabla ya kufika kwenye jengo la Kampuni ya rangi ya Sadolins.

Ghafla lango la uwa la bohari moja lilifunguliwa na bila hata kupunguza mwendo, gari hii ilikata kushoto na kuingia ndani na hapo lango likafungwa. Mimi nilipitiliza kama kwamba sina habari na watu hawa. Ilikuwa inakaribia saa moja za jioni, hivyo giza lilikuwa limeanza kuingia. Nilisimamisha gari langu kama mita mia mbili hivi, nikaanza kurudi haraka kwa miguu.

Bohari hili ambalo lilikuwa limezungukwa na ukuta wa matofali ya saruji, lilikuwa limeandikwa 'Mamlaka ya Pamba'. Mimi nilishangaa sana kwani sikujua hii ni maana gani. Ukuta wa uwa huu ulikuwa na urefu usiozidi futi kumi na mbili, hivyo kwangu ukuta kama huu kuupanda ni kazi ndogo. Nilikwenda kwenye upande wa lango kubwa, nikazunguka pembe ya kushoto ya uwa huu. Ukuta huu ulikuwa unapakana na ukuta wa bohari nyingine la namna hiyo hiyo kwa upande huu wa kushoto.

Nilikwenda kama hatua tatu hivi kwenye nafasi hii ya kati ya mabohari haya, nikavua viatu, nikarudi nyuma kidogo halafu nikaurukia huu ukuta na kuukwea huku mikono yangu ikikamata juu yake. nilivuta mwili wangu wote kimya kimya kama paka nikachungulia ndani ya uwa.

Pale karibu na mlango nilimwona mtu amevaa koti refu la khaki rangi nyekundu lililokuwa linavuka magoti yake kidogo huku ameshikilia bunduki ya aina ya 'SMG' na akiangalia mlangoni. Bila kufanya hata chembe ya kelele nilivuta mwili wangu wote na kutambaa kama nyoka juuya ukuta huu uliokuwa na upana wa futi moja. Nilitambaa mpaka nikawa karibu kabisa na mtu huyu kwa juu yake bila yeye kufahamu. Nilijirusha chini na kufanya kishindo kidogo nae akageuka. Mimi nilikuwa tayari nikamkata karate ya shingo kabla hajajua nini kinamjia. Akazilai. Nikamshikilia na kumlaza chini taratibu. Muda kitambo aloikufa.

Nilimvua lile koti lake nikalivaa mimi, halafu nikamnyanyua tena nikamlalisha chini na kumwegemeza kwenye ukuta. Nilichukua bunduki yake ambayo ilikuwa imejazwa risasi, nikafurahi sana kishika silaha namna ile. Mimi nikiwa na silaha namna ile hata likija jeshi la watu mia hawaniwezi. Nilijidhatiti tayari kwa mapambano zaidi nikanyata kwenda nyuma ya jengo la bohari ambako niliamini kuna mlango mwingine. Nilipofika kwenye pembe ya ukuta wa kushoto nilichungulia. Niliona kuna mlango wa mbele wa mlango alisimama mlinzi mwingine akiwa amevaa sawasawa na yule wa kwanza; koti refu jekundu.

Alikuwa nae ameshika bunduki ina ya 'SMG', niliona anafungua mlango anasema kwa sauti kali "Fanhyeni haraka bwana, kama hataki kueleza si niambieni mimi akaonane na babu zake huko ahera". Alirudisha mlango akaangaza huku na huku. Kutokana na maelezo yake ni kwamba Sherriff alikuwa anaswalishwa na majahiri na bila shaka alikuwa akipata kipigo kikubwa.

Nilitumbukiza mkono ndani ya mifuko ya koti nililovaa nikakuta mna sigara na hamna kiberiti. Wazo likanijua nikamfanyia yule mlinzi 'sss' aligeuka akaniona akidhani ni mwenzake, nilimuonyesha sigara na kuwa nataka moto. Bila kusita akaja akatoa kiberiti na kwa ajili ya giza sasa hakuweza kunitambua sababu ya lile koti. Aliponyoosha mkono kunipa kiberiti. Kama radi nilimrukia na kumpiga karate ya mikono miwili shingoni. Sikuwa na haja ya kumwangalia maana nilijua kwa kipigo hicho hawezi kuishi. Nilimvutia upande huu wa kushoto na kumwegemeza kwenye gari lao. Nilichukua bunduki yake iliyokuwa na ukanda mrefu nikaingika begani na kuiweka mgongoni.

Sasa njia ilikuwa wazi kwenda mpaka mlangoni, kwa kutokana na ujuzi wangu wa kuiga sauti ya yule mlinzi wa nje kwa maneno yake aliyosema mimi nilisema. 'Vipi hajasema lolote?," nikiwa nimefungua mlango kidogo na kuchungulia ndani. Bohari lilikuwa limejaa robo tu ya marobota ya pamba. Sherriff alikuwa ameshikwa na watu wawili na mmoja alikuwa amebeba bao akimtandika tumboni kwa nguvu sana.

"Sema nyie si waandishi wa magazeti ila ni wapelelezi, ndio".

"Yote ya kweli nimeshaeleza ".

Kabla hajaanza kumpigab tena nilisema. "Mmoja wenu aje hapa, mimi mnanijua hivyo hatachukua dakika kabla hajasema uweli wake".

Shomvi alikuja akikimbia, nikamfungulia mlango na kurudisha mara moja. Alipoangalia ba kutambua mimi si Luis akataka kupiga kelele lakini nilimwahi karate ya katikati ya kichwa akafa bila kelele. Watu wa mle ndani waliokuwa wamemshikilia Sherriff walikuwa hawana bastola mikononi ila zilionekana kwenye mapaja. Nilifungua mlango ghafla SMG mkononi nikamwahi mmoja wao kabla hata hawajaelewa nini kinatokea.

"Ukijaribu chochote umekufa", nilisema kwa sauti ya kutetemesha.

Sherriff alishangaa kuniona akaruka ile maiti akasimama upande mwingine. Niliona ile SMG ya pili nikampa, akatabasamu. Jinsi alivyoijaribu mkononi nilikua huyu mtu anajua kuitumia.

"Chukua hizo silaha zake", Sherriff alimkagua akatoa bastola mbili zenye sailensa na visu viwili vyenye mpini mwekundu.

"Ah, ni wakati wako sasa kujibu maswali yetu, nyinyi ni nani", nilimwuliza.

"Mimi sijui, mimi niliajiriwa tu leo hii asubuhi na Kimkondo, huyu uliyemwua hapo chini, kuwa kuna kazi ya kumkamata mtu mwenye habari ambazo wakubwa wake wanataka. Pesa tulizolipwa zilikuwa nyingi, shilingi elfu kumi kwa kila mtu kwa kazi ya masaa machache tu nami nikakubali, kusema ukweli sijui lolote".

"Yeye Kimkondo anafanya kazi gani?".

"Yeye ni jambazi tu anayepewa kazi ya ujambazi hapa na pale".

Kutokana na maelezo ya huyu mtu nikajua anasema kweli. Nilijilaumu kumwua Kimkondo maana yeye huenda angetupa mwanga zaidi. Lakini hii yote inaonyesha jinsi majahiri hawa yalivyokuwa yamepanga ujahili wao kwa ufundi.

"Lo Willy asante sana".

"Sahau", nilimjibu kwa mkato.

Ile sura ya kikatili ilikuwa tayari imekuja usoni mwangu. Katika hali kama hii sura yangu hubadilika na kuwa mtu tofauti kabisa. Hivyo nilipomwambia Sherriff sahau niliona anashituka kidogo.

"Twende zetu tutoke hapa Sherriff, huyu nitajua mahali ya kumpeleka".

Tulimtangulia, tukafungua mlango wa bohari tayari kurudi mjini. Tulipokuwa tumefika kwenye kona niliyotokea, tukasikia honi ya gari ya namna ile ile waliokuwa wamepiga hawa majahili wa kwanza.

"Sherriff na wewe mtu mjifiche nyuma ya hili gari, kwa vile mimi nimevalia koti lao ambalo naona ndicho kitambulisho chao nitakwenda kufungua lango, unayo ile bastola uliyochukua kwake?".

"Ndio".

"Basi akifanya ushenzi unajua la kufanya; maiti hazisemi'.

Niliwaacha nikakimbia mpaka kwenye lango nikafungua. Gari aina ya VW Kombi iliingia imejaa watu wamevalia makoti kama langu, Gari hili lilisimama nyuma ya lile gari la kwanza. Milango ikafunguliwa wakaanza kutoka. Mimi nilikuwa tayari na SMG yangu.

"Rudini ndani......." niliona yule mtu tuliyekuwa tumemshika ameruka juu ya gari na kutoa onyo, lakini kabla hajamaliza Sherriff alimlamba risasi ya kichwa akaanguka juu ya gari, mimi nikajua tayari mambo yametibuka, hivyo sasa ni kazi.

Dereva wa gari hii na watu wengine waliokuwa bado ndani ya gari walifunga mlango ili waondoke. Wale waliotoka nje walianguka chini na kutoa bastola tayari kwa mapambano. Mimi nilikuwa nimeishavua koti nimerukia ukutani na tayari SMG mkononi. Nilikuwa nimelalia tumbo juu kabisa ya ukuta. Lile gari lilipopiga moto, nililenga mlango wa dereva na kuachia risasi mfululizo kama mchezo.

Sherriff alikuwa bado kimya hajaanza shughuli. Wale watu watano waliokuwa wametoka ndani ya gari nao walikuwa wametambaa upande mwingine wa kombi. Kumbe mmoja wao aliniona kule juu baada ya kuona risasi zilizoua wenzake zikitokea juu. Mimi nilikuwa bado sijamwona hivyo akainuka kunimaliza. Lakini kumbe Sherriff alimwona kabla hajafyatua risasi, akamwahi. Nilipomwona Sherriff akanionyesha ishara. Alikunja kiganja halafu akainua kidole kimoja kuonyesha kuwa ni watano na mmoja tayari kafa.

Mimi nilijirusha chini toka ukutani na kujiviringisha huku nakoswa koswa risasi za maadui. Niliposimama huku nikikimbia zigizaga na wakati huo nikipiga risasi ovyo kuwazuia wasipige. Nilifika mlango na kufungua kama ninakimbia nje. Wale kwa woga wao walipoona hivi nao walianza kukimbia kuwahi mlangoni.

Kumbe ndipo walikuwa wanampa fursa Sherriff kuwachukua mmoja mmoja vizuri sana. Na mimi ghafla nilijitokeza tena na kumimina risasi kwa wawili waliokuwa mbele. Bahati nzuri Sherriff alijitupa chini la sivyo ingetokea ajali kwani yeye alifikiri nitawasubiri nje hivyo naye alikuwa anawafuata nyuma.

"Kazi nzuri Sherriff, la sivyo ningekuua, pole sana", nilimpa mkono.

"Hali kama hizi nimezizoea sana hivyo huwa niko tayari katika tahadhari kila mara kwani lazima kama huna uhakika mwenzako atafanya nini baadaye tegemea lolote", Sherriff alijibu.

Tulikimbia kutoka pale mpaka kwenye gari langu. Tuliingia na kuwasha gari moto na kuelekea zetu mjini.

"Mimi nilijua ndio mwisho wangu", Sherriff aliniambia.

"Kwa nini?".

"Maana walivyonivamia hata nilishindwa la kufanya halafu nilijua wewe utakuwa unanisubiri New Afrika na kumbe mimi nimeshauawa. Na kweli wangeniua".

Alitoa shati lake kuonyesha uvimbe mbaya sana kwenye tumbo lake.

"Nasikia maumivu ya ajabu. Watu hawa ni katili sana".

"Pole sana. Jambo la kusikitisha ni kwamba imebidi tuwaue wote. Hivyo bado tumerudi pale pale; hatujui lolote, isipokuwa tu kwamba watu hawa ni majahili wa hatari sana wanaovaa makoti mekundu na bunduki wanazotumia ni SMG za kichina, bastola za kirusi zenye sailensa. Zaidi ya hapo bado tuko mbali sana na ukweli wa mambo. Ila kinachonifurahisha ni kwamba sasa watashtuka baada ya mapambano haya ambamo tumeua watu wao karibu kumi na tano. Kule kushtuka ndiko kutatusaidia maana lazima watahaha na kufanya makosa".

"Sawa kabisa. Lakini mimi nataka kujua jinsi ulivyojua nimekamatwa na namna ya gari umeweza kuniokoa. Maana mimi sikuamini nilipokuona, nilidhani huenda ni malaika kashuka toka mbinguni katika sura yako".

Tukiwa bado tunaelekea mjini nilimweleza jinsi nilivyofanya.

"Lo ndio sababu wewe ni mpelelezi namba moja katika Afrika; mimi sasa nadhani hata katika dunia. Tukirudi London salama nitailisha komputa maelezo zaidi juu yako tuone itakuonyesha katika nafasi gani katika wapelelezi wa ulimwengu".

Mimi nilicheka tu sikujibu kitu.

"Na kule kubadili gari kulisaidia sana maana walipochungulia na kulikosa gari lako walinidhihaki kwa kusema kuwa sasa nitakufa peke yangu hata rafiki zangu hawatathubutu kuja hata kama wangeniona wakati ninakamatwa".

"Mimi ni mjuzi zaidi yao; lazima tuzidiane maarifa".

Tuliingia barabara ya Independece Avenue.

"Nitakupeleka kwa daktari wangu hapa Zanaki Street, na utalala hapo. Nafikiri kesho utakuwa katika hali nzuri, kwa leo lala hapo usirudi New Afrika ili daktari aweze kukupa matibabu kwanza. Nitakuja kukupitia asubuhi".

"Sawa wewe ndiye bosi", Sherriff alijibu.

Nilimpeleka kwenye zahati ya rafiki yangu Dk. Kiluwa na kumweleza amtibu na malipo yatalipwa na AIA. Nilimwacha nikawaahidi kuwaona asubuhi yake.
 
ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU