UCHU

KAZI KWAKO

III

Willy Gamba alipofika ofisini kwake kwenye jengo la Sukari, Mtaa wa Ohio, ilikuwa saa nne na robo. Dudu aliangalia saa yake na kumwangalia Bosi wake kwa macho ya kumshitaki kuwa kachelewa.

"Shikamoo bosi", Dudu alimsalimia Willy.

"Marahaba, najuwa umeninunia kwani sikuwahi kutimiza miadi na wateja.

"Kumbe unajuwa, na ukafanya makusudi", Dudu alijibu.

"Siyo makusudi, ila ndiyo sababu kuna usemi kuwa, bosi hachelewi kazini, huwa amepita kwenye shughuli kadhaa wa kadha, nami nilipita kwenye shughuli kadha wa kadha. Sasa sikiliza, mimi naondoka kwenda Arusha kwa ndege ya ATC saa tano unusu, nina muda mfupi sana. Kumetokea dharura. Nataka nirudi leo jioni, maana dharura hii inaweza kunifanya nisafiri kwa muda wa wiki kadhaa nje ya nchi. Kwa vile ATC hawana ndege kutoka Kilimanjaro jioni, nimemuomba msichana mmoja aitwaye Mariam pale kwenye ofisi ya mauzo ya ATC anifanyie mpango wa ndege ndogo ya kukodi ya Tanzanair. Hivyo, uende ulipie na ndege iwe kwenye uwanja wa ndege wa Arusha saa kumi na mbili jioni, umeelewa?".

"Nimeelewa bosi, naona kweli dharura, mpaka kukodi ndege, nani atalipia gharama hizi bosi?".

"Nina mteja ambaye atalipia", Willy alijibu.

Dudu alikwisha fanya kazi na Willy kwenye ofisi yao hii ya watu wawili kwa muda wa miaka mitatu. Hivyo alikwisha mwelewa vizuri Willy na alifurahi sana kufanya kazi na mtu sifa na mwenye roho nzuri kama Willy. Hata siku moja hakupata ugonjwa wa moyo toka kwa bosi wake huyu. Alikuwa mtu tofauti sana na watu wengine ambao Dudu aliwahi kufanya nao kazi.

Baada ya kuacha kazi serikali, ambako alifanya kazi kama mpelelezi, na akawa mpelelezi wa kutegemewa si Tanzania tu bali Afrika nzima, Willy Gamba aliamua kuanzisha ofisi yake binafsi ya upelelezi, hasa iliyohusu mambo ya Bima. Aliamua kuacha kazi akiwa na umri mdogo wa miaka 42 tu. Kwa vile alitaka aoe kwani kazi yake serikalini ilimfanya asafiri sana nje, kitu ambacho kilimfanya asioe maana ndoa yake ingekuwa ya wasiwasi. Hivyo aliomba na kwa shingo upande na baada ya malumbano ya muda mrefu na waajiri wake huku akisaidiwa na Chifu ambaye alikuwa Bosi wake kabla hajastaafu, alikubaliwa kuacha kazi. Ndipo baada ya kuacha kazi, akamwoa mchumba wake ambaye alikuwa amesubiri kwa muda mrefu huku akimvumilia kwa safari zake nyingi.

Huyu mchumba wake aliitwa Pepe. Pepe alikuwa mtoto wa watu, msichana aliyeumbika, mzuri wa sura na tabia, na kwa uzoefu wake mwingi kwa wasichana, Willy aliamua lazima amwoe Pepe na kila wakati alimwambia mama yake ambaye kila siku alikuwa akimpigia kelele aoe, na asipomuoa Pepe basi hataoa tena.

Mama yake Willy alikuwa na wasiwasi sana na Pepe, kutokana na jinsi mtoto yule alivyokuwa mzuri wa sura. Alifikiri kuwa msichana mzuri kiasi kile hawezi kuwa mke wa nyumbani kwani lazima atakuwa na maringo. Lakini Mama yake Willy alikuwa kakosea kabisa. Huyu msichana alikuwa amelelewa kwao, wazazi wake walimlea kwa kumtayarisha ili aje awe mke wa mtu. Walimsomesha vizuri mpaka chuo kikuu, lakini walihakikisha kuwa Pepe anapata mafunzo ya namna ya kuishi na watu na maisha ya ndoa yanapewa kipaumbele. Na kweli pamoja na uzuri usioelezeka wa maumbile ya Pepe, tabia yake ilikuwa nzuri isiyoweza kuelezewa vilevile. Hii ndio inaonyesha kuwa tabia ya mtu haitokani na maumbile yake, bali zaidi inatokana na malezi.

Hivyo, baada ya kuacha kazi, Willy alifanya vitu viwili kwa mara moja. Alianzisha ofisi yake binafsi na akamwoa Pepe. Na hii miaka yao mitatu ya ndoa ilikuwa miaka mitamu iliyojaa kila aina ya raha, starehe na mapenzi yasiyo kifani. Kila mtu aliyewaona na kujuwa walivyokuwa wanaishi, aliwaonea wivu.

Dudu naye aliajiriwa na Willy alipofungua tu ofisi yake, Chifu ndiye aliyemtafutia mfanyakazi huyu. Hivyo hata ofisini kwake kazi zilifanyika vizuri na kwa uelewano mkubwa. Kweli Willy alikuwa hatoka nje ya Tanzania kikazi, ila tu kwa mapumziko ambayo alisafiri pamoja na Pepe wakitalii nchi nyingi sana, na kumwonyesha dunia ilivyo.

"Kama ndege inaondoka saa tano na nusu itabidi uwahi maana siku hizi msururu wa magari kwenye barabara ya Nyerere ni hatari".

"Kweli kabisa, niitie taksi, AVIS, na uwaeleze waje wanipokee jioni, kama yule dereva wao Ismail yupo ningependa aje yeye".

Ofisi za AVIS zilikuwa ofisi mpya jijini Dar es Salaam na haikuwa mbali na ofisi za Willy. Tangu ianzishwe ilikuwa na uhusiano wa karibu na ofisi ya Willy vilevile meneja wao walikuwa rafiki wa Willy.

"Pepe ana habari", Dudu aliuliza baada ya kuagiza taksi.

"Hajui, na ndio maana ningependa nirudi jioni ili kama nitasafiri nje ya nchi nijuwe nitamwelezaje. Na maelezo ili yaeleweke usiku ndio mzuri, hasa mkiwa ndani ya shuka".

"Au vipi", Dudu alidakia.

"Hivyo akipiga simu mwambie nitachelewa kurudi nyumbani, huenda hadi saa mbili usiku. Pale shuleni kwao kama kawaida ya Dar es Salaam, simu bado haifanyi kazi".

"Nitamweleza baba, usiwe na wasiwasi".

Taksi ilifika. Willy akachukua mkoba wake tayari kuelekea uwanja wa ndege.

"Shikamoo", Ismail alimwamkia Willy.

"Marahaba Ismail, maana sasa abiria tayari wana 'check-in' fanya kila njia sitaki kuachwa na ndege hii".

"Inaondoka saa ngapi?".

"Saa tano u-nusu".

"Dakika hamsini zimebaki, utawahi acha mimi nifanye kazi yangu", Ismail alimjibu Willy wakaondoka.   

Kweli Ismail aliijuwa kazi yake maana walipotoka kwenye jengo la Sukari aliingia Mtaa wa Ohio ili kukwepa msururu wa magari, akaingia Barabara ya Titi Mohamed, alipofika Mnazi Mmoja akaingia Mtaa wa Uhuru, halafu Lumbumba na kisha Mtaa wa Lindi tukatokea Ilala na kushika tena Mtaa wa Uhuru, tukaingia Barabara ya Nelson Mandela. Ndipo akashika Barabara ya Nyerere kwenye taa za Tazara, na ndani ya dakika ishirini tulikuwa Uwanja wa Ndege.

"Asante Ismail", Willy aklimshukuru na kumkabidhi shilingi elfu moja kama asante. "Usisahau jioni?".

"Nimeshaelezwa mzee, utanikutwa nakusubiri".

Willy alijulikana sana na wafanyakazi wa ATC na Dahaco, kwenye kaunta ya kujiandikisha kabla ya kuondoka na kwa vile alikuwa na mkoba wake tu walimchukuwa mara moja na kulipia kodi ya kiwanja na kuelekea chumba cha kuondokea.

Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania ATC iliondoka Dar es Salaam saa tano na nusu kamili. Willy alikuwa na tiketi ya daraja la kwanza, na alipoingia ndani ya ndege akitafuta mahali pa kukaa alimwona mwalimu wake, mzee Petro Magoti, akimchekea.

"Njoo ukae hapa Willy, habari za siku nyingi?".

"Nzuri, shikamoo", Willy alijibu huku akiuweka mkoba wake chini ya kiti chake.

"Marahaba, nimefurahi kukuona baada ya miaka kama mitatu hivi".

"Asante mwalimu, unajuwa nilikwambia wakati tulipoonana Mwanza kuwa nilikuwa natarajia kuacha kazi ya kuajiriwa ili nijiajiri mwenyewe, sasa tayari nimefanya hivyo. Na pia sasa nimeoa.

"Aha, hongera, nimefurahi sana nikisikia wanafunzi wangu mkiendelea vizuri", Mzee Magoti alijibu.

Mzee Magoti alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ambako Willy alisoma. Kwa vile Willy alikuwa na akili nyingi sana darasani, walimu wengi walimpenda sana na kumheshimu. Hata wakati matokeo ya mtihani wa Cambridge wa darasa la kumi na mbili yalipotoka Willy alipata ushindi wa juu kuliko mwanafunzi mwingine yeyote katika Afrika Mashariki na hivyo kuiletea shule ya Mwalimu Magoti heshima kubwa. Kutokana na matokeo hayo mazuri hata Mwalimu Magoti alipandishwa cheo hata kushika nyadhifa mbalimbali katika Wizara ya Elimu hadi kufikia kuwa Kamishna wa Elimu. Na alipostaafu walimu walimchagua kuwa Mwenyekiti wa Chama chao kama miaka miwili iliyopita.

"Nimekusikia ukiunguruma kwenye magazeti kuhusu matatizo ya walimu", Willy alimzungumzia.

Ndege ilikuwa inaweka speed ili iruke. Hivyo kama ilivyo kwa abiria wengi wakati huu kila mtu hunyamaza kimya akingojea ndege ipae ndipo waendelee na mazungumzo.

"Ndio kijana wangu, hali ni mbaya sana mashuleni mpaka sasa walimu wana mgomo baridi. Watoto hawasomi kabisa,  shule ambazo zinasemekana zinasoma, hasa zile za Sekondari, mwalimu anaweza kuingia darasani mara moja kwa wiki. Sasa utasema huku ni kusoma kweli, si hatari kwa maendeleo ya hawa vijana wetu ambao watakuwa viongozi wetu wa baadaye", Magoti alijibu.

"Lakini mzee, wewe ukiwa kiongozi wa walimu si uzungumze nao waelewe athari za kufanya hivyo kwa taifa hili", Willy alimshauri.

"Bwana mdogo, wewe unaweza kumshauri mtu mwenye njaa! Walimu hawa wote wana njaa, ndicho kilio chao. Mishahara ya serikali wewe mwenyewe unaijuwa. Na kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, mshahara wa mwalimu wa kawaida anaweza kuutumia kwa siku tatu tu katika mwezi na ukaisha, je, siku ishirini na saba afanyeje?", Mzee Magoti aliuliza.

"Lakini mzee hii inahusu watu wote walioajiriwa serikalini. Wote mishahara yao haitoshi", Willy alijibu.

"Ahaa, sasa unasema. Yote hii inategemea unyeti wa kazi. Ili watu wajiongezee kipato wanahangaika na kufanya shughuli nyingine. Sasa hivi ukienda kwenye maofisi mengi ya serikali hukuti watu, ukiuliza katoka nje kikazi. Kweli kikazi, maana anakwenda kufanya kazi kwenye miradi yake binafsi, iwe kwenda kukamua ng'ombe wake maziwa au kuwatafutia majani, au iwe kwenda kununua bia kwenye kampuni ya bia ili apeleke kwenye kiduka chake pale nyumbani, yote wanasema kaenda nje kikazi. Sasa kwa mwalimu hahitaji kutoka. Mimi nimekuwa mwalimu karibu maisha yangu yote, ualimu ni kazi ambayo unahitaji saa ishirini na nne, siyo kazi unayoweza ukafanya na kazi nyingine, hutaweza kuifanya sawasawa, Saa hii unafundisha. saa hii unasahihisha kazi za wanafunzi, saa hii unatayarisha masomo kwa ajili ya kesho. Kweli kazi ya ualimu ni nyeti inayohitaji muda wako wote. Sasa walimu nao wanapofanya kama wafanyakazi wengine na kuwa na miradi matokeo yake ndio hayo! wanafunzi hawafundishwi", Mzee Magoti alieleza.

Mhudumu wa ndani ya ndege alifika na kuwauliza watakunywa nini.

"Mimi chai", Mzee Magoti alijibu.

"Na mimi chai", Willy naye pia alijibu.

"Msingependelea bia au pombe nyingine kali", yule msichana aliendelea kuwashawishi.

"Hapana ni mapema mno", Mzee Magoti alijibu huku Willy akitingisha kichwa kukubaliana naye.

Hata kama Willy angependa bia lakini haikuwa heshima mbele ya mzee aliyemheshimu kama huyu kufanya hivyo.

"Haya, chai yenu inatengenezwa.

"Asante", walijibu, tena kwa pamoja. Kisha wakaendelea na mazungumzo yao.

"Sasa Mzee Magoti, si mmeieleza serikali na serikali inajuwa tatizo hili, na athari zake kwa taifa hili! Maana hawa vijana ndio taifa la kesho, na kama hawasomi ina maana karibuni tu tutakuwa na taifa la wajinga. Yaani wakati dunia inaingia kwenye karne ya ishirini na moja, elimu ndio kitu muhimu kwa taifa lolote, ili liweze kwenda sambamba na mataifa mengine katika sayansi na teknolojia: kama maneno unayosema ni kweli basi tuko hatarini", Willy alieleza mawazo yake kwa Mzee Magoti.

"Maneno yako ni kweli kabisa kijana. Na hiki ndicho tunachopigia kelele sisi mpaka sasa hatuelewani na viongozi wakifikiri tunajaribu kuwachochea wananchi. Lakini viongozi wetu hawajali kabisa. Jibu lao kila siku ni kwamba hali ya uchumi ni mbaya, na serikali haina fedha. Lakini sababu kubwa kwa nini hawajali. ni kwa sababu wao na marafiki zao hawaathiriki na tatizo hili walimu hapa nchini, maana wao wanasomesha watoto wao nje. Hivyo hawajali kama watoto hawasomeshwi: wa kwao wanasoma nje na katika shule za hali ya juu", Mzee Magoti alijibu kwa uchungu sana.

"Mzee Magoti umegusa kitu cha hatari sana. Yaani viongozi wetu wamekuwa na ubinafsi. Kwa vile wao wana pesa, basi wanapeleka watoto wao nje na hawajali nini kinawapata watoto wa wakulima na wafanyakazi, ambao hawana uwezo wa kupeleka watoto wao nje".

"Barabara kabisa Willy, lakini zaidi ya hapo wanajenga tabaka la watawala na watawaliwa. Kwa vile watoto wa wakulima na wafanyakazi ambao ndio wengi katika nchi hii, watapata elimu duni, basi hawa watoto wa viongozi na matajiri ambao ni kama asilimia (2%) ya idadi ya watoto wote wa nchi hii, watarudi na elimu nzuri na hivyo ndivyo watakavyoshika madaraka hapo baadaye maana wao watakuwa wamesoma vizuri, na kama ulivyosema ndivyo wataenda sambamba na mataifa mengine. Hii ni hatari kubwa kwa taifa hili", Mzee Magoti alijibu tena kwa uchungu.
   
"Ina maana viongozi wetu wanaiachia hali hii ya kushuka kwa kiwango cha elimu nchini kwa makusudi kabisa ili wawape watoto wao na wa matajiri nafasi ya kuendelea kuiongoza nchi hii, na kuwanyima watoto wa watu wa kawaida nafasi hii! Kama hii ni kweli, basi tunaelekea kubaya, maana katika nchi hii tangu uhuru watoto wa watu wa kawaida, ambao ndio sisi, serikali ilitupa nafasi nzuri na kutusaidia ili tuinuke na tuweze kuliondoa taifa katika ujinga na kuweza kuinua taifa na familia zetu kutoka katika hali duni", Willy alieleza.

"Nchi imegeuka, ubinafsi umetawala roho za viongozi wetu, wanajifikiria wao tu. Si viongozi wa wananchi tena, ila wanatafuta uongozi kwa faida yao wenyewe. Hata ukiangalia ni viongozi wachache sana kwa sasa ambao sio matajiri. Wanaingia katika uongozi wakiwa hawana kitu, lakini baada ya muda mfupi unawakuta wamejilimbikizia mali. Afadhali wangefanya hivyo halafu wakaendelea kuwasaidia wananchi ili na wao hali zao ziinuke, la hasha, sera zao ni za kuwadidimiza wananchi wawe masikini pamoja na vizazi vyao ili wasiwe na sauti kabisa. Sauti wanataka ibaki yao na vizazi vyao ili wabaki madarakani kama vile wafalme.

"Sikilizeni... tunakaribia kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro. Mabibi na mabwana, inuweni viti vyenu wima, fungeni mikanda yenu ya viti tayari kwa kutua", sauti ya msichana ilisema.

"Mzee, basi nitakutafuta ili unielimishe zaidi kuhusu mambo yalivyo katika nchi yetu hii kwa sasa, maana kwa muda mfupi huu nimeelimika kwa kiasi fulani", Willy alimweleza Mzee Magoti maana ndege ilikuwa inaelekea kutua na hivyo wasingekuwa na muda wa kuzungumza zaidi.

Mzee Magoti alitoa kadi yake yenye anwani na simu.

"Basi ukirudi Dar es Salaam, nipigie simu tuonane".

"Asante Mzee".

Ndege ilipogusa chini wote wakawa kimya mpaka iliposimama kabisa.

"Haya kwe heri Mzee Magoti", Willy alimpa mkono. Akachukuwa mkoba wake na akawa wa kwanza kutoka. Alipoiangalia saa yake ilikuwa saa sita na nusu mchana .

Willy aliposhuka kutoka ndani ya ndege, alimkuta Musoke anamsubiri.

"Shikamoo".

"Marahaba, habari za siku nyingi, haujabadirika bado, ila umetia uzito kidogo", Musoke alimweleza Willy.

"Asante, unajua nimeoa, sasa mapochopocho yananimaliza". Wote walicheka na kuelekea kwenye gari ambalo lilikuwa la kukodi lakini Mzee Musoke alikuwa analiendesha mwenyewe.

"Nimefurahi sana umekubali wito".

"Unajua tena Chifu, ni vigumu sana kumkatalia kitu, hasa anachokiamini yeye kuwa ni kitu muhimu".

"Najua, lakini lazima nikushukuru", Musoke alijibu huku kiroho kikizidi kumdunda kwa furaha kwa kuwa na uhakika kuwa Willy yuko naye tayari kwenda kutekeleza kazi hii nyeti, ambayo inaweza kuleta ufumbuzi mkubwa kwa mataifa ya Afrika.

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU