HOFU

ARUSHA

VII

Ilikuwa saa saba na nusu za mchana. Willy, Bon na Rocky walikuwa wakila chakula pale pale New Arusha Hoteli. Ilikuja simu ambayo ilimhitaji Willy.

"Wewe mzee ndiye Willy Gamba?", mhudumu mmoja alimwuliza Willy.

"Ndio".

"Kuna simu yako".

"Sawasawa", Willy alisema huku akiweka kisu na uma kwenye sahani.

Alikwenda kusikiliza simu.

"Hallo, Willy hapa", Willy alisema baada ya kuunyakua mkono wa simu na kuupachika katika sikio lake la kushoto.

"Hapa ni mapokezi. Kuna mgeni wako ngoja uzungumze naye".

Hallo, Mike Maina", sauti ilisikika.

"Wewe unafanya nini hapa", Willy aliuliza kwa mshangao kwani alikuwa hakumtegemea.

"Nimekuja kukutafuta. Kwani wewe unafanya nini hapa", Maina aliuliza.

Willy alifahamu kwa nini Chifu alikuwa amemtafuta; Maina alikuwa ameletwa ili kuongeza nguvu.

"Njoo kwenye ukumbi wa maakuli. Utatukuta kwani nafikiri una njaa", Willy alimwambia.

"Nitakuja kwa haraka kama jeti", Maina alijibu.

Maina alimkuta Willy na wenzake wakiendelea kula chakula.

"Hallo Maina, karibu", Willy alimkaribisha Maina huku wenzake wakisimama.

"Ahsante Willy, mambo?", Maina aliuliza.

"Mambo ni segemnege", Willy alijibu huku akivuta kiti na wote wakakaa.

"Hebu nikujulishe kwa hawa ndugu zetu hapa. Naamini hamfahamiani", Willy alisema. "Huyu ni Bon Sipele wa wapigania uhuru na huyu ni Rocky Malele wa Zimbabwe".

Kisha Willy alimgeukia Maina na kusema. "Na huyu jamani ni Mike Maina kutoka Kenya".

Wote walisalimiana.

"Nilipata habari zake Angola alipokuwa naye. Mlifunga kazi takatifu", Bon alisifia.

"Basi, huyu ndiye Mike Maina", Willy alisisitiza.

Mhudumu alifika mezani na Maina akaagiza chakula.

Wakati huo Willy, kwa sauti ya chini, alikuwa anaeleza sifa za kipelelezi za kila mmoja.

"Basi mambo yanazidi kujipa", Rocky alisema.

"Sasa Mike, tupe habari za huko Nairobi. Nikisoma sura yako nahisi kuna mambo", Willy alichokoza.

"Haya, nisikilize kwa makini halafu na nyinyi baadaye mnijulishe mambo ya hapa", Mike alisema.

Mike aliwaeleza yaliyotokea Nairobi huku akiendelea kula chakula. "Nilipopita mpakani leo nilishangaa. Nilikuta rafiki yangu Peter Gerrit kaishapita. Alitumia jina la Peter Anderson na kudai yeye alikuwa ni Askofu kutoka Zimbabwe akija kuhudhuria mkutano wa wapigania uhuru. Kwa sababu hiyo maafisa usalama na uhamiaji wakampitisha haraka. Hivyo yuko hapa na mnaweza kuona wenyewe hali ya mambo".

"Kwa hiyo rafiki zangu", Willy alimalizia. "Mji huu umeingiliwa na balaa. Bila shaka damu itamwa

gika. Tuwe tayari kujitoa mhanga ili wale watakaobaki wawezi kufaidi matunda ya uhuru. Uhuru ni kitu muhuimu kwetu na kwa vizazi vijavyo".

Bon alisema. "Na sisi watu wa Afrika Kusini tunaamini kwamba kabla ubaguzi wa rangi haujatokomezwa ni lazima damu ya wazalendo itamwagika. Tuko tayari kwa yote hayo. Kama mnavyosikia, hata vijana wadogo wameamua kujitoa mhanga ili kutokomeza utawala wa Makaburu kwa faida ya walio wengi. Kwa hiyo Willy, mimi niko tayari kufa kwa ajili ya nchi yangu. Lakini kabla sijafa, nitahakikisha nao wanakiona cha mtema kuni".

"Kwa sasa hivi mipango gani?", Mike aliuliza.

"Kwanza kabisa nimempigia simu mtu wetu hapa, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa, Ndugu Hamisi", Willy alieleza. "Ameweka vijana wa kumfuatilia Chris Tondo. Ninayo imani kuwa yeye anaweza kutufikishia walipo hawa majasusi. Sina shaka mtu huyu anahusika nao kwa namna fulani".

"Kama inao uhakika", Mike alishauri. "Kwanini tusimufuate sisi wenyewe, ikibidi tumsakame mpaka atueleze tu? Wewe mwenyewe unajua kuwa tuna uwezo wa kumfanya mtu hata mwenye kichwa ngumu kama, atatapika maneno".

"Hapana, tusifanye haraka, maana watu kama hawa wanazo mbinu nyingi", Willy alieleza. "Lakini hata sisi tunazo mbinu zetu. Tunaweza kumfanya akatueleza mahali walipo bila kutumia nguvu zetu nyingi. Unajuwa bado tunahitaji nguvu zetu hasa kwa kupambana na hawa majahili", alieleza Willy, halafu akaanza kuwapa mipango kwa ajili ya usiku ule".

"Sisi tutasimama badala ya hawa viongozi wa wapigania uhuru. Sisi pamoja na wao ndiyo wanaowindwa. Hivyo kuanzia saa tatu tutajipoteza maana watu hawa watakuwa wanatuvinjari".

"Tumekuelewa barabara", Rocky alidakia. "Na ninaamini mipango yako ni sawasawa kabisa".

"Mike, kula", Willy alishauri mara mhudumu alipoleta chakula. Mhudumu alipoondoka. Willy na wenzake waliendelea na mazungumzo yao.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU