HOFU

MAMBO BADO

IV

Baada ya kumtelemsha Willy, Nyaso alielekea New Arusha Hoteli huku akiwa na mawazo mengi sana juu ya Willy. Kitu kimoja kilimshangaza sana na jinsi alivyokuwa ametokea kumpenda kijana huyo. Alikuwa amempenda ghafra kiasi cha kuhatarisha maisha yake wakati alikuwa hamjui sawa sawa kijana huyu.

"Kweli dunia ni msongamano", Nyaso alijisemea huku akiegesha gari karibu na hoteli.

"Mtoto huyo", dereva mmoja wa taksi kati ya wale walioegesha nje ya New Arusha alimnong'oneza mwenzake.

"Sijui mtoto huyo ana nini. Labda F.K. amesafiri kwani namwona anayo njemba moja hivi", dereva mwingine alijibu.

"Ni kweli hata mimi njemba huyo nimemwona. Jamaa mwenyewe mkali na vitu anavyoweka toka chini mpaka juu ni vya ukali tupu", dereva wa tatu alisema.

"Yule ni saizi yake siyo huyo F.K. ambaye anafuja mtoto wa watu bure", dereva wa pili aliongeza huku wakichekelea. Wakati huo Nyaso alishatoka kwenye gari na alikuwa anapotea hotelini. Macho ya watu hao yakimfuata yeye.

"Ama kweli Mungu ana upendeleo angalau kwa kiumbe yule", kijana mmoja wa mapokezi alimnong'oneza mwenzake baada ya Nyaso kuwapita na kusimama akisubiri lifti.

"Huyo msichana mimi simwangalii kwa sababu nikifanya hivyo najisikia msisimko. wakati najuwa fika kwamba hata nishitakie mbingu, siwezi kumpata", mwenzake alijibu.

"Si lazima kupata kila kitu ukipendacho. Hata macho pekee yanatosha kuangalia tu. Mimi ninapoona sura yake humsifia Mungu muumba; halafu kusema kwamba kuna wanaume duniani waliobahatiwa", yule kijana wa kwanza alisema kwa masikitiko.

Bila kujuwa kuwa watu walikuwa wanauguwa roho kutokana na sura yake murua. Nyaso alipanda lifti. Alikuwa na wazo moja tu kwamba kama angekuta akina Bon wamerudi angewataka wamfuate Willy. Alifikiri kwamba kama kweli F.K. amemuua Tondo hata Willy atauawa kama hakujihadhari.

Nyaso alifika kwenye chumba cha Willy. Alibisha hodi lakini hakupata jibu. Alibisha mara ya pili lakini kukabaki kimya. Aligonga tena mara hii kwa nguvu lakini bado hakujibiwa. Mara alitokea kijana mmoja mhudumu katika hoteli alisema huku akitabasamu.

"Samahani dada, nimeona jamaa wanaondoka haraka haraka".

"Wangapi", Nyaso aliuliza.

"Wawili", yule mhudumu alijibu.

"Ahsante", Nyaso aliitikia huku nusu akitembea nusu akikimbia, alielekea kwenye ngazi. Alikuwa na wazo la kuwafuata akina Bon na Mike huko kwa F.K. kwani aliamini Willy alikuwa kwenye hatari. Yule mhudumu alimwangalia Nyaso kwa butwaa.

"Ama kweli duniani kuna wanaume! Mimi nikiwa na miadi na msichana kama huyu siwezi kutoka hata itokee nini. Labda niambiwe mama yangu kafariki", yule mhudumu alijisemea mwenyewe.

ITAENDELEA

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU