HOFU

SEHEMU YA TATU

II

Wakati Mike anazungumza na Mkurugenzi wa Upelelezi, ofisini mwa Peter Gerrit, katika mtaa wa Koinange, ambako ndiko yaliko makao ya Kinyonga Tours and Safaris, simu ya siri ilikuwa ikilia. Simu hii ilikuwa inajulikana na watu wachache sana. Kila simu ilipokuwa inalia moyo wa Peter ulishtuka kidogo.

"Hallo, Peter hapa,"Peter alisema mara baada ya kuunyakua mkono wa simu na kuupachika katika sikio lake la kulia.

"Masoga hapa," upande mwingine wa simu ulimwitikia.

Masoga alikuwa ni afisa mwingine katika kurugenzi ya upelelezi. Lakini alikuwa kwenye orodha ya kulipwa na Peter Gerrit. Masoga alikuwa ni msaliti wa serikali ya wananchi wa Kenya kwa sababu ya tamaa ya pesa. Hivyo alikuwa anampa habari muhimu sana Peter ambazo alikuwa anzitumia dhidi ya wanamapinduzi wa Afrika.

Wajati Mwaura alipokuwa anamweleza Mike asubuhi ile jinsi alivyokuwa na wasiwasi juu ya wageni waliokuwa wakiingia nyumbani kwa Peter, Masoga alikuwa amepitia ofisini kwa Mike akiomba ruhusa kwenda nje. Na kwa vile hawakuwa na wasiwasi nae, Mwaura aliendelea kueleza wasiwasi wake kuhusu Peter Gerrit na wageni wake. Ndipo Mike aligeuka na kutaka kujuwa Masoga alikuwa na shida gani. Lakini Masoga alikuwa amesikia sehemu ya mwisho ya taarifa ya Mwaura juu ya wazungu walikuwa wakienda kwa Peter.

"Ehee, kuna nini?. Peter aliuliza kwa sauti kali.

Masoga alikuwa anapiga simu kwenye kibanda cha posta kando ya posta kuu, alisema, "Kuna habari ofisini kwetu kuwa unao wageni nyumbani kwako ambao wanaingia tu lakini hawatoki, idara yetu inao wasiwasi, vipi?".

Bila kujua umuhimu wa habari alizokuwa akizitoa kwa Peter, Masoga alitabasamu.

"Wana wazimu! naona sasa idara yenu haina kazi ya kufanya. Mimi sina wageni wa namna hiyo. Kama wana wasiwasi, kwanini wasije kuona?". Hivi ni nani anasema maneno hayo?", Peter aliuliza kana kwamba hajali kitu ingawa kwa kweli moyo wake ulikuwa ukidunda vibaya kwa hofu aliyokuwa nayo.

"Kijana mmoja anayeitwa Mwaura".

"Acha nae". Peter alimjibu. "Huenda anapalilia cheo".

"Huenda. Lakini mimi niliona ni vizuri kukwambia.

"Hivyo ni sawa. Lakini hakuna chochote wala usiwe na wasiwasi. Hata hivyo, asante. Njoo umuone Kanabhai. Utakuta anayo bahasha yako.

"Asante", alijibu Masoga huku anasikia raha alipojuwa kuna bahasha yake.

Baada ya Peter kuweka simu chini, alianza kufikiri. Alikuwa ameshangazwa na habari hizi kwani hakutarajia kabisa kuwa idara ya upelelezi ya Kenya ilikuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kiwango cha juu kiasi hicho. Ni kweli kwamba Peter alikuwa na makomandoo maarufu kumi na wawili nyumbani kwake kutoka kwenye jeshi hatari la makaburu liitwalo KULFUT. Watu hawa walikuwa wameingia nchini Kenya kwa siri na ni yeye aliyetayarisha mpango huo. walikuwa wameingia nchini Kenya kupitia Mombasa. Walisafiri kwa mashua mpaka kwenye Bandari ya Mombasa baada ya kushushwa katika Bahari ya Hindi kutoka kwenye Meli moja ya makaburu walikuwa wamefika kwenye ufuko wa Nyali walipojifanya wao ni watalii waliokuwa wakicheza tu na mashua. Peter alikuwa ametayarisha kila kitu.

Akitumia wadhifa wake kama mfanyabiashara wa kuhudumia watalii, aliweza kuwasafirisha. Awamu kwa awamu, hadi Nairobi. Aliamua kutowasafirisha kwa mkupuo ili asije kugutukiwa. Hivyo watu hawa walikuwa nchini Kenya kinyume cha sheria. Idadi yao ya watu kumi na wawili kuwa yenye nguvu sawa na kikosi kizima cha jeshi. Vile vile walikuwa wamepewa mafunzo ya kila aina kuhusu kuua. Wawili kati ya hao walikuwa NINJA. Ninja ni mtu aliyehitimu mafunzo ya pekee ya karate na kung fu huko Ujapani na Korea. Kuelezea ninja kwa kirefu inaweza kuchukua siku nzima. Hivyo ridhika na ukweli huu kwamba ninja anakuwa amejifunza zaidi ya njia elfu moja za kuua. Mtu mmoja anaweza akakiangusha kikosi kizima. Ni watu wachache katika ulimwengu huu ambao wamehitimu mafunzo hayo. Askari jeshi mia moja na silaha zao hawawezi kufua dafu kwa ninja mmoja.

Makomando hawa wa makaburu walikuwa bado kufika mwisho wa safari yao. Walikuwa wanaelekea Tanzania. Hivyo kama wangegutukiwa bado wakingali Kenya, Peter angepata matatizo makubwa kutoka kwa wafadhili wake. Hivyo ilibidi abadili mpango haraka ili aweze kuingia Tanzania ambako ndiko walikuwa wakafanye kazi. Peter aliendelea kujifikiria yeye mwenyewe. Yeye pia alikuwa ni komando katika jeshi la KULFUT kwenye kikosi cha ujasusi. Alikuwa amehitimu kila aina ya mafunzo ya upiganaji na ujasusi. Alikuwa ameletwa Kenya kusubiri wakati wake wa kufanya kazi. Alikuwa tayari kufanya kazi wakati wowote alipohitajiwa na wakubwa wake. Na wakati huo sasa ulikuwa umewadia. Wakubwa zake Peter walikuwa wameamua kufanya kazi sehemu hii ya Afrika mashariki.

Kila wakati alipofikiria mpango huu na utekelezaji wake, Peter alisisimkwa na damu. Alikuwa amefikiri sana juu ya siasa za nchi huru za afrika na kuona vyema kuzitokomeza ili Afrika kusini iweze kulitawala bara zima la Afrika. Aliamini kabisa kwamba mtu mweusi hakuwa na haki ya kujitawala. Mtu mweusi alipaswa kuwa mtumwa wa wazungu. Kwake Peter mtu mweusi alikuwa kama paka au kwani hata mbwa anayo thamani. Mara nyingine alishangaa aliposikia mtu mweusi anazungumza neno la busara. Kwake yeye kama makaburu na pia kufuatana na walivyofunzwa na kulelewa, aliona mtu mweusi kama kitu kisichokuwa na thamani yoyote. Kwa sababu hiyo Peter alisisimkwa damu alipofikiri kuwa yeye mwenyewe angeshiriki kuwaangamiza watu weusi katika nchi zao ambazo walidai ni huru.

Ili mipango yake isije ikaharibika, Peter aliinua simu akazungusha namba kazaa, kisha kusubiri kuitikiwa.

"Hallo, hapo ni Arusha ?" Peter aliuliza baada ya kuitikiwa.

"Ndiyo. Habari gani, P. G.?"

"Nzuri, F. K."

"Mipango imebadilika. Tungoje mpakani saa mbili usiku. Naamini mipango yote iko shwari mpakani."

"Nimeisha suka kila mpango kama tulivyozungumza. Hakuna tabu kamwe."

"Ahsante F. K."

"Ahsante P G."

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru