HOFU

NYASO

II

Chris Tondo alikuwa anaishi sehemu inayojulikana kama 'Corridor Area! Wakati Willy na Nyaso walikuwa wanaelekea huko kupitia barabara ya Haile Sellasie, walipishana gari dogo aina ya Datsun.

"Gari hilo ni la F.K. na anaendesha mwenyewe. Kwa kawaida huwa haliendeshi gari hilo. Mara nyingi huwaachia watumishi wake na yeye anatumia ile Benz yake, kwani anazo gari tatu hapo nyumbani kweke", Nyaso alimwambia Willy mara walipopishana na ile Datsun.

F.K. alikuwa hakuwatambua.

"Huenda amechoka kuendesha magari makubwa", Willy alisema.

"Nyumba ya Chris Tondo ni ya nne kutoka nyumba hiyo hapo".

"Basi, egesha mahali pazuri na mimi nitatoka kwa muda wa robo saa", Willy alimwambia Nyaso.

"Mimi nitaingia katika nyumba hii kumwona rafiki yangu", Nyaso alisema "Nitatoka baada ya robo saa ambapo wewe pia utakuwa tayari. Tafadhali Willy, kama watu hawa ni hivyo unavyohisi, basi ni watu wabaya, ni vizuri kuchukua tahadhari wasije wakakudhuru".

"Usijali, tutaonana baada ya dakika hizo", Willy alisema huku akitokomea gizani.

Nyaso aliyekuwa anamwangalia Willy huku akimwemwesa alijikuta anajisemea kimoyomoyo. "Jinsi nilivyomzoea! Utafikiri tumeishi naye miaka mingi. Hivi sasa ninavyojisikia ovyo kumkosa hiyo robo saa".

Nyaso aliondoka akaenda kubisha hodi mlangoni kwa rafiki yake.

Willy aliambaa kwenye nyufa za nyumba jirani na ile ya Chris Tondo. Aliwaona vijana wawili kwa mbali wakipotea kwenye giza la michongoma ya nyumba iliyotazamana na ile ya Chris Tondo. Mara alitambua wale walikuwa vijana wa Hamisi. Kwa kuwa hakutaka wamwone, Willy alijipeneyza kwenye sehemu ya kushoto ya ua. Kwa ustadi kama wa paka Willy alipanda ukuta na kudondoka uwani bila kishindo.

Aliangaza huku na kule na kwa bahati nzuri aliona dirisha kwa upande huo liko wazi. Aliona taa ilikuwa inawaka kwenye chumba upande wa sebule. Willy alihisi kilikuwa chumba cha kulala cha Chris. Basi alijinyanyua, akakwea hadi ndani ya nyumba kupitia dirishani. Huku bastola ikiwa mkononi mwake. Willy alijikuta kadondoka bafuni. Alipofungua mlango taratibu alijikuta yuko kwenye njia nyembamba iliyokuwa inatenganisha vyumba. Aliamua kwenda sebuleni ambako alihisi Chris angekuwepo.

Willy alifungua mlango kwa ghafla ili asimpe nafasi Chris ya kuwa tayari kujihami. Lakini alishangaa kukuta chumba kile kilikuwa kitupu. Taa ya mle chumbani ilikuwa inawaka na Willy aliona jinsi chumba kile kilivyokuwa cha fahari isiyo kifani. Alijongea na kuelekea kwenye chumba kingine ambacho kilikuwa kinawaka taa pia. Hata hivyo, Willy alishangazwa na ukimya uliokuwa ndani ya jumba hilo.

Alifikiri labda walipopishana na gari la F.K. Nyaso alikuwa hakuona vizuri kwani huenda hata Chris alikuwa kwenye gari lile lile. Wakati anafikiri yote hayo, aliamua kuendelea na mpango wake. Kwa kasi kama umeme Willy alifungua mlango wa chumba hicho. Kumbe loo mle ndani alikuta maiti tatu! Baada ya kuangalia vizuri aligundua kuwa watu watatu hao waliuawa kwa kupigwa risasi. Walikuwa ni Chris Tondo, msichana mmoja mrembo sana ambaye Willy alihisi kuwa alikuwa binti yake Chris pamoja na mlinzi mmoja kutokana na mavazi yake..

"Bila shaka kazi hii ni ya F.K.; ameniwahi", Willy alijisemea kwa uchungu.

Bila kupoteza muda, alitoka nje kwa kupitia njia aliyokuwa ameingilia. Alipokuwa nje alimwona Nyaso naye anatokea kwenye lango la nyumba ya rafiki yake, walipoingia ndani ya gari, Willy alimwambia Nyaso.

"Hebu endesha gari haraka ili tutoke kwenye sehemu hii. Chris, mlinzi wake pamoja na binti yake wameuawa. Nipeleke hotelini kwangu kwani sasa kazi imeanza", Willy alimwambia Nyaso.

"Huyo ni F.K. Willy, ndiyo sababu tulikutana naye akitoka huku", Nyaso alisema.

"Bila shaka", Willy alikubaliana na Nyaso.

"Masikini Betty kauawa bure mtoto wa watu. Mimi ndiye niliyemfahamisha kwa Chris, oh Betty! Willy uliyohisi ni kweli. F.K. utakiona ", Nyaso alisema kwa uchungu. Aliendesha kuelekea New Arusha Hoteli. Willy alipoangalia saa ilikuwa saa tatu na robo. Alikuwa amechelewa robo saa lakini alikuwa amejua mengi.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU