HOFU

SEHEMU YA TANO

DAR ES SALAAM
III

Wakati Willy alipokuwa anaelekea kwake alianza kuwafikiria akina Bon na Rocky. Kule kuwafikiria kulimfanya apate nguvu rohoni mwake. Hii ilitokana na kwamba Willy aliwafahamu fika hao wenzake na zaidi ya hayo aliwaamini. Alifikiri sana juu ya kazi iliyokuwa mbele yake. Ni kweli kwamba kazi hiyo ilikuwa imewekewa uzito wa hali ya juu kama ilibidi kuwatuma watu wote hawa watatu katika operesheni moja. Mchukue Bon. Kwa mara kwanza Bon kufahamiana na Willy ilikuwa huko Japan ambako wote wawili walikuwa wanachukua mafunzo ya Ninja. Willy alikuwa amehitimu mapema na kumwacha Bon ambaye alikuwa amejiunga na chuo hicho nyuma yake. Willy alikuwa amemsaidia sana Bon katika masomo yake na alijuwa fika kwamba Bon nae angehitimu tu.

Bon alimchukulia Willy kama kaka yake na wote wawili walipendana sana. Baada ya mafunzo yake Bon alirudi Zimbabwe ambako alikuwa anakaa. Wakati huo Kamati ya Ukombozi ya nchi huru za Afrika iliwatuma kazi muhimu ambayo waliifanya kwa mafanikio makubwa. Kazi hiyo ilifanyika ndani ya Afrika Kusini na mpaka leo makaburu hawaamini kwamba kazi hiyo ilifanyika na watu wawili. Kisa hiki kukieleza kingechukua siku nzima, hivyo naachia hapa. Bali tu niseme kuwa safari yao huko Afrika Kusini iliwafanya wafahamiane vizuri na kila mmoja kudhibiti ujuzi na uwezo wa mwenzake. Kwa hiyo Willy, alipojuwa kuwa angekuwa na Bon katika kufanya kazi hii, basi wasiwasi ulitoka.

"Ninja wawili kutumwa Arusha. Kwani huko kuna nini?, labda makaburu watume jeshi zima", Willy alijisemea kimoyomoyo. Alimfikiria Rocky pia. Ingawa ni mara yake ya kwanza kufanyakazi nae, umaarufu wake ulijulikana Afrika kote. Walikuwa wameonana mara mbili. Lakini ilijulikana Rocky alishatumwa kazi ambazo zilifanana sana na kujituma mikononi mwa kifo. Pamoja na hali hiyo, Rocky alikuwa amefanyakazi hizo na kurudi salama. Kuweza kufanyakazi kama hizo kulimdhihilishia Willy kuwa Rocky alikuwa mtu jasiri sana. Willy aliamini kuwa yeye na vijana hao wawili walikuwa na uwezo wa kuwazuia makaburu kusababisha maafa katika mkutano huo muhimu wa wapigania uhuru.

Kulikuwapo habari za kipelelezi kuwa baada ya mkutano huo, mapambano ya kupigania uhuru yangeahamia ndani ya Afrika Kusini. Kwa hiyo kama makaburu walikuwa na fununu juu ya habari hizi, ilikuwa ni dhahiri kwamba wangejitahidi kuvuruga mkutano huo, kinyume cha kufanya hivyo ilikuwa kufungua mlango ili wapigania uhuru waiangishe serikali ya makaburu. Makaburu walijuwa fika kuwa mkutano huo ulikuwa hatua ya kwanza muhimu katika safari ya kuuangusha utawala wao bila kujali safari hiyo ilikuwa ndefu kiasi gani. Kuzuia hatua hiyo ilikuwa lazima kwao.

Alipofika nyumbani Willy alikwenda bafuni na kuoga. baadae alifungua sanduku lake ambamo alikuwa anatunza zana zake muhimu za kufanyia kazi. Alizichukua na kuziweka kwenye mkoba wake, alipiga simu kwa Sammy ambaye alimwarifu kuwa alikuwa anasafiri kwenda Arusha na kuwa habari zaidi angezipata ofisini. Vile vile aliomba atumwe mtu uwanja wa ndege kwa ajili ya kurudisha gari lake. Sammy alikuwa chini ya Willy kikazi lakini walikuwa marafiki wakubwa sana na mara nyingi walifanyakazi pamoja. Baada ya kupiga simu aliondoka kuelekea Mwenge ili kumwaga Mwana.

Alifika nyumbani kwa Mwana mnamo saa moja usiku. Tiketi yake ilikuwa inaonyesha kuwa safari yake ilikuwa saa tatu na nusu usiku. Hivyo Willy alikuwa bado na muda kuzungumza machache na mpenzi wake. Alipofika alibisha hodi na kufunguliwa mlango. Alikaribishwa ndani. Mwana alikuwa amejinyoosha na huku amejifunga kanga tu.

"Afadhali umekuja, nilikuwa na wasiwasi! vua ulale", Mwana alimwambia Willy.

"Nimekuja kukuaga", alijibu Willy.

Mwana aliinuka na kanga aliyokuwa amejifunga ikadondoka. Willy alitupa macho yake na kuona mwili wa mtoto huyu ambaye ubichi wake ulisisimua na kuchangamsha roho. Matiti yalisimama kwenye kifua chake kilichokuwa kinatweta utafikiri ni mapera yaliyoiba. Mwana alimrukia Willy aliyekuwa amekaa kwenye tendegu la kitanda na kumkumbatia. Joto la msichana huyu lilimwingia willy kama kisu kinavyotoka na kuingia ndani ya siagi. Ilihitaji mtu mwenye roho ngumu kama Willy kushinda jaribu hili.

"Mwana tafadhari niache niende", Willy alimsihi.

Mwana ambaye sasa alikuwa anatokwa na machozi alisema kwa uchungu, "Willy, kwanini unanitesa? kama hunitani si heri unieleze tu. Kama huna hamu na mimi kwanini ulinidanganya tangu siku ya kwanza. Kwanini usingeniambia ukweli kuliko kunitesa hivi, ooh! mungu wangu nimekosa nini mie".

Mara Mwana alijitupa kitandani na kuanza kulia; machozi yakimtililika kama mtoto mdogo.

"Mwana tafadhali, kuna kazi imetokea ghafra. Nilipotoka tu hospitali kumpeleka mzee nilikuta tiketi na ujumbe kutoka kwa mkubwa wetu wa kazi kuwa lazima niende Arusha. Kama ujuavyo sisi wafanyabiashara safari zetu ni za ghafra ghafra tu. Wewe unafikiri ni kijana gani ambaye anaweza kumwacha msichana mbichi kama wewe kwa siku na saa kama hii, na hasa baada ya raha ya leo mchana? Huyo huenda siyo mwanaume kamili", Willy alijibu kwa uchungu pia kwani hata yeye alikuwa amesisimka.

"Basi lala angalau kidogo. Dakika tano tu", Mwana alimwomba Willy.

"Mwana mambo haya hayaendi namna hiyo. mimi nitarudi baada ya siku mbili au tatu. Baada ya hapo wewe mwenyewe utajua kuwa nina hamu kiasi gani mimi na wewe," Willy alijibu.

"Haya nenda. Nakuruhusu," MWana alisema kwa uchungu.

Willy aliinama na kumbusu. Alisikia lile joto tena. Bila kusita aliinuka, akafunga mlango nyuma yake na kwa maudhi alijisemea, "Kwa kweli kazi nyingine......!".

Alipoingia ndani ya gari aliweka nyuma mawazo kuhusu Mwana. Wakati akiendesha gari, alifikiria safari iliyokuwa mbele yake.

Alifika uwanja wa ndege saa mbili usiku. Aliweka gari lake kwenye maegesho. Kisha alitoa swichi kwenye funguo zake na kuiweka mahali pa hifadhi ya swichi za magari. Hivyo ingemwezesha kijana ambaye angekuja kurudisha gari lake kuichukua hapo. Alifunga milango mitatu na kuacha mmoja umerudishiwa. Kisha kuchukua mkoba wake na kuelekea kwenye jengo la uwanja wa ndege.

"Tiketi yake tafadhari", aliomba Afisa Usalama hapo uwanjani.

Wakati anatoa tiketi yake alikuwa akiangaza huku na kule katika jengo zima.

"Haya endelea", alisema Afisa Usalama huku akimrudishia Willy tiketi yake.

Alielekea ndani. Kwenye kaunta alimkuta msichana aliyemfahamu.

"Willy, safari tena?", msichana aliuliza.

"Ndio", alijibu Willy.

"Wapi".

"Arusha".

"ZIko ndege mbili usiku huu. Wameongeza nyingine kwa sababu wageni wengi wanakwenda Arusha kwenye mkutano", msichana yule alimweleza Willy.

"Alaaa, sasa mimi niko ndege ipi?", Willy aliuliza.

"Chaguo lako. Sema unataka ipi. Iko ya saa tatu na nusu na pia ile ya saa nne na nusu", mischana alijibu.

"Subiri kwanza, ile ndege kutoka Harare imefika?".

"Ndio. Imefika saa moja".

"Kulikuwamo wageni wangu wanaopitiliza kwenda Arusha", Willy alisema.

"Majina yao tafadhari", msichana aliomba huku akimsogeza Willy pembeni ili watu wengine wasiweze kusikia. Halafu alimtaka aendelee.

"Sipele na Malele".

Msichana yule aliangalia kwenye orodha ya majina ya wasafiri kisha akainuka.

"Ya, wote wapo. Sasa hivi wanakula kwenye mghahawa hapo juu. Wataondoka kwa ndege ya saa nne na nusu", msichana alieleza.

"Oke, mimi niweke kwenye ndege ya saa tatu na nusu", Willy alisema.

Jina lake liliwekwa katika orodha.

Halafu alisema, "Hebu nikawaangalie hapo juu".

Alipopanda kwenye baa na mghahawa alikuta watu wamejaa ndii. Huku akisalimiana na watu huku na pale, Willy alijipenyeza kupita kwenye baa mpaka kwenye mghahawa. Mara aliwaona Bon na Rocky wamekaa kwenye kona wakila na kuzungumza. Aliwaendea polepole na Rocky ndiye alikuwa wa kwanza kumuona Willy.

"Bon, Willy yule".

"Aaaa mzee!", Bon alisema kwa furaha huku akiinuka na kumkumbatia Willy.

"Usinipakazia uzee, Bon, au huoni humu ndani kuna watoto. Unataka kuniharibia soko, vipi?", Willy alisema kwa mzaha.

"Hujaacha matani yako tu?", Bon aliuliza huku wakipeana mikono.

"Keti, bwana", Rocky alimvutia kiti.

"Ehee, leteni habari", Willy alisema.

"Mambo safi", Rocky alijibu.

"Safari, je".

"Safi kabisa", alijibu tena Rocky.

"Tulipata habari kuwa tungeungana hapa", alisema.

"Mimi nimeambiwa leo mchana", Willy alijibu.

"Kila mara huyo mzee wako anapenda kukushtusha", Bon alitania.

"Wazee wengine kama ujuavyo...", alisema Willy.

"Chakula vipi", Rocky alimuuliza willy.

"Mimi ndiye napaswa kuwauliza swali hilo kwa kuwa mko nyumbani kwangu", alisema Willy.

"Tumwisha jikaribisha", Bon alijibu.

"Vipi mzee wako kakupasha kidogo?", Rocky alimuuliza Willy kwa sauti ya chini.

"Kanipasha", Willy alijibu.

"Je, tutasafiri katika ndege moja".

"Hapana, mimi sina budi nitangulie na ile ya tatu na nusu, kama ujuavyo wote hatuwezi kusafiri katika ndege moja, ikianguka, je", aliuliza Willy.

"Willy hubadiliki", Rocky aliuliza.

"Siku nikibadilika ndio siku nitakapoacha kazi hii", Willy alijibu.

"Ni kweli, maana waati huo itakuwa ni hatari kwa maisha yako", Bon aliongeza.

Waliendelea kuzungumza huku wakiangalia kwa chati; kila kona ili kuona kama kuna watu waliowatia maanani. Lakini kufuatana na hali ya mambo ilionekana kila mtu alikuwa anashughulika na mambo yake.

"Tukutane hotelini kwangu mnamo saa sana usiku", Rocky alieleza.

"Wewe uko hoteli gani?", Willy aliuliza.

"Mimi niko Equator Hoteli kwa leo halafu nitahamia Maunt Meru hapo kesho, Bon alitaka Safari Hoteli", Rocky alimjibu.

"Basi mimi naona tukutane kesho asubuhi, mpate kupumzika leo kwani huenda kukawa na kazi kali baadaye. Mimi nitafikia New Arusha Hoteli", Willy alieleza.

"Mimi nafikiri maneno yako ni sahihi Willy", Bon alijibu.

"Oke, tuonane wapi na saa ngapi".

"Njooni hotelini kwangu saa tatu asubuhi", alijibu Willy.

"Oke, ahadi........", Rocky alijibu.

Mara walisikia tangazo;

Shirika la ndege Tanzania: Ndege namba 1001 iendayo Arusha, niko tarari kuondoka, abiria wote wanaosafiri na ndege hii wanaombwa kuelekea kwenye ndege hiyo sasa hivi.

"Jamani eeh, kwaherini. Tutaonana kesho", Willy aliwaaga wenzake na kukimbia akitelemka chini.

Alipofika kwenye kaunta alimkuta tena yule msichana.

"Siku nyingine utaachwa wewe".

"Niko macho", Willy alijibu.

"Utaniletea nini ukirudi?".

"Vitunguu".

"Nitafurahi sana. Haya safiri salama", yule msichana alimwaga.

"Ndipo Willy alikumbuka kuwa alikuwa hajakata tiketi ya malipo ya kiwanja. Hivyo alifanya karaka na kukata tiketi hiyo. Halafu alirudi na kwenda kwenye chumba cha kuondokea. Hapo chumbani Willy alikuta msururu bado mrefu sana.

"Lo! Leo pana jua nini iko. Watu hapana panda", Mhindi mmoja alilalamika.

Huenda kuna mtu anayo bastola. Labda wanaogopa kutekwa nyara maana hapo ndani wanakagua sana", Kijana mmoja alijibu.

Msururu huo ulikwenda pole pole, lakini hatimaye wote walipekuliwa. Kisha waliruhusiwa kuingia ndani ya ndege. Willy alikuwa ameridhishwa na upekuzi ule kwani ulikuwa upekuzi kweli kweli.

Willy alikaa nyuma kiti cha mwisho kama kawaida yake. Alifunga mkanda na kisha na kisha akakaa akisubiri matangazo ambayo alishayasikia mara elfu kidogo. Hayo yalikuwa matangazo ya IATA yahusuyo usalama wa usafiri wa anga. Baada ya matangazo hayo, ndege yao aina ya Boing 737 ilirushwa na vijana hawa wa Kitanzania.

Willy aliinamisha kiti chake kikakaa sawa. Akaanza kufikiri juu ya yale yote aliyokuwa akiambiwa na Chifu. Alichambua kipengele kimoja baada ya kingine na namna ya utekelezaji wa kazi nzima.

"Patakuwa na kazi", Willy alisema moyoni kwake.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru