MEATU WASHNIKIZA UKOMO WA RAIS

WAKAZI wa Mwanhuzi, Wilayani Meatu, mkoa Simiyu wamependekeza kwa Kamati ya Katiba mpya ya Tanzania kuzingatia ukoma kwa madaraka ya Rais anapokuwa madarakani ili kuepusha wanaomaliza muda wao kuvunja katiba ya nchi.

Wakazi hao walisema kwa mujibu wa katiba ya sasa marais wote waliopita hapa nchini wamekuwa wakifunja katiba ya nchi kutokana na kuendelea na urais wao hata pale muda wao unapokuwa umekoma rasmi ambapo wameshauri katiba ijayo iweke wazi ibara hiyo na iwe na nguvu za kisheria.

Wakichangia hoja katika mdahalo ulioandaliwa na Azaki ya MENGONET wilayani Meatu wananchi hao walisema kwa mujibu wa katiba ya sasa muda wa madaraka ya Rais aliyeko madarakani unakoma pale bunge linapovunjwa.

Walisema Ibara ya 38 kifungu kidogo cha (2) (a) ndani ya katiba ya sasa inatamka wazi kwamba bunge la Jamhuri ya Muungano linapovunjwa rasmi na kiti cha urais hupaswa kuwa wazi utaratibu ambao haufuatwi wala kuzingatia kutokana na Rais kuendelea na madaraka yake hata baada ya bunge kuvunjwa.

Kifungu hicho kinaeleza; “Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya katiba hii, kiti cha Rais kitakuwa wazi, na uchaguzi wa Rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa katiba hii, kadri itakavyokuwa kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:  (a) Baada ya bunge kuvunjwa.”

Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, Bw. Joshua Kalando alisema ni vizuri sasa ili kuwezesha demokrasia kuchukua mkondo wake ni vizuri katiba ijayo ikaeleza baada ya bunge kuvunjwa na kukoma kwa madaraka ya Rais aliyeko madarakani nchi itakuwa  chini ya mamlaka ya mtu au chombo kipi.

Bw. Kalando alisema uzoefu unaonesha marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekuwa wakiendelea kuhesabika kama Rais wa nchi hata baada ya kuvunjwa rasmi kwa bunge la Jamhuri ya Muungano hali ambayo ni kuvunja katiba ya nchi.

“Kwa kweli Rais kuendelea na madaraka yake hata kipindi cha kampeni anakuwa anavunja katiba ya nchi, ni vyema katiba mpya ijayo iweke mkazo  kwamba baada ya kuvunjwa kwa bunge na madaraka ya Rais aliyeko yakome papo hapo,”

“Anapoendelea kuhesabika kama Rais, katika kipindi cha kampeni tumeona wanaendelea kupata upendeleo na ulinzi mkubwa kama Rais wa nchi tofauti na wagombea wengine kutoka vyama vya siasa, sasa lazima tuweke utaratibu utakaowatendea haki wagombea wote bila kuwabagua, katiba ijayo ieleze,”  alisema Bw. Kalando.

Kwa upande mwingine washiriki wa mdahalo huo ambao pia ulijadili umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya wananchi na madiwani na wabunge walipendekeza katiba ijayo iweke ibara itakayoruhusu kuadhibiwa kwa watu wanaokataa kuwatambua viongozi wanaochaguliwa kihalali na wananchi.

Bw. Alex Emmanuel alisema ili kuondoa malumbano yasiyomalizika ya wana siasa, katiba ijayo iweke ibara itakayoruhusu watu wote wanaokataa kuwatambua madiwani na wabunge waliochaguliwa kihalali, wakatangazwa na wakala viapo, basi washitakiwe na wafungwe gerezani.

“Baadhi ya kata na majimbo hivi sasa ambayo kwa madiwani wake na wabunge wanatokana na vyama vya upinzani kumekuwepo na matatizo makubwa sana, wanasiasa ambao wagombea wao walishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 wamegoma kabisa kuwatambua watu walioshinda, sasa hii kimaendeleo inakuwa tatizo,” alisema Bw. Emmanuel.

Wananchi hao walisema iwapo patakuwepo na sheria hiyo, ni wazi hapatakuwepo na vikwazo vya maendeleo katika kata na majimbo ambayo madiwani na wabunge wake hawatokani na vyama vya siasa vilivyopo madarakani.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru