NJAMA

SEHEMU YA SITA

CHIMALAMO

III

Ilikuwa saa tano tulipofika New Afrika baada ya kumchukua Sherriff kutoka kwa daktari akiwa anajisikia vizuri kabisa. Veronika ndiye nilikuwa nimewahi kumchukua kabla ya Sherriff.

"Kavae upesi, twende zetu Komredi", nilimwambia Sherriff aliyetaka.

"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka haraka.

Ilikuwa saa tano na dakika kumi na tano tulipoondoka kuelekea Ofisi za PLF. Njiani tulimweleza yote yaliyokuwa yametupata jioni ile tukibakiza tu ile habari ya kwenda kwetu pamoja kulala nyumbani kwangu.

Ofisi za PLF zilikuwa mtaa wa Makunganya karibu na Achells Limited hivyo haikutuchukua muda kufika pale kutokea New Afrika.Tulitokea barabara ya Azikiwe, tukaingia mtaa wa Independence pale kwenye mzunguko wa sanamu ya Askari halafu tukakata kulia pale kwenye taa za usalama barabarani za mtaa wa Independence na Postway, na kuingia Postway. Tukatelemka kidogo mpaka kwenye mtaa wa makunganya moja kwa moja kwenye ofisi za PLF. Tuliegesha gari pale pale mbele ya ofisi tukatelemka na kuingia mapokezi. tulimkuta kijana mmoja akiwa mapokezi.

"Habari zako ndugu", nilimsalimu.

"Salama, sijui niwasaidie nini?".

"Tunaomba kumwona ndugu Cecil Chimalamo".

"Mna miadi naye?'.

"Hapana, lakini ukimweleza kuwa kuna waandishi wa habari toka gazeti la Afrika natumaini anaweza kutuona".

"Subirini hapa kwenye viti".

Tulikaa kwenye makochi mazuri sana. Cecil Chimalamo nilikuwa ninamfahamu kwa sura na vile vile mambo yake kwani nilikuwa nimeshasoma faili lake mara nyingi ofisini. Kwa kifupi wanasiasa wengi walimpenda kwa sababu ya imani zake za kisiasa ambazo mara nyingi zilikuwa na msimamo. Alitambulikana kama kiongozi mmojawapo mashuhuri mpinga ubaguzi na mpenda serikali ya wengi katika Afrika ya Kusini, makaburu walimchukia sana.

Punde yule kijana alirudi akayakatisha mawazo yangu juu ya Chimalamo.

"Mnaweza kumwona chumba namba tatu".

"Asante', nilishukuru kwa niaba ya wenzangu.

Tulikwenda moja kwa moja mpaka chumba namba tatu tukabisha hodi.

"Karibu".

Nilifungua mlango tukaingia ndani tukajikuta katika ofisi.

"Karibuni", alitukaribisha huku akisimama.

"Asante".

"Nyinyi ndio mmetoka kwenye ofisi za gazeti la Afrika".

"Ndio".

"Twendeni mzee anawasubiri".

Alifungua mlango, tukaingia ndani na kumkuta ndugu Chimalamo amekaa anavuta sigara. Alipotuona alisimama.

"Karibuni, ketini chini".

Kabla hatujakaa nilichukua mwanya huu kujijulisha mimi pamoja na wenzangu kwake.

"Mimi naitwa Willy Gamba na ni Meneja Mkuu wa Kampuni iitwayo Afrika Internation Agencies (AIA), na hawa ni waandishi wa gazeti la Afrika. Huyu anaitwa Veronika Amadu na huyu ni Ahmed Sherriff. Wote ni wananchi wa Sierra Leone", tulishikana mikono na kusabahiana halafu tukaketi chini.

"Imekuwaje wewe uwe pamoja nao?", aliuliza.

"Kampuni yangu ndiyo wakala wa gazeti la Afrika hapa Tanzania kwa hivyo haja zao zote naziwakilisha mimi.

"Aisii, nafikiri tumeshaonana mara nyingi. Wewe si mgeni kabisa kwangu ", aliniambia na kuniangalia kwa macho ya kudadisi.

"Bila shaka tumeonana mara nyingi hasa katika tafrija za vyama hivi ingawaje hatujawahi kujulishwa moja kwa moja".

"Ehe gazeti la Afrika linataka nini?", Nilishangaa sana maana hata hakuuliza vitambulisho. Mara moja nikajua mtu huyu aliweza kuwasoma watu na kujua ni watu wa namna gani. Alikuwa mtu mwenye busara nami nikaondokea kumpenda.

"Sisi tumekuja hapa mjini baada ya kupata habari za tukio lililokikabiri chama chako na serikali ya Tanzania kwa ujumla. Jumuia ya Ulimwengu mpaka sasa imegawanyika katika pande mbili. Moja inalaumu Serikali ya Tanzania kuwa ndiyo inahusika na wizi wa silaha hizi ambazo ni za kisasa kabisa, upande wa pili unaamini kuwa hizi ni njama za mabeberu zinazopiga vita harakati za ukombozi wa Afrika Kusini. Kwa hiyo gazeti la Afrika likiwa kila siku linafuatilia kwa makini harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kuweza kusaidia inapowezekana, linahitaji hasa ukweli wa tukio hili. Hii ndio sababu tuko hapa. Tumeshawaona wakuu wengine katika OAU na katika Serikali ya Tanzania na tumeona hatuwezi kufika mbali bila kujua mawazo yako wewe ambaye ndiye hasa uliyehusika na mali iliyopotea", Sherriff alieleza kwa kinagaubaga.

"Kwa hiyo mnataka kujua mimi niko upande gani katika mawazo hayo mawili ya Jumuia ya Ulimwengu?".

"Hilo ndilo swali letu la kwanza", Sherriff alijibu.

"Mimi nawaunga mkono wanaoamini kuwa hizi ni njama za mabeberu. Wale wanaosema Tanzania inahusika wanajaribu kuongeza petrol kwenye moto huku wakijua kuwa Tanzania ni nchi pekee katika Afrika ambayo haiwezi kufanya jambo hili. Nakuhakikishia kwamba tangu nikae hapa nina miaka sita na sijaona Serikali ya kimapinduzi kama hii. La hasha, Tanzania haiwezi kabisa kufanya jambo hilo ila hizo ni mbinu za mabeberu za kutugonganisha sisi na wenyeji wetu ili mambo yaharibike kabisa. Mimi sitakubali washenzi hao watugonganishe. nafikiri umenielewa.

"Nimekuelewa sana. Sasa unafikiri silaha hizi zimepotea poteaje?. Hapa nataka mawazo yako binafsi".

"Hata mimi sijui. Ni njama ya hali ya juu iliyofanyika, hivyo nimeachia shauri hilo Serikali ya Tanzania ambayo imeniahidi itafanya juu chini kufichua njama hizi".

"Na isipowezekana?", Veronika aliuliza.

"Tutajua la kufanya wakati huo.

"Ilibainikaje kama wewe umekwenda Urusi kutafuta silaha za kisasa na hali naamini jambo hili lilifanywa kwa siri?", Sherriff aliuliza.

"Siku hizi hakuna kitu cha siri. Nafikiri hata kabla sijaondoka hapa Dar es Salaam kwenda Moscow ilikuwa imeshajulikana nini nafuata. Ulimwengu huu wa teknolojia hakuna kitu cha siri. Hata mkutano uliofanyika huko camp Davis Marekani, kati ya Marais wa Israel, Misri na Marekani na kuweka hali ya uficho wa hali ya juu, bado watu walijua kabla mazungumzo hayo ya kisiri ya hali ya pekee hayajatangazwa rasmi. ili kujibu swali lako hata sisi hatukutegemea tutajulikana.

"Watu wanafikiri kuwa, silaha hizo zimefanyiwa njama za kuibiwa kwa sababu ni silaha za kisasa kabisa na za hali ya juu. Ndio sababu watu wanasema Tanzania isingeweza kuziona zinakwenda hivi hivi. Sasa swali langu ni kwamba kwa nini uliamua kuomba silaha za kisasa za jinsi hii wakati vita havijafikia hali ya juu sana kuhitaji silaha za namna hiyo.

"Ahaa, swali lako zuri sana. Ili mwelewe kwa nini nilichukua hatua hiyo ni lazima niwape maelezo kamili, juu ya hali ya silaha alizonazo adui tunayepigana naye", alinyamaza kidogo akaegemeza mikono yake mezani.

"Maana mtu hawezi kupigana kwa rungu dhidi ya mtu mwenye bunduki. Kwa hiyo hamtajali naona nikiwaeleza kwa kirefu jinsi wapinzani wetu walivyojidhatiti kijeshi na ndipo tu mnaweza kuona kwa nini niliagiza silaha za kisasa".

"Sisi tutafurahi sana kupata fursa ya kusikia maelezo hayo", nilijibu kwa niaba ya wenzangu.

"Katika miaka 15 iliyopita", alieleza Chimalamo. "Makampuni ya kimataifa yamezidisha rasilimali zao ili kuimalisha uchumi wa Afrika Kusini. Makampuni makubwa ya Marekani na Ujerumani Magharibi yamepanua rasilimali zao katika sehemu muhimu za utawala wa Makaburu. Na makampuni haya yana ushirikiano mzuri sana na utawala wa Makaburu.

"Miaka michache iliyopita mabenki ya kigeni yameikopesha afrika Kusini mamilioni ya fedha ili kuwezesha kukabili migogoro ya kiuchumi iliyosababishwa na kulegalega kwa uchumi wa nchi za magharibi na kuendelea kukua kwa mapambano ya wazalendo wanaokandamizwa na utawala wa Makaburu.

"Mabenki ya kigeni yametoa mtaji mkubwa kwa utawala wa Makaburu kwa mahitaji ya fedha kwa ajili ya mambo ya kijeshi na kiuchumi, katika miaka michache iliyopita deni la kigeni la Afrika Kusini limeongezeka haraka kufidia gharama za mafuta yake, kupanua ununuzi wa silaha na gharama za mipango ya kuuwezesha utawala huo dhalimu ujitegemee. Kwa taarifa yenu mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1976 utawala wa Makaburu ulikuwa na deni lipatalo Shs.72 bilion, lakini idadi inaweza kuwa kubwa kuzidi hapo maana mikopo kwa Afrika Kusini ni siri. Sijui mnanielewa?".

"Tunakuelewa sana", tulijibu kwa pamoja, huku Veronika akiwa anaandika maelezo hayo.

"Kuna ukweli unaoonysha jinsi biashara ya makampuni ya kigeni na rasilimali zao zilivyosaidia kuimarisha viwanda vya kijeshi vya Afrika Kusini hata kuuwezesha utawala wa Makaburu kuwa na kiburi na kupuuza maoni ya dunia na kuendelea kudumisha udhalimu wake na kuwakandamiza wananchi walio wengi wa Afrika Kusini.

Makampuni ya kigeni yamejihusisha moja kwa moja katika kuimarisha kijeshi Afrika Kusini. Kumbukumbu za kampuni moja inayoshughulika na utengenezaji wa silaha katika nchi zinazoendelea zinaonyesha kuwa makampuni ya kigeni yametoa liseni kwa makampuni ya Afrika Kusini kutengeneza zana za kijeshi za aina mbali mbali, pamoja na ndege za kijeshi, mabomu, risasi na bunduki. Vile vile kuna makampuni yanayotengeneza vipuri na vifaa vingine kwa madhumuni ya kijeshi. Shirika la Baruti na madawa la Afrika Kusini 'AECI' linatajwa kuwa linamiliki viwanda vitatu vinavyotengeneza silaha na linashirikiana na kampuni moja ya viwanda vya madawa ya Uingereza. "Imperial Chemical Industries", Kampuni hiyo ya Uingereza., imetoa utaalamu na vifaa vinavyotumiwa na Shirika la AECI la Afrika Kusini. Na wakati huo huo kampuni ya Darman Long ya Afrika Kusini iliyounda manowari moja yenye uzito wa tani 220 inashirikiana na Shirika la vyuma linalomilikiwa na serikali ya Uingereza katika shughuli za utengenezaji silaha".

Alinyamaza kidogo, akachukua sigara akaiwasha kisha akavuta mara tatu hivi halafu akaendelea.

"Kutokana na misaada hii toka nchi za Magharibi, Afrika Kusini imejiimarisha sana kijeshi. Utaona kuwa miaka ya sitini, matumizi ya kijeshi ya Afrika Kusini yameongezeka mara sita kutoka Shg 520 milioni hadi mwaka 1977/78 matumizi ya kijeshi yalikuwa yameongezeka tena na kufikia kiasi cha Shg 16,450/- milioni kwa mwaka. Nimetoa maelezo hayo pamoja na tarakimu ili kuwaonyesha kimsingi kuwa Afrika Kusini ina uwezo kifedha kutengeneza au kununua silaha za kisasa kabisa.

Alitua tena ili kuvuta sigara yake kisha akaendelea huku sisi tukimsikiliza kwa makini kama wanafunzi wanavyomsikiliza mwalimu katika somo wanalolipenda.

"Vijana lazima mtu ujue nguvu za adui yako kabla hujamkabili, la sivyo, utakuwa unafanya mapambano yasiyo ya kimsingi. Ili kuwapa ukweli hasa uliopo, jeshi la Afrika Kusini limekuwa likitumia zana za kisasa zilizoko duniani tangu mwaka 1970. Matumizi ya kijeshi kwa ajili ya kununulia silaha na vifaa maalumu vya kisasa vya kijeshi badala ya vya zamani yaliongezeka kwa asilimia 32 mwaka 1971 kufikia asilimia 53 mwaka 1973. Kati ya mwaka 1970 na 1979 Shg 2,240 milioni zilitumika kwa mambo ya ndege za kijeshi, shs 1,000/- milioni kwa ajili ya kununua radio, mitambo ya kutazama ndege angani (radar) na vifaa vingine vya kisasa. Kama nilivyokwisha kuwaeleza hapo awali, wakati huo huo utawala wa Afrika Kusini umekuwa ukichukua hatua kuimarisha utengenezaji wa zana humo humo nchini kadiri vipuli na vifaa vya mahitaji yake ya kijeshi yanavyozidi kuongenzeka.

"Kwa mjibu wa toleo moja la kijeshi la Marekani, tangu tangu mapema mwaka 1971 makaburu walikuwa wanaweza kutengeneza mabumu na baruti kiasi cha kujitosheleza na wanaweza kuuza nchi za nje. Juu ya risasi Afrika Kusini inatengeneza aina 100 za risasi. Kwa bunduki inajitosheleza kabisa. Kwa silaha za jeshi la nchi kavu, ama imejitosheleza ama imefikia hatua za utoaji, na itajitosheleza hivi karibuni kwa zana za jeshi la maji na sasa inatoa zana zote za moto inazohitaji. Bunduki za kisasa kama vile Rifle na Machine-gun vile vile zinatengenezwa. Hivi utengenezaji wa mizinga unaanza, na kuna huduma ya kuweza kutengeneza karibu kila aina ya magari ya kijeshi. Radio za ndege, vifaa vya kutegulia mabomu na vifaa vingine vya kisasa vya kijeshi vinabuniwa na kutengenezwa huko huko Afrika Kusini.

Alinyamaza na kuwasha sigara nyingine na kwa nguvu zile zile akaendelea kueleza.

"Hivi karibuni ilidokezwa kuwa Afrika Kusini inaunda aina fulani za bunduki, mabomu ya kudondoshwa na ndege yenye uzito wa kufikia ratili 1,000 kila moja na inaendelea na utengenezaji wa makombora ya kuangusha ndege. Mabomu hayo inasemekana yalifanyiwa majaribio mwezi Septemba 1977 kwa kutumia ndege za aina ya 'Mirage'. ndege hizi za mirage zilianza kuundwa huko Afrika Kusini chini ya liseni ya kampuni ya ufaransa ya Sessoult mnamo mwaka 1974. Kama hatua ya mwanzo. Afrika Kusini ilinunua vipande 50 vya ndege za aina hiyo na kuunda yenyewe ndege za mirage".

"Wakati huo vile vile ilikuwa tayari imeanza kuunda ndege za kijeshi aina ya Impala za muundo wa Italia-Armachi MB-326, magari ya kijeshi aina nyingi ya silaha ndogo ndogo pamoja na bunduki za aina ya rifle muundo wa Ubelgiji. Na kwa mjibu wa Waziri wa Uliniz wa Makaburu. Afrika Kusini ilitegemewa ianze kutengeneza vifaru vyake. Vile vile Afrika Kusini inasemekana imeanza kuendeleza utengenezaji wa mizinga ya kutungulia ndege aina ya CAC-TUS, ikisaidiwa na kampuni moja ya Ufaransa".

Alipofika hapa aliinua simu na kumwamru mwandishi wake mahsusi atuletee vinywaji baridi na sambusa kisha akaendelea.

"Naona nitawachosha lakini kwa sababu nyie wenyewe mmeuliza mimi nitawapa hali halisi ilivyo na mkiwa kama waandishi wa habari ni vizuri kujua hali ya kijeshi ya huyu adui wetu mkubwa katika Afrika. Kwa kutumia gazeti lenu mnaweza kujulisha jumuia ya ulimwengu ukweli wa nguvu za adui yetu huyu zilivyo, hivyo msitahimili karibu nitamaliza.

Mwandishi wake alileta vinywaji barudi na sambusa.

"Habari unazotueleza ni za kusisimua mno kwani kwetu sisi wengine ni habari mpya, hivyo hata ukiendelea mpaka usiku tutakuwa tayari kabisa kukusikiliza", nilimhakikishia.

"Kama hivyo basi nitaendelea. Magari ni muhimu sana katika mambo ya kijeshi. Kuna makampuni kadha wa kadha ya kigeni ambayo yamekuwa yakiisaidia Afrika Kusini kijeshi katika mambo ya magari. Makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya Marekani ya General MOtors (GM), kampuni kubwa duniani inayotoa magari kwa wingi baada ya Vita Kuu ya kwanza. Hivi sasa ina mtambo wa kuunganisha na kuunda magari huko Port Elizabeth, na mtambo wa kutengeneza injini za magari nje kidogo ya mji huo. 

"Kampuni nyingine ya magari ni ile ya Ujerumani inayotengeneza magari ya aina ya 'Benz'. Magari ya kijeshi ya aina hii ndiyo yanatumiwa sana na majeshi ya Afrika Kusini. Msemaji mmoja wa kampuni ya magari ya Benz na BMW, alijigamba hivi karibuni kwamba kampuni yake inatengeneza magari hayo Ujerumani kwenyewe na Afrika Kusini na inakusudia kutumia Afrika Kusini kama kituo cha kuuzia magari hayo kwa nchi za nje zilizoko Kusini kwa Ikweta. Hii inaonyesha dhahiri kuwa Afrika Kusini inayo magari haya zaidi ya mahitaji yake ya kijeshi".

Alinyamaza tena akachukua glasi yake iliyojaa Coca-cola akainywa kwa mara moja kisha akainua macho yake na sura yake ikageuka kuwa nzito kisha akaendelea.

"Na mwisho napenda kuwaeleza jambo la mwisho lakini muhimu si kwa sisi wapigania uhuru tu bali kwa Afrika nzima. Katika mwaka 1974 Shirika la Nyuklia la Marekani lililoko Oak Ridge lilipeleka kilo 45 za madini ya 'Uranium' kwa mtambo wa utafiti wa nyuklia uliopo Palandaba huko Afrika Kusini baada ya Tume ya Nyuklia, chombo pekee cha Marekani kinachotoa liseni za usafirishaji nje vifaa vya nyuklia kukubaliana na Afrika Kusini kwamba haitaruhusu madini hayo yapelekwe pengine au kutumiwa vinginevyo. Marekani vile vile mwaka 1975 na 1976 iliipa Afrika Kusini madini hayo yanayotumiwa kutengeneza zana za nyuklia na kuahidi kuuza zaidi madini hayo kwa mtambo wa pamoja na nguvu za nyuklia wa Marekani na Ufarasa unaotazamiwa kujengwa Afrika Kusini mwaka 1984. Kwa jumla Marekani imeiuzia au imeahidi kuiuzia Afrika Kusini ratili 300 za madini hayo kwa ajili ya mtambo wa utafiti wa nyuklia uliopo Palandaba. Kwa taarifa yenu ratili 300 za Uranium zinawza kutengeneza mabomu 15 ya Atomiki".

Kila mmoja alipiga mluzi wa mshangao.

"Nafikiri ndugu Willy nimejibu swali lako kwa kirefu, kwa hiyo utaona sisi wapigania uhuru hatuna budi kuomba silaha za kisasa zinazoweza kukabili nguvu hizi kubwa ya kijeshi za adui yetu. Kwa hiyo tukio hili lililotokea linaonyesha dhahiri kuwa hawa makaburu wameona hatari inayowajia hivyo kuiba silaha hizi ni mbinu moja ya kujihami. Na mimi nimeapa sitarudi nyuma nitaondoka tena karibuni kwenda kutafuta silaha za kisasa na kali toka nchi rafiki ambazo naamini zitaamini kuwa tukio hili ni njama za mabeberu. Hivyo njama zao zinazidisha tu moto katika wapigania uhuru na ndugu zao wanaowasaidia. Huu si mwisho wa mapambano. Ila ni matayarisho tu ya mapambano - historia itanihukumu. Mna swali zaidi?".

Tuliangalia na kukawa hakuna mtu mwenye swali kwani risala yake ilituchoma mioyoni kama miali ya moto wa umeme.

"Asante, tumetosheka", nilijibu kwa niaba ya wenzangu.

"Oke mnakaribishwa tena siku yoyote kwani katika kuzungumza nanyi ndipo tunapoweza kujua hali halisi ya Kusini mwa Afrika. Asante sana vijana wa Afrika kuja kunitembelea". Alitupa mkono wa kuagana.

"Asante sana", tulijibu na kuondoka ofisini mwake kimya kimya.

Tulipofika kwenye gari langu niliona ni saa saba u-nusu, kweli tulikuwa tumekaa sana ndani. Tuliingia ndani ya gari.

"Sasa twende tukaonane na Ray Sikazwe. Rais wa Chama za SANP

ITAENDELEA 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru