HOFU

ARUSHA

IV

"Hallo, naomba kuzungumza na ndugu Hamisi".

"Wewe ni nani?", sauti ya Katibu Muhtasi ilisikika.

"Mwambie ni mdogo wake aitwaye Willy".

"Mbona yeye analo jina la Ki-islamu na wewe na Kikristo? Utakuwaje mdogo wake".

"Kamwulize".

"Haya, babasubiri".

Baada ya muda kitambo Willy alisikia sauti kwenye simu. "Hallo, Hamisi hapa".

"Willy. Shikamoo, mzee".

"Marahaba. Vipi unaingia mji wa watu bila kuwaona wenyeji?".

"Hivi sasa ndio nawaeleza wenyeji kuwa nipo", Willy alisema.

"Sawasawa. Vipi, sasa unakuja?".

"Nisubiri. Nitakuwa ofisini kwako mnamo dakika tano zijazo".

"Willy alikuwa amepiga simu kutoka kwa rafiki yake karibu tu na ofisi ya upelelezi ya mkoa. Hivyo haikumchukulia muda mrefu kufika ofisi hapo.

"Eh, wewe binti ndiye unayetaka kujua ndugu za mkubwa wako wa kazi? Haya niulize vizuri au umeshamwuliza?", Willy alimwambia Katibu Muhtasi.

Msichana yule alimwangalia Willy kwa jicho la kuibia. Alimwona ni mvulana mwenye sura ya kupendeza na nadhifu. Roho ilimdunda.

"Aha, wewe ndiye Willy", aliuliza.

"Bila shaka", Willy alijibu.

"Kaka yako anakusubiri. Amesema ukifika uingie moja kwa moja", yule msichana alisema huku akilembua macho.

Willy naye alimtolea tabasamu la mwaka akamwacha amebung'aa.

Alifungua mlango na kuingia ndani ya ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa.

"Lo! Mwanaume huyu anaweza kukutia kiwewe. Anavutia hasa", yule msichana alibaki anajisemea kimoyomoyo.

Willy alifungua mlango na kuingia ndani ya ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa mkoa.

"Karibu, Willy", Hamisi alitoa tabasamu.

"Ahsante, mzee", Willy alimjibu Hamisi.

"Kazi iliyofanyika jana usiku nimearifiwa".

"Vizuri".

"Sijui watu hawa wameweza vipi kuingia maana polisi na sisi pia tulifanya tulivyoweza kuhakikisha kwamba watu wanaostahili tu ndio wale wanaingia nchini".

"Mzee Hamisi, lazima ufahamu kuwa watu hawa ni majasusi wa hali ya juu. Hivyo usione ajabu jinsi walivyoingia kwani hiyo ni moja ya kazi yao".

"Ni kweli Willy. Mimi nimeogopa sana. Jana usiku mpigania uhuru mmoja aliuawa kati ya saa tisa na saa kumi huko Maunti Meru Hoteli. Alikuwa chumbani kwake. Hii inaonyesha kwamba, kutokana na kazi mliyofanya, ni dhahiri kwamba siyo hao tu. Kuna kundi kubwa la majasusi tayari liko hapa mjini. Hivi sasa tunakabiliwa na upinzani mkubwa wa kutisha. Ingawa hata wewe uko hapo".

"Hii ni kazi na sisi tuko hapa kwa ajili ya kazi hii. Tunachokiomba ni Mungu atusaidie tuweze kuyasaka na kuyaangamiza majahili hayo, ili mkutano uanze hapo kesho kama ulivyopangwa. Lakini nakubaliana na wewe kwamba kazi kubwa lazima ifanyike, na tutaomba ushirikiano wenu".

"Sisi tuko hapa masaa ishirini na nne na hatutalala".

"Vizuri. Sasa ningependa kujua kama mmekagua hoteli zote ili kuhakikisha kuwa wageni wote waliojiandikisha kulala kwenye hoteli hizi wanatambuliwa sawasawa?".

"Hilo limefanyika baada tu ya kukuta Wazungu wamefariki". Hamisi alijibu. "Polisi pamoja na vijana wangu wamefanya ukaguzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni. Ajabu ni kwamba hata wale Wazungu waliouawa walikuwa hawakujiandikisha kulala mahali popote".

"Basi hii ina maana hawalali hotelini wala katika nyumba za kulala wageni. Hivyo tunabaki na jibu moja; Majasusi hawa wanaishi nyumbani kwa mtu". Willy aliongeza.

"Sasa huyo atakuwa ni mtu gani?", Hamisi aliuliza.

"Hiyo ndio kazi yetu. Ninyi na sisi lazima tutafute watu hawa wanaishi nyumba gani. Ila tu nasema hii itawezekana kama vijana wenu watafanyakazi vizuri. Ili kuwa na uhakika naomba warudie kufanya ukaguzi kwenye hoteli hizo".

"Sawa, tutafanya hivyo. Lakini ikiwa ni nyumbani kwa mtu itakuwa ni vigumu", Hamisi alisema. "Kukagua nyumba hadi nyumba litakuwa jambo la ajabu".

"Sikiliza mzee", Willy alidakia. "Nyinyi hapa mnajua ni watu gani ambao mnahisi wanaweza kununuliwa kwa pesana kufanya kitendo kama hicho, watu mnaowashuku sharti kuwapeleleza usiku na mchana ili kufahamu ni nani wanaingia au kutoka kwenye nyumba zao. Kama mkihisi au kugundua kitu chochote, tafadhali tunaomba mtujulishe".

"Mawazo yako ni sawa kabisa. Hata hilo pia nitalitekeleza", Hamisi aliitikia."

"Kuna habari nilizoleta ofisini kwako kuhusu magari mawili ili yachunguzwe ni ya aikina nani, sijui kama umepata majibu?", Willy aliuliza.

"Ndio, lile walilokuwa wanaendesha wale Wazungu linaonekana halikusajiliwa hapa Arusha. Wala popote nchini Tanzania. Ni jambo la ajabu sana kwani namba za injini siyo namba za gari ya aina hiyo iliyoingia hapa nchini, bali gari aina ya Peugeot 505 na muundo wa karibuni. Tumepeleleza na kushirikiana na wenzetu wa Kenya nao wanasema nambari hiyo hawana", Hamisi alieleza.

"Basi anchana nalo. Je, na lile gari lenye namba ARKK 5677?".

"Gari hilo linamilikiwa na kampuni ya kitalii ya Nyota Tours and Safari ya hapa mjini Arusha. Lakini tumechunguza na wenye gari hilo. Wao wanasema gari hilo halikwenda uwanja wa ndege jana. Aidha ni watu tunaowaamini sana hapa mjini. Mwenye Kampuni hii ni Mhindi mmoja tajiri sana ajulikanaye kwa jina la Feroz Kassam; mtu ambaye anaaminiwa sana hapa mjini. Ni Mhindi wa aina yake hapa nchini.

Willy alikumbuka habari kuhusu Mhindi huyo. Alikuwa ameelezwa sifa zake siku nyingi. Hasa alisifika kutokana na misaada yake na utiifu wake kwa Chama na Serikali.

"Aha, ni nani aliyetoa majibu haya? Ni F.K mwenyewe, kama mnavyomwita, au ni mtu mwingine", Willy aliuliza.

"Hapana. Ni meneja mkuu wa kampuni hiyo anaitwa Chris Tondo".

"Huyo ni nani?".

"Nilisema ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo".

"Nina maana ya kuuliza ni mtu wa namna gani kutokana na mwenendo wake kiusalama?".

"Huyu amewahi kuwa afisa wa cheo cha juu katika Jeshi la Polisi na alistaafu kwa manufaa ya umma miaka iliyopita. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na tuhuma kwamba alikuwa anasaidia wafanya magendo kuvusha mali nje ya nchi. Lakini toka siku hizo mpaka leo rekodi yake ni nzuri sana. Hajawahi kuwa na tatizo kiusalama wala katika maisha ya kawaida".

Willy alifikiri kidogo halafu akauliza tena. "Je, katika jalada lenu kuna habari kuhusu ilikuwaje mpaka akafanyakazi kwa F.K?".

"Hapana, bali tulifikiri aliombewa hiyo kazi na rafiki zake".

Willy alikuwa hakuridhika juu ya Chris Tondo. Aliinuka na kuaga akisema. "Nafikiri wewe tekeleza hayo mambo tuliyozungumza halafu tuonane baadaye".

"Sawa", Hamisi aliitikia.

Waliagana na Willy aliondoka kwa kupitia mlango wa Katibu Muhtasi.

"Wewe unaitwa nani?", Willy aliuliza.

"Naitwa Carol!" Yule msichana alijibu huku moyo wake ukimdunda.

"Iko siku Carol", Willy alimwambia Carol huku akifungua mlango na kupotea.

Alimwachia Carol kiu ya maelezo zaidi Willy alipoondoka pale ofisini aliamua kwenda Nyoka Tours and Safaris.

ITAENDELEA...

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru