NJAMA

SURA YA SABA

BINTI TANZANIA

"Lo, hiyo ilkuwa alimanusura", veronika alisema huku jasho likimtoka na akihema.

"Nakuambia", Sherriff naye huku akihema.

"Eddy, moja kwa moja nyumbani kwangu, akili yangu imevurugika", nilimwambia Eddy aliyekuwa akiendesha kwa kasi sana.

"Huyu Eddy ni nani na katokea wapi?, maana bila yeye sasa hivi sote tungekuwa maiti", aliuliza Sherriff.

"Katika kazi hizi Komred Sherriff lazima uwe na plani bila plani huenda mimi ningekuwa nimeuawa siku nyingi. Huyu kijana ni mfanyakazi mwenzetu, na toka asubuhi yuko pamoja nasi lakini kazi yake ilikuwa ni kutulinda sisi. Na kwa jumla ndivyo hivyo tunavyofanya kazi".

Eddy alisimamisha gari mbele ya nyumba yangu. Tulitelemka ndani ya gari, nikafungua mlango tukaingia sebuleni wote na kuketi. Nilikwenda katika barafu na kutoa chupa ya whiski na chupa za soda kali. Nilitenga glasi, wote wanne tukaanza kunywa. Nilipoangalia saa ilikuwa saa tisa kasoro robo.

"Eddy nafikiri hatuna muda wa kupika hapa nyumbani, hivyo nenda Palm Beach Hoteli wakakufungie chakula cha watu wanne", nilimwambia Eddy".

"Sawa".

Eddy aliondoka kwenda kutafuta chakula.

"Willy, watu hawa wamepania sana", Sherriff alisema kwa sauti nzito.

"Mimi nilijua watapania, ndio sababu nikaweka tahadhari yote hii. Ngoja Eddy arudi atueleze ilikuwaje mpaka wakaweza kutufuata mpaka pale walipotushambulia. Ni bahati nzuri sana kwamba wote mna mafunzo ya kijeshi hivi mlitii amri za Eddy bila hata kufikiri. Jambo hili limenifurahisha sana maana kama mtu angesita, sasa hivi tungekuwa tunamuombolezea".

"Naona wote tumejenga silika ya hali ya juu kwa wakati wa namna hii", Sherriff alijibu.

"Tukimsubiri Eddy, sijui mmewaonaje hawa Maraisi wa vyama hivi vile vile", Veronika aliuliza.

"Mimi moja kwa moja nimempenda Chimalamo maana ni mtu aliye wazi. Nafikiri ni kiongozi mwenye busara. Kutokana na maelezo aliyotupa nafikiri anajua anafanya nini, na mtu kama huyu anaweza kabisa kuendesha harakati za ukombozi dhidi ya Makaburu maana anawajua nje na ndani. Ukikumbuka mazungumzo yetu siku ile huko Freetown juu ya Afrika Kusini sasa ukiongeza haya aliyotupasha ndugu Chimalamo hata wewe unazidi kupata mwanga mkubwa juu ya Afrika Kusini. Kwa ujumla nafikiri Chimalamo ni kiongozi mzuri na halisi. Juu ya Sikazwe nina dukuduku nae moyoni, maana sikumwelewa sawasawa sababu si mtu wazi. Hata nidhamu ya ofisi yake ilivyo kabla hujaonana naye, inaonyesha kasoro fulani. Nafikiri bila Willy kuwa mtu anayejua mbinu nyingi tusingemwona maana mbinu aliyotumia mimi mwenyewe mkufu. Halafu kuna kitu fulani ndani ya Ndugu Sikazwe ambacho sijui ni nini lakini kinanidundadunda sijui wenzangu mmemuonaje?", Sherriff alieleza.

"Nafikiri mawazo yako na ya kwangu hayako mbali. Nakubaliana na wewe kuwa Ndugu Chimalamo ni kiongozi mzuri. Na vile vile kuhusu Sikazwe hata mimi kuna kitu fulani ambacho sikukielewa ni nini kilicho ndani yake, lakini huenda nitakijua nikipata muda mrefu kufikiri. Lakini huenda ni mtu wa tabia ya namna hiyo, na kwa namna yake hiyo anaweza kuwa ni kiongozi mzuri zaidi kuliko hata Chimalamo. Huenda kila kitu kilicho ndani yake ni uongozi bora", nilieleza.

"Mimi sina la kuongeza, naona mawazo yetu yameoana", Veronika alijibu.

"Kusema kweli jamani sijastuka kama leo, kweli tumeponea chupu chupu, asante sana Willy kwa kuweka tahadhari".

"Bila asante Vero, maana ni kazi yangu kuhakikisha usalama wenu na wangu, hivyo uwe na amani kuwa nitafanya kila jitihada kuhakikisha usalama wetu, kama nikishindwa itakuwa nje tu ya uwezo wangu".

"Naomba sigara", Sherriff aliniambia.

"Hapa mimi nina aina ya sigara iitwayo Tropicana, sijui kama itakufaa".

"Wewe nipe tu, sigara zangu ziko hotelini. Baada ya kashikashi nahitaji sigara kama kufa".

"Nilitoa pakiti ya Tropicana nikaiweka mezani tukaanza kuivuta.

"Lo, mbona sigara safi kabisa, ni sawa sawa tu na 555, zinatengenezwa wapi?", Sherriff aliuliza.

"Hapa hapa nchini kwetu".

"Lo, mmeendelea sana, mnaziuza na nje?", aliuliza Veronika ambaye naye alichukua moja akavuta ingawaje hakuwa mvutaji sana.

"Sijui maana wameanza kuzitengeneza hivi karibuni, lakini naamini watafanya hivyo".

Mara Eddy akawa amerudi tukapata chakula ambacho tulikishambulia vizuri sana maana njaa zilituuma vibaya.

ITAENDELEA.....

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU