HOFU

FUNGA KAZI

V

"Hallo!", sauti ilisikika kwenye simu.

Hallo, mimi naitwa Willy Gamba".

"Ndiyo mzee", Kamanda wa polisi wa mkoa alijibu kwa hofu. Alikuwa amepokea simu kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kutoka Dar es Salaam. Alikuwa ameambiwa asitoke nyumbani mpaka Willy ampigie simu.

"Haya sikiliza. Rafiki yako F.K. amekufa. Vile vile kuna rafiki zake wamekufa. Mzee Hamisi naye amekufa na maiti yako nyumbani kwake. Tondo pia ni maiti. Yapo nyumbani kwake. Naamini sasa unajuwa cha kufanya", Willy alieleza, wakati wakitelemka kwenye gari, kamanda aliuliza.

"Mzee Hamisi amekufa. Amekufa saa ngapi".

"Kati ya saa tatu na nusu na saa nne", Willy alijibu.

"Hiyo haiwezekani. Mimi nilipata habari kuwa mnamo saa nne na robo Mzee Hamisi alikuwa kwenye jengo la mikutano la AICC", Kamanda alisema.

"Yeye mwenyewe ama gari lake?", Willy aliuliza.

"Eah! Askari wanaolinda huku waliripoti kuonekana gari lake. Halafu waliripoti kuwa chumba kilichotayarishwa kwa ajili ya mkutano kiliwashwa taa. Wao walifikiri Mzee Hamisi alikuwa anaangalia na kuhakikisha usalama, kama kawaida yake", Kamanda alijibu.

"Haya, wewe shughulikia taarifa niliyokupa na kwa heri", Willy alijibu na kukata simu. Mawazo ya Willy yalikuwa yanakwenda haraka haraka.

Willy alipiga simu kutoka hotelini kwake New Arusha Hotel. Alikuwa na wenzake akiwemo Nyaso.

"Anasema nini?", Bon alimuuliza Willy. Willy alimweleza maneno ya Kamanda.

"Kama ni hivyo F.K. na wenzake waliweza kuingia kwenye chumba cha mkutano. Na kama waliingia walifanya nini?", Mike aliuliza.

"Maneno yako ni kweli. Bila shaka walikuwa na sababu", Willy aliitika. Kisha aliinua simu na kupiga namba ya mwandalizi wa mkutano wa wapigania uhuru.

"Hallo".

"Hallo. Willy hapa".

"Lete habari. Nimekaa nikisubiri kwa hamu hata mate hayamezeki. Wazee wana wasiwasi mkubwa. Kwani wanapiga simu kila baada ya dakika kumi. Heri tupate taarifa yako. Vinginevyo, kabla ya asubuhi watakuwa wamekufa kutokana na ugonjwa wa moyo", mwandalizi wa mkutano alisema. Willy alimweleza kwa kirefu yote yaliyokuwa yametokea.

"Hure? Afrika huru imeshinda", alijibu kwa ghafla na furaha kubwa.

"Kwa hiyo mkutano utaendelea kesho kama ulivyopangwa. Waeleze wazee kwamba sasa kazi kwao, kazi yetu sisi vijana wao tumeimaliza", Willy alisema.

"Sijui watawashukru vipi", yule mtu alisema huku akionyesha furaha.

"Hivi si wewe unayeshughulikia maandalizi ya mkutano?", Willy aliuliza.

"Ndiyo".

"Basi, naomba tuonane huko. Sisi tunakwenda huku sasa hivi.

"Oke!".

"Haya sasa twendeni. Tayari nimepata wazo. Wewe Nyaso lala na kupumzika. Hayo uliyoyafanya yanakutosha kwa siku moja". Willy aliwaambia wenzake.

"Nani abaki hapa? tunakwenda wote", Nyaso alijibu huku tayari akiwa amefika mlangoni.

ITAENDELEA...

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU