HOFU

SEHEMU YA NANE

NYASO

Ilikuwa saa kumi na mbili juu ya alama, Nyaso alipoegesha gari lake hapo New Arusha Hoteli. Willy alikuwa anaranda pale nje ya hoteli akimsubiri.

"Nimeamini kuwa unajuwa kuweka ahadi mtoto we, Wasichana wengi wa Kiafrika hawaweki muda maanani", Willy alisema huku akifungua mlango wa gari na kuingia ndani.

"Wacha kutuonea, siku hizi tumebadilika, hujui kuwa wakati huu unajulikana miaka ya elekttroniki! Watu lazima kwenda kwa wakati", Nyaso alijibu huku akiondoa gari.

"Unanipeleka wapi?", Willy aliuliza.

"Nilipiga simu 'Kambi ya Fisi' na kuomba watuwekee nyama ya kuchoma", Nyaso alijibu.

"Hiyo ni maridadi", Willy aliitikia aliitikia halafu akaendela. "Vipi maisha hapa".

"Mwenyezi Mungu anatusaidia".

"Umeishi hapa Arusha kwa muda mrefu?".

"Miaka mitano hivi".

"Mimi nakuja hapa mara kwa mara lakini sijawahi kukuona, sijui huwa unajificha wapi?".

"Mbona maswali mengi? Unajuaje, huenda mwenzio nimewekwa kinyumba?", Nyaso alimtolewa Willy jicho la kiwiziwizi.

"Unasema kweli, hebu nisiulize maswali mengi kwani ninaweza kujiumiza roho bure".

"Pole sana".

Waliendelea na safari mpaka 'Kambi ya Fisi'.

Walipowasili Willy aligundua kuwa wahudumu wa pale walikuwa wanamfahamu sana Nyaso. Hiyo ilitokana na kwamba walipowasili Willy aliona wahudumu wakimkimbilia Nyaso na kuwapa mahali pazuri pa kukaa.

"Nyama uliyoagiza karibu itakuwa tayari", mhudumu alisema. "Utasubiri kidogo tu".

"Hakuna tabu", Nyaso alijibu wakati wakikaa kwenye viti.

Watu wengi walikuwa pale ambapo pia walikuwa wamekuja kuchoma nyama.

"He, leo ni maajabu! Umemwona Nyaso kaja na mwanaume! Siyo maajabu haya?", kijana mmoja aliwauliza vijana wenzake wapatao watano.

"Huenda ni kaka yake", kijana mwingine alisema. "Huoni kuwa hata kijana mwenyewe anayo sura nzuri".

"Watu wanasema eti Nyaso hana ndugu, sasa huyo kaka katoka wapi", kijana wa kwanza alidadisi.

"Ya nini kuingilia maisha ya watu? Ndio sababu nyinyi waswahili hamwendelei. Mnapenda kuchunguza maisha ya wengine huku yale ya kwenu yanawashinda. Kama huyo kijana kaka yake au bwana yake nyinyi inawahusu nini? Iwapo mtu anavutiwa si heri akatafute nafasi yake halafu abahatishe tu? Vinginevyo kama Nyaso kapata bwana mwingine na kumwacha F.K hicho ni kilio chake F.K", kijana mwingine aliyeonekana kuwa mkubwa kidogo kuliko wengine aliwaasa wenzake. Hivyo iliwabidi kujali yaliyowaleta.

"Unafanya kazi wapi?", Willy alimwuliza Nyaso wakati wakinywa vinywaji baridi.

"Sasa hivi sifanyi kazi yoyote, ila naadaa kitabu".

"Eh, kitabu kuhusu nini?".

"Kinahusu uchumi wa nchi yetu"."Wewe ni mtaalam wa mambo ya uchumi?".

"Ndiyo. Ninayo shahada ya kwanza katika uchumi".

"Ahaa vizuri sana. Hata mimi ni hivyo hivyo".

"Na wewe unafanya kazi gani?".

"Mimi niko Dar es Salaam ambako ninafanya biashara".

"Na hapa Arusha umekuja kufanya nini?".

"Mimi ni shabiki wa siasa, hivyo nimekuja kusikiliza mkutano wa hawa wapigania uhuru".

Nyaso alimwangalia bila kuamini masikio yake.

"Mkutano kama huu utakusaidia nini na wewe ni mfanya biashara?", Nyaso aliuliza.

"Nimekwambia kuwa mimi ni shabiki wa siasa. Madhumuni ya shabiki wa kitu chochote siyo kupata faida ya mali, bali kufanya mioyo yao ifurahi".

"Lakini wewe huelekei kuwa mtu wa kushabikia kitu hivi hivi tu".

"Sijui sasa", Willy alijibu kisha akaendelea. "Mimi nilifikiri unafanya kazi Nyoka Tours and Safaris maana kabla hujavamiwa na yule jambazi nilikuona unatoka kwenye ofisi zao".

"Hapana, mwenye kampuni hiyo ndiye bwana yangu", Nyaso alijibu huku akiangalia chini.

Willy alisikia damu inamsisimka.

"Una maana ya F.K au Chris?", Willy aliuliza.

"Ni nani katika nchi hii ambaye hamjui F.K? Yule ni mtu maarufu sana".

"Basi, ni huyo F.K".

"Hongera, Nyaso kwani kwa mara ya kwanza nimeona msichana wa Kiafrika ambaye ni binti wa mvulana wa Kihindi kiwaziwazi bila kujificha".

"Nimekwambia Willy dunia inageuka.

Willy aliisifu tena nyota yake, kwani kama kweli msichana huyu alikuwa bibi yake F.K, basi bila shaka alimfahamu sana Chris Tondo. Ilikuwa ni bahati kwamba Willy, kama alivyofikiri, angejua mengi kutoka kwa Nyaso.

"Bahati yangu mbaya. Mimi nilifikiri nimepata mchumba kumbe wameisha niwahi", Willy alinung'unika.

Nyaso alimwangalia Willy na kumhusudu. Alifikiri ingekuwa furaha iliyoje kama angeolewa na kijana mzuri kama yule. Akimlinganisha Willy na F.K, Nyaso alijilaumu. Alijua alikuwa anaishi na F.K kwa sababu ni yeye tu amabaye aliweza kumtimizia mahitaji yake kipesa, hakuwa na mapenzi yoyote juu ya F.K. Lakini sasa matayarisho ya mpango wake yalikuwa yanakaribia kukamilika. Nyaso alikuwa na nyumba tayari. Alikuwa na gari na pesa pia. Hivyo angeweza kuanza opereshani wakati wowote. Alipofikiri hayo, Nyaso alijisikia machozi yanamlengalenga.

"Nini sasa, dada umekuwa nini?", Willy aliuliza alipomwona msichana huyu akitokwa na chozi la hudhuni. Na ilikuwa ajabu kwamba Nyaso alipotokwa na machozi ndiyo alivyozidi kupendeza.

"Usijali, kila mtu huwa na matatizo yake. Nimekumbuka jambo ambalo limenigusa moyoni, lakini siyo kutokana na wewe".

"Basi, pole".

"Ahsante".

Kutokana na uzoefu wake wa siku nyingi kuhusu wasichana, Willy aligudua kwamba Nyaso hakuwa na furaha katika uhusiano wake na bwana yake. Hivyo aliamua kutumia nafasi hiyo ili aweze kujua mengi zaidi juu ya Chris Tondo na F.K.

"Wewe na F.K mnakaa pamoja", Willy aliuliza.

"Hapana".

"Wewe unakaa wapi?".

"F.K alininunulia nyumba huko Kijenge, na yeye anaishi kwenye jumba lake huko Themi Hill".

"Anasubiri nini asikuoe msichana mrembo hivi. Anafikiri watu wengine hawakuoni?", Willy alimtolea Nyaso tabasamu la kumlainisha.

"Hiyo ni shauri yake".

"Au ni kwamba wazazi wako hawataki wewe uolewe na Mhindi?", Willy aliongeza. Mara aliona machozi yanamlengalenga Nyaso mara ya pili.

"Hapana", Nyaso alijibu.

Willy alihisi wazo fulani lilimjia akilini mwake.

"Nyaso, wazazi wako wako wapi?".

Nyaso hakumjibu Willy. Wote wawili walikaa kimya kwa muda mpaka nyama ilipoletwa.

"Basi, sahau yote hayo unayofikiria ili tule nyama na kufurahi", Willy alimshauri Nyaso.

"Uliniambia jina lako ni Willy nani?", Nyaso aliuliza kwa unyonge.

"Willy Gamba".

"Nimewahi kusikia jina kama hilo mahali fulani", Nyaso alisema.

"Kama siyo redioni, basi ni kwenye magazeti".

"Sijui, labda ni mtu mwingine. Kama ujuavyo, baadhi ya watu wanayo majina yanayofanana".

"Willy sijui nianzie wapi", Nyaso alisema halafu akasita.

"Naona kama kuna kitu kinakukera rohoni", Willy alisema. "Nakushauri ukiseme tu. Mimi ni kijana mwenzako. Unajua Nyaso, kama kuna jambo linalokukera moyoni, dawa ya kuleta nafuu ni kumwambia mtu. Ni vizuri zaidi ukamwambia mtu kama mimi ambaye hatufahamiani. Hivyo itasaidia sana kwani huwezi kuwa na wasiwasi kwamba nitawaambia watu wengine. Mimi sijui marafiki zako na wewe hujui marafiki zangu".

"Willy, nitakupa siri yangu ya maisha ambayo hakuna mtu mwingine anayeijua isipokuwa mimi mwenyewe. Pamoja na mwito wako wa kutaka nikueleze, huenda nisingekueleza. Lakini kwa kuwa wakati wa kutekeleza mpango umekaribia, nitakueleza tangu mwanzo.

Mara mhudumu alifika kwenye meza yao.

"Nyama ya hapa ni safi sana", Willy alinena.

"Ndiyo sababu ilinifanya nikulete hapa hapa", Nyaso alidakia.

"Msee, hapa nyama ni safi kabisa kabisa", mhudumu aliongeza.

"Wewe ni Mchagga?", Willy aliuliza.

"Ndiyo".

"Biashara kweli mnaijua", Willy alimsifia.

"Utafanya nini, babangu?", mhudumu aliitikia halafu akaondoka zake.

"Hebu endelea", Willy alimkumbusha Nyaso.

"Mimi nilizaliwa miaka ishirini na sita iliyopita nikiwa ni mtoto wa tatu wa Dk. Soni", Nyaso aliendelea. Baba yangu alikuwa daktari wa mifugo na mama yangu alikuwa muuguzi. Miaka saba baada ya mimi kuzaliwa tulivamia na majambazi wakati wa usiku, huko nyumbani Moshi. Majambazi hayo yalivunja nyumba na kuua watu wote wa familia yangu isipokuwa mimi tu. Mtumishi wetu wa nyumbani, akiwemo mlinzi wetu waliuawa pia. Hata mimi nilidhaniwa kuwa niliuawa. Majambazo yalipompiga mapanga dada yangu mkubwa aliniangukia na sote wawili tulianguka chini. Majambazi walifikiri kuwa nami nilikuwa tayari nimekufa".

Aliposema hayo, Nyaso alinyamaza kidogo huku machozi yakimtoka.

Willy ambaye alikuwa akimsikiliza Nyaso kwa makini na mshangao alimshauri asilie.

"Unajuwa kuwa hapa tuko hadharani, hivyo nakuomba usilie".

"Sawa", Nyaso alijibu, halafu akaendelea. "Walipoamini kuwa wameua kila mtu, ndipo alipotokea yule mtu ambaye alikua amekodi majambazi. Lengo lake lilikuwa kuhakikisha kwamba kazi aliyowatuma ilikuwa imetekelezwa ndipo awalipe ujira wao. Mtu huyo nilimwona na kumtambua. Halafu nafikiri nilizirai, kwani nilipopata fahamu nilijikuta hospitali huku nimezungukwa na wauguzi pamoja na askari polisi. Baada ya siku mbili niliruhusiwa kutoka hospitali. Nilichukuliwa na polisi kisha niliulizwa maswali mengi. Ni ajabu kwamba sikuweza kukumbuka jambo lolote. Mwisho wake waliniachia kisha nikachukuliwa na Masista wa madhehebu ya Kikatoliki. Wao ndio walionitunza na kunipekeka shule hadi nilipomaliza kidato cha sita".

Nyaso alinyamaza ili kumeza mate ya kulainisha koo.

"Ulisema huyo mtu ulimwona na kumtambua, lakini ulipopata fahamu ukawa hospitali hukuwa na kumbukumbu tena?", Willy aliuliza.

"Ndiyo, lakini hebu nikwambie jambo nililotaka ulisikie: Kwa sababu hiyo, mimi sina baba wala mama, sina hata ndugu yeyote. Ndugu wa pande mbili za wazazi wangu walikaa kimya. Hakuna hata mmoja wao aliyejitokeza kunichukua kutoka kwa masista ili anitunze. Ufahamu Willy kwamba mimi nilikuwa mdogo hivyo sikujua mambo mengi. Ndio sababu naitwa Nyaso tu, basi!".

Nyaso alinyamza kidogo na kisha akaendelea. "Maisha yangu ya utoto yalikuwa ya ukiwa ingawaje wafadhili wangu walinipa kila kitu nilichohitaji. Sasa jambo la ajabu ni kwamba, nilipokuwa nasoma Kidato cha Sita, wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kibosho tulipatwa na ajali. Baada ya kumaliza muhula wa kwanza shule ilifungwa. Tulikodishiwa gari litupeleke mjini Moshi tayari kwa safari ya kwenda likizo. Lakini humo njiani, kabla ya kufika mjini, gari lilipinduka. Mimi nilikuwa mmoja wa wanafunzi waliopata majeraha kichwani, hivyo nikalazwa K.C.M.C. Nilipokuwa nimelazwa niliota ndoto kuhusu siku ile ya mauaji ya familia yetu. Ndoto hiyo ilinionyesha mambo yote yaliyokuwa yametokea siku hiyo; mpaka mtu yule aliyekodi majambazi yaliyoteketeza familia yangu. Niligutuka toka usingizini na kujikuta nimezungukwa na madaktari na huku jasho likinitoka mwili mzima".

"Nilipoulizwa na madaktari nilikuwa najisikia vipi, niliwajibu kuwa nilikuwa najisikia salama wote walishangaa! Hapo hapo muuguzi mmoja alinieleza kwamba wakati nikiwa usingizini nilikuwa napiga kelele na kuhangaika. Alisema kwamba hata wao walikuwa na wasiwasi kuwa huenda nilikuwa karibu kukata roho".

"Ina maana njozi ile njozi hiyo ilikufanya umkumbuke yule mtu aliyekodi majambazi", Willy aliuliza kwa shauku kubwa.

"Ndiyo, na siku hiyo hiyo niliruhusiwa nikatoka hospitali nikiwa mzima kabisa. Mtu yule nilikuwa namfahamu tangu nikiwa mtoto, kwanza alikuwa rafiki yake marehemu baba yangu", Nyaso alisema na kuanza kulia tena.

"Jikaze ili uweze kunimalizia kisa hiki", alidakia Willy.

"Je, ukimwona sasa unaweza kumtambua".

"Ndiyo, kwani mara nilipotoka usingizini nilimkubuka barabara. Zaidi ya hayo, mtu huyo anaishi hapa hapa Arusha na ni mtu mkubwa sana. Wakati huo nilipata wazo la kwenda polisi kueleza kisa hicho, lakini nilijuwa hakuna hata mtu mmoja ambaye angeniamini. Kwanza miaka mingi ilikuwa imepita, na pili, mtu huyo alikuwa tayari kizito. Watu wangefikiri mimi nimekuwa kichaa kwa sababu ya ajali".

"Wewe uliamua kufanya nini", Willy aliuliza.

"Nilifikiri sana juu ya hali hii, halafu nikaamua kulipiza kisasi".

"Niliamua kuchukua hatua mimi mwenyewe, kwani Serikali ilishindwa kuwakamata na kuwaadhibu wauaji hao. Niliona ni bora kuendelea na masomo kwanza, kitu ambacho nimefanya mpaka nikahitimu elimu ya Chuo Kikuu. Baada ya masomo niliwaomba ruhusa masista ambao walinitunza ili niweze kufanya kazi serikalini. Waliniruhusu na kunitakia kila la heri. Lakini mpaka sasa huwa ninakwenda kuwajulia hali kwa sababu nawaona kama wazazi wangu. Unaelewa, wakati nikiwa shuleni nilikuwa naitwa Nyaso wa masista".

"Sasa wewe umeamua kulipiza kisasi kwa njia gani?", Willy aliendelea kuuliza.

"Usiniulize swali hilo. Tangu nimeota ndoto ile sasa yapata miaka minane. Kwa muda huo nilikuwa nikipanga na kupangua. Sasa naamini nimefikia uamzi sahihi juu ya namna gani nitalipiza kisasi. Jukumu hili ni langu mwenyewe. Willy. Najua nitafanya nini. Kulipiza kisasi ni lazima".

"Nilipohitimu masomo ya Chuo Kikuu nilipangwa kufanya kazi katika Wizara ya Uchumi na Mipango. Niliomba kituo changu cha kazi kiwe Arusha, kwani hapo ndipo alipo mbaya wangu".

"Je, mtu huyo anajuwa kuwa wewe ni mtoto wa Dk. Soni?".

"Hapana. Hawezi kujua kwa sababu mimi situmii jina hilo. Najulikana kama Nyaso wa masista, basi. Na hii imeweza kunisaidia sana, kwani huyu mtu naonana naye mara nyingi, lakini hawezi kunitambua. Yeye ni mtu maarufu hapa, hivyo ni rafiki wa watu maarufu kama akina F.K".

"Ahaa, kwa hiyo urafiki wako na F.K una uhusiano na mtu huyo?".

"Siyo hivyo. Urafiki wangu na F.K ulitokana na sababu tofauti kidogo".

"Kuhusu mpango wangu wa kulipiza kisasi, mimi nilihitaji uwezo mkubwa kipesa. Ilinibidi nifanye kila liwezekanalo ili nipate mtu anayeweza kunipa uwezo huo. F.K ndiye aliyeonekana kuwa mtu wa kukidhi haja yangu. Hivyo nilitupa ndoano yangu, na F.K akanasa. Kwa hiyo lengo langu limetimizwa; fedha za kuendeshea operesheni yangu sasa ninazo. Ninaweza kuanza pole pole kutekeleza mpango wangu. Sasa najisikia nafuu kwani nimemweleza mtu historia yangu".

Willy alimwangalia Nyaso kwa makini na mshangao vilevile. Mara alikumbuka maneno aliyoambiwa na mama yake mzazi: Mwanangu Willy kila mara jihadhari na wasichana warembo kwani wana mambo.

"Lo, kumbe Nyaso umeishi maisha ya taabu sana, lakini napenda nikushauri kuwa siyo vizuri kulipiza kisasi kwani matokeo yake yanaweza kuwa mabaya zaidi; janga linazua janga. Hivyo ninaku....".

"Ngoja ngoja, Willy", Nyaso alimkata kilimilimi. "Mahali nilikofikia siyo pa kurudi nyuma. Janga gani linaweza kunitokea mimi zaidi ya kufa? Mie siogopi kufa. Unajua kwa nini familia yangu ilipouawa Mungu alininusuru? Alifanya hivyo ili niweze kulipiza damu ya familia yangu ambayo ilimwagika bila makosa".

"Je, unajua kwanini mtu huyu alipanga familia yako iangamizwe?".

"Ndiyo, najua lakini siwezi kukwambia. Nimekwambia mambo mengi ambayo nafikiri yanakutosha. Najua wasiwasi wako unatokana na kuwaza kwamba nikauawa pia. Mimi niko tayari kufa ili niungane na familia yangu huko peponi. Kula nyama uondoke wala usiniangalie kwa masikitiko hivyo".

Pale pale Willy alijuwa kuwa Nyaso alikuwa amepania kutekeleza matakwa yake. Lakini alimsikitikia sana msichana yule kwani alijua kwamba alikuwa mgeni katika mambo kama hayo. Hivyo alijua kwa vyovyote Nyaso angekuwa na mwisho mbaya, hata kama mipango yake ilikuwa mizuri. Hata hivyo Willy alimwona Nyaso alikuwa msichana jasiri na kwa sababu hiyo alimheshimu sana. Kutokana na hali hiyo, Willy aliamua kumpasha mambo ambayo yangemfanya msichana huyu awe tayari kusaidiana naye, hasa kuhusu Chris Tondo na F.K.

"Sikiliza Nyaso", Willy alisema. "Tangu nilipokuona mara ya kwanza nilijua wewe ni mtu wa aina gani. Wewe ni msichana mwenye sura nzuri sana. Ninathubutu kusema umependelewa sana jinsi ulivyoumbika. Vile vile wewe una akili nyingi sana na usafiri kinyume cha wasichana wengi. Unao uwezo wa kumdu mapambano".

"Hebu wacha kunipamba na sifa nyingi". Nyaso alimkatiza. "Mimi nimeshasikia nikipewa sifa za kila aina".

"Sikiliza, Nyaso. Sifa ambazo umezisikia ni kutoka kwa wanaume walaghai wenye kukutaka mapenzi. Nia yangu siyo hiyo, la hasha. Kama hali ya mapenzi ikitokea kati yangu na wewe, basi itakuwa katika hali ya kawaida na siyo kwa kughilibu. Kitu ninachotaka kusema ni kwamba nilikuwa sijaona msichana aliyebarikiwa kama wewe mpaka akawa na akili nyingi, sura nzuri isiyoelezeka na pia hekima na ujasiri. Kwa sababu ya yote hayo. nimekuheshimu. Ndiyo sababu nami nimeamua kukueleza juu ya maisha yangu mwenyewe na kwanini niko hapa".

Willy alimtolea Nyaso jicho la mahaba.

"Usiniangalie hivyo na kuniumiza roho", Nyaso alilalamika. "Sema tu unavyotaka kusema".

"Kama nilivyokwambia hapo awali", Willy alisema. "Mimi naitwa Willy Gamba. Watu wengi wananijua kama mfanyabiashara. Lakini ukweli ni kwamba mimi ni mpelelezi katika Idara ya Upelelezi Tanzania".

"Kweli", Willy alimthibitishia.

"Nimewahi kusikia tetesi kama hizo", Nyaso alidakia. "Ndiyo sababu nikakwambia nimewahi kusikia jina lako. Lakini watu wengine husema kuwa habari zote kuhusu jina hilo huwa ni hadithi tu na wala hakuna mtu wa namna hiyo ambaye anaishi hapa duniani. Lakini tangu nilipokuona kwa mara ya kwanza, niliona vitendo vyako vinafafana na vile vya huyo Willy anayesifika. Sasa naamini kwamba ni wewe hasa. Nafikiri ninayo bahati kubwa kukufahamu. Sina shaka wewe utakuwa mwali wangu katika operesheni ninayotarajia kuendesha ili kullipiza kisasi".

"Usijali, ngoja kwanza nikueleze kilichonileta hapa", Willy alimwambia Nyaso. "Baadaye utaona kwamba mambo mengine pamoja na hayo ya kwako ni kama mchezo".

"Sawa, Willy, ninakusikiliza".

"Basi tega masikio nikueleze toka mwanzo hadi mwisho".

Willy alimweleza Nyaso yote yaliyokuwa yametokea, kwanini alikuwa Arusha na tuhuma zake dhidi ya Chris Tondo na huenda F.K vile vile.

"Kwa hiyo Nyaso", Willy alimaliza. "Ninakuomba unisaidie kwa kunipa habari ambazo zinaweza kunisaidia katika mapambano dhidi ya majasusi wa Afrika Kusini. Ushindi wetu ni wako vile vile".

Nyaso aliyekuwa anamsikiliza Willy kwa makini, alimtolea tabasamu la mwaka kisha akasema. "Usiwe na wasiwasi, Willy. Mtu kama wewe ndiye nilikuwa natafuta tokea siku nyingi. Tangu sasa hivi mimi niko mikononi mwako. Msaada wowote utakaohitaji kutoka kwangu hesabu kuwa umepata".

Willy alijisikia joto la mwili likipanda, lakini akaamua kutoruhusu hali hiyo iendelee mpaka hapo kazi iliyokuwa mbele yao itakapokuwa imemalizika.

"Nyaso", Willy alisema. "Ninakuomba unieleze yote kuhusu maisha ya F.K pamoja na shughuli zake kibiashara. Yale yanayohusu maisha yenu kama bibi na bwana unaweza kuyaacha".

Nyaso alimweleza Willy yote anayojuwa kuhusu F.K., Chris Tondo pamoja na shughuli za Nyoka Tours and Safaris.

"Kama unahisi hapa majasusi wamejificha mahali, basi ni nyumbani kwa F.K", Nyaso alisema. "Kama nilivyokueleza mimi na F.K tumekuwa marafiki kwa muda mrefu. Lakini nimefika nyumbani kwake mara chache. Nyumba yenyewe imejengwa kinamna, kwani White House ni Wihite house hasa. Ni kama Ikulu; hata sijui unaweza vipi kuingia ndani ya jumba hilo".

"Je, F.K hajawahi kukueleza kitu chochote ambacho kinaweza kunisaidia kuingia ndani ya jumba hilo?".

"Kitu ninachokumbuka ni kwamba, wakati penzi letu lilipokuwa bado moto moto, F.K alinichukua ili nikalale kwake. Hii ilikuwa moja ya safari tatu tu ambazo nimewahi kulala kwake. Wakati tulipokuwa tunazungumza, nilionyesha wasiwasi wangu kuhusu yeye kuishi peke yake katika jumba kubwa vile. Nilimweleza kuwa angeweza kushambuliwa na majambazi kwani alijulikana kuwa ni mtu tajiri sana. Lakini yeye alinihakikishia nisiwe na wasiwasi kwani jumba lake lilikuwa limejengwa kwa namna yake. Aliongeza kusema kuwa kama angevamiwa, angweza kutumia njia za siri ambazo ziko chini kwa chini mpaka akatokea nje ya seng'enge, ili akawajulishe polisi. Kwanza nilifikiri alikuwa anajigamba tu. Unajuwa wanaume wengi hupendelea kujionyesha mbele ya wanawake kwamba wao ndio wenyewe. Lakini baada ya kusikia tuhuma dhidi yake, naamini alikuwa anasema kweli".

"Sehemu yake ina eneo gani?", Willy aliuliza.

"Ekari kumi na mbili", Nyaso alijibu.

Willy aliangalia saa yake na kuona ilikuwa saa mbini na nusu usiku.

"Nyaso", Willy aliomba. "Hebu twende ukanionyeshe kwa Chris Tondo. Ningependa nizungumze naye kidogo".

"Sawa Willy, lakini huenda tusitumie gari langu kwani linajulikana sana. Hapo nyumbani kwangu kuna gari la rafiki yangu kutoka Nairobi, aliliacha pale halafu alipanda ndege kwenye Dar es Salaam. Heri tukatumie gari hilo".

"Mawazo yako ni sahihi. Je, lina namba za Kenya?".

"Ndio".

"Haya twende. Si wewe mwenyewe unataka pilika pilika? Sasa basi zimeanza", Willy alimtania Nyaso.

Waliunuka toka vitini na kuondoka.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru