HOFU

SURA YA SITA

MAMBO

III

Mnamo saa nne na nusu ndege namba TC 1001 iliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Willy Gamba alikuwa mmoja wa abiria walioteremka. Alijichanganya na kundi la abiria wenzake mpaka akafaulu kutoka nje ya uwanja bila mtu yeyote kumtambua. F.K, Paul na Fouche walikuwa kwenye kundi la wapokeaji wakichunguza watu kwa makini. F.K hakuweza kumtambua Willy. Mawazo ya Paul na Fouche yalikuwa juu ya Bon na Rocky na hata chembe hawakumfikiria Willy, mbali ya kumtambua.

Alipofika nje ya jumba, Willy alikuta madereva taksi wakigombania abiria. Ingawa taksi za kawaida huwa haziruhusiwi uwanjani hapo, siku ile zilijaa tele. Ziliruhusiwa kwa vibali maalum kutokana na haja ya kuhudumia wageni ambao walikuwa ni wengi sana.

"Oh, mzee njoo huku", teksi dereva mmoja aliyemfahamu Willy alimwita huku madereva wengine wakimwandama na kumsihi apande magari yao.

"Oh, Omari, habari za siku nyingia?", Willy alimsalimia.

"Nzuri tu, mzee, ila wewe tu umepotea", Omari alijibu huku akipokea mkoba wa Willy na kuelekea kwenye gari.

"Sababu ya biashara, bwana. Siku hizi imekuwa ngumu", Willy alijibu.

Wakati walipokuwa karibu kuondoka Willy alisita kidogo.

"Hebu subiri kidogo, kuna kitu nimekumbuka", Willy alisema.

Omari ambaye alikuwa ameliwasha, gari alilizima.

Ilikuwa jambo la kawaida kwa Willy kulitumia gari la Omari. Mara nyingine Omari alimwachia gari Willy aendelee yeye mwenyewe kwa malipo fulani.

Baada ya kupanga na kupangana Willy aliamua kuwangojea wenzake ambao wangekuja kwa ndege ya pili.

"Omari, samahani nitakusumbua, kuna mahali ambapo nataka niende lakini nataka niende peke yangu. Je, sijui kama utaniachia gari yako ili nifanye shughuli yangu? wewe unaweza kupanda gari nyingine", Willy alisema "Mambo mengine kama kawaida yetu".

Bila kusita Omari alikubali ombi la Willy, alijua fika kwamba Willy alikuwa kizito na kila alipochukua gari lake kwa shughuli zake kwa muda mfupi, aliweza kulipwa kiasi ambacho angeweza kukifanyia kazi kwa zaidi ya mwezi mzima.
"Bila shaka", Omari alijibu kwa furaha, Petrol imejaa mzee na gari kama kawaida halina matatizo. Ukisha maliza kazi utanipigia simu kunijulisha hata kama ni baada ya juma zima.


"Ahsante", Willy alijibu huku akichukua swichi ya gari.

Omari alimwaga Willy na kuambaa zake.

Omari aliachana na Willy kwenye maegesho ya magari uwanja wa ndege. Katika gari la sita katika safu kutoka alipokuwa Willy. F.K. pamoja na wenzake walikuwa wamekaa ndani. Walifanya hivyo ili kusubiri maadui zao ambao wangefika kwa ndege ya pili.

"Mimi nafikiri niwaache maana hakuna usalama tukionekana pamoja. Nisingependa mambo yetu yagundulike kabla hata kazi yetu hatujaianza", F.K. aliwashauri wenzake.

"Wewe nenda, kazi hii sisi ni saizi yetu, mambo yote tuliyotaka umefanya. Kazi yako umemaliza", Paul alimruhusu.

"Nawatakia bahati njema", F.K aliwaambia huku akiondoka kuelekea kwenye gari lake jingine ambamo Tondo alikuwa anamsubiri.

"Ahsante", PAul alijibu.

Bila kujua, Willy. Paul na Fouche walikuwa wakisubiri wageni wale wale, lakini kwa nia na madhumuni tofauti.

Ndege iliwasili mapema kuliko ilivyotarajiwa. Ilifika saa tano kasoro dakika kumi.

"Ndege hii imewahi kuondoka Dar", Willy alijisemea moyoni huku akiwa tayari kwenda kuwapokea wenzake.

Paul na Fouche walitoka kwenya gari lao mara moja na kwenda kujichanganya tena na wapokeaji wengine waliofika kuwalaki wenzao.

Ndege ilisimama na abiria wakatelemka kama kawaida.

Willy aalikuwa tayari amejigeuza kimawazo na kimazingira kutokana na ujuzi pamoja na uzoefu wa muda mrefu katika kazi hii. Alijibanza katikati ya nguzo moja kama asiyekuwa na hili wala lile. Hata hivyo aliweza kumwona kila mtu aliyetoka nje ya jumba la uwanja kutoka pale aliposimama. Paul na Fouche pia, wakitumia ujuzi wao walijitosa kwenye vurugu la wapokeaji kiasi kwamba hakuna mtu ambaye angewahisi chochote. Hii ilitokana na kwamba wao hawakuwa wazungu peke yao hapo uwanjani. Watu waliotoka kwanza ni wale waliokuwa wanasafiri bila mzigo mikubwa.

Hatmaye Rocky Malele alitokea. Paul alimgonga Fouche begani na wote wakamtambua Rocky. Willy nae alimwona Rocky lakini akaendelea kubana. Rocky aliangaza huku na kule kisha akaamua kupanda Kombi ya shirika la Taifa la Huduma za Kitalii.

"Wakati kama huu wa usiku ni vizuri kupanda gari la watu wengi kwa tahadhari na usalama", Rocky alijisemea.

Kulikuwa na watu wengine ndani ya gari hili lakini lilikuwa bado kujaa. Hivyo iliwabidi kusubiri abiria wengine zaidi. Paul, Fouche na Willy Gamba walimwona Rocky akipanda gari hilo. Ingawa Paul na Fouche hawakujuana na Willy. Wote waliendelea kumsubiri Bon atokee.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba Bon hakutokea. Pande zote mbili zilitarajia kuwa angefika kwa ndege hii. Lakini kwa mshangao mkubwa Bon hakuonekana kamwe.

Willy ambaye alikuwa anachunguza nyendo za hapa kwa makini, aliona wazungu hawa wawili wanaondoka na kuelekea kwenye gari lao. Katika akili yake Willy alifikiri kitu fulani kilichojitokeza kama hakieleweki. Ilikuwa kwamba Willy aliwaona wakati anafika. Na sasa alikuwa amewaona tena Wazungu wale wale. Ilionekana kama kwamba nao pia walikuwa wanasubiri mgeni ambaye hakuwasili kwani wao pia walikuwa wa mwisho.

Pamoja na hayo, Willy alijisemea, "Lakini inawezekana walikuwa wamekuja kuwapokea wageni wao halafu wakakuta hawakuwasili. Hii inawezekana na haina ubaya wowote".

Hata hivyo Willy aliamua kufuatilia nyendo za Wazungu hao. Aliwaangalia wakiingia kwenye gari naye pia aliamua kuingia ndani ya gari lake. Mara gari alilokuwemo Rocky liliondoka.

"Tulifuate gari hilo", Paul alimwambia Fouche ambaye alikuwa anaendesha.

"Itakuwa vigumu kulishambulia gari hili; ingekuwa vizuri kama angekuwa amechukua teksi yeye peke yake", Fouche alieleza.

"Kuna wakati atabaki peke yake. Usiwe na wasiwasi kwani tunayo siku nzima ya kufanya kazi hii", Paul alijibu.

Gari la akina Rocky lilifuatwa na gari moja, halafu lilifuatwa na gari la akina Paul na Fouche. Willy alisubiri gari lingine lifuate ndio naye aweze kujiunga na msafara. Alipotaka kuondoka aligundua kuwa tairi mbili za nyuma hazina upepo!

"Shenzi", Willy alilaani.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU