HOFU

ARUSHA

V

P.G aliwasili nyumbani kwa F.K kwa miguu baada ya teksi kumtelemsha karibu na ofisi ya mbao. Alisema amedai ndiko alikokuwa akienda ili kununua mbao za kununua. Alitembea kwa tahadhari kubwa. Ilikuwa saa nne na nusu alipojipenyeza kwenye ua wa nyumba ya F.K na kubisha hodi. F.K ndiye aliyefungua mlango. Alishangaa kumwona P.G.

"Hakuna mtu aliyekuona unakuja huku?", F.K alimwuliza huku uso wake ukionyesha huzuni na mashaka.

"Hakuna, F.K".

"Karibu ndani, P.G".

"Ahsante".

F.K alimwongoza P.G mpaka kwenye chumba cha siri. Majasusi wengine walikuwa ndani wanapumzika. Walipomwona walipomwona tu P.G wote walikaa kitako huku wakihisi kuna tatizo limetokea.

"Hebu tupe habari", F.K aliomba.

P.G alieleza yote yaliyotokea usiku ule na jinsi alivyokuwa ameamua kuja kuwaongezea nguvu wenzake baada ya kupoteza watu wake wote na kubaki yeye na mtu mmoja tu.

"Hivi nimemwacha Smith Namanga. Ataingia hapa mchana huu. Nimeona siyo vizuri sisi wote wawili kuja pamoja mchana huu", alisema P.G. 

"Pole sana", walimjibu kwa pamoja.

Baadaye F.K naye alimweleza mambo yaliyokuwa yamewatokea.

"Hii ina maana kwamba mpaka sasa hivi mambo hayaendi vizuri. Lakini nina hakika tutashinda maana sasa tunajua nguvu za adui; na yeye hajui nguvu zetu wala maskani yetu". F.K alieleza.

"Sasa mipango ikoje", P.G aliuliza.

"Mipango iko kama ifuatavyo", F.K alieleza. "Usiku tutagawanyika mafungu mafungu. Kwanza lazima tuwamalize hawa watu watatu sababu ni kwamba sasa tunafahamu vyumba vyao na hoteli. Vile vile sasa tunafahamu mienendo yao. Muda mfupi tu uliopita Chris alinipigia simu. Amesema kwamba amepata habari kuwa Willy Gamba amemwambia Mkuu wa Upelelezi kwamba hakuridhika na maelezo kuhusu gari letu nambari ARKK 567. Ameongeza kuwa Willy angeendelea kufanya uchunguzi kuhusu gari hilo. Hivyo nimemwasa Chris ajaribu kumkwepa Willy maana huyo ndiye mtu hatari zaidi. Yeye ndiye aliyefanya mauaji ya jana".

"Je, huyu Mkuu wa Upelelezi yuko upande wetu?". P.G aliuliza.

"Ndio na hapana", F.K alijibu. "Huyu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa ni mtu ambaye tumemsaidia sana kifedha. Zaidi ya hayo yeye anaamini kwamba sisi ni watu wanaotii sana Serikali. Kutokana na misaada yetu kwake, neno lolote linaloweza kutudhuru sisi yeye atatusaidia kwa kila njia. Lakini akijua ukweli katika swala kama hili, lazima atatuuza. Kutofanya hivyo kunaweza kuwa na yeye kupoteza kazi yake au hata kupewa adhabu kali ya kifo kama mhaini. Kusema kweli wanamwogopa sana Willy".

"Hao viongozi wa wapiganian uhuru watakaohutubia mkutano wameshaisha fika".

"Watatu wamefika na wengine wawili watafika jioni hii, kuhusu wale ambao wamefika tayari tumechukua habari juu yao. Mienendo yao pia tumeisha ifahamu. Hata wale wawili wakiingia tutapata habari zao. Kama ujuavyo P.G, mimi naaminika hapa kama mwanamapinduzi. Habari zozote ninazozitaka nazipatamoja kwa moja kutoka kwa watayarishaji wenyewe wa mkutano huo. Hivyo lazima tuwafungie kazi hawa viongozi leo usiku, halafu tuone kama mkutano utafunguliwa", F.K, alisema.

F.K alisema. "Sasa hivi natoka ili nikamilishe mipango ya usiku kwa kupata habari zaidi. Na wewe Peter, George atakupa mipango yote ambayo tumeifanya kwa ajili ya usiku. Kwa vile na wewe umeongezeka. ni dhahiri kwamba tutashinda. Tutatenda kitendo ambacho kitaiacha dunia nzima inagwaya".

"Vizuri. Mimi nitaelewana na George halafu nitapumzika maana mpaka sasa sijalala. Wewe kakamilishe mipango hiyo kuhusu kazi", P.G alijibu huku yeye na George wakielekea chumba kingine

ITAENDELEA 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU