HOFU


SEHEMU YA TANO

DAR ES SALAAM

Jijini Dar es Salaam, Tanzania, siku hiyo watu walikuwa wanasherehekea Sikukuu ya Iddy El Fitri kwa hoi hoi na vifijo. Mchana huo watu walikuwa wamejaa katika hoteli ya Kunduchi. Baadhi yao walikuwa wanaogelea, wakati wengine wakitafuna na kula vitu laini. Watu wengine walikuwa wanacheza disco la mchana. Vile vile kuna wale ambao walibaki nyumbani kwa kujuwa wangekosa nafasi kwani hoteli ya Kunduchi ilikuwa imejaa kibati. 

Nje ya hoteli hiyo, karibu na ufukwe, kulikuwepo na meza moja kubwa. Kwenye meza hiyo walikaa vijana wanane. Wanaume wanne na wasichana wanne hii ina maana kuwa kila mtu alikuwa na kitu chake. Wote hawa walikuwa wamefika kusherehekea Iddy pia. Walikuwa wamekaa wakibishana huku wanauchapa mtindi. Wakati huo walikuwa wanabishana juu ya siasa ya ujamaa nchini Tanzania.

"Mimi nawaambieni, hii siasa ndio inayoturudisha nyuma. Mbona kabla ya siasa hii mambo hayakuwa hivi?", Eddy aliuliza.  

"Lakini nchi nyingine zina shida vile vile", alijibu Khadija, "Siyo. Sisi peke yetu".

"Shida za nchi nyingine siyo kama zetu. Ukienda nchi za jirani, utaona wana kila kitu. Kwanini?, kwa sababu hawana siasa hii, bwana. Tusidanganyane", Eddy alisisitiza.

"Hata mimi nakubaliana na wewe Eddy", Rashid aliunga mkono.

"Mimi nilikulia kijijini. kulikuwepo mabasi manne kila siku, lakini juzi nimekwenda huko sikukuta basi hata moja. nilitembea kwa miguu umbali wa kilometa arobaini. Hivi sasa sina hata hamu ya kwenda likizo nyumbani".

"Sikilizeni jamani", Esther alianza kutoa nasaha zake, "Dunia nzima ina matatizo. Mimi naamini siasa yetu ni nzuri, ila kuna mahali ambako makosa yamefanyika. Mnajuwa kila kitu kina uzuri na ubaya wake. Inawezekana siasa hii imeleta madhala ya kiuchumi, lakini tumefaidika kwa upande mwingine watanzania tumekuwa watu wanaopendana na kuheshimiana. Tunao umoja, na mtu mkubwa hamnyanyasi mdogo. Hatuna ukabila. Katika nchi nyingine mnazozungumzia, kama wewe ni mtu mdogo kama sisi wengine hapa unaonekana huna thamani hata kidogo. Achani jamani, siasa hii imetuletea hadhi na haki kwa kila kitu".

"Kwenda zako! wewe utakula au kuvaa heshima?, hii siasa inatuumiza, bwana, acheni", alijibu Rukia kwa hasira.

Mmoja wa vijana hao aliyekuwa anasikiliza maendeleo ya mabishano alimwemwesa, kisha akasema, "Rukia, usikasilike. Hapa tunazungumza tu na kila mtu anatoa mawazo yake. Hivyo poa mtoto, ngoja mimi niwaelezeni jinsi nyinyi mnavyobishana bila msingi. Mnajuwa, kama mtu anataka kubishana juu ya jambo fulani, lazima alielewe kwa undani jambo lenywe. Kila mtu hapa anasema ujamaa ndio umeleta hali ngumu. Lakini hali hiyo imesababishwa vipi na siasa hii?".

"Haya basi, tueleze kama unafahamu", Sammy alichokoza. "Wewe si unajiita mchumi?", Kwanza nyinyi mliosomea uchumi ndio mnatoa ushauri mbaya kwa wanasiasa hapa nchini".

Hapa vijana wote waliangua kicheko.

Kijana huyu alitabasamu kisha akawaashiria wanyamaze na yeye akaendelea kusema. "Azimio la Arusha lilitangazwa mnamo mwaka 1967. Kutokana na tangazo hilo, makampuni makubwa ya binafsi yalitaifishwa. Hatu hiyo ilifanya siasa ya ujamaa ianze kuonekana. Lakini utaona kwamba tangu kutaifishwa kwa makampuni hayo uchumi wa nchi uliendelea kukua kwa kiwango kilichoridhisha. Uchumi ulikua kwa asilimia tano kila mwaka, hadi mwaka 1977. Tulikuwa na fedha za kigeni kiasi cha kutuwezesha kuagiza bidhaa za kukidhi mahitaji ya taifa kwa muda wa miezi mitano. Wakati huo wote sisi tulikuwa hatupati msaada wa fedha kutoka benki ya dunia wala shirika la fedha la kimataifa".

"Hao wenzetu mnaowasema, uchumi wao wakati huo ulikuwa ukikuwa kwa asilimia mbili tu kwa mwaka. Na kukuwa kwa uchumi wao huo kulitokana tu na misaada ya fedha kutoka benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa. La sivyo hali yao ingekuwa mbaya zaidi kuliko sisi. Kwa muda wa miaka kumi ya kwanza ya siasa ya ujamaa, uchumi ulikuwa vizuri sana. Ni muhimu kukumbuka kuwa mnamo miaka ya 1973 - 1976 bei ya mafuta ilipanda. Vile vile kulitokea ukame. Lakini uchumi wa nchi uliendelea vizuri hii inaonyesha wazi kuwa siasa ya ujamaa haikuwa chanzo cha kuanguka kwa uchumi wa taifa letu".

"Ngoja nikukate kilimi", Sammy alimkatiza yule kijana.

"Sasa unafikiri nini kimetokea kama kweli sababu zako ni sawa sawa?".

"Nilikuwa naelekea huko", yule kijana aliendelea kusema.

"Kuanzia mwaka 1978 mambo yalikwenda mrama. Na mambo yote yalitokana na chanzo kilizho nje ya siasa ya aina yoyote. Kwanza Jumuia ya Afrika Mashariki ilivunjika. nyinyi mnajuwa kuwa hiyo ilitifanya tukose vitu kadhaa pamoja na huduma kutoka nchi wanachama wa jumuia hiyo. Bei ya mafuta iliongezeka sana kiasi cha kuathiri uwezo wetu utokanao na fedha za kigeni. Ukame pia uliathiri uchumi wetu. Zaidi ya hayo kulitokea vita kati yetu na majeshi ya uvamizi ya Nduli Iddy Amin. Mambo hayo ndiyo yalifanya uchumi wetu kuyumba. Na mbali na hayo, kumetokea hali fulani ndani kwa ndani. Ari ya mfanyakazi imedhorota".

"Hali ngumu ya maisha imewafanya maafisa wa ngazi za juu kuendekeza rushwa. Ni dhahiri kuwa kuna maamuzi yanafanywa na maafisa wa serikali bila kujali maslahi ya umma. Si ajabu kuona vibari vinatolewa kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kwa shughuri ambazo siyo muhimu. Wakati ule ule sekta za uzalishaji kama kilimo na viwanda zinanyimwa fedha za kigeni za kununulia pembejeo na kadharika siyo sahihi, kwa kweli, kusema kwa njia ya mkato kwamba mambo haya yamesababishwa na siasa ya ujamaa. Na kama nilivyokuwa nimesema hapo awali, shirika la fedha la kimataifa na benki ya dunia havikutupatia hata senti tano. Wakati huo huo wenzetu walipewa mamilioni ya fedha za kigeni".

"Nia ya vyombo hivi ilikuwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unaanguka kwani vilichukia siasa ya ujamaa ambayo ni ya kimapinduzi. Walikataa kutusaidia huku wakifahamu fika kuwa matatizo yetu hayakutokana na siasa ya ujamaa. Lakini iliwafaa kutusingizia. Sasa pia na nyinyi mmejiunga na mabepari katika kulaumu badala ya kujiimarisha...".

"Mara muhudumu mmoja wa hoteli hiyo alifika hapo mezani na kuuliza, "Wewe si ndiye Willy Gamba?".

"Ndio", yule kijana alimjibu haraka muhudumu.

"Kuna simu yako mapokezi".

"Ahsante. Hebu nikasikilize simu halafu nitakuja tuendelee".

Yule kijana aliondoka na kuwaacha wameduwaa kutokana na maelezo yake mazito na yenye msingi.

Pale mapokezi alimkuta muhudumu wa kike.

"Wewe mwanamume, hapo ulipokaa una bibi na bado unatafutwa na bibi mwingine", muhudumu wa kike alimtania yule kijana. "Hutosheni mwenzetu?".

"Nifanye nini, bibie, na wakati ndio huu! lazima niutumie ujana wangu, sitaki kuujutia nikishazeeka", Willy alijibu, kisha akauchukua mkono wa simu na kuupachika kwenye sikio lake.

"Unauchapa tu mwenzetu", sauti ya Maselina ilisikika waziwazi sikioni mwa Willy Gamba.

"Unataka kuja?", Willy aliuliza.

"Unataka huyo bibi yako anikate masikio?" Sina haja ya kuharibiwa sura mwenzako.

"Sasa unasemaje?".

"Nasema hivi: niko ofisini pamoja na Chifu. Unatakiwa kama ulifikili mambo yamekunyookea na huyo msichana uliyenae, basi ulie tu. Unatakiwa sasa hivi. Umenielewa?", Maselina alisema kwa kebehi.

"Hamniachii angalau sikukuu hii nikala raha kidogo?".

"Njoo umweleze mwenyewe maneno hayo huyu babu yako, kwani mimi hiyo raha siitaki? Au kwa kuwa umenizoea unafikiri mabwana hawanitaki. Hata mimi nimechomolewa kutoka kwenye raha na pilika pilika safi za Iddy El Fitri.

"Wacha utani; nakuja sasa hivi".

Willy aliyakata mazungumzo, kisha akaiweka simu chini.

"Vipi huyo mkeo?", yule msichana wa mapokezi alimuuliza Willy mara alipokata simu.

"Afadhali ningekuwa na mke", alijibu Willy huku akielekea kwa wenzake.

Alipofika mezani ilibidi anywe pombe yake haraka ili aweze kuondoka. Jambo zuri ni kwamba vijana wote walikuwa wanafanyakazi ofisi moja na Willy ndiye alikuwa mkubwa wao wa kazi.

"Samahani", Willy aliwataka radhi vijana wenzake. "Imenilazimu nikitoe. Kuna mZee wangu ameshikwa na ugonjwa wa ngiri. Lazima nimpeleke hospitali".

Wale vijana wenzake walielewa ana maana gani ila wale wasichana masikini walidhani maneno ya Willy yalikuwa ya kweli.

"Oh pole sana," Rukia na Esther walisema kwa pamoja.

"Ahsante. Mwana, tunakwenda au unabaki? Willy alimwuliza mpenzi wake.

"Nibaki vipi?" Mwana alihamaki, "huoni kitu mtu hapa? Je, ukiniacha halafu wenzangu wakaamua kuchukua vyumba vya kulala, mimi nitafanyaje?"

"Kwangu wawili ni saizi," Sammy alitania" usiwe na wasiwasi".

"Rukia mwenzetu, mbona unayo shida."

"Maneno tu. Atawahi? kila siku jasho linamtoka," Rukia alijibu huku Mwana na Willy wakiinuka kuondoka.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU