UCHU

 SURA YA KWANZA

ARUSHA II

Musoke aliangalia ndani ya kitabu chake cha simu, akaipata namba ya Chifu ya nyumbani na kumpigia simu.

Alipoangalia saa ilikuwa yapata saa tano usiku.

"Hallo", alisikia sauti ya Chifu, ikiwa na nguvu kama ya kijana wa miaka thelathini.

"Mzee, shikamoo, Musoke hapa".

"Marahaba Musoke, habari za siku nyingi, nini kinakufaya unipigie simu saa hizi?".

"Umekasirika Mzee?".

"Hapana, shauku".

"Bado tu uko vilevile, utafikiri hujastaafu?".

"Mwili ndio unastaafu lakini nafsi huwa haistaafu maana nafsi haizeeki isipokuwa mwili".

"Ahsante nitazingatia, huo ushauri, maana nami naitwa mzee sasa na nafsi yangu imeanza kukubali".

"Hapana usiruhusu kabisa. Haya, lete habari zinazokufanya umpigie simu mzee kama mimi saa hizi kwanza uko wapi?".

"Niko Arusha".

"Aha, nilifikiri uko Kampala".

"Niko Arusha, Chifu". Ilikuwa ukimwita Chifu mara moja anajuwa kazi imeanza.

"Haya lete hizo habari".

Musoke alimweleza habari zote toka mwanzo mpaka mwisho. Pia alimweleza jinsi idara za upelelezi za serikali zilivyokataa kumsaidia kwa kitu nyeti kama hiki.

"Pole sana", Chifu alimjibu baada ya kuyasikia yote.

"Tatizo lako ni kubwa, la kuangaliwa kwa makini sana. Mimi mwenyewe nimekuwa nikishangazwa sana na mambo yalivyo Rwanda. Enzi zetu sisi tusingeruhusu hali kama hiyo itokee, wewe mwenyewe unajuwa msimamo wetu ulivyokuwa".

"Ndio Chifu, lakini serikali zetu za sasa kila mtu eti na nchi yake, eti hiyo ndio wanaiita demokrasia", Musoke alijibu.

Wakati wanazungumza kwenye simu mawazo ya Chifu yalikuwa yanakwenda kama Kompyuta kutafuta nani angeweza kumsaidia Musoke na Chama chake cha PAM katika azma yao ya kutafuta kiini cha matatizo ya Rwanda. Chifu mwenyewe alikuwa mwana PAM, na aliamini Umoja katika Afrika.

"Jack", Musoke alishituka kusikia Chifu akimuita kwa jina lake la kwanza. Hii ilikuwa na maana amekwisha pata jawabu. "Nafikiri nitakupatia ufumbuzi wa tatizo lako. Mtu mmoja tu katika Afrika hii ambaye anaweza kuifanya kazi yako. Hivi sasa ameacha kazi za kiserikali maana ameowa na anafanya shughuli zake. Lakini kutokana na imani yake katika Umoja wa Afrika anaweza akaifanya kazi hii, huna haja ya kuwa na kikosi, maana yeye pekee ni kikosi. Nitazungumza naye, nipe namba yako ya simu na chumba chako; nitakupigia simu kesho asubuhi".

"Ahsante Chifu, nilijuwa wewe ndiye utakayenimalizia matatizo yangu", Musoke alijibu kisha akampa namba ya simu ya pale hotelini na namba ya chumba. Alipomaliza tu akasikia simu ikikatwa. Akajuwa tayari Mzee yuko kazini.

Chifu alipokata simu ya Musoke, alipiga simu nyingine.

"Hallo".

"Chifu".

"Aha shikamoo".

"Marahaba, tuonane kusho asubuhi, tutastafutahi pamoja pale Kili, kama kawaida.

"Sawa Mzee, kesho", Chifu alijibiwa.

"Kesho, ahsante", Chifu alijibu na kukata simu.

ITAENDELEA... 0784296253

 
   

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru