HOFU

SURA YA SITA

MAMBO

IV

Wakati F.K anawaaga Paul na Fouche ili aende kwenye gari alilokuwa ameegesha Chris Tondo, Chris Tondo alikuwa amemwona Willy Gamba akitoka nje ya uwanja na kumtambua. Vile vile wakati Chris Tondo alipokuwa ofisa wa polisi aliwahi kumfahamu Willy kikazi na kimaisha. Kwa upande mwingine, Willy hakumweka Chris Tondo maanani. Hivyo alikuwa hawezi kumkumbuka.

"Nimemwona Willy Gamba", Tondo alimwambia F.K.

Aliposikia hivyo F.K alishituka kwani alimfahamu Willy kutokana na umaarufu wake kama nilivyokwisha kusimulia.

"Oh, yuko wapi?", liuliza F.K kwa mshangao mkubwa.

"Namwona anangojea ndani ya teksi ile".

"Basi, bila shaka na yeye anawasubiri", F.K alisema.

"Anawasubiri akina nani?", Tondo aliuliza.

Pamoja na mambo yote ambayo Tondo alikuwa anayafanya kwa wizi nzima, F.K alikuwa hajamweleza kinagaubaga operesheni hii ilikuwa ya namna gani. Baada ya kufikiri kwa muda aliona ni vyena amweleze habari zote kwani kumficha Tondo kungeweza kusababisha makosa ambayo yangeweza kuleta hatari kubwa, hasa kwa wakati kama huu.

"Unajua Tondo, wewe nakuchukulia kama ndugu yangu. Ni mtu ambaye nakuamini katika maisha yangu. Hivyo wakati umefika na mimi kukueleza kinaganaga juu ya shughuli yote hii", F.K alimwambia Tondo na kisha akamweleza juu ya operesheni hii kuanzia mwanzo mpaka mwisho, kisha alisema. "Hivyo umefika wakati wa kulipa kisasi dhidi ya serikali ya Tanzania kama ulivyowahi kuahidi. Bila shaka utakuwa upande wetu".

"F.K wewe ni ndugu yangu. Mimi niko pamoja nawe. Naahidi kuwa nitatumia ujuzi wangu wa kipolisi kikamilifu ili nilipize kisasi changu cha kunionea na kunifedhehesha ", Tondo aliahidi.

Hivyo F.K na Tondo walibaki ndani ya gari lao wakimchunguza Willy alikuwa anafanya nini. Wakati ndege ilipwasili na Willy akatoka kuelekea mahali alipojibanza ili kuwaangalia akina Riocky. Tondo aliteleza gizani mpaka kwenye gari la Willy. Hapo hapo alitoa upepo kwenye matairi mawili ya nyuma.

"Nimemweza", Tondo alijigamba huku akirudi kwenye gari.

"Kazi hii itakuwa kubwa", F.K alisema. "Itakuwa ni vita vya kutafutana. Vita kwa akili na ujuzi kwani wapelelezi mashuhuri wa Afrika naona wako hapa. Heri sisi tutangulie tuwape habari wenzetu halafu tujitayaruishe kwa ajili ya mapambano makali. Hapa tulipo hatuna hata silaha yoyote. Kama tunapenda kuiona kesho tumkwepe Willy. Kazi tuliyofanya inatosha kwa leo. Willy anaweza kusubiri mpaka kesho. Waache Paul na Fouche nao wafanye kazi yao. Kesho tutakuwa tayari kumumaliza Willy. Hata yeye mwenyewe ataingiwa na woga baada ya kusikia wenzake wameuawa".

"Nafikiri tungoje tuone kama Willy alikuwa anawasubiri wenzake", Tondo alisema. "Ikiwa ni hivyo itakuwa rahisi kwa Paul na Fouche kuwamaliza wote kwa wakati mmoja".

"Sidhani, hawawezi kusafiri wote pamoja, Tondo", F.K alipinga usemi. "Mimi ni jasusi na mchezo huu naufahamu. Paul na Fouche wanajua sana mchezo huu pia. Hivyo wao waachie, wewe ni mchezaji wa ridhaa. Katika shughuli hii ya kijasusi vizuri kuwaachia wajuzi. Achana na Willy huyo atakuwa nyama yetu kesho".

Tondo aliwasha gari na kujipenyeza kwenye msururu na kuondoka.

Wakati Tondo anatoa upepo kwenye tairi za nyuma za gari la Willy. Lyimo alikuwa sehemu ile. Lyimoa alikuwa mwizi mkubwa. Wizi wake alifanya wa kuvunja magari yaliyoegeshwa na kuiba vitu vilivyomo ndani. Siku ile alikuwa katika pilika zake hapo uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, baada ya kusikia magari mengi yangekuwa hapo. Wakati huo Lyimo alikuwa hajabahatisha kitu chochote. Alikuwa amejibanza kwenye gari karibu na lile la Willy. Ndani ya gari lile Lyimoa alikuwa ameona mkoba ambao alikuwa anaunyemelea. Alikuwa anajaribu kufungua mlango wa nyuma. Mara alisikia mtu anasogea karibu na gari lililokuwa jirani. Aliinuka kidogo na kuchungulia. Alimwona mtu anakuja kwa kunyata. Kwanza kabisa Lyimo alifikiri yule alikuwa mwizi mwenzie. Lakini sura yake pamoja na jinsi alivyokuwa ilionyesha kinyume. Aliona huyo mtu anatoa upepo kwenye gari halafu kunyata na kuondoka.

Lyimo aligundua kwamba gari lile lilikuwa teksi ya Omari ambaye anamfahamu sana. Ili kuchunguza vizuri kisa hiki Lyimo alimfuatilia yule mtu na kuona gari alimoingia. Alichukua kalamu yake na kuandika namba za gari hilo kwenye kiganja chake cha mkono. Akitarajia kumweleza Omari kana angetokea. Mara nyingine Omari alikuwa akimsaidia. Safari hii aliona amepata nafasi ya kulipa ukarimu wake angalau kwa ishara hiyo ndogo.

"Mimi ni mwizi", Lyimo alijisemea moyoni. "Ninaiba ili nipate fedha za kunifanya niishi. Lakini watu wengine ni waharibifu tu. Kwa mfano mtu huyu amemsumbua mwenzake bure. Afadhali mara mia angekuwa na nia ya kuiba kitu".

Mshangao wake ulizidi alipoona lile gari linaondoka kuelekea mjini.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru