MAGUFULI AUFAGILIA UONGOZI WA NSSF

Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli akiwa ameshika nguzo kubwa ya daraja la Kigamboni, alipokagua ujenzi wa daraja hilo, Dar es Salaam leo. Kulia ni Meneja Mradi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mhandisi John Msemo na Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Karim Mataka wa NSSF.

 Na Nyakasagani Masenza, Dar es Salaam
WAZIRI wa Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli, amelimwagia sifa nyingi Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa kusimamia vizuri mradi mkubwa wa Ujenzi wa daraja la kisasa la Kigamboni, Dar es Salaam.

Amesema Serikali ya Awamu ya tatu imefurahishwa na mno na jinzi uongozi wa NSSF unavyosimamia kwa karibu mradi huo mkubwa wenye tija kubwa kwa taifa na kuahidi kuwa Wizara yake itashirikiana na NSSF ili kufanikisha mradi huo.

Waziri Magufuli amemwambia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Lodovick Mtoso kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa kuimarisha miundombinu unaofanywa wa shirika hilo na kumuomba afikishe shukrani za serikali kwa Mkurugenzi Mkuu, Dkt Ramadhan Dau.

"Kazi ya NSSF inaonekana, mradi huu na mingine iliyofanywa na shirika lenu ni kielelezo cha uchapakazi wenu, serikali inaomba ufikishe salamu hizi kwa Mkurugenzi wa NSSF na viongozi wake wote, tunaahisi kuwasaidia

Dkt. Magufuli ambaye alizungumza na waandishi wa habari, alipokagua ujenzi wa daraja hilo leo, amerudi kauri yake kuwa Serikali ya awamu ya tatu haitawavumilia watu wachache wenye tabia ya kukwamisha miradi ya maendeleo ya wengi kwa sababu zao binafsi.

Amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza awali kabla ya ujenzi wa daraja hilo, kwa baadhi ya wananchi waligoma kuhama kwa sababu zao binafsi ili kupisha mradi huo, ambao hatimaye ulianza kwa kasi na kutarajiwa kukamilika July mwaka 2015.

"Baadhi ya wananchi waligoma kuhama eneo la mradi, tulilazimika kutumia nguvu kwa sababu Utawala bora ni pamoja na kutumia nguvu kwa manufaa ya wengi, tukafanikiwa mradi ukaanza", alisema Waziri Magufuli.

Amesema daraja hilo lenye urefu wa kilomita moja na ziada, litakuwa na njia 14, saba kutoka upande wa Kigamboni na saba kutoka Kurasini. Amewataka NSSF na makandarasi wanaojenga daraja hilo kuhakikisha linazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, Juni, 2015 kwa sababu ndiye aliyefanikisha kuwepo kwa daraja hilo.

"Niliahidi wakati Rais Kikwete anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hili, leo pia nasema mbele yenu, sitaki kiongozi mwingine aje afunguwe daraja hili ili ajisifu, Rais Kikwete ndiye atakayezindua daraja hili", anasema Magufuli kwa msisitizo.

Waziri Magufuli amesema baada ya daraja hilo kukamilika pamoja na miundombinu ya kisasa inayoandaliwa na Serikali ikishirikiana na NSSF, Dar es Salaam itakuwa miongoni mwa majiji ya kisasa zaidi katika Afrika. Amesema Serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo JAIKA wametoa sh. Bilion 100 kufanikisha miradi ya maendeleo.

Awamu akimshukru Waziri Magufuli kutembelea mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Lodovick Mroso, amesema lengo la shirika hilo ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na mafanikio makubwa.

"Mheshimiwa Waziri, changamoto tuliyonayo ni kuhakikisha mradi huu unafanikiwa kwa wakati, fedha zipo na makandarasi wako kazini wakati wote, tunajitahidi mradi huu uwe tayari kabla ya wakati", anasema Bw. Mroso.

Amesema ujenzi wa daraja hilo la kihistoria kwa Tanzania, ni moja ya miradi mikubwa ya uwekezaji wa ndani inayofanywa na NSSF.

Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, akimpongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Lodovick Mroso (kulia), baada ya waziri kukagua mradi wa ujenzi wa darala la Kigamboni, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uwekezaji, Bw. Yakub Kidula.
Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli (wa nne kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Lodovick Mroso (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Uwekezaji NSSF, Bw. Yakub Kidula (wa pili kulia) na Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi John Msemo (kulia), wakimsikiliza msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Kigamboni Mhandisi Karim Mataka, wakati akiwaonyesha nguzo kubwa ya daraja la hilo.
Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa daraja la Kigamboni, kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mhandisi Karim Mataka (kulia), akiongoza Ujumbe wa Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli kupita kwenye daraja la Kigamboni, alipotembelea eneo la mradi, Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji NSSF, Yakub Kidula na Meneja Miradi, Mhandisi John Msemo.
Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli akisikiliza maelezo ya Mhandisi Karim Mataka, alipokagua ujenzi wa daraja la Kigamboni, Dar es Salaam leo na kulipongeza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru