HOFU

MAMBO

VIII

Fouche alikwenda katika sehemu ya mapokezi ya Equator Hoteli. Mhudumu wa mapokezi alikuwa akisinzia sinzia pale kwenye kiti.

Aliangalia kwenye bodi ya funguo na bila kusita akamwambia mhudumu. "Chumba mia mbili na ishirini".

Yule kijana bila hata kugutuka alichukua funguo. akampatia na kuendelea kustambari.

Fouche alipanda mpaka ghorofa ya pili na kwa tahadhali kubwa alielekea chumba namba 205.

Paul alizunguka na kuuangalia ukuta. Alivaa mifuko yake ya mikono. Mifuko hiyo ilikuwa ya aina yake, kwani iliweza kushika ukutani kama sumaku. Hivyo ilimwezesha kupanda ukuta bila matatizo. Aliangalia saa yake halafu akaanza kukwea.

Baada ya Rocky kupata simu ya Willy, aliyomtahadharisha, alitengeneza kitanda chake vizuri. Alikunja Blanketi na kuifunika na shuka mpaka ikaonekana kama mtu aliyelala. Baada ya kufanya hivyo, alibana mahali na kusubiri.

Akiwa katika hali ya kunyata. Willy alijipenyeza kwenye njia kati ya Equator Hoteli na Jengo la posta kwa upande wa kulia. Kwa haraka akamuoana mtu anaelekea kwenye ukuta. Mara akahisi ni nani. Aliendelea kunyata haraka haraka mpaka akafikia usawa wa mtu yule ambaye sasa alikuwa amekaribia kushika dirisha.

"Shiii", Willy alitoa sauti ya kustua mtu.

Paul aligeuka kumtazama mtu aliyetoa sauti hiyo. Kutokana na mwanga wa mbalamwezi. Paul alijikuta anatama kwenye mdomo wa bastola.

Willy alimwamru atelemke. Vinginevyo angemkita risasi ya matako. Kufumba na kufumbua, Paul alifyatuka kama risasi na kumwangukia Willy. Willy alipiga risasi ambayo ilimkosa Paul na wote wakaanguka chini. Bastola ya Willy ilidondoka umbali wa kama futi sita kutoka mahali walipokuwa. Hapo ndipo vita vya ana kwa ana vilipoanza. Willy alitaka kupiga mbio kuelekea kwenye bastola. Lakini Paul aliwahi kumrukia kwa pale pale chini. Hata hivyo, Willy alimpiga teke-farasi na Paul akaanguka upande mwingine lakini akaamuka mara. Hapo ndipo walipogundua kuwa walikuwa wamekutana wajuzi watupu.

Hapo mwanzo Paul alikuwa amefikiri huyu alikuwa askari wa kawaida, lakini sasa alikuwa na mawazo tofauti. Kupambana naye bila kutumia silaha isingewezekan. Alijaribu kutoa bastola yake iliyokuwa kwenye mkoba wake chini ya kwapa. Lakini Willy aligundua janja yake. Alimwahi kipigo cha karate kilichomfanya Paul aone nyota. Pale pale Paul alitoa mapigo manne ya karate haraka haraka. Lakini Willy aliyaona. Willy alimgeuzia Paul na kumpiga teke la kinena lililomwangusha chini. Alimrukia ili amumalize kabisa. Lakini Paul alijiviringisha kando na Willy akamkosa.

Lakini alijiviringisha tena kabla ya kutua na kumwahi Paul ambaye wakati huo alikuwa amechomoa bastola. Aliipiga teke ile bastola nayo ikafyatuka wakati ikitoka mikononi mwa Paul. Teke lile lile lilikuwa limevunja mkono wa Paul wa kulia. Paul aliamka ili akimbie, lakini Willy alimwahi kwa kumpiga ngwara. Alipoanguka chini Willy alimpiga Paul teke ambalo lilimvunja mbavu kama tatu hivi za upande wa kulia na hapo hapo moto ukamwishia. Akabaki kugwaya.

"Nyinyi ni nani?", Willy alimwuliza Paul, huku amembana pale chini asiweze kufurukuta.

"Sisi ni Wazungu", Paul alijibu kwa jeuri maana alijua huo ndio mwisho wa maisha yake, haraka sana alifikiri jinsi alivyokwisha waweka watu wengine katika hali kama aliyokuwemo kwa sasa hivi. Kwa mara ya kwanza kati maisha yake alijiwa na woga na hali ya kuogopa kifo. Hata hivyo alijuwa huo ndio ulikuwa mwisho wake kwani hapakuwa na ujanja wa kuokoka.

"Wenzako wako wapi?", Willy aliuliza kana kwamba alikuwa akijua.

"Niko peke yangu tu", Paul alijibu huku akisikia maumivu makali kutoka mbavuni.

"Aah, kumbe bado unafanya mchezo", Willy alitishia.

"Kama ni kuniua si uniue tu?, unataka nini zaidi", Paul alimuuliza Willy.

"Kwanza ujibu maswali yangu, vinginevyo bado unayo safari ndefu ya kwenda ".

"Hutapata jibu hata chembe, unapoteza muda wako".

"Basi, kama wewe ni Kaburu leo umefika kwa wazalendo wa Afrika. Utakiona cha mtema kuni. Kama hutaki kifo chako kisiwe cha maumivu makali bora uanze kusema", Willy alimwambia huku akigandamiza mbavu za Paul zilizovunjika.

Paul alisikia maumivu makali ambayo alikuwa hajawahi kusikia. Lakini pamoja na uchungu wote ilikuwa ni sheria ya 'KULFUT' kwamba hakuna askari wake kutoa siri bali kutafuta njia ya kujiua ili kupunguza muda wa mateso.

"Sema wenzako wako wapi, Kaburi wee", Willy alimuuliza huku akizidi kumbana mbavu kwa kukandamiza mkono wake.

Mara alishitukia Paul anatoa ulimi wake nje ghafla halafu akaukata kwa meno yake kama mkasi.

"Shenzi mkubwa we!", Willy alitukana.

Kaburu alikuwa ameamua kujiua kwa njia ya ajabu sana.

"Kweli tunayo kazi maana Majasusi hawa wa Makaburu siyo watu wa kawaida", Willy alijisemea moyoni.

Fouche aliendelea kuziparamia ngazi kana kwamba naye alikuwa mgeni aliyefikia chumba namba 205, aliangaza huku na kule, halafu akatoa bastola yake na kujiweka tayari. Kama ilivyo desturi, bastola yake ilikuwa na kizibo cha kuzuia sauti. Alichukua funguo zake malaya akafungua kufuri la mlango.

Rocky, ambaye alikuwa ndani amezima taa lakini akiwa amevuta pazia kuacha mwanga wa mbalamwezi uingie kidogo, alisikia kwa mbali kufuli likifunguliwa. Hivyo alijiweka tayari.

Fouche alikuwa amelidhika kwamba kufuri halikupiga kelele. Hivyo alishika komeo. Kwa kasi ya umeme. Fouche alifungua mlango na moja kwa moja akamimina risasi kama kumi pale kitandani. Halafu aliingia chumbani na kuwasha taa huku akiangaza kitandani.

"Umefanya kazi nzuri", Rocky alisema kwa sauti ya kebehi.

Fouche aligeukia kule sauti ilikokuwa inatokea na pale pale akawa amegundua jinsi alivyokuwa amedanganywa. Alijuwa mambo yamekuwa mambo. Hivyo alifyatua risasi lakini Rocky alikuwa tayari amekaa imara. Alimpiga Fouche risasi moja ya kifua akaanguka chini. Alipomkaribia alimkuta kawa maiti tayari.

"Mara Rocky akasikia kitu kinadondoka bafuni. Aliruka ili azime taa. Hapo hapo mlango wa bafuni ukafunguliwa kama radi kabla hajazima taa. Huku bastola zikiwa zimeelekezana. Alishangaa kumwona Willy.

"Chunga sana. Willy", Rocky alisema. "Siku nyingine unaweza kuumia.

"Mimi nafikiri wewe chunga zaidi; ongeza kasi", Willy alijibu.

Wote wakacheka.

"Umempiga sachi ?", Willy aliuliza huku akiangalia maiti ya Fouche.

"Zaidi ya hii bastola yake", Rocky alijibu. "Hana kitu kingine".

"Hata yule wa nje hana kitu", Willy aliongeza Rocky alielewa mara moja.

"Hivi ulijuaje nia ya watu hawa?", "Kama si wewe Willy, mimi ningekuwa maiti hivi sasa.

"Hiyo ndio faida ya kuwa wengi", Willy alisema. "Hebu chukua vitu vyako tuondoke hapa. Nitakueleza zaidi huko njiani".

Waliondoka chumbani humo kwa kupitia dirishani.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru