APANDA KWENYE NGUZO YA UMEME NA KUVUA NGUO

Shija Machiya (30), mkazi wa kitongoji cha Butulwa akiwa amepanda juu ya nguzo ya umeme mkubwa unaoelekea kwenye mgodi wa dhahabu Bulyanhulu wilayani Kahama kwa zaidi ya masaa matano kabla ya kuteremshwa na askari wa Jeshi la zimamoto na uokoaji.


MKAZI wa kijiji cha Butulwa Kata ya Old Shinyanga, aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Shija Machiya (30), hivi karibuni alizua kizaazaa kwa muda wa saa tano baada ya kupanda kwenye moja ya nguzo za umeme wa njia kubwa inayopitisha umeme kwenda kwenye mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, ulioko Kahama, mkoani hapa.

Hatua ya Bw. Machiya kupanda katika nguzo hiyo inayosafirisha umeme wa msongo wa KV 220 katika eneo la iwanda cha nyama  ilisababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ambao waliacha shughuli zao kwa muda wakihofia maisha yake.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama mzazi wa Bw. Machiya, Bi. Mondesta Madirisha, alisema kwa muda wa wiki moja mwanae alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kuchanganyikiwa akili kutokana na kile walichohisi kuwa ni malaria kali, ambapo waliamua kumpatia dawa za kienyeji na hali yake ilionesha kuwa ya kuridhisha.

Hata hivyo Bi. Madirisha alisema, jana mnamo saa 2.00 asubuhi hali ilibadilika ghafla na alianza kupiga kelele na kutoroka nyumbani kwao na kuanza kukimbia ovyo barabarani hali ilisababisha baadhi ya wanakijiji kuanza kumfuatilia.

“Leo asubuhi wakati natokea shamba, ghafla nilikutana naye akikimbia mbio, nilimsemesha na kumuomba asimame lakini aligoma kabisa na kukimbilia eneo ambalo kulikuwa na watu wakilima, niliwaomba msaada ili waweze kumkamata, lakini aliwazidi mbio na hapo hapo aliamua kupanda katika nguzo ya umeme na kwenda juu kabisa,” alisema Bi. Madirisha.

Alisema baada ya kuona hali hiyo waliamua kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya kitongoji na kijiji ambao walichukua hatua za kuualifu uongozi wa Shirika la umeme (TANESCO) waliofika eneo la tukio na kuwasiliana na Polisi pamoja kikosi cha zimamoto.

Waandishi wa habari walishuhudia harakati za kuteremshwa kwa kijana huyo juu ya nguzo hiyo ambapo mbinu zilitumika ili kumteremsha bila ya kuleta madhara yoyote huku akirajibu kuwachenga kwa kupanda juu zaidi ya nguzo na kuvua nguo zote mwilini na kubaki uchi wa mnyama.

Kwa upande wake Mhandisi wa njia kuu za umeme mkoani Shinyanga, Bw. Job Bidya, alisema kitendo cha Bw. Machiya kupanda katika nguzo hiyo kingeweza kuhatarisha uhai wake kutokana na njia hiyo kupitisha umeme mkubwa wa msongo wa KV. 220.

“Baada ya kupata taarifa na kufika eneo la tukio tulilazimika kuzima umeme haraka katika njia hiyo, ambapo juhudi za kumteremsha kijana huyo zilifanyika kwa ushirikiano wa kikosi cha zima moto na uokoaji manispaa ya Shinyanga, jeshi la polisi na wananchi na kufanikiwa kumteremsha bila ya madhara,” alieleza Bw. Bidya.

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba kijana huyo hivi sasa anashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kuweza kuelewa iwapo alifanya kitendo hicho kutokana na kuchanganyikiwa au kwa makusudi.Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru