HOFU

ARUSHA

VI

Willy alikaribia ofisi za Nyota Tours and safaris. Hapo hapo alimwona msichana mrembo sana akitoka nje ya ofisi hiyo. Kila wakati Willy alipokutana na wasichana warembo namna ile aliwaona kama sumu kwake kwani alikuwa mgonjwa sana juu yao.

Willy alibana kwa mbali kidogo ili aweze kuyapa nafasi macho yake yapate chakula chake. Alipenda amwone vizuri mrembo huyu ambaye aliumbwa ili wanaume wajisikie raha. Willy aligundua kwamba hakuwa yeye peke yake aliyekuwa anamwangalia, bali wanaume wengine pia walikuwa wanalisha macho yao kwa chati.

Msichana huyu alitembea mpaka kwenye gari moja. Alitoa funguo kwenye pochi yake na kusimama ili afungue mlango. Willy alijuwa kuwa gari hiyo mpya aina ya Toyota KE 30, ilikuwa ya huyo msichana. Lakini hakushangaa kwani msichana mrembo kama yule angeweza kumpata mtu yeyote mwenye pesa akamnunulia kitu chochote. Hata gari angemnunulia ili mradi tu aridhike.

Wakati huyo msichana anaingiza funguo kwkenye tundu la kufuri katika mlango wa gari. Ghafra akatokea kijana. Alikwapua pochi yake halafu akakimbia. Huku akiwa ametoa jisu kali alitisha mtu yeyote ambaye angethubutu kumfuata. Yule msichana wa watu alitoa sauti kali yenye kutia hofu halafu akaanguka chini. Watu waliokuwa karibu walisambaa kwa kuogopa hilo jisu kali.

Willy ambaye alishuhudia kitendo hicho cha kijambazi, alianza kumfukuza yule kijana. Alipoona kuwa watu wote wamesambaa isipokuwa mtu mmoja tu aliyekuwa bado anamsakama, yule kijana alisimama kumsubiri Willy apambane nae ana kwa ana.

"Hunijui mimi eh? Mji mzima wananijua mimi ni nani... sogea nikukate kichwa ", alitamba yule jambazi kijana.

willy alimwendea kwa tahadhari kubwa huku watu wote wakipiga makelele kumsihi arudu nyuma kusalimisha maisha yake. "Rudi, rudi! Kimbia! huyo ni mwuaji! Anamaliza watu hapa".

Kama kwamba hasikii Willy alizidi kumsogelea yule jambazi. Mara yule jambazi alimvamia Willy kama mchezo vile. Willy alikwepa shambulizi la kwanza na lile jisu. Alimnasa mkono wake na kumkata mkono mmoja wa karate kwenye bega lile jisu lilianguka. Willy alilipiga ngwala lile jambazi mpaka chini. Kuona vile yule msichana alikimbia mpaka pale. Huku akiwa ameshikilia kiatu chake mkononi alimpiga na kisigino yule jambazi. Hapo ndipo watu wengine walipofika pamoja na polisi wa doria. Akiwa ameshika pochi aliyoporwa, Willy alimvuta kando yule msichana.

"Ahsante sana", msichana alimwambia Willy. "Ahsante bwana. Sijui nikushukuru vipi kwa kujitolea maisha yako ili kuokoa mali yangu".

"Sijali", Willy alisema. Kwa mtoto kama wewe. Kila mwanaume kamili yuko tayari kujitoa mhanga maisha yake".

Polisi alimfuata Willy akimtaka akatoe maelezo ya wizi huo katika kituo cha polisi. Lakini Willy alimnong'oneza Polisi huyo naye akamwacha huru. Huku amemfunga pingu jambazi yule na kundi la watu walimfuata. Polisi alianza safari kuelekea kituo cha polisi. Alimwacha Willy akizungumza na yule msichana hapo pembeni mwa barabara. Yule msichana alianza kutokwa na hofu na kurejea katika hali ya kawaida. Sasa alimwangalia yule kijana aliyekuwa ameokoa mali yake. Alikuwa kijana mwenye sura ya kupendeza sana. Vile vile alikuwa na kitu kingine ambacho ilikuwa vigumu kukieleza. Huyo kijana alisisimua damu yake.

"Ehe, unaitwa nani?", Willy alimwuliza.

"Naitwa Nyaso", msichana alijibu.

"Nyaso tu, basi?".

"Ndio, Nyaso tu basi! Na wewe waitwaje?".

"Mimi naitwa Willy".

"Oh, vizuri. Sijui nikupe nini Willy!".

"Usijali, sasa hivi nina shughuli. Tunaweza kuonana jioni mnamo saa kumi na mbili hivi, angalau kwa muda mfupi, niweze kukununulia kinywaji", Willy alimwuliza.

Nyaso alifikiri sana kwanza. Alimwogopa sana F.K. angechukia ikiwa angejua alitoka nje na mtu, hasa mtu mgeni. Hali hii aliipima na jinsi F.K. alivyokuwa hataki kumwona siku hizi kwa kisingizio eti alikuwa na shughuli nyingi. Alifikiria sana jinsi F.K. alivyokuwa amemkaripia eti kwa kumpigiapigia simu nyumbani kwake wakati yeye alikuwa na kazi nyingi. Kama namna moja ya kumkomoa F.K. Nyaso alikubali mwaliko wa huyu kijana ambaye alimsisimua damu.

"Sawa, una miadi!" Nyaso alijibu.

"Arusha, Oke, nichukue hapo New Arusha saa kumi na mbili kamili", Willy alisema.

"Nitafika bila kukosa", Nyaso aliahidi.

Huku akitingisha matako yake huku na huku, alielekea kwenye gari lake na kumwacha Willy ameshikwa na butwaa. Alipoingia ndani ya gari Nyaso alimrushia busu Willy ambaye alisikia kama vile moyo wake umekosa pigo moja. Nyaso alipopotea ndipo Willy alipokumbuka safari yake ya kwenda kwenye ofisi ya Chris Tondo, ambayo ilikuwa karibu na hapo alipokuwa. Vile vile ndipo alipogundua kwamba Nyaso alikuwa anatokea kwenye ofisi ile ile wakati alipovamiwa.

Chris Tondo alikuwa katika pilika pilika humo ofisini kwake. Alikuwa akikusanya makaratasi na kutatunza kwenye visanduku. Alifanya shughuli hii haraka ili atoke ofisini. Alikuwa ameambiwa na F.K kufanya hivyo ili Willy asije kumkuta.

Wakati huo huo Willy alifika kwenye ofisi za Nyoka Tours and Safaris.

"Habari za leo", Willy alimsalimia kijana mmoja aliyekuwa kwenye ofisi ya nje.

"Nzuri, mzee. Nikusaidie nini?".

"Naomba kumwona ndugu Chris Tondo".

"Una miadi naye".

"Yupo?", Willy aliuliza.

"Ndiyo yupo, lakini huwezi kumwona huna miadi", kijana alisema

"Mimi ni rafiki yake. Ukinirudisha bila kumwona halafu akasikia umefanya hivyo ujuwe wewe huna kazi", Willy alitishia huku akielekea kwenye ofisi iliyoandikwa Meneja Mkuu.

Aliwaacha wafanyakazi wote kwenye ofisi ile wakimwangalia wasijue la kufanya. Alifungua mlango na karibu wagongane na Chris Tondo ambaye pia alikuwa anafungua mlango huo ili atoke nje.

"Oh, pole sana", Willy alisema.

Tondo alipogundua huyo alikuwa Willy, alisikia moyo wake unapiga haraka na akashindwa kupumua sawasawa.

"Karibu", Tondo alijikuta amebabaika.

"Ahsante", Willy aliitika huku akifunga mlango nyuma yake.

"Hawa vijana hawakunieleza kuna mgeni", Tondo alisema huku akionyesha kukasirika.

"Samahani, kwa kweli wao hawana kosa kwani ni mie ambaye sikuwasikiliza", Willy alijibu.

"Ehe, nikusaidie nini ndugu...?".

"Willy Gamba", Willy alimalizia.

Tondo alishangaa kumsikia Willy akijitambulisha kwa jina lake la kweli kwani alifikiri angejificha. Hii ilimtia hofu zaidi."Ya, nikusaidie nini ndugu Gamba?".

"Natumaini wewe ni ndugu Tondo. Meneja Mkuu wa Kampuni hii?", Willy alimwuliza huku akimtazama machoni.

Moyoni Tondo alijua mambo yameanza kutibuka. Alijisikia kujuta kwani alifahamu jinsi gani Willy aliweza kusoma mawazo ya mtu aliyezungumza naye. Kitu hicho ndicho kilichomfanya Willy kufanikiwa katika kazi yake ya upelelezi. Tondo alitafakari alipoulizwa vile.

"Ndio", Tondo alitumia uzoefu wake wa kipolisi kujibu swali hilo. Kwani alifahamu majibu mafupi yalikuwa mazuri kwa mtu anayehojiwa.

"Mimi ni afisa usalama kutoka Dar es Salaam. Nimefika hapa kwa shughuli za kiserikali. Nimeshawishika kuzungumza na wewe niliposikia uliwahi kuwa afisa wa cheo cha juu katika idara ya polisi".

"Vizuri", Tondo alijibu huku akishangaa kuona jinsi Willy alivyokuwa akijieleza.

"Sijui uliwahi kufika kwenye uwanja wa ndege jana usiku?", Willy aliuliza.

Mate yalimkauka Tondo alipofikiri juu ya uwezekano kwa kwamba Willy alikuwa amemwona wakati anatoa upepo ndani ya gari. Tondo alijuwa watu kama hawa walikuwa hatari.

Baada ya kusita kidogo, alijibu kwa sauti hafifu. "Hapana!".

"Nasikia gari nambari ARKK 567 ni lenu?", Willy alimpachika swali Tondo.

"Ndio".

"Nani huwa analiendesha mara kwa mara?".

"Unajua sisi tunafanya kazi ya kuhudumia watalii. Hivyo tunayo magari mengi na madereva wengi. Hatuna dereva maalum kwa gari fulani", Tondo alijibu.

"Nani alikuwa anaendesha gari hilo jana?".

Tondo alisita kujibu kwani alijua jibu la swali hili lilikuwa muhimu sana kwa Willy.

"Jana halikutoka", Tondo hatimaye alijibu.

Willy alijua alikuwa ameongopa tena.

"Kwa nini, lilikuwa bovu?".

"Wakati tunapokuwa hatuna kazi nyingi, magari yetu hufungiwa tu katika gereji".

"Gereji yenu iko wapi?".

"Iko nyuma tu ya ofisi hii", Tondo alijibu.

"Kwa hiyo gari haliwezi kutoka bila ruhusa kamili", Willy alipendekeza.

"Kabisa".

"Oke, ndugu Tondo, vizuri. Samahani kwa kuchukua muda wako", Willy alisema huku akiwa amesimama tayari kuondoka.

"Hivi kuna jambo gani kuhusu hilo gari? Naona sina budi niulize", Tondo aliuliza.

"Wewe umekuwa afisa wa polisi kwa muda mrefu, kwa hiyo ni lazima unaelewa mambo haya", Willy alimjibu. "Wakati mwingine tunapata habari fulani fulani. Inatubidi kuchunguza na kuthibitisha, vinginevyo watu wanaweza wakaumia bure".

"Ni kweli", Tondo alijibu.

"Oke, kwaheri".

"Karibu tena, ndugu Gamba".

"Willy alifungua mlango na kutoka ofisi ya nje. Aliwaaga wale wafanyakazi wa ofisi ile.

Tondo alirudi akaa kitako kitini mwake na kuanza kufikiri.

Willy alipotoka tu nje alitembea haraka sana na kuzunguka nyuma ya ile ofisi. Huko aliona lango la kuingilia katika gereji. Alibisha hodi maana lilikuwa limefungwa. Mara mlinzi alifungua. "Tukusaidie nini, mzee", aliuliza yule mlinzi.

"Jana nilipewa lifti na ndugu Tondo. Lakini kwa bahati mbaya nilisahau miwani yangu ndani ya gari lake. Sasa amenishauri nije nikaangalie kama bado imo iwapo gari hilo halijatoka", Willy alijibu.

"Ahaa, gari alilokuwa anaendesha jana. Si ni lile ARKK 567?".

"Nafikiri", Willy alijibu.

"Basi, limetoka kwenda kujaza mafuta kwenye kituo chetu", alijibu mlinzi.

"Siyo kitu, nitamwambia yeye anitazamie miwani hiyo wakati gari likirudi".

"Haya, kwaheri", mlinzi alijibu huku akirudisha lango.

"Kwaheri", Willy alijibu huku akimwemwesa.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru