HOFU

FUNGA KAZI

IV

Walifika sehemu walikokuwa Willy pamoja na George. Ilibidi Bon amshike Nyaso ambaye alikuwa ameshikwa na kiwewe. Sababu ilikuwa ni kwamba vita vya maninja vilikuwa vimeanza.

"Willy! Willy! Ooooh", Nyaso aliita.

"Nyamaza! Hivi ni vita vya maninja. Sikiliza Nyaso. Wote wawili ni maninja. Maana yake ni watu wenye ujuzi wa hali ya juu wa kupigana. Wote wawili wamehitimu mbinu za hali ya juu za mapigano ziitwazo ninja. Sheria yao inasema maninja wawili wakianza kupigana, watu wengine hukaa kando. Mapigano huisha babada ya mmoja wao kuuawa", Bon alimweleza Nyaso kwa haraka.

"Hivi unaweza kumwacha Willy auawe ati kwa sababu ya sheria?, mimi nakwenda kumsaidia", Nyaso alisema huku akijaribu kujitoa mikononi mwa Bon.

"Kama Willy atauawa mimi nitachukua nafasi yake. Hii ni "sanaa" ya mauaji, nayo ina miiko yake. Hata mimi mwenyewe ni ninja", Bon alisema huku akimwangalia Nyaso usoni. Kwa mara ya kwanza Nyaso aliona macho ya Bon yamegeuka na kuwa kama hayana uhai.

"Mimi sikujuwa kama watu walio hai wanaweza kuwa maninja. Nilidhani ni hadithi tu ama michezo ya sinema. Mpaka sasa siamini", Nyaso alisema huku machozi yakimtoka.
Willy na George walikuwa wametazamana. Bon alimshikilia Nyaso kwa nguvu zaidi. Alipogeuka nyuma alimwona Mike amejiegemeza kwenye ukuta. Alionekana kuwa na wasiwasi. Bon alipomwangalia Mike alitoa ishara kuonyesha kwamba F.K. alikuwa amekufa. Hapo hapo wote waligeuza macho yao kuangalia mapigano makali yaliyokuwa yameanza. Mbinu zilizotumika zilikuwa za hali ya juu. Hata Bon mwenyewe alikiri. Pamoja na yeye kuwa ninja. Alikuwa hajaona mapigano makali kama hayo.

"George aliruka juu. Kana kwamba alikuwa anatembea hewani, alirusha mateke kumi mfululizo. Willy aliyakwepa yote. Kabla hajatua chini. George alichomoa upanga kutoka mgongoni mwake. Akaanza kumkabiri Willy.

Mike alihamaki akataka kuingia kwenye uwanja wa mapambano. Bon alimpa ishara ya kuzuia. Nyaso aligeuka na kulala kifuani mwa Bon. Alihofia Willy angeuawa wakati wowote. George alirusha upanga wake mara saba. Nia yake ilikuwa ni kumkata Willy. Lakini hakuweza kufanikiwa. Willy alikuwa ni mwepesi kama unyoya. Ghafla George aliruka juu na kumkuta Willy hayuko tayari. Bon na Make walifumba macho. Ilikuwa vigumu kuamini jinsi Willy alivyojipindua. Upanga wa George ulimpita kwenye mkono. Ulichana shati yake na kumkata kidogo.

Damu ilianza kumtoka Willy. Hata George mwenyewe alishangaa jinsi Willy alivyokwepa upanga huo. Willy aliangalia damu yake. Hasira ilimpanda. Alisikia harufu ya damu mpaka ule upanga akauona si kitu kwake. Alichana shati lake na kulitupa. Halafu alimrukia George na kumpiga dhoruba ambayo hakuitarajia. Aliupiga mkono wake wa kulia ambao ulikuwa umeshika upanga. Upanga uliruka na kuanguka karibu na miguu ya Bon. Kishindo cha upanga kilimshitua Nyaso. Aligeuka na kushuhudia jinsi Willy alivyokuwa akimtandika yule kaburu.

"Willy alimpiga George mapigo matano mfululizo, ambayo yalimfanya achanganyikiwe.

"Willy, muuee! muuee", Nyaso alipiga kelele. Lakini George alijibu mapigo. Alimpiga Willy kichwa cha aina ya pekee mpaka wote wawili wakaanguka chini. George aliwahi kuinuka, mara hii alitoa kisu kirefu. Halafu alimrukia Willy ili ammalize. Lakini Willy alikuwa macho. Aliruka kutoka mahali alipokuwa na George akamkosa. Bila kuchelewa Willy akamtupia George teke la tumbo akaanguka chini. Katika kuanguka kisu kilimtoka mkononi. Willy alitumia nafasi hiyo. Alimpiga George pigo la pekee ambalo lilimbomoa kifua. George alijuwa amekwisha.

"Aaaa! Nakufa! Willy, heri ungenikata kichwa ili nife kwa heshima za kininja", George alisema Bon alimtupia Willy upanga. Willy alikata kichwa cha George kwa pigo moja.

Nyaso alikurupuka kutoka mikononi mwa Bon, alimkimbilia Willy na kumkumbatia.

Aaaah. Willy! Siamini", Nyaso alisema kwa sauti kali. Bon na Mike walibaki wameduwaa.

"Haya tutoke hapa haraka, kazi iliyobaki ni ya polisi", Willy aliamrisha. Nyaso alitoa kitambaa na kumfunga mkono Willy. Wote waliingia ndani ya gari la F.K. Ingawa lilikuwa limevunjika taa za upande wa kulia. Willy aliendesha na wote wakarudi mjini.

ITAENDELEA...

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru