NJAMA

SURA YA TANO
 TWATOANA JASHO
III
"Eddy nafikiri unaweza kwenda kupumzika. Acha vijana wa zamu waendelee, maana kesho tunaweza kuwa na kazi nyingi sana".

"Asante tutaonana asubuhi", alijibu huku akikusanya kusanya karatasi zake.

Mimi niilimuaga nikaondoka zangu kuelekea New Afrika tayari kuonana na Veronika. Nilipofika New Afrika nilikuta duka la kahawa limejaa watu na ile sehemu ya Patio Baa ndio usiseme, maana vijana walikuwa wamejazana wakifurahia saa zao za baada ya kazi.

Nilishikashika mfukoni, nikachukua funguo za gari mkononi nikaelekea kwenye gari langu, niliona Vero alikuwa bado hajafika kwani hamkuwa na mtu ndani ya gari. Nilifungua mlango wa upande wa dereva ili nikae nimsubiri, maana nilijua asingechukua muda mwingi.

Nilipoingia na kukaa kitini na kuanza kutelemsha kioo, nilisikia kama kuna kitu kwenye viti vya nyuma vya gari langu. Nilipotaka kugeuka kuangalia nilisikia sauti ikisema. "Usigeuke la sivyo utakuwa ndio mwisho wako. Washa gari ondoka, na ufuate maelezo yangu".

Nilisikia mdomo baridi wa bastola ukigusa shingo yangu.

"Sawa mzee", nilijibu huku nikijifanya kama sijali.

"Siyo mzee, sema wazee. Tuko wawili na wote tuna bastola na tunajua kuzitumia hivyo usijaribu kitu chochote cha kuleta matatizo".

"Mimi sina wasiwasi, maana sijui kwanini natekwa nyara, kama nia yenu ni gari niambieni niwaachie. Mimi ni mfanyabiashara nitapata gari nyingine, kwangu pesa si tatizo".

"Funga domo lako, sisi hatuna haja na gari lako wala pesa yako, sisi tuna pesa kuliko wewe".

Kabla sijasema lolote aliniambia. "Kata kushoto ingia Independence Avenue, halafu ukifika 'Clock Tower' ingia mtaa wa Railway halafu shika barabara inayopita kwenye kituo cha polisi wa usalama barabarani, halafu ukifika kwenye mzunguko ingia kushoto, fuata barabara ya Kilwa mpaka nitakapo kueleza tena. Nasema tena ujanja wowote utakutokea puani".

"Usiwe na wasiwasi", nilijibu kiume.

"Nyamaza", alijibu kwa sauti ya ukali.

Nilijilaumu sana kwa kutochukua tahadhari zaidi kwa watu hawa.

Nilifikiria kama naweza kufanya lolote sasa nitakuwa kwenye upande wa hasara hivyo nikakata shauri la kufuata maelekezo mpaka mwisho ndipo nione la kufanya. Maana nafikiri kama nia yao ilikuwa ni kuniua wasingesita, walikuwa na mwanya mzuri sana nilipoingia bila tahadhari ndani ya gari. Nilijua nia yao si kuniua ila kuna habari walizozitaka. Nilimfikilia Veronika nikajua atahangaika sana kwani hatanikuta halafu hatajua Sherriff aliko.

Tulipokaribia uwanja wa Sabasaba aliniamuru nikate kushoto kwenye njia inayoelekea kwenye ofisi mojawapo za reli ya Tazara ya Kurasini. Tulipotelemka kidogo aliniamuru nikate kulia na kuingia kwenye mlango wa pembeni wa uwanja wa Monyesho ya Sabasaba.

Tulipofika kwenye mlango huu aliniamuru nipige honi. Nilipopiga honi mlango ulifunguliwa. Taa zangu zikamwulika mlinzi aliyevaa joho jekundu, nikajua mara moja ni nani nimepambana nae tena. Tena huyu mtu aliongeza na kofia nyekundu juu.

Nilishangazwa sana na mbinu za watu hawa, maana sehemu zo walizokuwa wanazitumia kama kambi zao za kufanyia uovu zilikuwa sehemu za kiserikali. Hii ilionyesha jinsi mbinu za watu hawa zilivyozidi kiwango.

"Ingia ndani moja kwa moja, fuata barabara mpaka nitakapokuabia simama", niliamriwa.

Uwanja ulikuwa kimya kabisa. Giza lilitanda kote ila taa za gari langu peke yake. Tulikwenda mpaka katikati ya vibanda.

"Simama hapa, zima taa na telemka taratibu. Ukifanya makosa usinilaumu", alinieleza. Nilipozima taa tu niliona vivuli vya watu vikinyata polepole kuja kwenye gari. Nilipokanyaga nje tu gari likawa limezungukwa na watu watatu. Wale waliokuwa ndani ya gari walitelemka.

"Mmemleta?", mmoja wa wale waliozunguka gari aliuliza.

"Ndio", alijibu yule mtu aliyekuwa ananipa amri".

"Kazi nzuri, haya twendeni".

Yule mtu aliyezungumza alitangulia mbele mimi nikaambiwa nimfuate huku nimezingirwa na watu wanne. Yaani wale wawili walioniteka, na wengine wawili waliokuwa wamebeba bunduki aina ile ile ya SMG, ilionekana hawa watu walitumia sana aina hii ya bunduki.

Niliongozwa moja kwa moja mpaka kwenye kibanda kimoja katikati kabisa ya uwanja wa maonyesho wa Sabasaba. Nilikumbuka kuwa kibanda hiki kilikuwa kinatumiwa na nchi za Zambia katika maonyesho ya Kimataifa. Mlango ulifunguliwa tukaingia. Ndani tulimkuta mtu mwingine anavuta mtemba amekaa kwenye kiti huku akitabasamu. Watu hawa wote walivalia majoho mekundu. Na hawa wanne niliowakuta huku kiwanjani walivaa kofia nyekundu isipokuwa wale walioniteka ndio hawakuwa na kofia.

"Karibu Willy Gamba, keti chini kwenye kiti", aliniambia yule mtu tuliyemkuta ndani.

"Asante, mimi ningependa kusimama", nilijibu.

"Mimi sitaki kukukarisha kwa nguvu, lakini kama unaona ni lazima nifanye hivyo ninao uwezo, Willy", aliniambia taratibu huku wale watu wengine wakinisogelea. Niliona hakuna haja kuchachamaa hapa hivyo niliketi kwenye kiti.

Chumba hiki kilikuwa kimewekwa fenicha nzuri sana, hata nikashangaa saa ngapi watu hawa waliweza kuaandaa chumba hiki kama ofisi na huku uwanja huu siku zote unalindwa.

"Romano na Charles mnaweza kwenda nje kusudi muwe tayari kukabiri jambo lolote linaloweza kutokea hapo nje wakati nikiwa na mazungumzo mafupi na Willy hapa", alitoa amri polepole kiasi kwamba ungeweza kuamini kuwa ni mtu mzuri sana, lakini macho yake yalionyesha uovu usio kifani.

NIlifurahi sana kwani nilijua kuwa sasa ninaonana na mtu wa maana katika kundi hili la majahili. Macho yetu yalipokutana ana kwa ana mara moja tukatambuana, maana huyu alikuwa jasusi wa hali ya juu. Sisi tuko kama mbwa tunajuana kwa harufu. Wale watu wawili wenye SMG walitoka nje tukabaki na wale watu walioniteka nyara, yule mtu aliyetupokea na huyu mtu tuliyemkuta humu ndani. Walipotoka nje waliufunga mlango.

"Bwana Gamba, mimi ni mtu nisiyependa kuumiza kwa sababu mimi huwa sijisikii vizuri nikiona mtu anaumizwa. Lakini nikilazimika kufanya hivyo, basi mimi hufumba macho. Nisingependa nifumbe macho kwako kwa hiyo naomba sana uwe mtu mwungwana katika kujibu maswa yangu".

"Nadhani ungependa kujua sisi ambao tuko hapa ni nani, sisi ni WANAMAPINDUZI WAPINGA MAPINDUZI".

"Wanamapinduzi wapinga mapinduzi maana yake nini?. Sikuelewi.

"Ni kwamba sisi tunapinga watu wanaojiita Wana mapinduzi, wanaofikiri wataleta uhuru Afrika Kusini kwa njia ya vita. Sisi ni wanamapinduzi ambao tuna imani kuwa tutaleta uhuru Afrika Kusini kwa mazungumzo bila kuua mtu hata mmoja. Sasa swali langu ni hili; Wewe na rafiki zako mna nia gani katika kupeleleza upoteaji wa silaha?, Kwanini msiwaachie watu wanaohusika?".

"Mimi si mwana siasa hivyo unayonieleza juu ya namna gani uhuru utakavyopatikana huko Afrika Kusini sina haja ya kujua. Lakini wageni wangu ni waandishi wa habari na kumetokea hapa mjini Dar es Salaam wizi wa silaha uliotingisha ulimwengu.Hivyo wakiwa waandishi lazima wapeleleze wapate kueleza ulimwengu mambo haya yametokeaje. Sidhani kama kitu hocho ni dhambi. Ni kitu cha kawaida". Nilimjibu taratibu nikijaribu kupima hali ndani ya chumba hiki.

"Imeonekana hawa waandishi wa habari wamekwenda zaidi ya kiwango cha upelelezi wa kigazeti, kiasi cha sisi kuamini kuwa si waandishi wa gazeti ila wapelelezi. Jioni hii kama huna habari rafiki yako Sherriff ameua vijana wangu zaidi ya kumi. Mtu mmoja, Willy, mtu mmoja?, siamini kabisa kuwa yeye ni mwandishi".

"Swali langu la pili nataka nujue yeye ni nani na sasa hivi yuko wapi?. Ukijibu maswali haya nitakuachia, usipojibu jua ya kwamba kesho huioni".

"Mimi ninavyojua ni kwamba yeye ni mwandishi wa habari, kama ni mpelelezi haya ni maneno yako, Kampuni yangu ni wakala, hivyo nilivyofanya mkataba na gazeti la Afrika na watu hawa walipokuja nilijuwa ni waandishi. Pili sijui aliko sasa hivi, tuliachana saa nyingi na tulipanga tuonane saa kumi na mbili New Afrika Hoteli lakini sikumkuta.

Baada ya kufikiri kidogo akasema, "La hasa, unajua".

"Sijui".

"Au unataka mpaka nifumbe macho".

"Hata kama ukifumba macho, sijui".

"Lucas na Moshi hebu mmwonyesheni huyu namna ya kujibu", alisema tena pole pole.

"Simama", alisema Lucas.

Sikusimama. Basi walinijia wote pale kitini kama faru, na mimi Willy tayari nilikuwa nawashwa kumwonyesha huyu mkubwa wa kuwa Willy hasukumwi ovyo.

Kama umeme nilisimama upesi na kukwepa ngumi ya Lucas na kwa sababu alikuwa ameitupa kwa nguvu sana alipepesuka mimi nikampiga teke kwenye mapumbu akalia kama nguruwe na wkati huo shoto langu lilimfikia Moshi singoni nae akapepesuka mpaka chini. Yule mtu mwingine aliyetuongoza toka mwenye gari alitoa bastola yake lakini mimi niliona hatua hiyo nikaruka upande mwingine wa chumba na risasi zikanikosa, na wakati huo mlango nao ulifunguliwa na mtu aliyevaa joho jekundu na kofia nyekundu akiwa na SMG mkononi akampiga risasi ya mgongo kabla hajanimaliza pale niliporukia, na yule mtu akafa pale pale. Huyu mtu wa SMG alimimina risasi kwa wale wengine waliokuwa wanajaribu kutoa silaha zao na kuwamaliza hapo hapo. Mimi katika harakati za kujiokoa niona yule mkubwa wao anaruka nyuma ya kiti, nikatoa bastola yangu, lakini nikawa nimechelewa, kwani nyuma ya kiti chake kulikuwa na mlango mdogo kimo cha urefu wa kochi. Hivyo alijitumbukiza.

"Anaondoka huyo Willy", nilisikia sauti nya Veronika akimimina risasi pale kwenye mlango lakini yule mtu alikuwa anajua nini anachofanya, hazikumpata akakimbia nje.

Mimi nilishangaa sana kumwona Veronika katika joho jekundu na kofia nyekundu na SMG mkononi amefika wakati kabisa uliohitajika kuniokoa.

"Oh Vero mkombozi wangu, umetokea kama malaika vile".

Alitupa bunduki akavua kofia na joho, haraka hara akaja akanirukia shingoni na kuanza kunibusu, kisha akaniachia.

"Tutoke hapa mpenzi, nitakueleza baadae", alininong'oneza.

Tulitoka ndani ya banda hilo na kusikia gari linaondoka.

"Mshenzi amepona", Veronika alisema.

"Iko siku yake", nilijibu.

Niliokota bunduki mbili pale nje. tukaenda kwenye gari letu tukaziweka ndani. Tukawasha gari na kuelekea mjini. Tulipofika Kilwa Road Veronika alianza kunisimulia,

ITAENDELEA...

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU