HOFU

SEHEMU YA PILI

HARARE

Ilikuwa tarehe 1 Aprili, Juma moja baada ya Mkutano uliofanywa na Maafisa wa Makaburu na vikaragosi vyao Mjini Port Elizabeth. Siku hiyo kulifanyika mkutano mwingine. Mkutano huo ulikuwa kati ya watu tofauti na wale Makaburu, mikutano yao ilikuwa na uhusiano. Mkutano huu ulifanyika mjini Harare, Zimbabwe, katika ofisi za wapigania uhuru wa Afrika Kusini. Tofauti na ule mkutano wa Makaburu uliofanyika usiku, mkutano wa wapigania uhuru ulifanyika mnamo saa nne hivi asubuhi. Mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Chama cha kupigania uhuru. Waliohudhuria mkutano huu ni yeye Mkuu wa Upelelezi, Mkurugenzi wa Upelelezi na Serikali ya Zimbabwe pamoja na kijana mmoja aitwae Bon Sipele.

Huenda itakuwa kwa faida yako kama nitakueleza kidogo juu ya kijana huyu mradi usiniite mmbeya. Lakini kwa kuwa mimi huwa sisengenyi, fahamu kwamba mambo nitakayokueleza ni kweli tupu. Kijana Bon Sipele alikuwa na umri yapata miaka ishirini na nane. Kijana huyu alikuwa mzalendo wa Afrika Kusini ambaye alizaliwa katika kijiji cha Soweto. Kijana huyu alianza kujulikana kama mwana mapinduzi akiwa bado mbichi. Alipokuwa na umri yapata miaka kumi na tisa, yeye na wenzake baada ya kumaliza darasa la kumi na nne walivamia mitaa wakiwa na mawe na chupa kuupinga utawala wa kibaguzi wa Makaburu. Serikali ilijibu kuwa kuwauwa baadhi ya vijana hao na kuwatia ndani wengine. Bon pamoja na wenzake walipata bahati ya kutoroka. Huku wakisaidiwa na wapigania uhuru, waliweza kuingia Zambia na hatimaye Tanzania. Bon alijaa uchungu kutokana na vitendo vya kikatili vya Makaburu. Hivyo aliapa kuwa angejitoa mhanga kupigania uhuru wa nchi yake.

Bon alipewa nafasi ya kwenda nje ambapo alipata mafunzo ya kijeshi kijana huyu alipitia mafunzo magumu huko Urusi, China, Cuba na Korea Kasikazini. Aliporudi kutoka kwenye mafunzo alikuwa na ujuzi wa hali ya juu. Aliombwa kukaa katika ofisi za wapigania uhuru zilizo Tanzania ili awe mkuu wa idara ya uendeshaji vita. Lakini, Bon alikataa kazi hiyo kwani alitaka kuishi katika hali halisi ya vita. Hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka Msumbiji kupambana na Wareno na Makaburu huko msituni. Baadaye aliweza kuhujumu viwanda kadhaa, mitambo ya umeme pamoja na Reli ndani ya Afrika Kusini. Bon aliwatia homa Makaburu.

Vyama vya wapigania uhuru viliona Bon alikuwa anafaa kuwa mpelelezi ili awakabiri majasusi wa Makaburu kutokana na ujasili wake na mafunzo aliyokuwa nayo. Baada ya muda siyo mrefu Bon alitokea kuwa mpelelezi aliyesifika na kuogopwa katika sehemu hii ya Kusini mwa Afrika. Makaburu walimhala kutokana na hasara kubwa aliyowatia. Serikali ya Afrika Kusini ilikuwa inamtafuta bila kufanikiwa. Kijana huyu ndiye Bon Sipele.

Tunarudi kwenye mkutano uliokuwa ukifanywa na watu hao watatu.

Mkurugenzi wa upelelezi wa Zimbabwe ndiye alikuwa mtu wa kwanza kutoa hoja yake. Alisema, "Tumekusanyika hapa ili niweze kuwaeleza ama sote kuzungumza suala muhimu. Habari kuhusu suala hilo nimezipata kutokana na kazi yangu, suala hili linawahusu nyinyi pia. Ndio sababu nimeona ni vizuri niwahusishe".

Alimeza mate kulainisha koo akaendelea, "Mnakumbuka kuwa hapa majuzi watu wetu walifanya operesheni kwenye sehemu ya Beitbridge katika mpaka wetu na Makaburu. Mtakumbuka pia kuwa watu wetu waliweza kuvunja kundi la Majasusi waliokuwa wanafanya ujahili dhidi ya nchi yetu kutokana na amri za Makaburu".

"Tunakumbuka", walijibu kwa pamoja.

"Katika operesheni hiyo", Mkurugenzi aliendelea, "Tuliweza kuwakamata Majasusi ishirini. Baada ya kuyakamata, vijana wetu kama mjuavyo walishughulika kikamilifu. Baada ya kuhojiwa mmoja wao alitoa taarifa ambayo imetufanya tuwe macho. Kwa sababu hiyo nimelazimika kuwapa habari hizi. Kutokana na ripoti niliyopata ofisini kwangu ni kwamba, Makaburu wamebuni mpango wa kukomesha mashambulizi dhidi yao. Utekelezaji wa mpango huo ni kwamba Makaburu watatoa kipigo kitakatifu ambacho kitamaliza kabisa nguvu za wapigania uhuru kiasi kwamba wale watakaobahatika kubaki hawatathubutu kufanya mashambulizi dhidi yao. Vile vile kuna mpango wa kushambulia nchi yetu baada ya kipigo dhidi ya wapigania uhuru. Sasa kama inavyofahamika, viongozi wa wapigania uhuru wamesambaa katika nchi mbali mbali. Wako kwenye nchi zilizo katika mstari wa mbele. Vilevile wako katika nchi kadhaa za Afrika na hata nchi rafiki za Ulaya. Hivi tumefikiri sana juu ya hali hii lakini hatujapata ufumbuzi. Ndio sababu imeonekana ni vizuri tutafute ufumbuzi wote kwa pamoja".

Mkurugenzi wa upelelezi wa Zimbabwe alipomaliza kusema chumba kikajaa ukimya.

Baada kimya kirefu kilichoambatana na kutafakari maelezo hayo, Bon alisema, "mtakumbuka tarehe 21 machi, siku ambayo yalitokea mauaji ya kikatili katika kitongoji cha Langa. Siku mbili baadaye niliweza kujipenyeza na kuingia Afrika kusini. Wakati huo wazalendo walikua wamepamba moto wakiwaua polisi wa kiafrika waliomo katika jeshi la polisi makaburu. Mimi na watu wetu walio ndani ya Afrika kusini tuliweza kumpata mmoja wa polisi weusi aliyekuwa anakimbia. Kabla wazalendo hawajamfikia sisi tulimkimbiza na kumshika. Lakini tulimfanya asituogope kwani tulimridhisha na akaamini tulikua upande wake. Tulimchukua na kumficha.

"Tulipomwuliza maswali alitwambia kuwa watu weusi walikuwa hawajui kwamba Makaburu walikuwa hawawezekani. Kwamba weupe walishaamua kuua weusi bila kujali mpaka ghasia ikome kabisa. Vile vile nchi zote zinazosaidia wapigania uhuru zitakiona cha mtema kuni  kwani sasa hivi makaburu walo jeshi liitwalo Gongo la chuma'ambalo halijawahi kutokea duniani. Sasa hivi jeshi hilo lipo tayari kufagia aina yeyote  ya upinzani baada ya kutayarishwa kwa muda wa miaka kumi. Nakumbuka niliporudi nilileta ripoti hii. Sasa ukilinganisha ripoti yangu na maelezo aliyotoa mkurugenzi sasa hivi ni dhahiri kwamba yanaoana. Hii inaonyesha ni kwamba ni kweli Makaburu wanao mpango huo."

"Hata mimi naafiki kuwa yaliyosemwa ni kweli," alisema mkuu wa upelelezi wa wapigania uhuru. "Lakini kitu ambacho ni lazima kukiweka maanani ni hicho kipigo wanachotishia watakifanya. Je kipigo hicho kitafanywa wapi; lini na kwa namna ipi?"

Hapo mkurugenzi wa upelelezi wa Zimbabwe aliinua kichwa akasema, Hata mimi jambo hilo ndilo linalonipa wasiwasi maana kutokana na maneno ya jasusi tuliyemteka, nchi zetu zitaanza kushambuliwa mara tu baada ya kipigo hicho. Huenda wanataka kutupumbaza ili watushambulie wakati sisi tunasubiri watoe kipigo kwa wapigania uhuru  kwanza . Hata hivyo ni lazima tupate ufumbuzi wa suala hili."

"Mnajua kwamba sasa hivi makaburu wana wasiwasi mkubwa na wanatuogopa. Hivyo sasa hivi hawana njia yeyote ile bali kutafuta njia za kututeketeza. Uchumi wao umeanguka. Hivi juzi juzi tu wafanyabiashara wa Uingereza waliitisha mkutano huko mjini Leeds na kuwataka wafanya biashara wa Afrika Kusini wajaribu kutetea haki za wafanyakazi weusi. Waliwataka pia waibane Serikali yao ili iwaruhusu weusi kufanya biashara kwenye sehemu wanazoishi weupe. Vile vile waliwataka wapinge vikali siasa ya kibaguzi ili Waingereza waendelee kupeleka rasilimali zao huko Afrika kusini. Hivyo makaburu wamehaha kwani msimamo huo umewauma sana. Ni kama mjuavyo, mtu anayehaha anaweza kufanya jambo lolote. Hatuna budi kuwa macho kabisa kwani hali hii imewafanya makaburu kujizatiti. Sasa hivi wamebanwa sana ndani na nje".

"Nilikuwa nikifikiri sana sasa hivi", Bon alianza kusema na hapo hapo wale Wakuu wawili wakageuka kumsikiliza yeye. Walikuwa wanajuwa kuwa Bon alikuwa kijana mwenye akili sana na ubongo wake ulifanya kazi kama komputa. Kila lilipotokea tatizo, Bon aliweza kutoa ufumbuzi sahihi. Ndio sababu alihusishwa katika mikutano ya ngazi za juu kama huu.

"Mnajuwa kuwa mwezi ujao kutafanyika mkutano wa pekee wa wapigania uhuru wote wa Afrika Kusini huko Tanzania, baada ya ule uliofanyika mwaka 1969. Kuna uwezekano kwamba Makaburu wameshapata habari na wanajitayarisha kutushambulia huko. Maana kama wakiweza kutekeleza tishio lao hilo la kipigo, wakateketeza wajumbe wote kwenye mkutano huo. Basi hivyo wanavyojigamba itakuwa ni sahihi kabisa. Viongozi wetu wote kutoka sehemu mbalimbali duniani watakuwapo pamoja na watu wale wanaotuunga mkono".

Wakuu wale walimwangalia Bon na kumsikiliza kwa makini.

"Bila hata kuzungumza zaidi, nafikiri Bon amesema ukweli kabisa", Mkurugenzi alisema huku akikiri rohoni kuwa kweli Bon alikuwa kijana mwenye akili za kuzaliwa. "Hata mimi nafikiri hilo ndilo jawabu lake, asante sana Bon. Lakini kuna jambo moja, Tanzania iko mbali sana. Sijui watatumia mbinu gani?", aliuliza Mkuu wa Idara ya Upelelezi huku akiwaangalia wale wajumbe wawili.

Akidakia haraka kujibu swali hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Zimbabwe alisema, "Usiwachezee hawa Makaburu. Wanao uwezo wa kufanya jambo lolote. Wako mbali na Tanzania ndio, lakini wakijigamba ujuwe wanao mpango madhubuti. Hivyo ni juu yetu kujiweka tayari kutekeleza jukumu letu".

"Jibu tumeshalipata", alipaza sauti Mkuu wa Idara ya Upelelezi. "Hakuna haja ya kuhangaisha vichwa vyetu zaidi. Lililobaki ni kwamba mimi nitaitisha mkutano wa wenzangu niwaeleze tuliyogundua. Halafu tuzungumzie nini la kufanya kabla ya mkutano huo kuanza. Makaburu wasije wakatuchezea kama watoto wadogo".

"Hata mimi nafikiri hilo ndilo wazo la busara wazee wenzangu. Tusipochukua hatua za tahadhari tutaadhirika." Bon alijibu huku akili yake ikiwa mbali kwani alishachekecha akilini mwake na kuona jinsi jukumu hili lilivyokuwa  gumu na la hatari sana.

"Yote niachie mimi alirukia mkuu wa idara ya upelelezi. Leo hii nitaitisha mkutano ili mpango yote ya tahadhari ikamilike. Ahsanteni sana. Mimi nitawajulisha kila hatua ambayo tutafikia. Nitawapa habari zote kuhusu matokeo ya mkutano. Bon usiondoke hapa mjini. Kila wakati nataka kujua mahali utakapokuwa. Ninaweza kukuhitaji ghafla. Kuhusu wewe ndugu mkurugenzi, mimi nitakujulisha tarehe ya mkutano hapo baadaye kwani ni lazima uwepo."

Mkutano ulifungwa na watu watatu hao wakaagana


INAENDELEA


MAONI USHAURI WASILIANA NASI 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU