Yanga hucheza pungufu dhidi ya Simba?

Wachezaji wa Yanga wakiomba dua kabla ya kuingia uwanjani kucheza na mahasimu wao wakubwa Simba (picha ya chini), katika mchezo wa kirafiki wa NANI MTANI JEMBE, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Decemba 21, mwaka jana. Simba walishinda 3-1.
WATANI wa jadi katika soka la Tanzania Yanga na Simba wamekuwa na kasumba ya muda mrefu ya kuchukuliana wachezaji kwa lengo la kuimalisha vikosi vyao huku wachezaji hao wakiwa na mapenzi makubwa na upande mmoja wa timu hizo baada ya kusajiliwa na upande mwingine.

Kasi ya timu hizo kuchukuliana wachezaji ilianza kuota mizizi wakati wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara miaka ya 1990, (Sasa ligi kuu), wakati huo timu hizo zilikuwa na wafadhili wakubwa kama Hayati Abbas Gulamali aliyekuwa Yanga na Azim Dewji aliyekuwa Simba.

Katika kuoneshana umwamba, Gulamali alifanikiwa kumteka kiungo mahili wa Simba wakati huo Deogratias Njohole ambaye mashabiki wa Simba walimpachika jina la 'OCD' (Kamanda wa Polisi) kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukabiliana na adui uwanjani.

Pamoja na Dewji kuhaha huku na huku kuhakikisha mchezaji huyo aliyekuwa tegemeo la Simba wakati huo haendi kwa mahasimu wao Yanga, Gulamali alifanikiwa kutinga Uwanja wa Taifa (sasa uhuru), akiwa amemvisha Njohole jezi namba tano ya Yanga.

Kutokana na pigo hilo kubwa kwa Simba, Dewji alijibu mapigo baada ya kumsajili kiungo mchezeshaji mahili kabisa wa Yanga wakati huo, Athuman Abdallah China, ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa klabu yake ya Yanga wakati huo.

Kufuatia majeraha hayo, Yanga na Simba ziliendelea kuchukuliana wachezaji, ambapo Yanga ilifanikiwa kuwasajili, Hamisi Thobias Gagalino na Methord Mogella Fundi (ambao wote ni marehemu), nao Simba wakawachukuwa, Said Mwamba Kizota (marehemu) na Nico Bambaga.

Nimejaribu kufafanua hivyo ili mashabiki wa soka nchini Tanzania waelewe kuwa timu za Yanga na Simba hazikuanza kuchukuliana jana. Pia mfumo huo hauko kwa timu hizo tu kwani hata Ulaya timu fulani ikimhitaji mchezaji hufuata taratibu za uhamisho.

Hivi karibuni umeibika ushindani mkali kwa viongozi kwa timu hizo kugombea wachezaji, ambapo Yanga wamefanikiwa kwa kiasi fulani kusajili wachezaji kutoka. Mwaka juzi Yanga ilifanikiwa kumsajili beki Mbuyu Twite aliyekuwa APR ya Rwanda, baada ya Simba kusuasua kumfanyia uhamisho wa kimataifa (ITC).

Awali kabla ya hapo Yanga ilifanikiwa kumchukua aliyekuwa beki kisiki wa Simba, Kelvin Yondani, ambaye alitua Yanga kwa dau la shilingi milioni 30, huku Simba wakihaha kumsaka beki mwingine mbadala wa Yondani ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara.

Baada ya Yondani kusajiliwa Yanga, maumivu mengine yalifuata ambapo timu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani Jijini Dar es Salaam ilifunga kazi kwa kumsajili mshambuliaji kipenzi wa Simba, Emanuel Okwi, aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Tunisia alitua Jangwani.

Awali kabla ya Okwi kutua Jangwani na kuvaa jezi ya kijani namba 25, wachezaji wengine kama makipa Juma Kaseja, Ali Mstafa Baltez na kiungo Athuman Iddi waliokuwa wachezaji wa Simba, kabla ya kutua Yanga akianza Iddi, Baltez na baadaye Kaseja aliyeachwa kwa madai ya kushuka kiwango chake.

Kipa mwingine wa Yanga, Deogratius Munisi (Dida), ambaye pia aliwahi kucheza Simba, kama golikipa wa akiba, nae alisajiliwa Yanga kama mchezaji huru, baada ya kuachwa na timu yake ya awali ya Azam FC. Huyu ndiye alipaswa kuwa kipa namba moja wa Yanga kwa sasa tofauti na wengine.

Hakuna ubishi kuwa Klabu ya Yanga ndio yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka katika ligi kuu ya soka Tanzania Bara, ikiwa imesheheni wachezaji wenye vipaji kama Mrisho Ngasa, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Jerryson Tegete na wengine wengi lakini inapokutana na Simba haifui dafu.

Hii inatokana na Yanga mara kadhaa kucheza wakiwa pungufu uwanjani, huku wapinzani wao Simba wakicheza wakiwa zaidi uwanjani. Matokeo ya hivi karibuni, ambapo Simba wakiwa nyuma kwa mabao 3-0 hadi mapumziko, waliweza kusawazisha mabao hayo dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu.

Katika mchezo uliofuata, Yanga waliokuwa wakitamba kupitia vyombo vya habari kwa kuwa na kikosi bora, hawakufua dafu kwa kuburuzwa mabao 3-1, katika mchezo wa nani mtani jembe. Ushindi huo wa Simba dhidi ni kielelezo kwa Yanga kucheza soka wakiwa pungufu uwanjani.

Si kwa sababu katika mchezo huo Yondani aliondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu, la hasha, ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Yanga hata iwe na kikosi imara chenye wachezaji wazuri zaidi ya Christian Ronaldo bado hawatafua dafu kwa Simba.

Kwanini?. Kwa sababu Kaseja ni shabiki nazi wa Simba, ambaye hawezi kuisaidia Yanga kushiinda timu anayoipenda. Akiwa Yanga kabla ya kurejea Simba mwaka 2011, Yanga ikiwa katika kiwango bora, Kaseja akiwa golini timu hizo zilitoka sare kwa kufungana mabao 2-2.

Simba wameepuka kusajili wachezaji kutoka Yanga, hivyo wamesajili wachezaji chipukizi, ambao husaidiwa na wachezaji wakongwe waliosajiliwa na Yanga, kuisaidia timu yao kupata ushindi mnono.

Kelvin Yondani na Athuman Iddi ni wachezaji wazuri sana katika sehemu ya kiungo na ulinzi, lakini wachezaji hao wanapokutana na Simba hucheza chini ya kiwango na kuruhusu wapinzani wao kufunga mabao kirahisi kama alivyofanya Amisi Tambwe katika mchezo wa nani mtani jembe.

Hata zile goli tatu ambazo Simba walisawazisha katika mchezo wa Ligi Kuu, zilitokana na sababu kama hizo, kwani hata golikipa Ali Mstafa, niliyemwelezea mwanzo hakustahili kufungwa mabao kama yale kutokana na umahili wake.

Yanga wanapaswa kujiangalia upya, vinginevyo hata makocha wazalendo wenye mapenzi makubwa na timu hiyo kama Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali watafukuzwa muda mfupi baada ya kufungwa na Simba, kwani ndani ya jeshi la Yanga kuna Simba ndani yake.


 





Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU