UCHU

KAZI KWAKO

II

Ilikuwa saa tatu na nusu Chifu alipompigia simu Jack Musoke kule Arusha.

"Naam Chifu. Nilikuwa nasubiri huku kiroho kinanidunda. Haya nipashe".

"Willy Gamba ndiye mtu wako, mpokee uwanja wa ndege saa sita na nusu mchana".

Musoke alipigwa na butwa. Hakuweza kujibu kwa ajili ya furaha na msisimko. Hata Chifu alipokata simu hakusikia. Utafikiri kapigwa na radi.

"Willy Gamba! Willy Gamba! Jamani huyu Chifu nitamfanyia nini kwa kumleta willy Gamba! Mungu anatupenda sana Waafrika maana sasa kazi itafanyika", Musoke alijisemea kama kichaa.

Baada ya kuachana na Chifu, Willy Gamba alikwenda tena kwenye ofisi za Shirika la Ndege Tanzania ATC kujua kama kutakuwa na ndege ya kurudi siku ile ile jioni, maana Chifu alimkatia tiketi ya kurudi kesho yake jioni ambayo hakuiafiki. Alitaka arudi siku ile ile.

"Kuna ndege toka Kilimanjaro jioni", Willy alimuuliza kimwana mmoja kati ya vimwana walikuwa kwenye kaunta wakiwashughulikia wateja.

"Hakuna ndege jioni, kuna inayoondoka saa tano na nusu hapa na kuondoka kule saa saba na dakika kumi basi', yule kimwana alijibu huku akimrembulia macho.

"Hakuna ndege ya shirika lingine lolote?".

"Hakuna, labda uchukuwe ya kukodi huko Tanzanair", kimwana alijibu kwa kebehi akijuwa kuwa Willy hawezi kumudu gharama za kukodi ndege.

"Unaweza kunifanyia mpango ili hiyo ndege inichukuwe uwanja wa ndege wa Kilimanjaro saa kumi na mbili jioni?", Willy aliuliza katika hali ya kuomba.

"Sisi haturuhusiwi, sisi tunahusika na kuuza tiketi za ATC tu", yule kimwana alijibu kwa wasiwasi. Willy alitoa kadi yake, na kumweleza. "Mimi ni mteja wenu mzuri sana. Nenda hapo Tanzanair kanikodishie, nitamtuma katibu mahsusi wangu, atakuja kukuona mkalipe na kwa kufanya kazi hiyo na wewe utapata chochote kwani hakuna kazi ya bure siku hizi. Wewe unaitwa nani?".

Akiwa amepigwa na butwa yule msichana alijibu. "Naitwa Mariam".

"Oke, Mariam fanya hiyo kazi kungali mapema, mimi naenda uwanjani kuwahi ndege yenu ya saa tano. Katibu wangu anaitwa Dudu, atakuja kumaliza mambo ya malipo na wewe".

Kabla Mariam hajaanza kulalamika Willy alikuwa amekwisha nyanyuka na kuondoka.

"Wanaume wengine utafikiri wana dawa. Huyu mwanaume kanitia butwa, sasa itanibidi nifanye hiyo kazi yake; nimeshindwa hata kupata mwanya wa kukataa", Mariam alimweleza mwenzake aliyekuwa amekaa karibu naye.

"Hukuona macho yake! Akikuangalia tu roho inadunda, hiyo ndiyo dawa yake, ni mwanaume anayevutia sana, ana sumaku ya kiume, mwanamke hawezi kumkatalia kitu naye anajuwa hivyo", Husna alimjibu Mariam.

Mariam aliondoka na kwenda kumtafutia Willy ndege huku kiroho chake kinarukaruka. "Sijui nitamwona tena yule mwanaume, kaniachia kadi yake, ngoja nitamtafuta", Mariam alifikiri huku akielekea ofisi za Tanzanair.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru