HOFU


SEHEMU YA NNE

F. K

"Nyoka Tours and Safaris," Tondo aliitika kwenye simu.

"Njoo nyumbani haraka." Tondo alisikia sauti ya tajiri wake ikimwamrisha.

"Sawa mzee," aliitika kwa unyenyekevu.

Tondo aliweka simu chini na kuinuka. Bila hata kuaga alielekea kwenye gari lake ili aende kwa tajiri yake. Alipoangalia saa yake aliona inaonyesha saa nane na nusu mchana.

Chris Tondo alikuwa meneja mkuu wa kampuni ya Nyoka tours and Safaris ya mjini Arusha ambayo ilikuwa ni mali ya Mhindi mmoja. Mhindi huyo alikuwa anajulikana kwa jina la Firozali Kassam na watu wengi walimwita F. K. Yeye alikuwa tajiri sana. Alikuwa akiishi sehemu ya Them Hill ambako alijenga nyumba kubwa sana ambayo mashabiki waliita "White House" au Ikulu ya Arusha.

F. K alipendwa sana na wakazi wa Arusha kutokana na tabia yake ya kuwasaidia watu wenye uwezo mdogo wa kipesa. Alikuwa mtu mkarimu sana. Inasemekana nusu ya teksi zote za Arusha zilinunuliwa na wenyewe kwa mkopo usio na riba kutoka kwa F. K. Inasemekana kuwa alifuta madeni mengi ya watu walioonekana hawana uwezo wa kulipa. Ingawa hakuwa muumini wa dini ya kikristo, F. K alisaidia kujenga makanisa mengi ya madhehebu mbalimbali mjini Arusha.

Kwa muda mrefu F.K alikuwa mstari wa mbele katika kusaidia Chama na serikali katika mkoa huo, kufanya shughuli zake nyingi. Inasemekana. Kwa mfano alichanga pesa nyingi kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya chama cha mkoa. Hivyo alipewa heshima kubwa sana na wakuu wa chama na serikali hapo mkoani Arusha. Kusema kweli kama angetokea mtu akasema kwamba F.K alikuwa ni mtu mbaya, basi angeuawa kwa kupigwa mawe hadhalani.

F.K alijulikana kama mtu wa watu, raia mwema na mpenzi wa watu wa rika zote. Alikuwa mtu maarufu na murua. Watu wote walimwelewa hivyo. Sifa zake zilizidi kuvuma kwani F. K alikuwa mfadhili, asiyebagua mtu awe mweupe au mweusi, masikini, fukala au tajiri. Watu wote mbele ya F.K walijiona sawa. Huo ulikuwa upande mmoja tu wa F.K.

Lakini F.K alikuwa na upande mwingine ambao ni watu wachache sana walioujuwa. Hata mtu kama Chris Tondo nae alimjuwa F.K juu juu tu.

F.K alikuwa mzaliwa wa Dar es Salaam, Tanzania, baba yake alikuwa mfanyabiashara maarufu sana Jijini Dar es Salaam, alikuwa na maduka makubwa matatu ya vipuri vya magari na alikuwa wakala wa makampuni mengi ya nchi za nje hapa Tanzania. Hivyo huyo mzee Kassam alikuwa tajiri sana. F.K alizaliwa mnamo mwaka 1945. Baada ya kusoma shule ya msingi hapo nchini, baba yake alimpeleka Uingereza ambako alipata elimu ya sekondari na chuo kikuu. Hii ilitokana na kwamba baba yake alikuwa na uwezo wa kumlipia F.K ada ya shule.

Mnamo mwaka 1967 serikali ya Tanzania ilitaifisha makampuni makubwa ya watu binafsi na kuyaweka katika mikono ya wananchi. Hatua hiyo ilifuatia kutangazwa kwa siasa za ujamaa na kujitegemea katika Azimio la Arusha. Mnamo mwaka 1972 serikali ilichukuwa hatua nyingine zaidi. Majumba makubwa ya watu binafsi yaliyaifishwa vilevile.

Wakati huo F.K alikuwa anasoma chuo kikuu huko Uingereza. Baba yake alimpigia simu na kumweleza mkasa uliokuwa umewapata nyumbani. Alimfahamisha kuwa nyumba zao therathini ambazo walikuwa wamejenga na nyingine kununua vile vile zilikuwa zimetaifishwa. Aliposikia vile F.K alipatwa na wazimu. Aliilaani serikali kiasi ambacho hajapata kusikia.

Siku hiyo jioni alienda kwenye baa na kuchapa mtindi barabara. Mara alisikika akiapa, "Naapa kwa jina la Mungu, kuna siku nitalipiza kisasi dhidi ya serikali ya Tanzania", Kwa bahati mbaya au nzuri katika baa ile kulikuwemo jasusi mmoja kutoka Afrika Kusini lililokuwa kwenye shughuri zake lenyewe. Liliposikia hivyo lilikumbuka kuwa shirika la ujasusi la Afrika Kusini lilikuwa linamtafuta mtu raia wa Tanzania ambaye angelifanyia kazi ya kijasusi huko.

Hivyo ndivyo alivyopatikana F.K na kuwekwa katika orodha ya kulipwa na shirika la ujasusi la Afrika Kusini. Pamoja na kulipwa ili afanye kazi ya ujasusi, F.K aliahidiwa kuwa angepewa msaada kulipiza kisasi dhidi ya serikali ya Tanzania. Inasemekana kuwa baadae alipotea kwa muda wa miaka mitatu na haikujulikana mahali alipokuwa. Lakini habari zilisema kuwa alikuwa huko Afrika Kusini akipewa mafunzo ya kijasusi kwenye makambi mbali mbali.

Aliporudi Tanzania alikuta wazazi wake wako kwenye pilikapilika za kuhama na kwenda Canada F.K alikataa kuondoka na wazazi wake na kusema kwamba yeye alikuwa mzaliwa wa Tanzania hivyo hakuwa na sababu ya kuihama nchi yake na kwenda nchi nyingine. Hivyo familia yake ilimugawia sehemu ya mali iliyobaki naye akaamua kuhamia mjini Arusha. Huko ndiko alikoanzisha kampuni yake ya kuhudumia watalii iliyojulikana kwa jina la nyoka tours and safaris.

Alichagua jina hilo kwa sababu alizozijua mwenyewe. Mabwana zake walimpa fedha nyingi ambazo alizitumia kufanya mambo niliyoyaeleza na pia kujenga white house. Kutokana na utajiri wake F.K aliweza kuisarti nchi bila mtu yeyote kumshuku. Fedha zake ziliwafumba watu macho. Nyumba hiyo iliyoitwa White House ilikuwa imejengwa kwa aina yake. Ilikuwa imejengwa kwa shabaha ya kufanya ujasusi. Nyumba hiyo ilikuwa na vyumba vingine chini ya ardhi. Kulikuwa na barabara kadhaa chini kwa chini ambazo zilitokea nje ya sengenge ilizunguka ekali kumi na mbili za kiwanja cha nyumba hiyo.

F.K alikuwa hajaowa wala kuwa na watoto. Hivyo aliishi katika nyumba hii peke yake. Watumishi wake waliishi kwenye nyumba kando kando ya jumba lake. Kwa muda wote huo F.K alifanikiwa kujenga kwa nje, akaonekana kama mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo. Alionekana mzuri kwa nje lakini alikuwa hatari kwa ndani.

Dhamila yake kubwa ilikuwa ni kulipiza kisasi. Kwa kufanya hivyo F.K angekuwa amefanya kazi katika upande wa adui namba moja wa Afrika huru na Ulimwengu mzima kwa ujumla. Hii ndiyo ilikuwa upande wa pili wa F.K ambayo ilikuwa sura yake halisi.

Chris Tondo ambaye sasa alikuwa anaelekea Themi Hill ndiye aliyejuwa F.K hakuwa mtu mzuri kama watu wengine wa mjini Arusha walivyoamini. Yeye Tondo walikuwa wakionana na kufahamiana kiajabu. Tondo alikuwa na umri karibu sawa na F.K. Walionana mara tu baada ya Tondo kustaafishwa kutoka Jeshi la Polisi kwa manufaa ya umma. Alikuwa tayari amefikia cheo cha Kamishna Msaidizi, akiwa kati ya waafrika wa kwanza kufikia ngazi hiyo. Tondo alichukulia kustaafishwa kwake kama kitendo cha fitina na hivyo alikuwa na chiki dhidi ya serikali. Aliamini kuwa alionewa wivu kwani alikuwa na nafasi nzuri ya kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba huyu Chris Tondo alikuwa akitumia cheo chake kusaidia wahujumu uchumi. Aliwasaidia kutorosha vipusa vyote vya thamani kwa njia ya magendo. Alipostaafishwa jina lake lilitolewa kwenye magazeti ya kila siku. Kwa njia hiyo F.K ambaye alishaambiwa habari za Tondo na wale wahujumu aliowasaidia, alijuwa kuwa amepata mtu aliyekuwa akimuhitaji. F.K alijuwa Tondo hakuwa mwaminifu kwa serikali. Vile vile alishakuwa mtu mkubwa na hivyo mwenye uzito katika jeshi la polisi. Huyu ndiye mtu aliyefaa katika mpango wake waliokuwa nao F.K pamoja na wafadhili wake.

Siku moja F.K alimfuata Tondo Jijini Dar es Salaam. Alimdanganya kwamba kuna mtu amemwelekeza kwake. Alimwambia kuwa kama ingewezekana alipenda wafanye kazi pamoja kwa kuwa hakuwa na kazi. Bila kusita Tondo alikubali akaona ni bahati iliyoje. Siku hiyo Chris Tondo alimweleza jinsi alivyoichukia serikali ya Tanzania akidaiwa kuwa ilimstaafisha bila sababu ya msingi.

"Wewe tulia tu, kuna siku mtu atalipa", F.K alimhakikishia.

Baada ya kusikia maelezo ya Tondo, F.K alijuwa amempata mtu aliyekuwa akimtafuta. Tondo aliteuliwa kuwa Meneja Mkuu wa Nyoka Tours and Safaris. Kusema kweli kampuni hiyo ilikuwa ni kisingizio. Mambo ambayo F.K na Tondo walifanya kwa siri katika kuhujumu uchumi aliyejuwa ni Mungu peke yake.

Tondo alisimama na kuegesha gari nyumbani kwa F.K. F.K alifungua mlango na kumkaribisha ndani Tondo.

"Karibu ndani.

"Asante", alijibu Tondo.

"Nimekuita ghafla kwa sababu nimepata habari sasa hivi kutoka kwa yule rafiki yangu wa Nairobi kwamba wale wageni waliokuwa wafike kesho wataingia leo jioni. Kitu ninachotaka ufanye ni kwenda kubadiri mipango huko mpakani. Kama nilivyokuwa nimekueleza awali, watu hawa wataingia bila kupitia sehemu za kawaida. Wageni hao wanayo mizigo ambayo sitaki ikaguliwe wala wao wasionekane na mtu yeyote", alieleza F.K na kisha akaelekea kwenye chumba fulani. Aliporudi alikuwa amebeba pasporti kumi na mbili na bahasha moja.

"Pasporti hizi ni za hawa wageni. Nenda nazo huko mpakani kwa mtu wetu akugongee mihuri ya idara ya uhamiaji. Unajuwa ni siku nyingi hatujaangalia maslahi yake. Hivyo mpelekee hii bahasha yake".

F.K alimkabidhi Tondo hivyo vitu.

"Aidha nenda kwa Hasanali mwambia kuwa wale wageni watakwenda nyumbani kwake kwa kupitia njia ya porini mnamo saa mbili usiku. Mimi nitafika hapo kuwachukuwa mnamo saa mbili na nusu usiku, na yeey tuonane hapo. Kazi ifanyike kama kawaida Tondo".

"Sawa nitatekeleza yote kama ulivyosema".

Tondo alibeba mzigo wake akaelekea nje huku akisindikizwa na mwenyeji wake.

Wakati akielekea nyumbani kwake alifikiri kwamba wakati mwingine mambo waliyofanya yalikuwa ya ajabu kama sasa alishangaa alipoona F.K anazo pasporti za watu ambao walikuwa bado kuingia nchini hata hivyo Tondo alijuwa haikuwa juu yake kuuliza maswali. kazi yake kubwa ilikuwa utekelezaji.

Tayari alikuwa amejenga nyumba tatu. Nyumba moja ilikuwa Dar es Salaam na aliipangisha kwa Ubalozi kwa elfu hamsini kwa mwezi. Nusu ya kodi hiyo Tondo alilipwa kwa fedha za kigeni. Nyumba nyingine alikuwa amejenga nyumbani kwao Njombe ambayo kwa viwango vya huko nyumba hiyo ilikuwa ya hali ya juu. Nyumba ya tatu ni hiyo aliyojenga Arusha. Tondo alikuwa hajawahi kuoa lakini alikuwa na watoto watatu aliowapata nje ya ndoa. Watoto wake wawili wakubwa walikuwa wanasoma shule ya msingi huko London, wakati yule mdogo alikuwa anakaa na mama yake huko Njombe.

"Tangu nistaafishwe na kuungana na F.K mafanikio yangu yamekuwa ya makubwa kuliko ya mtanzania wa hali ya juu. Kweli kazi hii inanifaa shauri yao watanikoma", Tondo alijisemea kimoyomoyo.

Mara alikutana na gari lilimumulika kwa taa zake. Kabla ya kupishana alitambua ni Nyaso, hivyo akapunga mkono, Nyaso naye akampungia mkono pia.

Nyaso alikuwa ni msichana mrembo sana. Hapakuwepo msichana mwingine mjini Arusha ambaye wangeweza kushindana naye kwa urembo. Nyaso alikuwa hawala yake F.K. Watu waliojuwa penzi lao walisema kuwa Nyaso alikuwa saizi ya F.K kutokana na utajiri wake. Bali tu walishindwa kufahamu kwanini hawakuoana. Hata hivyo rafiki zake na F.K ndoa ingekuwa kinyume cha mila za wahindi. Kwa kuamua kuishi na Nyaso kama hawala kulionyesha watu unafiki wa F.K na Wahindi wengine. Waliopenda kufanya mapenzi na waafirika lakini ilikuwa mwiko kuwaoa. Wahindi walitembea na wasichana wa kiafrika na baadaye kuwatupa jalalani.

Kila wakati Tondo alipofikiria uhusiano wa watu hawa wawili aliona kuwa Nyaso hakumhitaji sana F.K. Alijuwa msichana yule alitaka pesa zake tu. Hii ilionyeswa na majibu ya mkato aliyompa F.K mara kwa mara. Lakini hata hivyo F.K alikuwa amemjengea Nyaso nyumba nzuri sana. Nyaso alikuwa haruhusiwi kwenda kwa F.K. Hivyo F.K alikuwa akienda kulala kwa Nyaso. Hata Tondo hakujuwa kwanini F.K hakupenda Nyaso aende kwake bali alilidhika alipoambiwa na F.K kwamba hiyo ingekuwa kukiuka mila za Kihindi.

"Acha mtoto wa Kitanzania amule kidogo Mhindi huyu", Tondo alijisemea.

Aliegesha gari yake nyumbani kwake halafu akajitayarisha kwa safari ya kuelekea mpakani.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU