CCM SHINYANGA WAKATAA MRADI WA LAMBO


Sehemu ya Lambo linalalamikiwa na wananchi wa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kuwa limetengenezwa chini ya kiwango na kudaiwa kutumia sh. milioni 35 zilizotolewa na TASAF chini ya mpango wa uhakika wa chakula kwa wakazi wa kijiji hicho. (Picha na Suleiman Abeid)


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Shinyanga mjini kimetishia kuiagiza serikali kuanza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wake wote ambao watabainika kuhujumu miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Shinyanga.

Hali hiyo inatokana na malalamiko ya wakazi wa kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga kulalamikia ujenzi wa lambo lililokuwa likijengwa kwa msaada wa fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa chini ya kiwango.

Wananchi hao walitoa malalamiko mbele ya katibu wa uenezi na itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shinyanga mjini, Bw. Charles Shigino, walisema pamoja na lambo hilo kugharimu sh. milioni 35, kazi iliyofanyika hailingani na kiwango hicho na limetengenezwa kama jaluba la mpunga.

Akizungumza kwenye eneo la mradi huo, Bw. Shigino na watendaji wa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, akiwemo mratibu wa TASAF, Bi. Theonestina Bairu, walisema CCM haitokaa kimya itakapobaini kuwepo kwa hujuma dhidi ya miradi ya wananchi.

Alisema CCM Shinyanga mjini imesikitishwa na jinsi ya mradi huo ulivyotekelezwa ambao lengo lake kubwa ilikuwa ni kuwasaidia wafugaji wa kata hiyo ya Ndembezi kuwa eneo la kunyweshea mifugo na wanakijiji kuendesha shughuli za kilimo cha bustani za mbogamboga.

Amesema pamoja na fedha hizo kulenga uchimbaji wa lambo la kusaidia wakazi wa kijiji cha Ndembezi walengwa walioshiriki hawakulipwa fedha zao.

“Kwa kweli kwa hali hii CCM haitokaa kimya, lazima tuhakikishe wahusika wanachukuliwa hatua za kinidhamu, hili siyo lambo kabisa, ni sawa na jaluba la mpunga, ukilinganisha na kiasi cha fedha kilichotolewa hakilingani na kazi iliyofanyika, lazima tuhakikishe utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi unakwenda kama ilivyoahidiwa,”

“Tutawaelekeza hawa watu wa serikali ili waanze kuwachukulia hatua watendaji wao wanaofanya mchezo na udanganyifu katika utekekezaji wa miradi ya wananchi, hapa pamefanyika mchezo mchafu, hata kama fedha hiyo ililenga kuwasaidia wananchi kuweza kupata fedha za kununulia chakula, lakini ilibidi wafanye kazi kwanza ndipo walipwe” alisema Bw. Shigino.

Alisema hata kama ni suala la kuwasaidia wanachi waweze kupata uhakika wa chakula kama lengo la mradi lilivyokuwa kwa hali halisi ilivyo ni bora wananchi hao wangepewa fedha hizo mikononi badala ya kuwafanyisha kazi ili iwe kama ‘danganya toto’ ambapo lambo lenyewe haliwezi kuhifadhi maji hata kidogo.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Ndembezi Bi. Christina Jagadi alisema yeye ni kati ya wanakijiji waliofanya kazi katika lambo hilo lakini jambo la kusikitisha yeye pamoja na baadh ya wanakijiji wenzake mpaka sasa hawajalipwa chochote baada ya kuelezwa kwamba fedha zimemalizika.

“Kama kweli suala lilikuwa ni kutusaidia tupate fedha za kununulia chakula, mbona mimi mpaka leo nadai kiasi cha shilingi 25,000 kama malipo yangu baada ya kufanya kazi, kila tunapouliza tunaelezwa fedha ilimalizika, sasa mradi huu uliletwa kutusaidia au kutuumiza tu sisi wananchi?” alihoji Bi. Jagadi.

Hata hivyo kwa upande wake mratibu wa TASAF Manispaa ya Shinyanga, Bi. Theonestina Bairu alisema fedha yote iliyotolewa katika utekelezaji wa mradi huo ilitumika kama ilivyopangwa na kwamba suala la lambo hilo kuwa chini ya kiwango linatokana na fedha kumalizika kabla ya kukamilika kwa mradi wenyewe.

“Si kweli kwamba kuna watu wanatudai, kila mtu alilipwa kwa kadri alivyofanya kazi, na moja ya sababu ya kutokamilika kwa mradi huu ni kumalizika kwa fedha zilizokuwa zimetengwa ambazo asilimia kubwa ilikwenda kwa walengwa wenyewe, hivyo hakuna mtu aliyekosa fedha zake,” alisema Bi. Bairu.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru