HOFU

SURA YA SITA

MAMBO

V

Wakati Willy alipokuwa anaangalia matairi, Lyimo alitokea."Habari gani, mzee", Lyimo alimsalimia Willy kwa heshima.

"Nzuri", Willy alijibu huku akimwangalia Lyimo kwa makini. Kisha aliendelea, "Ngoja kidogo".

Willy alisogea mbele na kuandika namba za gari la Wazungu lililokuwa linapita mbele yake halafu akarudi.

"Eh, unasemaje?", Willy alimsaili Lyimo."Mwenye gari hii ni rafiki yangu. Siyo gati la Omarui hili", Lyimo aliuliza.

"Ndio, na mimi ni rafiki yangu. Ameniachia gari hili. Lakini ajabu nimekuta limepata pancha mbili sasa hivi", Willy alijibu.

"Nimeona mtu anatoa upepo ndani ya matairi haya", Lyimo alieleza.

Mara Willy alisikia kengele zinalia kichwani mwake.

"Eh, mtu wa namna gani?", Willy aliuliza kwa shauku kubwa.

"Mtu mmoja nadhifu sana. Mwanzo nilifikiri ni mwizi. Lakini hakuonyesha dalili ya wizi. Aliinama, akatoa upepo na kuondoka. Aliingia kwenye gari ambalo lilikuwa na mtu mwingine ndani halafu wakaondoka zao. Hata hivyo, mimi nilichukua nambari za gari hilo ambayo ni ARKK 567", Lyimo alimwambia Willy huku akisoma kwenye kiganja chake.

Willy alikariri nambari hiyo na kushangaa, kwa kujiona alikuwa na bahati iliyoje.

"Wewe unaitwa nani?", Willy aliuliza

"Naitwa Lyimo".

"Na wewe ni dereva wa teksi?".

"Hapana, mimi ni shanta".

"Shanta maana yake nini?".

"Mimi huwa nawasaidia madereva kama wanao usingizi. Huwa naendesha halafu wao huwa wananilipa chochote", Lyimo aliongopa.

Wakati huo akili ya Willy ilikuwa inafanya kazi haraka haraka. Mara alipata jawabu.

"Ninaweza kupata gari nyingine hapa?".

"Subiri niangalie", Lyimo alijibu na kuondoka.

Punde si punde Lyimo alirudi na kijana mmoja.

"Huyu anaitwa Tarimo, ni rafiki yangu vile vile, hata Omari ni rafiki yake pia", Lyimo aliwajulisha.

"Aah, mimi naitwa Willy. Omari ni rafiki yangu. Kiniachia gari lakini nimepata mkasa".

"Sasa unataka tukusaidie vipi?", Tarimo aliuliza.

"Unayo pampu?".

"Ndio", Tarimo alijibu.

"Nafikiri kama utakubali utanipatia gari lako, mimi nitakulipa shilingi elfu tatu. Weka upepo kwenye gari la Omari halafu tuonane kesho asubuhi huko New Arusha Hoteli. Gari lako utalikuta hapo".

Bila kuchelewa Willy alianza kutoa fedha na kumhesabia Tarimo. Tarimo aliona kama ameangukiwa na ngekewa. Alichukua fedha na huku Lyimo akibeba mizigo ya Willy, wakielekea kwenye gari.

"Lyimo umenisaidia sana. Chukua hizi shilingi tano ukanywe angalau bia moja", Willy alimwambia Lyimo.

"Lo! ahsante sana. Leo siku nzima nilikuwa sijapata kitu. Mungu akuongezee.

"Amina", Willy alijibu huku akifikiria namna Lyimo alivyokuwa amemsaidia bila kujua.

"Kesho asubuhi", Tarimo alisema.

"Kesho asubuhi", Willy alijibu na kuondoka.

"Sasa ni lazima niyakamate yale magari", Willy alijisemea moyoni.

Gari la Tarimo lilikuwa aina ya Peugeot 404 lenye umri kidogo. Lakini lilikuwa na nguvu ya kutosha. Tangu yale magari yaondoke ilishapita muda wa dakika kumi na tano. Willy alilipamba moto na kuendesha kwa mwendo mkali sana. Wakati akiendesha Willy alifikiri mambo yote haya. Na ajabu zaidi, Willy alimfikilia Bon Sipele ambaye alikuwa hakuonekana hapo uwanja wa ndege.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru