HOFU

SEHEMU YA TATU

NAIROBI

Mike Maina aliingia ofisini kwa mkubwa wake wa kazi akiwa ameshika jalada mkononi. Maina alikuwa ofisa upelelezi katika idara ya upelelezi nchini kenya. Kijana huyu alikuwa anategemewa sana na serikali ya Kenya kwa kazi yake kubwa ya kulinda usalama dhidi ya hujuma za kisiasa, kijeshi na kiuchumi. Alikwisha tokomeza mipango mingi dhidi ya serikali.

"Ehe, hebu nieleze Maina ." Mkurugenzi wa upelelezi alisema, "Ingawa nimeitwa huko Ikulu, afadhali tuzungumze kwanza ndiyo nielekee huko baadaye."

Katika kumkumbusha mkubwa wake wa kazi, Mike alitasua midomo yake na kusema, "Unakumbuka mwaka 1981 wakati mamluki, wakiongozwa na Michael Hoare, walipojaribu kuiangusha serikali ya visiwa vya Shelisheli; halafu wakashindwa?"

"Ndivyo, kwani vipi? Wanataka kuishambulia Shelisheli tena?"

"Hapana. Unakumbuka serikali ya Shelisheli iliilaumu serikali ya Kenya kwa kuhusika; na serikali yetu ikakanusha vikali madai hayo? Unakumbuka serikali hata hivyo, ilituamuru tuchunguze suala hilo. Unakumbuka kuwa mimi ulinipa kazi hiyo?".

"Nakumbuka sana, mike."

Ripoti yangu ilionyesha kwamba, ingawa serikali haikuhusika, kuna watu binafsi au hata wakazi tu waliohusika. Kutokana na ushahidi tulioupata watu wengine wenye heshima wamepoteza kazi zao. Wakazi wengine hata wamefukuzwa nchini."

"Nakumbuka."

"Wakati wa upelelezi wetu kuna mtu ambaye tulimshuku sana. Lakini kutokana na kukosa ushahidi thabiti, hakuchukuliwa hatua. Hata hivyo jalada lake lilibaki wazi. Niliweka kijana kuchunguza mienendo yake. Vile vile nilikuwa nimemwagiza achimbe historia ya maisha yake toka kuzaliwa kwake mpaka hivi leo. Mtu huyu anaitwa Peter Gerrit. Yeye ni mfanya biashara. Anayo kampuni ya kuhudumia watalii ijulikanayo kama Kinyonga Tours and Safaris."

"Lo, jina lenyewe linasisimua," alisema kwa mzaha mkurugenzi.

"Sasa jana huyu kijana wetu aliniletea ripoti ambayo ilinifanya niwe na wasiwasi mkubwa kiasi kwamba lazima nikueleze. Kwa muda wote huu kijana wetu alikuwa anampeleleza mtu huyu."

"Mtu huyu anajulikana katika idara ya uhamiaji kama Mjerumani. Vile vile Idara ya uhamiaji inayo taarifa kwamba biashara hii ya kuhudumia watalii aliianza huko huko Ujerumani. Baadae aliamua kuja kuianzisha hapa nchini Kenya. Hayo tu ndiyo wanayoyafahamu maafisa wa Uhamiaji. Lakini sisi kitu kinachotugutua ni kwamba siku ambayo askari wa kukodiwa walipovamia Visiwa vya Shelisheli, huyu Peter alikuwapo. Na wakati askari hao walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Victoria. Maana ripoti inasema Peter alikuwa uwanjani hapo. Ni baada tu ya kugutushwa na mapigano yaliyotokea pale wakati Peter alipojisalimisha kwa majeshi ya usalama ya shelisheli.

"Wakati wa kuhojiwa Peter alieleza kwamba alikuwa hapo uwanjani kusindikiza rafiki zake waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la India ambayo ilitekwa nyara. Askari wa Shelisheli walipoangalia pasipoti yake na kuona kuwa yeye ni mkazi wa Kenya na mfayabiashara ya utalii walimwachia mara moja. Wakati wa uchunguzi wetu tulipata fununu kuwa huyu Peter alikuwa kwenye uwanja wa ndege kwa nia ya kuwapokea askari wa kukodiwa. Lakini kwa kuwa tulikosa ushahidi wa kutosha, hatukuweza kumchukulia hatua, bali tulibaki tunamtuhumu tu. Wewe unajua tena jinsi mahakama zetu pamoja na serikali vinavyotaka haki itekelezwe. Heri kumwachia huru mhalifu kuliko kumwadhibu yule asiye na hatia.

"Sasa katika uchunguzi uliofanywa na kijana huyu kwa muda wa miaka yote hii. umegundua mambo yenye kututia wasiwasi. Kwanza kijana wetu amegundua kwamba Peter hakuzaliwa Ujerumani, bali yeye ni mzaliwa wa Afrika kusini. Ila mjomba wake alikuwa anaishi Ujerumani. Ndiye huyo huyo aliyemchukua Peter na kumpeleka huko. Aliishi na kukulia huko ambako alipata masomo. Alipofikia umri wa miaka ishirini alirudi Afrika kusini katika mji wa kwao wa Pietermaritzburg.  Inasemekana aliisha fanya kazi kwa Michael Hoare kama askari wa kukodiwa. Baada ya hapo alipotea na kisha akaibuka huko Ujerumani. Wakati huo mjomba wake alikuwa ameanzisha kampuni ya kuhudumia watalii ambayo alijiunga nayo. Baada ya muda kitambo, ndipo akaja Kenya. Sasa unaweza kuona kuwa kuwako kwake Shelisheli hakukuwa kwa bahati tu ila kwa sababu maalumu.

"Zaidi ya hayo, kijana wetu amegundua kitu ambacho kimetia wasiwasi na pia kunifanya mimi nifanye hima . Nikwamba kwa muda wa majuma mawili sasa kumekuwa kunakuja wazungu wanaume wawili wawili kila baada ya siku tatu. Wazungu hao wanakwenda nyumbani kwa Peter huko Red hill kwenye njia ya kwenda Limuru. Kijana wetu anahisi kwamba baada ya hao wazungu kuingia nyumbani hawatoki nje tena. Wako kama watu sita sasa. Unajua kuwa analo shamba kubwa na pia nyumba kubwa. Katika shaba hilo kuna nyumba za wafanyakazi. Sasa tunajiuliza hivi: kama kweli hawa ni wageni wa kawaida, kwa nini hawaonekani angalau kutembea tembea au hata kwenda mjini? kwa nini wasithubutu hata kuzurura hapo kwenye shamba?"

"Huenda wanatembea usiku," alipendekeza mkurugenzi.

"Kama kweli ni usiku, kwa nini usiku? aliuliza Mike.

"Nafikiri unayo sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi. Kufuatana na maelezo yako inabidi mtu huyu apelelezwe kikamilifu zaidi kwani huenda akawa na jambo. Bali kama mtu huyu anayo mahusiano na serikali ya makaburu, yafaa apelelezwe kwa uangalifu na tahadhari zaidi. Akigundua kuwa anachunguzwa si ajabu akateleza tena kama alivyofanya hapo kwanza. Hivyo, kwa baraka zangu, nakuruhusu uendelee na kazi ya kumpeleleza ili tujuwe hasa anapanga kufanya kitu gani. Umesema kuwa kipindi fulani alikuwa haonekani na haikujulikana alikuwa wapi. Basi ni dhahili kuwa anaweza kuwa jasusi wa makaburu ambaye alikuwa mafunzoni. Hapa inawezekana kaja kikazi, kwa hiyo chunga sana mtu huyu kwani anaweza kuwa hatari|".

"Asante. Nitafanya hivyo na kisha nitakujulisha maendeleo ya kila siku".

Mike Maina alichukuwa jalada na kutoka nje ya ofisi ya mkubwa wake.

Mike alipofika ofisini kwake alimwambia Katibu Muhitasi wake amuite kijana Mwaura. Kwa muda wa miaka yote hii Mwaura ndiye alikuwa akimpeleleza Peter.

"Mwaura", Mike alisema mara Mwaura alipoingia ofisini kwake. "Nimezungumza na Mzee na tumekubaliana kwamba tuendelee na upelelezi wetu. Sasa nitakuongezea vijana wengine na ninataka ripoti juu ya maendeleo yote ya mtu huyu, kila kitu atakachofanya, na mahali atakapokwenda".

"Nashukru sana, Bosi". Mwaura alijibu. "Nafikiri ukinipa vijana wawili, kama vile Onyango na Kipukoachi, kazi itafanyika vizuri".

"Maombi yako yatatimizwa mara moja, unafanya kazi nzuri Mwaura. Kuna haja ya idara kufikiria kuongeza maslahi yako".

"Asante sana, Bosi, kazi kwanza".

"Ningependa kazi hii ianze mara moja leo hii na mhakikishe kwamba Peter hapati mwanya wa kufanya jambo lolote dhidi yetu", alisema Mike.
"Kitu ambacho nimekosea bosi ni kwamba tangu asubuhi sikuweka mtu wa kuendelea na uchunguzi juu ya maendeleo ya mtu huyu. Katika muda huu wa masaa tisa huende amefanya majambo", Mwaura alijilaumu.

"Tusililie maji yaliyomwagika. Kuanzia sasa hivi fanya kazi kama kawaida".


 ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU