NSSF YAVUNA WANACHAMA 211 TEMEKE, DKT. DAU AWAKABIDHI KADI

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhan Dau akifafanua jambo, wakati akizungumza na wanachama wapya 211 waliojiunga na NSSF, baada ya kuwakabidhi kadi za uanachama kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Mbunge wa Temeke, Bw. Abbas Mtemvu na Naibu Meya wa Temeke Bw. Juma Mkenda.
 Akiwasalimia wanachama wapya 211 walioffika kupokea kadi za uanachama.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WATANZANIA wameaswa kujiunga na vikundi vya ujasiriamali na kutumia fursa zilizopo kupata mikopo kwa masharti nafuu na kuirejesha kwa wakati ili waweze kujiletea maendeleo ya haraka.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhan Dau (pichani), wakati akikabidhi mkopo wa sh. bilion 1.5 kwa vikundi 150 vya Vicoba vinavyoratibiwa na Poverty Fighting Tanzania (PFT).

Wakati wa hafra hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dkt. Dau pia aliwakabidhi kadi wanachama wapya 211 waliojiunga na shirika hilo, Dar es Salaam juzi.

Dkt. Dau amewaeleza wanachama hao kuwa fedha hizo zimetolewa kwa mkopo na NSSF kwa jitihada na dhamana ya Mwenyekiti wa PFT, Mbunge wa Temeke, Bw. Abbas Mtemvu, aliyemwita king'ang'anizi.

Amesema NSSF inatoa mikopo kwa masharti nafuu ili kuboresha maisha ya watanzania, tofauti na mabenki yanayohitaji faida, riba na dhamana kubwa, ambapo wananchi wenye vipato vya chini hushindwa kupata mikopo hiyo.

"Ombi langu kwenu, fedha hizi hazikutolewa kama sadaka, ni mkopo kutoka NSSF, mzitumie vizuri ili ziwaletee maendeleo, mkilipa awamu ya kwanza, mtakopeshwa tena na tena, naamini kupitia Mwenyekiti wenu Mtemvu, zitarejeshwa kwa wakati", amesema Dkt. Dau.

Amewapongeza wanachama wapya 211 waliojiunga na NSSF kuwa watafurahia maamuzi yao kwani watapata huduma za afya bure pamoja na wategemezi wao. Amesema NSSF inajenga maisha ya watanzania hivyo kujiunga nayo ni faida.

Amesema Bw. Mtemvu ni king'ang'anizi kwa ufuatiliaji. "Amekuwa akinipigia simu  mara kwa mara kuniuliza, anafika ofisini na nyumbani kwangu kuhakikisha mkopo unapatikana kwa wakati".

Dkt. Dau alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi kuwa mkopo huo ni shinikizo la kuutaka Ubunge wa Temeke. Akatumia nafasi hiyo kuwaasa kuwa hana mpango wa kugombea Ubunge wa Temeke. "Mimi ni Mtendaji, si mwanasiasa, nitaendelea kusimamia haya tunayotenda kwa wananchi".

Mwenyekiti wa PFT, Mbunge wa Temeke, Bw. Abbas Mtemvu akarudia maneno ya Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuri, aliyemwambia Rais Jakaya Kikwete, kuwa Dkt. Ramadhan Dau anastahiri kupata nishani ya utendaji kazi uliotukuka kutokana na mchango wake kwa watanzania.

Bw. Mtemvu amesema wananchi wa Temeke wanahitaji maendeleo ya haraka, iwapo Dkt. Dau atatangaza kuutaka Ubunge wa Temeke, yeye (Mtemvu), atakuwa Kampeni Meneja wake kwa lengo la kuifanya Temeke ipate Mbunge mbunifu kama Dkt. Dau.

Bw. Mtemvu amesema hakuna asiyemjuwa Dkt. Dau ndani na nje ya Tanzania, hivyo akitangaza nia ya kuutaka Ubunge, atakuwa mpiga debe wake namba moja akiamini kuwa Temeke itapata maendeleo ya haraka zaidi, itakimbia mbele.

Amesema NSSF inajipanga kujenga nyumba za kisasa katika eneo la Temeke Qts ambapo Dkt. Dau amekubali kuwa nyumba hizo zitajengwa kwa madaraja yote ili kila mwananchi amudu kuzipata kutokana na hali yake ya uchumi.

"Nani hamjui Dkt. Dau, miradi mikubwa yote inayofanywa katika nchi hii, kuna mkono wa NSSF, mfano Daraja la Kigamboni, nyumba za bei nafuu zinazojengwa mikoa mbalimbali nchini, sasa wanajenga kijiji cha kisasa cha Dege Eco Kigamboni", anasema Mtemvu na kuongeza kuwa PFT itakuwa na kijiji chake.

Amesema imani huongeza imani, NSSF imekubali kujenga nyumba 7000 za wananchama wa PFT katika kijiji cha NSSF iwapo hali ya urejeshaji mikopo itafanywa kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhan Dau akikabidhi kadi kwa BW. Mussa Maarifa, mmoja wa wanachama wapya 211, waliojiunga na NSSF Dar es Salaam. Kushoto ni Mbunge Jimbo la Temeke, Bw. Abbas Mtemvu, Meneja Kiongozi na Huduma kwa Jamii, Enice Chiume na Meneja uwekezaji, Bw. Abdallah Mseli.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhan Dau akimkabidhi kadi ya uanachama Bi. Pili Matimbwa, mmoja wa wanachama wapya 211, waliojiunga na NSSF Dar es Salaam juzi Kushoto ni Mbunge wa Temeke, Bw. Abbas Mtemvu, Meneja Kiongozi na Huduma kwa Jamii, Bi. Enice Chiume na Meneja uwekezaji, Bw. Abdallah Mseli.

Mwenyekiti wa PFFT na Mbunge wa Jimbo la Temeke Bw. Abbas Mtemvu akishukru Uongozi wa NSSF 


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru