NJAMA

SURA YA TISA

MAPAMBANO NA VIBARAKA

Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu za asubuhi wakati nilipokuwa nakaribia kumaliza kunyoa ndevu. Nilikiangakia kidevu changu kwenye kioo nikaona nilikuwa sijajinyoa vizuri. Kila wakati nilipokuwa na mawazo mengi kitu kama hiki kilikuwa kinanitokea. Lakini hata hivyo nia yangu nionekane nadhifu hivyo nilichukua tena mashine ya ndevu na kuanza kujinyoa. Nilipoona mambo yanakuwa mazuri kwenye kidevu changu, nikaanza kuoga.

Nilitoka maliwatoni na kurudi chumbani nilikokuwa nimelala. Zabibu bado alikuwa hajaamka, hivyo nilivaa taratibu ili nisije nikamshtua toka usingizini. Alikuwa na sura ya mtoto mchanga isiyokuwa na maneno. Nilimwangalia huku nikivaa. Nilipomaliza kuvaa na kuweka kila kitu changu tayari, nilikwenda nikambusu Zabibu usingizini nikaondoka ndani ya chumba na kufunga mlango taratibu.

Niliwakuta Sherriff na Eddy wamekaa sebuleni wanakunywa kahawa.

"Karibu bosi, habari za kuamka?".

"Nzuri", nilijibu, nikaa kwenye kiti cha meza ya kulia nikavuta kikombe cha chai na kujiwekea kahawa ya kutosha.

"Lazima iwe nzuri", Sherriff alijibu huku akitabasamu nikajua alikuwa na maana gani kusema hivyo.

"Usinionee wivu".

"Lazima tukuonee wivu, maana chuma kama hicho si cha kawaida.

"Bosi, vijana wameleta habari kama ulivyoomba", Eddy alisema huku akibadilisha mazungumzo.

"Ndio, wamesemaje.

"Wamesema hawakuweza kumwona Sikazwe mpaka saa tisa za usiku. Walimpata akitokea kwenye barabara ya Bagamaoyo na akielekea nyumbani kwake. Hawakuweza kujua alikuwa anatokea wapi. Na mpaka sasa hivi bado yuko nyumbani amelala. Wamenieleza kuwa ofisi za SANP hazifanyi kazi siku za Jumamosi. Na kama unavyojua leo ni Jumamosi".

"Basi waambie waendelee na wahakikishe kuwa hawapotezi hata dakika moja. Atakapoondoka nyumbani nataka kujua anaelekea wapi. Sawa?".

"Hamna taabu".

"Sasa hivi mimi ninakwenda kumwona Chifu maana nilipata habari kuwa anataka ripoti toka kwangu, maana anasumbuliwa sana na Serikali".

"Nafikiri Sherriff anaweza kuendelea kupumzika hapa, mimi nitakujulisha wakati nitakapokuhitaji".

"Sawa", alijibu Sherriff kwa mkato.

"Naomba unipatie 'machine gun' inayoweza kuchukua risasi zaidi ya mia. Niliwahi kuzitumia nilipokuwa jeshini.

"Aina gani".

"Zilizotengenezwa Urusi".

"Zipo".

"Oke niletee moja ya aina hiyo. Ikiwezekana tuma mtu aniletee mapema kusudi niishughulikie".

"Hamna taabu, utapata.

Baada ya kuzungumza na hawa vijana tuliagana kisha nikaondoka. Nilitembea kwa mguu mpaka nyumbani kwangu, ili nikabadilishe nguo. Nilifika nikafungua mlango, nikaangalia saa yangu nikaona ilikuwa yapata saa mbili kasoro robo. Nilipoingia tu ndani, roho yangu ikashtuka lakini nilikuwa nimechelewa, nilipigwa na mfuko wa mchanga kisogoni nikaanguka.


ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU