UCHU

SURA YA KWANZA
ARUSHA

Christopher Temu, ambaye Jumapili hii nyumbani kwake Arusha, alikuwa amefikiwa na ugeni mkubwa kutoka Umoja wa wanaharakati wa Afrika (Pan African Movement PAM) kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Temu alikuwa mwanachama wa chama hicho.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa watu hawa kukutana nyumbani kwa Temu kwani watatu kati yao walikaa nyumbani kwake kwa muda usiopungua miezi sita. Mnamo mwaka 1992 na 1993 walihudhuria mkutano uliofanyika Arusha kuvisuruhisha vikundi mbalimbali vilivyokuwa vikipambana katika mgogoro wa nchi ya Rwanda, ili mgogoro huo umalizike kwa njia ya amani

Kikundi hiki cha PAM. ambacho kilikuwa kinahudhuria kama kikundi cha wapenda amani wa Afrika. Kilikuwa kinaweka shinikizo kwa kila upande uliokuwa unahusika na mgogoro huo ili umalizike kwa amani. PAM ilianzishwa mwanzoni mwa karne ya 19 ikiwa na lengo la kupambana na utumwa, ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo, kupigania haki ya watu weusi na kuhakikisha kuwa waafrika wanaweza kupambanua mambo yao wenyewe.

Hivyo, mara hii kikao kilichokuwa kinafanyika nyumbani kwa Temu kilikuwa cha kutathmini juhudi zote zilizofanywa kuumaliza mgogoro wa Rwanda kwa amani, lakini bila mafanikio. Wakiwa wamekaa kwenye bustani nzuri iliyokuwa nyuma ya nyumba hii iliyojengwa kisasa. Ikiwa kwenye barabara ya Njiro kwenye kilima kidogo ikiuangalia mji wa Arusha kwa upande wa Kijenge. Mkutano uliendelea mchana huu wa saa kumi alasiri huku bia aina ya safari na ndafu, iliyokuwa inachomwa hapohapo kwenye jiko la mkaa vikiendelea kuwa viburudisho vya wageni hawa.

"Ndugu zangu. Fundisho kwa Rwanda ni fundisho kwetu sote, na sisi tukiwa tumejitolea kuona Afrika inajikomboa na kujitawala kwa amani ni lazima tukae chini kulitafakari swala zima la Rwanda tuone makosa yalitokea wapi, na kwanini hali ilifikia hapo ilipofikia na watu zaidi ya milioni moja kuteketea bila Afrika wala dunia kufanya chochote", Jackson Musoke kutoka Uganda ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa PAM Kanda ya Afrika Mashariki alieleza.

"Ni kweli kabisa maneno uliyosema, lakini mimi nafikiri wakati mkutano wa amani ulipokuwa unaendelea hapa Arusha. Ukweli wa mambo Rwanda ulikuwa haufahamiki. Na hivyo maamuzi mengi yaliyofanyika hayakuzingatia hali halisi ya mambo ilivyokuwa Rwanda wakati huo. Na ningependa niseme kuwa hata hivi sasa tunavyokaa hapa hali halisi na ukweli wa mambo Rwanda bado haujulikani. Ndio maana Jumuia ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Nchi Huru za Afrika bado wanafanya maamuzi ambayo yanazidi kuleta matatizo nchini humo, na kuifanya serikali ya sasa iyumbe katika kutekeleza shughuri zake za kuleta amani iliyo ya kweli katika nchi hiyo", Alfred Kimani kutoka Kenya aliongezea.

"Sasa tutafanya nini ili huo ukweli wa mambo uweze kujulikana na matatizo yaliyo mengi katika nchi hiyo yaweze kutatuliwa?", Temu aliuliza.

"Mimi nafikiri tuunde tume ya uchunguzi, ikafanye uchunguzi, ichimbe chanzo cha matatizo Rwanda toka kabla ya uhuru mpaka sasa, na kujaribu kuelewa kabisa tatizo ni nini na nani anahusika na matatzo kwani mimi siamini kuwa tatizo hasa ni kabila tu. Miaka yote tumefikiria hivyo na kujaribu kumaliza tofauti za kikabila lakini mambo bado yako pale pale", Abdul Abakutsi toka Nigeria alijibu.

"Vilevile, kama tatizo ni la kikabila, lazima uchunguzi ufanyike ili ipatikane namna ya kulitatua tatizo hilo maana hatuwezi kukaa tu na kusema kwa sababu ni tatizo la kikabila, basi halina ufumbuzi", Lukaka Makwega kutoka Zambia aliongeza.

"Tulipokuwa hapa kwa ajili ya mkutano wa amani, ilionekana kwamba serikali tawala ndiyo iliyokuwa inachochea ukabila. Swali hapa ni kwanini serikali inachochea ukabila?. Ni kwa sababu inataka kubaki madarakani kwa njia ya gawa utawale au Rais alikuwa na sera za kikabila yeye mwenyewe au kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinachochea hali hii, maana kinachotisha zaidi ni jinsi mauaji hayo yalivyotokea. Inaonekana kuwa dakika ishirini tu baada ya ndege ilikuwa imemchukua Rais kutunguliwa mauaji yalianza sehemu zote. Hii inaonyesha mauaji yamepangwa kabla. Ina maana ilijulikana kuwa Rais atauawa siku hiyo?. Na kama Rais ndiye aliyepanga mauaji haya, je alijuwa kuwa atauawa, na kwa hiyo akapanga akiuawa alipiziwe kisasi?. Na kama alijuwa atauawa kwani alirudi na ile ndege! Mimi vilevile naanza kukubaliana na wenzangu kuwa huenda kuna mambo zaidi yasiyojulikana ambayo yanaleta matatizo nchini humo. Nami naamini kuwa mambo hayo yakifichuliwa ufumbuzi wa matatizo ya ndugu zetu hao utapatikana haraka", Charles Malisa wa Tanzania alichangia.

"Kuna kitu kingine nilichokisema mwanzoni ambacho kinatisha sana. Jumuia ya Kimataifa haikufanya kitu chochote pamoja na kuona jinsi watu walivyokuwa wakiuawa kinyama. Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yalikuwepo. Na Jeshi la Ufaransa lilikuwemo nchini humo wakati wa mauaji. Nchi kama Marekani ambazo zimejitokeza kama Polisi wa dunia, vilevile haikushtuka. Na kila mtu anakubali kuwa haya yalikuwa mauaji ya kikatili yaliyopangwa kuliko yale ya Hitler aliyowaua Wayahudi. Kwanini hali ilibaki hivi! Na nchi za kiafrika nazo zilikaa tu zikiangalia kabila moja ndani ya nchi ya kiafrika likiangamizwa kabisa ili lisiwepo tena. Jamani hapa kuna sababu na kuna jambo ambalo halieleweki. Uchunguzi ni kitu cha lazima", Musoke alisisitiza.

"Abakutsi ametoa ushauri wa kuunda tume ya uchunguzi, sijui ni tume ya watu wa namna gani anayozungumzia, maana nchi yenyewe ya Rwanda bado iko katika hali ya kivita bado wanauana. Serikali ya sasa bado haina uwezo wa kudhibiti hali ya usalama katika nchi hiyo. Mambo yote bado shagalabagala. Tukisema watu kama sisi twende huko kufanya uchunguzi hakika hatutaambulia kitu kama si kutafuta kuuawa. Uchunguzi ni muhimu lakini lazima tufikirie uchunguzi huu ufanywe namna gani", Makwega alishauri.

Watu wote waliohudhuria kikao hiki walinyamaza kimya wakitafakari kwa kina kuhusu uzito wa suala hili nyeti.

"Lete ndafu na utuongeze vinywaji, tunatakari huku tukilegeza makoo", Temu alimwagiza mtumishi wake. Bia baridi aina ya Safari zikaletwa na mabwana hawa wakaendelea kulegeza makoo na kutafuna ndafu, huku wote wakitafakari mazungumzo yao kwa makini.

Baada ya kimya kirefu Abakotsi alivunja kimya hicho. "Huenda ikawa ni lazima tuunde kikosi cha siri cha upelelezi, kipeleleze kwa sirisiri halafu kituletee taarifa maana serikali zetu zinao vijana wanaoweza kufanya upelelezi kama huo na ukazaa matunda. Kama bwana Makwega alivyosema, tume ya kawaida haiwezi kuambulia kitu, kwani mambo ni magumu huko. Nia yetu ni kupata ufumbuzi na si kupeleka watu wakauawe. Mnasemaje jamani?".

"Hapo umenena, hiyo ndio njia pekee ya kuweza kuingia ndani na kupeleleza kiini cha matatizo hayo. Mimi nakuunga mkono ila tutaiomba serikali gani itupe msaada huo?. Nyinyi wenyewe mliona jinsi serikali zetu zilivyonyamaza na kuacha kana kwamba hazikujua kuwa mauaji yalikuwa yakifanyika Rwanda", Makwega alinena.

"Wote tunakubaliana kuwa njia nzuri ya kupata kiini cha matatizo yaliyosababisha hali ya Rwanda ikafikia pale ni kutuma kikosi cha upelelezi?", Musoke aliuliza.

"Ndiyo", wote walijibu kwa pamoja.

"Basi, tuahirishe mkutano kwa leo, tuonane hapa kesho mchana saa kama hizi ili niweze kuwasiliana na watu fulani fulani ambao naamini wanaweza kutusaidia bila kugongana na serikali zetu", Musoke alisema.

Nyuso za wajumbe, ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zikionyesha wasiwasi, zilikunjuka na kuonyesha furaha. Ndipo wote walipokumbuka kuwa Musoke ndiye aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla haijavunjika. Hivyo, alijuana na wakuu wa idara hizi katika Afrika Mashariki, na alisemekana hadi sasa alikuwa akiombwa ushauri wa kiupelelezi mara kwa mara.

Baada ya kumaliza vinywaji vyao, wote waliondoka kuelekea kwenye hoteli zao walikofikia. Usiku ule Musoke aliporudi hotelini kwake, pale Mount Meru, aliwapigia simu rafiki zake, yaani wakurugenzi wa upelelezi wa Kenya, Uganda na Tanzania. Alizungumza nao kidiplomasia na kila mmoja alimuomba ushauri na kumweleza sababu za kufanya hivyo. La kusikitisha ni kwamba, kwa vile yeye alikuwa sasa anaongoza chombo ambacho si cha kiserikali, serikali zisingeweza kumsaidia mtu au kikundi cha watu, kwa vile ingeshindwa kujieleza iwapo mkasa wowote wa kiupelelezi ungetokea.

Hilo ndilo lililokuwa jibu la kila mkurugenzi wa upelelezi. Wote waliomba samahani kwa hilo kwani walimheshimu sana, lakini ilikuwa nje ya masharti yao ya kazi, hasa wakati huu ambapo siasa za nchi hizi ni kutoingilia mambo ya ndani ya nchi zingine!

Swala hili lilimkasilisha sana Musoke. Wakati wenzao katika PAM wanapigania Afrika iwe moja, wengine wanadai eti ni kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine!

"Ole wetu Afrika", Musoke alijililia. Ni wakati alipokaribia kukata tamaa, baada ya kufikiri sana namna ya kuweza kufanya ndipo alipomkumbuka Mzee mmoja mstaafu. Alifikiri huyu angeweza kumtatulia shida yake kwani ni Mzee aliyeisaidia sana Afrika, hasa wakati wa ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika. Yeye alijuana na wapelelezi wengi na maamuzi yake yalikuwa ya pekee, na ndiye aliyekuwa kitovu cha ukombozi Kusini mwa Afrika. Mpaka leo wengi walimjua kwa jina la "Chifu" tu.


ITAENDELEA.... 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU