SURA YA SABA
BINTI TANZANIA
"Lo, hiyo ilIkuwa alimanusura", veronika alisema huku jasho likimtoka na akihema.
"Nakuambia", Sherriff naye huku akihema.
"Eddy, moja kwa moja nyumbani kwangu, akili yangu imevurugika", nilimwambia Eddy aliyekuwa akiendesha kwa kasi sana.
"Huyu Eddy ni nani na katokea wapi?, maana bila yeye sasa hivi sote tungekuwa maiti", aliuliza Sherriff.
"Katika kazi hizi Komred Sherriff lazima uwe na plani bila plani huenda mimi ningekuwa nimeuawa siku nyingi. Huyu kijana ni mfanyakazi mwenzetu, na toka asubuhi yuko pamoja nasi lakini kazi yake ilikuwa ni kutulinda sisi. Na kwa jumla ndivyo hivyo tunavyofanya kazi".
Eddy alisimamisha gari mbele ya nyumba yangu. Tulitelemka ndani ya gari, nikafungua mlango tukaingia sebuleni wote na kuketi. Nilikwenda katika barafu na kutoa chupa ya whiski na chupa za soda kali. Nilitenga glasi, wote wanne tukaanza kunywa. Nilipoangalia saa ilikuwa saa tisa kasoro robo.
"Eddy nafikiri hatuna muda wa kupika hapa nyumbani, hivyo nenda Palm Beach Hoteli wakakufungie chakula cha watu wanne", nilimwambia Eddy".
"Sawa". 
Eddy aliondoka kwenda kutafuta chakula.
"Willy, watu hawa wamepania sana", Sherriff alisema kwa sauti nzito.
"Mimi nilijua watapania, ndio sababu nikaweka tahadhari yote hii. Ngoja Eddy arudi atueleze ilikuwaje mpaka wakaweza kutufuata mpaka pale walipotushambulia. Ni bahati nzuri sana kwamba wote mna mafunzo ya kijeshi hivi mlitii amri za Eddy bila hata kufikiri. Jambo hili limenifurahisha sana maana kama mtu angesita, sasa hivi tungekuwa tunamuombolezea".
"Naona wote tumejenga silika ya hali ya juu kwa wakati wa namna hii", Sherriff alijibu.
"Tukimsubiri Eddy, sijui mmewaonaje hawa Maraisi wa vyama hivi vile vile", Veronika aliuliza.
"Mimi moja kwa moja nimempenda Chimalamo maana ni mtu aliye wazi. Nafikiri ni kiongozi mwenye busara. Kutokana na maelezo aliyotupa nafikiri anajua anafanya nini, na mtu kama huyu anaweza kabisa kuendesha harakati za ukombozi dhidi ya Makaburu maana anawajua nje na ndani. Ukikumbuka mazungumzo yetu siku ile huko Freetown juu ya Afrika Kusini sasa ukiongeza haya aliyotupasha ndugu Chimalamo hata wewe unazidi kupata mwanga mkubwa juu ya Afrika Kusini. Kwa ujumla nafikiri Chimalamo ni kiongozi mzuri na halisi. Juu ya Sikazwe nina dukuduku nae moyoni, maana sikumwelewa sawasawa sababu si mtu wazi. Hata nidhamu ya ofisi yake ilivyo kabla hujaonana naye, inaonyesha kasoro fulani. Nafikiri bila Willy kuwa mtu anayejua mbinu nyingi tusingemwona maana mbinu aliyotumia mimi mwenyewe mkufu. Halafu kuna kitu fulani ndani ya Ndugu Sikazwe ambacho sijui ni nini lakini kinanidundadunda sijui wenzangu mmemuonaje?", Sherriff alieleza.
"Nafikiri mawazo yako na ya kwangu hayako mbali. Nakubaliana na wewe kuwa Ndugu Chimalamo ni kiongozi mzuri. Na vile vile kuhusu Sikazwe hata mimi kuna kitu fulani ambacho sikukielewa ni nini kilicho ndani yake, lakini huenda nitakijua nikipata muda mrefu kufikiri. Lakini huenda ni mtu wa tabia ya namna hiyo, na kwa namna yake hiyo anaweza kuwa ni kiongozi mzuri zaidi kuliko hata Chimalamo. Huenda kila kitu kilicho ndani yake ni uongozi bora", nilieleza.
"Mimi sina la kuongeza, naona mawazo yetu yameoana", Veronika alijibu.
"Kusema kweli jamani sijastuka kama leo, kweli tumeponea chupu chupu, asante sana Willy kwa kuweka tahadhari".
"Bila asante Vero, maana ni kazi yangu kuhakikisha usalama wenu na wangu, hivyo uwe na amani kuwa nitafanya kila jitihada kuhakikisha usalama wetu, kama nikishindwa itakuwa nje tu ya uwezo wangu".
"Naomba sigara", Sherriff aliniambia.
"Hapa mimi nina aina ya sigara iitwayo Tropicana, sijui kama itakufaa".
"Wewe nipe tu, sigara zangu ziko hotelini. Baada ya kashikashi nahitaji sigara kama kufa".
"Nilitoa pakiti ya Tropicana nikaiweka mezani tukaanza kuivuta.
"Lo, mbona sigara safi kabisa, ni sawa sawa tu na 555, zinatengenezwa wapi?", Sherriff aliuliza.
"Hapa hapa nchini kwetu".
"Lo, mmeendelea sana, mnaziuza na nje?", aliuliza Veronika ambaye naye alichukua moja akavuta ingawaje hakuwa mvutaji sana.
"Sijui maana wameanza kuzitengeneza hivi karibuni, lakini naamini watafanya hivyo".
Mara Eddy akawa amerudi tukapata chakula ambacho tulikishambulia vizuri sana maana njaa zilituuma vibaya.
II
Baada ya kula chakula cha mchana tulikaa kitako kumsikiliza Eddy, akitusimulia jinsi mambo yalivyotokea pale SANP.
"Baada ya nyinyi kuondoka kwenye ofisi za PLF, nilingoja hadi nikaona gari Peogeot 504 namba TZ 311251 likijitokeza kwa upande mwingine na dereva wake akichungulia kwenye kioo cha kuendeshea baada nafikiri ya kuona hakuna gari zaidi lililokuwa nyuma yake; liliongoza kufuata njia mliyofuata. Mimi nililitilia mashaka nikalifuata nyuma baada ya magari kama mawili hivi kuwa kati yangu na gari hilo. Gari hilo pia lilikuwa limeacha magari matatu kati yake na gari lenu. Tulifuatana hivyo hivyo mpaka kwenye taa za usalama barabarani za Jangwani.
"Hapo ndipo nilihakikisha kuwa huenda gari hili lilikuwa na jambo. Mlipoingia barabara ya Umoja wa Mataifa gari hili lilisita kidogo mpaka gari zingine zikalipigia honi kwani taa zingebadili kabla hatujapita. Inaonekana kulikuwa na ubishi. Baada ya hapo gari hili liliingia barabara ya Umoja wa Mataifa nami nikalifuata. Niliona nyinyi mnasimamisha gari kwenye ofisi za SANP. Nilitelemka na kufungua boneti ya gari langu kwamba limeharibika, huku nikifikilia kuwa lile gari litarudi.
"Nilichukua spana na kuanza kujifanya ninalishughulikia gari langu. Gari lile halikurudi. Mimi niliendelea kujishughulisha hivi kiasi cha nusu saa, wakati nyinyi bado mko ndani ya ofisi. Mara nilistukia gari moja linaingia pale gereji, kwa bahati lilisimama karibu tu na mimi. Ndani ya lile gari mlikuwa na watu wanne. Dereva wa gari hili alitoka na kuingia ndani ya ofisi ya gereji hii. Alikuwa amevalia vizuri sana. Nilimwangalia kwani alikwenda akazungumza na mfanyakazi aliyekuwa amekaa mezani akiandika risti na simu iko upande wake. Alizungumza na mtu huyu wakabishana kidogo kisha nikaona anatoa kitu kama shilingi moja akampa yule mfanyakazi. Halafu yule mfanyakazi akachukua funguo na kufungua kufuli la kwenye simu. Yule mtu akapewa simu akaanza kupiga. Mambo yote haya niliyaangalia kwa chati huku nikiendelea kujishughulisha na gari langu".
Eddy alitua akachukua sigara nikamwashia, akavuta kidogo kisha akaendelea.
"Sura za wale watu wengine ndani ya gari hazikuwa za kawaidana vile vile walikuwa na wasiwasi. Kila mara walikuwa wakigeuka kuangalia upande wa SANP. Yule mwingine alipomaliza kuzungumza na simu alikuja moja kwa moja akaingia ndani ya gari na kulizungusha. Mimi pale pale nikafunga boneti ya gari langu, maana tayari akili yangu ilikuwa imeshakuwa katika hali ya tahadhari nami nikageuza gari langu kuangalia barabarani. Hapo ndipo niliona mnatoka nje ya ofisi. Nikaona mmoja wa watu wale katika gari anainua "machine gun" kutoka chini na kabla hajaweka sawa nyinyi mlikuwa mmefika kwenye gari. Niliruka toka ndani langu na kuwapigia kelele. Nashukru kuwa mlinitii mara moja, kwani wakati ule ule mliporuka alimimina risasi pale pale mliposimama nikajua alikuwa mtu mwenye shabaha ya hali ya juu kwani gari lilikuwa likienda polepole.
"Mliporuka tu niliona mtu mwingine anatoa bomu la mkono na kuuma kifungo chake. Hapo ndipo nilipopiga kelele ya pili kisha nikarukia ndani ya gari wakati yule mtu anatupa hilo bomu na gari lao linaondoka kwa kasi. Ndipo na mimi nikaja na kusimamisha gari langu pale mlangoni baada ya ule mlipuko wa lile bomu. Pole sana bosi gari lako zuri sana limeteketea".
"Siku Eddy, nitapata jingine aina hiyo hiyo, nimetokea kupenda sana aina hiyo ya magari.
"Lo, inaonekana watu hawa wamejitayarisha vizuri sana", Veronika alisema kwa mshangao.
"Toka niliposikia jinsi walivyoiba zile silaha sikuwa na hamu nao tena. Nilijua ni watu wanaojua wanafanya nini. Ndio sababu niliwaasa hatari zitakazotokea toka mwanzo. Nafikiri sasa mnaamini mawazo yangu", hakuna aliyejibu; wote walinyamaza tu. Nafikiri walikuwa wakijutia kwa nini wamejiingiza katika janga hili.
"Vipi Eddy umepata habari zozote juu ya Kiki?", nilimwuliza.
"Kama nilivyokuahidi nimepata habari za kutosha".
Sisi wote tukawa tena tayari kumsikiliza huyu kijana na kusahau yote yaliyopita.
"Ehee hebu lete habari", nilimwambia.
"Nitaanzia toka ripoti nilizopata toka kwa makomredi wetu wa Soweto. Makomredi wetu huko wanakataa katakata kuwa hakukuwa na mtu mwenye jina au wa sura kama nilivyowaeleza huko Soweto. Wanasema mtu aliyetoroka gerezani kati ya wale waliokamatwa na kutiwa ndani, yuko huko huko Soweto na wanaye sasa hivi. Hivyo ni uongo mkubwa kuwa huyu mtu alihusika na matatizo ya Soweto. Inasemekana kuwa mara ya kwanza mtu huyu kuonekana Tanzania ni wakati alipofika Mbeya akiwa na hiyo hadithi yake kuwa ametoroka gerezani huko Afrika Kusini baada ya kutiwa ndani kutokana na machafuko ya Soweto. Habari hii aliitoa kwa ofisi ya Chama huko Mbeya na ofisi hiyo ndiyo iliyomleta Dar es Salaam baada ya kusema kuwa yeye ni mwanachama wa SANP. Hivyo alipofikishwa hapa alipelekwa kwenye ofisi za SANP ambako inasemekana aliwaonyesha kadi yake, hivyo katika hali ya kumsaidia wakampeleka kwenye Kamati ya Ukombozi ya OAU.
"Je umepata habari zozote kuhusu maisha yake hapa mjini".
"Ndiyo, vijana wetu wamefanya kazi nzuri sana. Wameweza kupata habari kuwa Kiki alikuwa mtu asiye na rafiki. Ila alikuwa na rafiki mmoja wa kike Mtanzania anayeitwa Zabibu Abeid. Wanasema msichana huyu aliingia hapa mjini toka Tanga miezi minne iliyopita kwani alikuwa amepatiwa kazi na Meneja wa Kampuni iitwayo Twiga Safari ambayo inashughulikia mambo ya watalii. Msichana huyu amesoma mpaka kidato cha Nne alichomaliza mwaka jana. Anasemekana kuwa na uuzuri wa pekee. Katika ripoti yao wanasema kuwa kama hujamwona msichana huyo basi hujamwona binti Tanzania. Hivyo baada ya Kiki kufanya urafiki na msichana huyu mrembo, muda wake na maisha yake aliyatoa kwa msichana huyu.
"Zababu anakaa mtaa wa Jamhuri, kwenye orofa karibu ya mzunguko wa mtaa wa Zanaki na Jamhuri. Yuko mwenye nyumba ya orofa ya Msajili wa Majumba. Jengo Nambari K orofa ya tatu, nyumba nambari 7a. Nyumba hii amepewa na waajiri wake. Inasemekana kuwa fanicha yote ya mle ndani imenunuliwa na Kiki pamoja na gari moja zuri aina ya Ford Mustang"
"Na huku Kiki alikuwa tarishi tu... nilimkata kauli Eddy.
"Ofisini alikuwa tarishi, lakini nje alikuwa na fedha nyingi za kutosha. Hivyo kwa nje alikuwa ofisa wa mkubwa katika Kamati ya Ukombozi ya OAU".
"Na ndio sababu aliweza kumpata msichana mrembo kiasi hicho?", Sherriff aliuliza.
"Bila shaka maana sura ya Kiki ilikuwa ya kupendeza sana hivyo sioni ajabu kumpata msichana mrembo kiasi hicho".
"Kwa hivyo zaidi ya msichana huyu maisha ya Kiki hapa mjini hayaeleweki".
"Ndiyo, Kiki hakuwa na rafiki mwingine zaidi ya Zabaibu, lakini muda mwingi alikuwa kwa Zabibu. Tumejaribu sana kupata habari nyingine zozote juu yake lakini tunashindwa. Huenda Zabibu anaweza kujua".
"Okejamani nafikiri nyinyi mnaweza kurudi matotelini kwenu. Ila mjihadhari sana maana hali ya sasa ni ya hatari, nitakuja kuwaona baadaye msitoke mpaka nimekuja. Eddy atawapeleka mkapumzike. Mimi nitakwenda kumwona Zabibu sasa hivi, nafikiri atakuwa ametoka kazini", niliwaeleza.
"Nafikiri atakuwa amerudi maana anatoka kazini saa kumi kamili", Eddy alinieleza.
"Twende wote", Veronika alinieleza huku akiniangalia kwa macho ya wizi.
"Hapana wewe nenda ukapumzike, kazi uliyofanya mpaka sasa inatosha. Usiwe na wasiwasi nitajiangalia".
Veronika alikuwa haamini kwenda kuonana na msichana mrembo namna hiyo peke yangu. Hiyo ndiyo ya kazi na dawa.
Waliondoka wakaniacha mimi nikienda maliwatoni. Baada ya kukoga na kubadili nguo, niliangalia saa yangu nikaona ni saa kumi na moja na nusu. Nilichukua bastola yangu nikaiweka ndani ya jaketi nililovaa, nikajiona nilikuwa tayari kupita kiasi kuonana na Binti Tanzania. Nilitoka nje nikafungua mlango, nikaenda mpaka Palm Beach ambako nilichukua teksi kunipeleka kwa Binti Tanzania.
 ITAENDELEA  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU