HOFU

MAMBO

VI

Karibu na mpakani, katikati ya sehemu ya Tengeru, nje ya mji wa Arusha. Willy aliyafikia magari yaliyokuwa yametangulia. Alilipita gari moja ndipo akaliona lile lililokuwa linaendeshwa na wazungu. Vile vile aliona ile Kombi iliyombeba Rocky. Hivyo aliamua kubana nyuma ya magari hayo.

Kituo cha kwanza cha ile kombi kilikuwa Saba Saba Hoteli. Rocky alikuwa amemwambia Willy kuwa angefikia Equator Hoteli. Alipofika Sabasaba Hoteli na kuona ile kombi pamoja na gari la wazungu vikiongoza kwenda hoteli hiyo, yeye Willy aliamua kwenda moja kwa moja akabane Equator Hoteli. Alifanya hivyo ili akaone kama alivyofikiri ilikuwa kweli. Akiliwa ameegesha gari katikati ya magari mengine karibu na Safari Hoteli, aliona ile kombi inasimama pale Equator Hoteli. Watu watatu wakiwa na mizigo walitelemka. Rocky alikuwa mmoja wapo punde si punde, Willy aliona gari lile la wazungu linaegeshwa karibu na Hoteli hiyo hiyo. Lakini kwa upande mwingine wa barabara.

Mzungu mmoja aliondoka na kuelekea huko Hotelini. Willy alisubiri. Baada ya kama dakika kumi hivi, yule Mzungu alirudi na kuingia ndani ya gari. Willy aliendelea kusubiri. Alipoangalia saa yake ilisema saa sita usiku.

Ilipofika saa saba usiku Paul alimwambia Fouche, "Sasa twende, mimi nitapita kwa nje wewe utapita kwa ndani. Kama nilivyokueleza, chumba chake kiko kwenye pembe ya kulia. Huwezi kukikosa kwani ni moja kwa moja. Mimi nitaingilia dirisha la bafuni ambalo ni kubwa la kutosha. Bila shaka atakuwa amelala".

Waliondoka ndani ya gari na kutokomea gizani, Willy naye aliondoka kwenye gari baada ya kuwaona wanafanya hivyo. Alifanya hima kuelekea kwenye kijumba cha simu kando ya barabara. Alipiga simu Equator Hoteli kwani aliyokuwa anatuhumu yajidhihirisha kuwa ni kweli.

"Hallo, Equator Hotel?", simu iliitika.

"Nipe mapokezi", Willy aliomba.

"Mapokezi hapa", Willy alijibiwa baada ya muda kitambo.

"Rocky Malele yupo chumba gani?", Willy aliuliza.

"205".

"Nipe nizungumze naye".

Baada ya muda kidogo, sauti ya Rocky ilisikika.

"Hallo, Rocky hapa".

"Willy hapa", Willy aliitika na kisha aliendelea, "Chunga tai wawili wanataka kula nyama yako sasa hivi".

"Chunga", Rocky aliitikia huku akiweka simu chini.

Aliamka haraka kutoka kitandani na kuchukua bastola yake kutoka chini ya mto. Aliikagua.

Willy naye alitoka kwenye kibanda cha simu, akaigusa kwa chati bastola yake huku akimwemwesa.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru