HOFU

SURA YA SITA

MAMBO

Ilikuwa sikukuu ya Idd. Siku ile Willy na Chifu walipozungumzia mipango kujidhatiti kiulinzi ili kuzuia uwezekano wa majasusi wa makaburu kuingia nchini bila kujulikana na kuvuruga mkutano wa wapigania uhuru. Wakati huo huo majasusi tayari wameshaingia mjini Arusha na tayari walikuwa wanapumzika nyumbani kwa F.K wakiwa tayari kuanza kazi. Hiyo ilikuwa na maana kwamba usiku wa jana yake F.K na Tondo kwa upande wa Tanzania na Peter kwa upande wa Kenya walikuwa wameweza kuwaingiza nchini kwa siri. Zaidi ya hayo, majasusi wa Makaburu walikuwa wameingiza mizigo yao yote. Asilimia mia tisini ya mizigo hiyo zilikuwa ni silaha za aina mbali mbali na vyombo vya kisasa vya kufanyia ujasusi.

Kwa kuwa gari la F.K lilikuwa halipekuliwi, safari yao kutoka mpakani hadi Arusha haikuwa na kisanga chochote. Pamoja na ulinzi mkali uliowekwa kwenye vizuizi njiani, watu hao waliweza kupita. Kila alipofika kwenye kizuizi F.K alitoa kichwa chake nje tu na maafisa wa polisi kimzaha walimpigia saluti na kumwashilia aendelee. Hivyo sifa za kinafiki za F.K ziliweza kusaidia majasusi wa makaburi wa Afrika Kusini kuingia Tanzania tayari kutoa kipigo dhidi ya wapigania uhuru wa Afrika huru kwa ujumla.

Baada ya kuvuka mpakani, Peter alirudi Nairobi akiwa ameridhika kuwa nusu ya kazi yake ilikuwa imefanyika tayari.

Mchana wote wakati majasusi walipokuwa nyumbani kwa F.K walikuwa wanajitayarisha walisafisha silaha zao, na wale Ninja wawili walifanya mazoezi madogo madogo. F.K alikuwa amewapeleka likizo wafanyakazi wake wote hivyo aliacha nyumba yake nzima itumike na majasusi. Walikuwa wakijipikia na kujifanyia mambo kadhaa. Kama nilivyoeleza hapo awali, nyumba ya F.K ilikuwa imejengwa kwa madhumuni kama hayo. Hata mtu angefika kwa F.K asingeweza kugundua kuwepo kwa majasusi kwani walikuwa wanatumia vyumba vya siri.

Ilikuwa yapata saa za jioni wakati F.K alipowakusanya majasusi ili kuwapasha habari.

"Sasa hivi nimepata habari kupitia kwenye chombo cha kupashana habari kilicho chumbani kwangu", F.K alisema "Wakubwa wetu wamepata habari kuwa mpelelezi mashuhuri wa wapigania uhuru, Bon Sipele na mpelelezi mwingine mashuhuri kutoka Zimbabwe, Rocky Malele, wameondoka leo mchana mjini Harare na Ndege ya shirika la ndege la Tanzania wakiwa njiani kuelekea Arusha. Taarifa niliyonayo inasema kwamba watu hawa ni hatari sana. Hivyo ni lazima wauawe, la sivyo watatia dosari katika mipango yetu. Vile vile nimeelezwa kuwa Paul na Fouche wanawafahamu watu hawa".

Nyumbani kwa F.K kulikuwa na chombo kupashana habari cha hali ya juu sana. Chombo hicho kilikuwa kinapokea habari kutoka kwenye Setelaiti. Setelaiti hiyo iliwekwa angani na Makaburu wa Afrika Kusini wakisaidiwa na Marekani. Kazi yake kubwa ilikuwa kupashana habari za kijasusi. Hivyo mawasiliano kati ya F.K na mabwana zake yalikuwa hayapitii njia za kawaida. Ndiyo sababu aliweza kupashana habari na hao bwana zake bila kugunduliwa na vyombo vya upelelezi vya Tanzania.

"Ndio, tunawafahamu vizuri sana", Paul alijibu.

"Kama kweli hawa watu wanakuja", Fouche alieleza "ni lazima kujiweka tayari. Hao mimi nawajuwa siyo mchezo. Kama maagizo yanasema wauawe mara moja ni sahihi kabisa. Wakisha fahamu na kuwa na wasiwasi wanaweza kufanya kazi yetu iwe ngumu. Ujuzi na uwezo wao ni mkubwa. Mimi naamini kuwa hata kama wanatutilia wasiwasi, bado hawajui kama tayari tumeingia. Wao wanatarajia sisi tuingie kwa ndege. Hivyo watajishughulisha na kuchunga viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro".

"Kama wameweza kutuma wapelelezi mashuhuri kama hao", John aliasa "Ina maana hata serikali hizi zinahisi kitu".

"Lazima. Lazima mjue nchi hizi sasa hivi siyo mchezo", F.K alionya "nchi hizi zina uwezo mkubwa wa kipelelezi. Hivyo mfahamu kuwa mmekuja kupambana na watu wenye ujuzi kama wenu hivyo msifanye mchezo".

"Watafika saa ngapi watu hawa", Geoger aliuliza. Yeye ndiye alikuwa mkubwa wa kikosi hiki na pia mmoja wa wale ninja wawili. Yeye na Dave walikuwa na uwezo mkubwa kuliko wale wenzao.

"Ndege hiyo inatarajiwa kufika hapa saa tatu na nusu", F.K alieleza "Lakini nimepata habari sasa hivi kutoka kwa watu wangu walioko uwanja wa ndege kwamba kutokana na wingi wa wageni kutakuwa na ndege mbili. Kama mnavyojuwa mpaka sasa wageni wengi wameshaingia. Hadi kufikia kesho kila mjumbe anatakiwa awe hapa kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano hapo kesho kutwa. Hii ina maana kwamba lazima tufunge kazi takatifu mnamo muda wa masaa sabini na mbili yajayo".

"Hiyo kazi itafungwa katika muda huo wala usiwe na shaka", George alijibu.

"Sasa umeamua nini juu ya watu hawa wawili Dave, ambaye wenzake wanamwita Devil, yaani shetani, aliuliza.

"Watu hawa lazima wauawe usiku huu huu". George alijibu "Kitendo hicho kitawafanya adui wapagawe. na hivyo kutupa sisi nafasi nzuri zaidi kufanya kazi yetu".

"Hali ya ulinzi huko uwanja wa ndege ikoje", aliuliza.

"Ilinzi mkali sana", F.K alijibu. "Na siyo tu kwenye uwanja wa ndege, hali katika mji mzima, wameletwa askari polisi wageni kabisa kutoka mikoa mingine kulinda mkutano. Hivyo ulinzi ni mkali sana.


"Waacheni waonge ulinzi. Jambo hilo lisiwafanye tumbo moto. Ikiwezekana F.K uiambie serikali ya Tanzania ilete jeshi lake zima hapa Arusha na bado cha mtema kuni watakiona tu", Dave alijigamba.

"Paul na Fouche, hiyo ni kazi yenu sitaki Bon na Rocky walione jua litakalochomoza  kesho. Mipango yote mnaijua ni kama kawaida", George alisema.

"Hesabu kwamba hiyo kazi imefanyika", Paul alijibu.

"F.K. Nataka unipatie majina ya viongozi wote wa vyama vya wapigania uhuru ambao wameshaingia. Vile vile nataka unipatie majina ya hoteli na vyumba wanakolala. Habari hizi nazitaka leo hii", George alimwagiza F.K.

"Utapata bila matatizo", alijibu F.K.

"Wengine mliobaki nitawaeleza baadaye nini cha kufanya kwa usiku wa leo", George alisema huku akigeuka upande mwingine. Na nyie Paul, Fouche na F.K nataka utekelezaji sahihi kutoka kwenu.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru