NJAMA


SURA YA KUMI

"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"

Tulipoingia ofisini tulikuta wanatusubiri kwa hamu.

"Chifu anataka kukuona", Eddy alinieleza.

"Mwambie Maselina haiwezekani, nitamwona baadaye. Sasa hivi hakuna nafasi maana tukichelewa hapa mambo yote yatakuwa yameharibika. Mwambie asitoke ofisini mpaka saa sita. Asipotuona ajue basi makubwa yametupata, akituona ajue tumerudi na ushindi. Umesikia Linda?".

"Nimesikia".

"Sherriff, Eddy na Isaack mko tayari kwenda kwenye uwanja wa mapambano", niliwauliza.

"Bila wasiwasi", walijibu kwa pamoja.

"Na mimi?", Zabibu aliuliza.

"Wewe utabaki hapa na Linda. Tutaonana saa sita kama tukiwa salama.

"Mimi nataka twende wote, kama ni kufa tukafe wote"

"Kwanini unataka ukafe naye kwani yeye ni nani wako", Linda alimuuliza kwa ukali.

"Acheni upuuzi, nyinyi bakini hapa, haya mambo ya kuleteana haraha, mtatupa mkosi bure".

"Twendeni zetu", niliwaeleza wenzangu nasi tukaondoka ndani ya ofisi na kuingia ndani ya gari.

Eddy ndiye alichukua usukani na Isaack akaa naye mbele. Mimi na Sherriff tulikaa nyuma.

"Twende moja kwa moja nyumbani kwangu tukachukue silaha zaidi. Halafu tutapita nyumbani kwa Eddy kuchukua silaha tulizoacha kule. Tuna saa moja ya kujitayarisha kabla ya kuingia kwenye uwanja wa mapambano.

"Itabidi tutoke kwa Eddy mnamo saa tatu na nusu. Hii itatupa nafasi ya kuwa nje ya nyumba ya Sikazwe saa tatu na nusu. Maana ndipo yeye ataondoka kuelekea huko walikoziweka silaha".

"Kisha niliwaeleza mazungumzo yote niliyoyasikia kati ya Harrison, Sikazwe na Max.

Kwa hiyo tutakuwa watu wanne tukikabiriana na zaidi ya watu mia", Isaack alisema kwa mshangao.

"Ndiyo sababu watu kama sisi tunaitwa ni hatari. Siku moja Isaack utakapokuwa komando kama mimi utakuwa na uwezo wa kukabiliana na maadui mia peke yako. Kwa hiyo mimi naona kama ni afadhali sana kama tuko watu wanne dhidi ya watu mia. Tukitumia hamasa na maadili na moyo wa kimapinduzi sina shaka Mungu atatusaidia na tutashinda na kufichua hizi njama za Makaburu na mabeberu ya jumuia ya ulimwengu", niliwatia moyo.

"Nikiwa niko na wewe bosi, huna sina wasiwasi wowote", Eddy alisema.

"Hata mimi", Sherriff aliongeza.

"Kama ni hivyo, hata mimi ninafurahi kuwa nina jeshi lililohai na kamanda wake".

"Kutokana na ulivyoeleza komredi, watu hawa walikuwa wamepanga kuzichukua silaha hizi kwa meli ndogo kama spea ziendazo Mtwara", Sherriff alieleza.

"Sawa'.

"Baada ya kufika Mtwara wangefanya nini?", aliuliza.

"Swali zuri. Watu hawa walikuwa wamejitayarisha vizuri sana. Hili kampuni kubwa la Euro-Afro lina meli zake. Meli yake moja itakuwa inapakua mizigo Mtwara kuingia kesho. Hivyo walikuwa wamepanga kutoa silaha hizi kwenye hii meli ndogo na kuzipakia katika meli kubwa ambayo ingelikwenda kuzitelemsha Afrika Kusini...

"Mipango yote hii iko ndani ya faili nililompa Linda ampelekee Chifu. Meli hiyo ingekuwa inangojwa bandari ya East London kutelemsha zana hizi. Sikazwe angeondoka kesho kwa ndege akidai anakwenda Botswana lakini angekwenda Pretoria ambako mimi nafikiri wangemtia ndani mana nia yao haikuwa kufanya kama walivyomdanganya ila tu walitaka awasaidie kuziiba silaha kwa sababu ilikuwa rahisi kwake".

"Kwa hiyo mpaka sasa Sikazwe anakazana bure tu", Isaack alisema huku akicheka.

"Wajinga ndio waliwao", Eddy alijibu. Tulifika nyumbani kwangu, nikabadilisha mavazi kuvaa mavazi ya kikazi yaani koti na suruali yenye mifuko mingi ili kuweza kubeba silaha za kutosha.

Baada ya hapo tukaelekea kwa Eddy ambako tulijitayarisha kwa kikamilifu. Kwa bahati nzuri tulikuwa na majoho mekundu matano tuliyoyateka kwa hawa majahili. Kila mtu alichukua joho moja, maana hii ingetusaidia kuwaingilia wakidhani ni wenzao. Tulipata vile vile kofia tatu ambazo niliwagawia wenzangu. Nakwambia tulipojaribu kuvaa tulifanana na wao kabisa. Hivyo tulichoomba ni kuwa tukute bado hawajabadili mvao wao unaowatambulisha. Baada ya kuona kila kitu kimekamilika tulijiandaa kuondoka huku roho zetu zikipiga haraka haraka.


ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU