TAFUTA
UKWELI
Ilikuwa
yapata saa saba unusu. Musoke na Willy walipofika nyumbani kwa Temu. Walimkuta
Temu akitembeatembea mbele ya nyumba yake katika bustani huku ameweka mikono
yake nyuma. Kwa vile nyumba ilikuwa juu kwenye kilima, na wao walimwona kabla
hajawaona mpaka walipopiga honi ya gari ili kufunguliwa lango la mbele.
Alipoona ni gari la kukodi la Musoke, mara moja alikimbia na kulifungua lile
lango hata askari wake anayelinda nyumba yake hakuwahi mbio za mzee huyu. Hii
yote ilionyesha shauku aliyokuwa nayo Temu juu ya suala hili la Rwanda.
"Shikamoo",
Willy alimshalimia.
"Marahaba,
karibu".
Temu
alipeana nao mikono na wote na kuwakaribisha kule uani kwenye bustani ya nyumba.
"Wengine?",
Musoke aliuliza.
"Saa
nane watafika".
"Vizuri".
Walipokuwa
wameketi kule uawani kwenye kivuli kizuri cha miti, Musoke alitumia nafasi hiyo
kuwafahamisha.
"Bwana
Temu, huyu ni kijana wetu, anaitwa Willy Gamba, sasa hivi anafanyakazi za
kujitegemea, lakini alikuwa kwenye idara ya upelelezi ya Tanzania kabla
hajaamua kuacha kazi ili ajitegemee. Yeye ameombwa na marafiki zetu wengine aje
atusaidie kwenye hili tatizo letu", Musoke alieleza huku Temu akionekana
kushikwa na butwaa.
"Na
bwana Gamba, huyu ni mzee Temu na ndiye Mkuu wa PAM upande wa Tanzania.
Willy
aliinuka na kumpa Temu mkono.
"Mimi
siamini macho na masikio yangu", Temu aliendelea kuonyesha kama mtu
aliyeshituka sana. "Hivi kweli Willy Gamba yupo! na ni wewe! Hivi ni kweli
baba yangu, ni kweli. Mimi siku zote husikia habari za Willy Gamba na huamini
kuwa ni hadithi tu, maana mambo ambayo ameyafanya wakati wa ukombozi wa nchi
zilizo kusini mwa Afrika tulifikiri ni propaganda tu ya kamati ya ukombozi ya
OAU. Kumbe mtu mwenyewe upo na ni kweli. Eehe, ama kweli kuishi kwingi kuona
mengi. Basi bwana Musoke, kazi yetu itafanikiwa", Temu alieleza.
"Huyu
kijana wetu Mwenyezi Mungu amemjaalia uwezo mkubwa sana katika kazi hii ya
upelelezi. Hakuna mtu unayeweza kumlinganisha naye hapa Afrika, sijui huko
Ulaya, lakini hata majasusi wa huko Ulaya ndiye aliyekuwa akiyakomesha wakati
wote huo. Kwa kweli hata mimi niliposikia amekubali na ni yeye anayekuja basi
roho yangu ilitulia, najuwa tutafanikiwa. Hivi kwanini wamekukubalia kustaafu
mapema hivi?", Musoke alimuuliza Willy lakini kabla ya kujibu, mhudumu wa
pale nyumbani alifika na kutaka kujuwa watakunywa nini.
"Bwana
Gamba unataka kunywa nini?, kunywa kitu kidogo, maana huko ndani wanatengeneza
chochote cha mchana, sisi wachaga ndizi ndicho chakula chetu, sijui wewe
utapendelea?", Temu aliuliza.
"Kinywaji
naomba klabu soda, na nitafurahia sana macharari", Willy alijibu huku Temu
akicheka na kufurahi kusikia macharari.
"Kumbe
unayajuwa eeh basi baba yangu tutakula hayo maana wanaandaa. Na wewe mzee
Musoke?".
"Mimi
nitakunywa ki-wiski kidogo, unajuwa sisi wazee lazima ushituwe damu kidogo
upate joto".
"Sawa
kabisa, nenda kalete haraka", Temu alimwagiza mhudumu wake.
"Ehe
Willy, kwanini umeruhusiwa kustaafu mapema hivi?, au kwa sababu ya Afrika
Kusini kupata uhuru?", Musoke aliuliza tena.
"Hapana,
mimi niliomba kustaafu ili niweze kuoa na kuanza maisha ya kifamilia maana kazi
hii haifai kama umeoa na una familia. Sasa hivi nimeoa na mke wangu ni
mjamzito. Na hata kazi hii nimekubali tu, kwanza kwa sababu na mimi nimeumwa
sana na hali hii ya mauaji ya Rwanda na pili kwa sababu Chifu alisema
nisipokwenda mimi atakwenda yeye. Na unajuwa bwana Musoke, mimi nisingependa
hata kidogo kuruhusu kitu kama hicho".
"Ni
kweli kazi hii inahitaji kuweka mawazo yako pamoja, usiwe na fikira zingine,
lakini ndivyo hivyo, taifa bado linakuhitaji mara kwa mara kama hivi, ingawaje
si sana kama ulivyokuwa jikoni", Musoke alikubaliana na Willy. Mara
wakaona wenzao wengine wanaingia na wote wakasimama kuwasalimia.
Temu
alichukuwa nafasi ya kuwafahamishe wenzake kwa Willy Gamba. "Hawa ni wana
PAM kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Na wamekuja kwa ajili ya kikao hiki cha
kutathimini jinsi mambo yalivyokuwa huko Rwanda. Huyu ni bwana Kimani kutoka
Kenya, huyo ni Abakusi toka Nigeria, huyu ni Makwega toka Zambia na huyu kijana
mwenzio ni Malisa kutoka hapa hapa Tanzania". Kisha akageuka na kumgusa
Willy. "Na huyu ndiye mgeni tuliyemtarajia kwa ajili ya kazi yetu. Bwana
Willy Gamba.
Kimani na
Malisa waliwahi kusikia habari zake nao walishikwa na mshangao kama wa Temu.
Musoko alitumia nafasi hiyo kunong'ona na Abakusi na Makwega kuwaeleza Willy
Gamba hasa alikuwa mtu wa sifa za namna gani. Bila hata kusema mengi,
alipoeleza kazi zake mbili alizofanya na kuutingisha ulimwengu kwa kuwazuia
majasusi wa Afrika Kusini tayari wote wakamtambua na kupigwa na butwaa
vilevile.
"Wakati
mwingine binadamu akili inashindwa kuamini kitu. Mimi nilisikia jinsi mpelelezi
wa Afrika alivyoyaangamiza majasusi kule Kinsasa, Zaire, na nikaamini kuwa
zilikuwa hadithi tu. Sasa namuona hapa mtu mwenyewe, akili inashindwa kuamini.
Inashangaza", Abakusi alisema.
"Kama
Willy Gamba ndiye huyu kijana, basi mambo yetu yameiva", Makwega naye
alinena na kutokwa na wasiwasi aliokuwa nao usiku.
Bila
kupoteza muda mkutano uliendelea huku wakipata huduma za vinywaji na chakula.
"Nafikiri
wasiwasi wetu wote sasa umepungua baada ya kumpata kijana huyu?", Musoke
alisema kama vile akitoa maoni ya mkutano.
Wote
walitingisha vichwa kama ishara ya kukubali.
Kwa vile
kijana huyu yuko hapa, tumpe maelezo tunataka atufanyie nini. Nafikiri mimi
niendelee na kama mtu ataona nimepwelea mahala naomba asisite kuongezea,
sawa".
"Sawa",
wote walimjibu mzee Musoke.
"Bwana
Willy, wewe mwenyewe naami unazo habari nyingi kuhusu matukio ya Rwanda. Ila
sisi, kama wana PAM tungetaka tupate undani zaidi wa mambo yalivyotokea huko
Rwanda mpaka yakafikia yalipofikia na watu zaidi ya milioni moja katika nchi ya
watu milioni tano kuteketezwa kwa siku kadhaa tu. Kitu hiki kinatisha na kama
hakiwezi kuangaliwa kwa undani na kuthibitiwa inaweza kutokea tena si Rwanda tu
bali hata mahali pengine Afrika. Sijui unanielewa?", Musoke alimuuliza
Willy.
"Nakuelewa,
ila nataka nijie ni nini hasa mnataka mimi nifanye maana kule sasa kuna
serikali ya RPF, kuna mashirika ya kimataifa, kuna mashirika yanayotetea haki
za binadamu, mnafikiri mimi nitafanya nini zaidi ya watu hawa na wenye uwezo na
mapesa mengi nyuma yao, maana na wao wanachunguza kwa kina maovu yaliyotendeka
Rwanda", Willy alisema akitaka ufafanuzi zaidi.
"Sawa
bwana Gamba, kitu tunachotaka sisi ni uchunguzi wetu wenyewe. Hawa watu wengine
wote wanaweza kuwa na nia zao tofauti. Serikali ya RPF ni mhusika kwa kiasi
fulani. hatuwezi kupata ukweli asilimia mia toka kwao. Mashirika ya kimataifa
yenyewe yanaweza kuwa na ajenda tofauti, tena wanaweza kutoa ripoti kutokana na
ajenda yao. Wanaotetea haki za binadamu nao wana mtazamo wao kwa maana ya
kuonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Rwanda. Sisi tunataka
uende zaidi ya pale, ujue kama haki za binadamu zilikiukwa, na kwa nini
zilikiukwa, lazima kuna sababu. Mauajiyaliyotokea nini kiini chake, maana
yanaonekana yalikuwa yamepangwa toka mapema. Na vilevile kwanini Afrika na
dunia kwa ujumla, ikiwa kimya pamoja na nchi jirani kama Uganda, Tanzania,
Zaire na Burundi hazikufanya chochote kuzuia mauaji haya. Tukishajuwa chanzo na
sababu zilizofanya mpaka binadamu akafikia kuwa mbaya kuliko mnyama, nafikiri
tutakuwa tumejifunza; na hili fundisho litatusaidia kuweka mkakati wa kuzuia
kitu kama hicho kitakapotokea. Vilevile tujue namna ya kukidhibiti kabla
hakijaleta maafa makubwa kama haya", Musoke alijibu.
"Oke,
nimeelewa nini mnataka, nitajitahidi niweze kuchimbua mambo uliyoyataja hapo
ili nipate vyanzo vyake", Willy alijibu.
"Lakini
haitakuwa kazi lahisi, lazima uwe macho maana ukweli wa mambo haya unaweza kuwa
na athari nyingi kwa watu mbalimbali ndani ya Rwanda na pengineko duniani. Kwa
hiyo ikijulikana kuwa kuna mtu anatafuta ukweli na ikaonekana kuwa ataupata,
basi ujuwe masiha yako yanaweza kuwa hatarini maana mpaka sasa tunaamini kuna
watu wanajaribu kufukia ukweli usijulikane. Na hawa watu watakuwa watu hatari.
Tafadhali, hadhari ni lazima", Abakusi alimwasa Willy.
"Nitalitazama
hilo", Willy alijibu na kuendelea, "Na malipo yangu yatalipwaje,
maana sasa ni mfanyabiashara na si mfanyakazi wa serikali tena. Kazi hii
nimeichukua binafsi".
"Malipo
utalipwa na PAM. Kwa ajili ya kazi hii PAM iliwaomba michango wafanyabiashara
wa kiafrika ambao wanaunga mkono msimamo wa PAM na wametoa michango mizuri sana
na tukitoka hapa tutapitia hotelini kwangu nikupatie malipo yako. Sijui
utahitaji kiasi gani?", Musoke aliuliza.
"Mimi
vilevile, kama nilivyosema, naunga mkono madhumuni ya PAM, kwani ni mpaka pale
Mwafrika atakapojitambua kuwa lazima azungumze na Waafrika wenzake kupambana na
ukoloni mambo leo ndipo atakapokuwa amejikomboa kutoka katika umasikini, ujinga
na maradh. Kwa jinsi hiyo na mimi nikiwa mshabiki wa PAM nitaomba nilipwe
gharama zangu tu nitakazotumia, lakini utaalamu wangu nautoa bure".
Makofi na
kupeana mikono ya shukrani vilisikika.
"Sijui
hii kazi unafikiri itachukuwa muda gani?", Kimani aliuliza.
"Mimi
nitawafanyia kazi, nipeni muda", Willy alijibu.
"Wiki mbili?",
Makwega aliuliza pia.
"Nitajitahidi".
"Basi
tuonane hapa baada ya wiki mbili", Musoke aliagiza.
"Sawa".
"Lakini
Willy Gamba atakuwa anawasiliana na mimi Kampala kwa kila hatua atakayofikia.
Kama ikionekana kazi inakuwa bado baada ya hizo wiki mbili,
nitawajulisha", Musoke alieleza.
"Sawa".
"Haya,
asanteni sana wazee, tutaonana Mwenyezi Mungu akitujaalia baada ya wiki mbili.
Sasa hivi ngoja niende na mzee Musoke akanikamilishie masuala ya mapesa",
Willy aliaga huku akiwachekesha.
"Nilitaka
kusahau. Tumekupatia nafasi ya kulala Impala, ukienda tu pale mapokezi watakupa
funguo, tumelipia kila kitu, kazi kwako. Sijui kama utahitaji usafiri kesho
kukupeleka uwanja wa ndege?", Temu alieleza na kuuliza.
"Hapana,
nitajitegemea kwenda uwanja wa ndege".
Musoke
alipoangalia saa ilikuwa saa kumi na nusu. Willy alipewa mkono wa heri na
wajumbe wa PAM huku kila mmoja akimwombea mafanikio na usalama. Willy aliupokea
mkono huo wa heri huku naye kimoyomoyo akiomba sala zao ziwe pamoja naye, kwani
hawa walikuwa watu wenye roho za ubinadamu, ambao walikuwa wakitumia muda wao
kujaribu kuwasaidia wengine bila malipo ya aina yoyote. Kweli Mungu awabariki.
Musoke na
Willy aliondoka, wakaelekea Maunt Meru.
"Kesho
umesema ndege saa ngapi?", Musoke alimwuliza Willy.
"Saa
tatu asubuhi".
"Nije
nikupeleke?".
"Hapana,
nina marafiki wengi hapa watanipeleka".
"Na leo
jioni tunaweza kula pamoja?", Musoke alimkaribisha chakula cha usiku.
"Hapana,
nitakwenda kwa dada yangu jioni, alifiwa na mjukuu wake na nilikuwa sijapata
nafasi ya kumsalimia na hii ndio nafasi pekee niliyopata".
"Umeua
ndege wawili kwa jiwe moja".
"Bila
shaka", Willy alijibu huku akijuwa kabisa kuwa angeondoka jioni ile. Willy
kama kawaida yake, aliendelea kuonyesha kama angelala Arusha. Hii inaonyesha
jinsi ambavyo Willy hamwamini mtu yeyote mara akishakuwa kazini.
"Huwezi
kujuwa, kikulacho ki nguoni mwako, uzoefu wa siku nyingi umenifundisha",
Willy alijisemea moyoni.
Walipofika
Hoteli ya Mount Meru, walikwenda chumbani kwa Musoke na kuanza kuelezana tena.
Kwa vile Musoke naye alikuwa na uzoefu wa siku nyingi na kazi ya upelelezi
alijuwa Willy angetaka nini.
"Bwana
Gamba, unajuwa kazi hii inaweza ikawa ngumu na ya hatari kuliko hata jinsi
tunavyotegemea. Hivyo, jitayarishe kwa yote, nadhani unanielewa?", Musoke
alimwuliza.
"Nakuelewa
sana, kazi hii naichukulia uzito uleule wa kawaida, sintaipuuza hata chembe.
Kwa kawaida uzoefu umenionyesha kuwa kwa kawaida kazi rahisi ndio hugeuka kuwa
ngumu sana".
"Vizuri,
mimi ninao wenyeji kule Rwanda, ambao nafikiri wanaweza kukusaidia kupata
fununu za awali", Musoke alisema na kufungua mkoba wake na kutoa kitabu
chake cha anuani. "Yuko rafiki yangu ambaye kwa miaka amekuwa akiipinga
siasa ya chama cha MRND. Yeye ni mwanajeshi. Alikuwa kamanda katika jeshi la
kumlinda Rais, lakini kwa vile hakukubaliana na sera yao, aliacha na kuanza kwa
siri kueneza habari kwa vyombo vinavyotetea haki za binadamu jinsi serikali ya
Rwanda ilivyokuwa inavunja haki za binadamu nchini humo. Wakati Rais alipouawa
Aprili 6, 1994, yeye alikuwa Nairobi kuonana na Katibu wa Chama cha kutetea
Haki za Binadamu ulimwenguni. Hata hivyo, huku nyuma mke wake na watoto wake
sita na wapwa wake wawili, wote waliuawa tarehe 7, Aprili. Hii ina maana
angekuwepo Kigali na yey vilevile leo angekuwa marehemu. Anakaa Kimihurura
nyumba namba 168. Simu yake kwa bahati ni moja ya chache zinazofanyakazi sasa
hivi na ni namba 50486. Yeye ni Mhutu.
"Umeishazungumza
naye?", Willy aliuliza.
"Nitazubumza
naye, tuna uelewano mzuri, na yeye anajuwa mengi kwa watu wachache waliokuwa
wanaipinga serikali waliobaki. Na ujuwe huyu mtu alikuwa karibu sana na serikali
ya Rwanda, na huenda karibu sana na Rais mpaka kufikia kuwa kamanda wa jeshi
lake. Hivyo, anajuwa serikali ilivyoondolewa madarakani na RPF vizuri sana, na
ndio sababu vilevile kumtafuta ili kumuua ili kuua ukweli wa mambo".
"Vizuri,
nikifika Rwanda nitamtafuta kama nitamhitaji".
"Tumekupangia
kwenye hoteli iitwayo Des Mille Collines. Hoteli hii ni maarufu maana wakati wa
mauaji watu wengi, hasa wa mataifa ya nje, walijificha hapa na hivyo hata
wanyarwanda waliokuwa wanatafuta ili kuuawa kati ya walionusurika ni wale
waliobahatika kufika hoteli hapo. Hivyo, nayo itakupa fursa nzuri kupata fununu
mbalimbali.
Vilevile
ningependa umwone Padre mmoja ambaye tunafahamiana na yeye alinusurika
kimiujiza baada ya mapadri, maburuda , watawa na watu wote waliokuwa kwenye
kituo hicho cha dini kiitwacho Centre Christus, kuuawa na Wahutu wenye siasa
kali. Padri huyu anaitwa Jean Marie Karangwa. Utapata mengi toka kwake
vilevile".
"Bado
yuko kwenye kituo hicho?", Willy aliuliza.
"Ndio
yupo, na anajaribu kukianzisha upya. Na wa mwisho ambaye ningependa umwone
ikiwa unahitaji msaada, maana huwezi kujuwa, unaweza kuwa kwenye hatari ambayo
inahitaji msaada wa kiserikali, hasa kijeshi. Huyu ni rafiki yangu saana,
tumekaa naye jirani mjini Kampala na ni mmoja wa makamanda wa RPF, mtu shupavu
kama wewe na msomi kama wewe na kijana wa rika lako. Naamini mkionana
mtashibana tu. ana roho safi sana. Anaitwa Col Thomas Rwivanga, namba yake ya
simu 60314".
"Asante,
nikihitaji msaada wake nitamtafuta", Willy alijibu.
"Utaondoka
lini na kwa njia gani?", Musoke aliuliza.
"Mimi
kesho kutwa nitakutafuta Kampala nikiwa Kigali kukujulisha nimefika".
Musoke
hakuuliza zaidi maana alielewa maana yake. Kisha akatoa bahasha kubwa iliyokuwa
na pesa za dola za Kimarekani. Idadi yake haikuzungumzwa, lakini bila shaka
ilikuwa maelfu ya madola.
Baada ya
kumpa mzigo huo walisimama na kuagana.
"Haya,
nakutakia safari njema na kazi njema. Nakuombea heri", Musoke alimshika
mkono akionyesha uchungu kidogo.
"Asante
sana, tuombe Mungu", Willy alijibu na kuondoka.
Willy
alipoachana na Musoke alikodi teksi pale nje ya Mount Meru Hotel na kuelekea
Impala. Alipofika Impala alijitambulisha. "Naamini nina nafasi ya chumba
hapa, naitwa Willy Gamba.
Msichana wa
mapokezi aliangalia kwenye orodha yake ya majina kisha akaliona jina la Willy
Gamba.
"Ndio
baba, chumba 212", alijibu huku akitoa funguo na kumkabidhi.
"Una
mizigo?".
"Hapana,
huu mkoba wangu una kila kitu".
"Kila
kitu?".
"Kila
kitu nakuambia, utashangaa nikiufungua, mrembo zaidi yako atatokea".
Yule
msichana akacheka na Willy akapandisha ngazi. Alikifungua chumba na kukuta kidogo lakini
kizuri sana. Aliangalia saa yake akaona ilikuwa saa kumi na mbili kasoro robo.
Alikwenda
kitandani akatoa blanketi, akaliweka
pembeni na kufunua shuka na kutengeneza kama kwamba kulikuwa na mtu aliyelala
pale. Kisha, akauweka ufunguo kwenye
kufuli la mlango kwa ndani, akachukua mkoba wake. Akafungua mlango na kuurudisha bila kuufunga
na funguo kwa vile aliziacha ndani makusudi na kutelemka chini. Alipoangalia pale mapokezi na kuona wapokeaji
wapo shughulini, alichepuka na kutoka
nje. Akelekea kwenye maegesho ya teksi na kukodi teksi kuelekea uwanja wa ndege
wa Arusha.
Ilikuwa
yapata saa kumi na mbili na robo alipofika uwanja wa ndege na kukuta ndege
imeshatua tayari. Rubani wa ndege alimfuata na kumpokea mkoba wake.
"Habari
za jioni?", Rubani alimshalimia.
"Za
jioni nzuri asante".
"Huna
mzigo zaidi?".
Sina, ni huo huo".
Rubani
aliufungua mlango wa ndege hii ya Tanzanair, aina ya Cessina Mark 4, na kumkaribisha abiria
wake huyu mmoja, ambaye walikaa pamoja kwenye viti vya mbele, na kisha akawasha
injini za ndege, na kuruka.
ITAENDEA
0784296253
Comments
Post a Comment