NJAMA

SURA YA SABA

BINTI TANZANIA

III

Ilikuwa yapata saa kumi na mbili wakati dereva wa teksi aliponishusha hatua chache kabla ya kufika kwenye mzunguko wa Mtaa wa Jamhuri na Zanaki.

"Hapo hapo pananitosha", nilimweleza huku nikimpa shilingi ishirini kisha nikatelemka. Niliangalia kwenye maegesho ya mtaa huu wa Jamhuri nikaiona gari ya Zabibu. Ilikuwa gari ya rangi ya kijani ambayo haikuiva sana, na ilikuwa ni aina ya Ford Mustang muundo wa kisasa. Kama umeshaiona Ford Mustang zilizoundwa vizuri basi hii ilikuwa mojawapo. Hata mimi niliipenda kwa umbo lake maana ilikuwa na milango miwili. Yaani 'Ford Mustang Sports Car', kama wanavyoiita wenyewe walioitengeneza.

Kule kuona gari hii kulinihakikishia kuwa Zabibu alikuwepo nyumbani, niliangalia jengo, nikaangaza huku na huku kuona kama kuna mtu ananifuata, nikaona hakuna. Kila mtu alionekana kuwa na hamsini zake. Basi mimi Willy nilijipenyeza kwenye lango linaloelekea kwenye ngazi za jengo hili. Nilipofikia ngazi nilianza kupanda taratibu kama mtu anayejua anapokwenda. Nilipanda mpaka orofa ya tatu, na nyumba iliyokuwa inatazamana na ngazi hizi ilikuwa namba 1a na nikajua 7a itakuwa mkono wa kulia hivyo nikafuatia taratibu.

Kwa sababu giza lilikuwa linaingia nyumba zingine zilikuwa zimewasha taa na zingine zikiwa giza kuonyesha wenye nyumba walikuwa bado hawajafika. Nyumba namba 5a na 6a zilikuwa giza ila 7a ilikuwa inawaka taa sebuleni. Nilitembea taratibu bila kupiga kelele mpaka kwenye mwisho wa namba 6a, niliposikia sauti ya msichana inapiga kelele ndani ya namba 7a. Harafu nikasikia sauti ya mwanaume.

"Mimi nisingependa kukuua Zabibu maana mimi nafurahia uumbaji wa Mungu mzuri aliokuumba lakini mimi nimeamriwa nikuue hivyo sina njia. Nisipokuua wewe, mimi nitauawa. Hivyo huna haja ya kupiga kelele, kufa hakika utakufa".

"Kwani mimi nimekosa nini masikini?", msichana aliuliza.

"Hata mimi sijui, haya kwa...".

Mimi nilikuwa nimejivuta na kuwa sawasawa na mlango wa hii nyumba, hivyo nilisikia mazungumzo haya. Niliona nikichelewa msichana huyu anaweza kuuawa. Basi nilitudi nyuma, bastola mkononi, niliurukia ule mlango na kuupiga teke ukafunguka. Hapo hapo mimi nikatumbukia ndani nikitanguliza kichwa chini lakini nikafyatua bastola na kumpata yule kijana niliyemuona ameshika kisu chenye mpini mwekundu. Ile risasi ilikuwa haikumpata vizuri hivi alisimama wakati na mimi nimeshasimama yakaanza masumbwi. Alitupa konde moja likanikosa mimi nikampa shoto langu lililompata shingoni akaenda chini na hakusimama tena.

Mambo haya yalitokea kwa muda mfupi sana. Zabibu alikuwa amepigwa na butwaa kiasi cha kwamba yule mtu alipoanguka chini na yeye akaanguka juu ya kochi na kuzirai. Nilienda kumwangalia yule mtu pale chini, sikuwa na haja hata ya kumgusa ili nijue kama amekufa. Niliona kulikuwa na barafu pale sebuleni, nikaifungua nikatoa chupa ya maji baridi nikammiminia Zabibu naye akashituka.

"Kweli huyu Zazibu alikuwa ndiye Binti Tanzania. Mimi nimeona warembo katika nchi hii, lakini huyu alikuwa ni zaidi. Ukiwa unaamini kuwa kuna binadamu wengine hushushwa moja kwa moja toka mbinguni, basi Zabibu alikuwa mmoja wao, kwani mpaka sasa siamini kama msichana huyu alizaliwa na binadamu. Ingawaje haiwezekani kuamini kuwa mtu anaweza kutelemshwa toka mbinguni, lakini ukimwona Zabibu wewe mwenyewe utaona uwezekano. Maana hata mimi niliona inawezekana kwa huyu kiumbe wa binadamu alikuwa ameumbwa bila kasoro. Palipo ukweli lazima tuseme; mwenzetu alikuwa na uzuri sio kifani. Mcho yake manene ya mviringo yaliyozungukwa na nyusi zenye rutuba yalifunguka na kuniangalia mimi.

"Umetoka wapi?", aliuliza kwa sauti nyororo iliyotoboa rohoni mwangu kama miali ya moto.

"Nimekuja kukuokoa".

"Kama wewe si mmoja wao umejuaje kuwa amekuja kuniua?".

"Kama mimi ni mmoja wao kwa nini nimwue wakati anataka kukuua?".

"Ndicho kinachonishangaza".

"Basi mimi si mmoja wao, mimi ni rafiki yako. Kama una akili timamu tuondoke hapa chumbani kwako maana kinanuka mauti".

"Sijui kwa nini naona kama ninakuamini".

"Kwa sababu ndio jambo la busara".

"Haya nichukue, nitoe hapa, yule mtu kweli angeniua. Huenda lazima nikushukuru, asante sana?".

"Bila asante, msichana kama wewe una haki ya kuokolewa, huna haja ya kushukuru, hiyo ni haki yako".

"Na huyu mtu tutamwacha humu?".

"Nitafanya mipango aondolewe, simu iko wapi?".

"Chumbani".

Aliniongoza chumbani, nikapigaa simu ofisini nikamkuta Eddy nikamweleza kwa kifupi, kisha nikamwambia afanye mpango mtu huyu aondolewe hapa. Eddy akasema atatekeleza.

"Wewe ni polisi?", Zabibu aliuliza.

"Hapana".

'Sasa wewe ni nani?".

"Mimi ni mtu ninayesaidia warembo kama wewe".

Nilimjengea tabasamu babu kubwa kisha nilimshika mkono tukazima taa, nakurudisha mlango, halafu tukaondoka. Nilipata teksi pale chini, tukapanda na kumwelekeza dereva nyumbani kwangu.

"Tunakwenda wapi?", Zabibu aliuliza.

"Nyumbani kwangu, unaonaje?".

"Nakuona wewe ni mtu wa ajabu ajabu tu, usingekuwa umeniokoa nisingekuamini hata chembe!.

Nilikuwa nimeingia na mashaka makubwa kwenda moja kwa moja nyumbani kwangu. Nilikuwa sijui kwa nini, hivyo nikabadili mawazo na kumwelekeza teksi dereva twende Ocean Road ambako ndiko Eddy alikuwa akikaa. Nilikuwa nina ufunguo mmoja wa nyumba yake kwa ajili ya nyakati kama hizi.

Tulikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Eddy baada ya kumwelekeza dereva nyumba. Nilimlipa dereva teksi pesa zake, halafu tukatelemka. Nilifungua mlango kisha nikawasha taa.

"Karibu ndani bibie".

Asante sana".

Nilikwenda kwenye barafu nikaifungua.

"Sijui utakunywa nini?".

"Baada ya vituko vilivyotokea nafikiri whiski na soda kali vitanifaa".

Nilichukua chupa ya whiski na soda kali halafu nikaendea glasi na kumimina kwenye glasi mbili ya Zabibu na ya kwangu halafu tukainua glasi zetu.

"Na tunywe kwa maisha yako marefu mrembo", nilisema.

"Na tunywe", alijibu kisha akanywa whiski ile haraka haraka.

Mimi nilikwenda kwenye simu nikapiga tena ofisini nikampata Eddy. Nilimpasha habari kuwa mimi na huyu mrembo Zabibu tulikuwa nyumbani kwake. Na yeye vile vile akanieleza juu ya kazi niliyokuwa nimemuagiza; vijana walikuwa wamempigia simu kuwa tayari walikuwa wameshaifanya. Nilimpongeza kwa jinsi kazi yake alivyokuwa anaifanya haraka kwa juhudi na maarifa.

"Nafikiri kwanza itabidi tufahamiane", nilimweleza Zabibu.

"Hasa ndilo litakuwa jambo la maana", alijibu.

"Mimi naitwa Willya Gamba, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?".

"Mimi naitwa Zabibu Abeid".

"Lo kweli aliyekuwa jina la Zabibu alijua kweli, kwani mimi naamini umtamu kama Zabibu".

"Ndio unataka kusemaje?".

"Nataka kusema wewe ni msichana mrembo ambaye sijawahi kumwona, na bila shaka aliyekuwa jina la Zabibu alijua utakuwa mtamu kama Zabibu".

"Usinivike kilemba cha ukoka. Kijana nadhifu mwenye sura nzuri na vituko vingi namna hii, haiwezekani kuwa haujamwona msichana mrembo kunizidi".

"Amini usiamini".

"Asante, lakini hata mimi leo nimemwona mvulana wa kipimo changu, sijui ulikuwa umejificha wapi mji huu hata nisikuone?".

"Mimi nilikuwepo nimejaa tele hapa mjini, lakini najua ingekuwa vigumu kuniona maana George Kiki alikuwa amekuganda kama kupe".

Pale pale sura yake iligeuka akainua macho yake marembo kunitazama machoni. Mimi nikamjengea tabasamu la sheria yake, Zabibu alionekana alikuwa amechanganyikiwa mawazo.

"Unajua nini juu ya George?".

"Hakuna haja ya kuzungushana sana, nafikiri inabidi sasa tuelezane ukweli. Na kabla hatujaendelea mbali ningependa kukuuliza lini umeonana na Kiki kwa mara ya mwisho".

Kwa kutokana na uzito wa sura yangu, Zabibu alilegeza sura yake kisha akajibu kwa sauti nyororo.

"Siku nne zilizopita, alisema atakwenda safari Botswana na atarudi baada ya wiki tatu".

"Na hauna habari nyingine yoyote kuhusu yeye?".

"Sina, kwani kumetokea nini?".

"Kwani yule mtu aliyetaka kukuua alikuwa amekueleza nini?".

"Hata, alinieleza tu kuwa alikuwa ametumwa kuja kuniua ingawaje yeye hakutaka lakini alikuwa amelazimishwa. Hakunieleza kabisa sababu.

"Nakuomba uwe na roho ngumu, rafiki yako George Kiki ameuawa jana. Maiti yake ilikutwa chumbani mwake ikiwa imechomwa kisu chenye mpini mwekundu".

Nilitoa kisu nilichokuwa nimekiokota nyumbani kwa Zabibu kabla hatujaondoka.

"Na watu wale wale waliomwua ndio walikuwa wanakuja kukumalizia wewe".

Zabibu alibubujikwa machozi na kidogo azirai tena.

"Lazima ujitulize kwa sababu mimi niko hapa kupeleleza mauaji ya mpenzi wako".

"Mimi nilijua tu wewe ni Polisi. Sura yako na namna ulivyoingia chumbani kwangu sijapata kuona kwa macho ila ndani ya sinema tu. Zile sinema za kijasusi".

"Mimi si polisi bali ni mpelelezi. Huenda polisi nao wakaja kufanya upelelezi wao, lakini mimi bahati nimewahi na kukuokoa huenda wao wangefika wakati wewe umekwisha kuwa maiti".

"Una maana gani kusema wewe ni mpelelezi wala si polisi?".

"Mimi ni mpelelezi wa siri kama umewahi kusikia watu kama hao".

Macho ya Zabibu yakapanuka.

"Usije ukawa wewe ndiye mtu ambaye huwa tunasoma habari zake kwenye magazeti akipambana na majasusi mbali mbali wanaofanya maovu dhidi ya Afrika".

"Ndio mimi".

Zabibu aliruka pale alipokaa akaja katibu na mimi.

"Ooh! Mungu ni bahati gani kuonana na mtu kama wewe maana mimi nilikuwa nafikiri ni maneno ya uzushi tu ya magazeti maana walikuwa hata hawatoi jina. Kila mara ukisoma unaona tu vijana wa Afrika wakiongozwa na mpelelezi mashuhuri kutoka Tanzania wamefaulu katika kuwateketeza majasusi ya mabeberu yaliyokuwa yanatenda mambo maovu dhidi ya Afrika. Nitawaeleza rafiki zangu kuwa ni kweli huyu mtu yupo na mimi nimeonana naye".

"Halitakuwa jambo la busara, tafadhali fanya hii iwe siri kati yangu na wewe, nimekueleza tu kwa sababu unaweza kunisaidia katika upelelezi wangu juu ya tukio la kutisha lililotokea hapa mjini siku chache zilizopita".

"Ahaa nimeelewa tumesikia kwenye maredio ya nchi za nje, kuwa silaha kali za wapigania uhuru zimeibiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam".

"Basi umebashiri sawa".

"Sasa George ana uhusiano gani na tukio hili?".

"Ndio sababu tumekuja kukuona, huenda ukajibu maswali yangu nitaweza kuambulia jambo lolote linalomwunganisha Kiki na tukio hili".

"Niko tayari kukusadia, kwanza kwa sababu umeniokoa, pili kwa sababu unapeleleza kifo cha mpenzi wangu na tatu nafikiri wewe ni kijana mwenye kupendeka".

"Asante, swali langu la kwanza nilitaka kujua kama ulikuwa unajua Kiki ni mtu wa Afrika Kusini?".

"Nilikuwa najua".

"Alikwambia alikuwa akifanya kazi gani?".

"Alisema yeye ni mwakilishi wa chama cha SANP katika Kamati ya Ukombozi ya OAU".

Nilishangazwa na jibu hili lakini sikuonyesha.

"Kwa hiyo mara nyingi alipokuwa anakuja kwako alikuwa akiandamana na wanachama wenzake wa SANP?".

"Hapana, George alikuwa mtu wa pekee, huenda ndio sababu nilimpenda. Alikuwa kila siku ananiambia kama ninataka kuepukana na matatizo nisizoeane na watu wengi. Na yeye kweli alikuwa hakuzoeana na watu. ila alikuwa na marafiki wawili tu. Ndugu Ray Sikazwe, rais wa SANP na Patlako Shuta ambaye ni ofisa mkubwa katika SANP. Sikumwona na mtu mwingine. Oh, kidogo nisahau, vile vile walikuwa na rafikio yao mwingine Mzungu ambaye George alifahamishwa kwake na Sembuche na mwenzake Shuta. Na hata gari nililo nalo, George aliuziwa na Mzungu huyu. Kwa vile yeye alikuwa hapendelei gari kwani alikuwa anatumia gari la ofisini alinipa mimi".

Kwa mara ya kwanza niliona mwanga kwa mbali, na nikajua kwa nini msichana huyu alitakiwa auawe. Nilijivunia bahati yangu kuwahi kabla hajauawa.

"Unaweza kujua Mzungu huyu anafanya kazi gani?".

"Lo! hawa ndio wenye lile kampuni kubwa lililo na makampuni kadha wa kadha katika nchi nyingi za kiafrika yaani EUROAFRO Limited. Na huyu Mzungu ndiye mwakilishi wa kampuni hilo hapa akiangalia akiangalia makampuni yake madogomadogo yaliyoko hapa".

Kapuni hili EUROAFRO Limited lilikuwa kampuni kubwa la kibepari lililokuwa na hisa nyingi katika makampuni katika nchi nyingi za Afrika. Kirefu chake kilikuwa EUROPE - AFRIKA COMPANY. Uhusiano huu kati ya wanachama wa chahama cha wapigania uhuru na kampuni ya kibepari ulinishinda kuelewa.

"Kwa hiyo unasema huyu Sikazwe na Shuta walikuwa marafiki wa karibu sana wa Kiki

"Ndiyo, hao ndio alikuwa anatembea nao mara kwa mara na vile vile walikuwa wanajuja kumwona au kumchukua pale kwangu mara kwa mara. Lakini zaidi ya watu hawa wawili na yule Mzungu, George hakuwa na rafiki mwingine".

"Huyu Mzungu unaweza kumkumbuka jina?".

"Ndiyo anaitwa Tony Harrison".

"Hawa marafiki wa Kiki uliweza kuzoeana nao?".

"Kusema kweli, Shuta na yule Mzungu walikuwa wananiheshimu kiasi cha kutosha lakini Sikazwe alikuwa wa ovyo sana. Amewahi kunitongoza mara nyingi na kunitaka nimwache George. Kwanza alikuwa anajivuna kuwa yeye ni Rais wa Chama na George alikuwa mtu mdogo tu, na kwamba msichana kama mimi sikufaa kutembea na George ila mtu kama yeye. Mimi nilimponda na kumwambia cheo na pesa havileti mapenzi, ila mtu anampenda mtu kwa vile alivyo, maana mtu na mtu ndio wanapendana". 

Lakini nakwambia uso wa msichana huyu unapoonyesha sura ya haya ndipo uzuri wake unapozidi. Ingekuwa wewe usingevumilia lakini mie nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi. Nilifikiria swali jingine nikaona nimepata maelezo ya kutosha ila nikaamua nimweke zabibu chini ya ulinzi wangu mpaka hapo baadaye.

Nilikuwa bado nafikiri hivi wakati tuliposikia gari linapiga breki mbele ya nyumba. Nilitoa bastola yangu tayari. Mlango ulipofunguliwa na Eddy akakingia.

"Bosi, twende haraka Veronika amenipigia simu anasema yuko katika matatizo. Nimekuja sababu nilijua huna gari", Eddy alisema huku akitweta.

"Oke Zabibu, subiri hapa tutarudi sasa hivi".

Nilifungua mlango kabla Zabibu hajasema neno lolote.

ITAENDELEA  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU