UCHU

TAFUTA UKWELI


III

Ilikuwa saa kumi na mbili alfajiri simu ya JKS ilipolia na kumwamsha usingizini.

"Hallo, nani?", JKS aliuliza huku amebanwa na usingizi.

"Phillipe".

"Ehe, sema", alijibu kwa shauku.

"Matanga hayatakuwepo, mtu wetu hakulala pale, na hata hajulikani kalala wapi, alionekana akiingia lakini hakuna aliyemuona wakati akitoka. Funguo za chumba kaziacha chumbani, Kavurugavuruga kitanda lakini hakukilalia. Tumefanya utafiti katika hoteli na nyumba zote za kulala wageni Arusha nzima,hayupo. Mtu wako ni mjuzi, naamini maneno yako", Phillipe alimalizia.

"Haya asante, kazi imeanza". JKS alikata simu baada ya kusema. 


IV
 
Baada ya kutelemka Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea Arusha alikwenda kwenye ofisi za Tanzaniar za pale uwanjani na kwa bahati alimkuta meneja hajaondoka, hivyo akafanya mipango ya kukodi ndege yao kesho yake alfajiri ili impeleke Kigali. Ingawa ndege zao zilikuwa na kazi nyingi kesho yake, lakini kwa vile ile biashara ya kwenda Kigali ilikuwa nzuri, meneja alimkubalia ila akaomba Willy asaidie kupata ruhusa ya kutuwa kwenye uwanja wa ndege wa Kavihanda wa mjini Kigali. Willy alilipa na kuahidi kuwa angejitahidi kupata hiyo ruhusa. Alipewa kila kitu ambacho kingehitajika kule Kigali ili kibali kipatikane.

Willy alifika nyumbani yapata saa mbili usiku baada ya kupokelewa uwanja wa ndege na kuletwa moja kwa moja nyumbani na Ismail, dereva wa AVIS. Alitoa shilingi elfu tano akampa Ismail kama bakshishi.

"Asante sana mzee, gharama zitawekwa kwenye akaunti yako", Ismail alijibu.

"Kama kawaida. Asante kwa kuja kunipokea na kwa heri", Willy alijibu na kutelemka kwenye gari.

"Kwa heri mzee", Ismail alimwaga.

Pepe alikuwa jikoni akipika wakati Willy alipoingia ndani. Mara alipomwona alitoka jikoni akamkimbilia sebuleni huku akiwa ameshikilia kipande cha nyama.

"Karibu nyumbani bwana wee", kabla Willy hajajibu, Pepe alimkumbatia na kumbusu. Tumbo la Pepe lilipoligusa la Willy, akahisi mtoto akicheza tumboni.

Kitu ambacho kilimwongeza furaha. Willy, bila kujua akadondosha mkoba wake, na kuendelea kumbusu Pepe. Mara Pepe akamsukuma kidogo na kuangalia jikoni asije akaunguza, na kumwekea Willy kile kipande cha nyama alichokuwa ameshikilia mdomoni, kisha alitabasamu na kukimbilia tena jikoni ambako Willy naye alimfuata.

"Siku nyingine utafanya moyo wangu usimame kwa raha unazonipa", Willy alisema akiwa amemshikilia Pepe begani, huku Pepe akikaangiza nyama kwenye chungu.

"Sasa nimpe nani raha kama si wewe mume wangu", Pepe alijibu.

"Kuoa kutamu", Willy alijibu.

"Kutamu sana, kama ukioa ama kuolewa na akupendaye ki-kwelikweli", Pepe alijibu huku akimtupia jicho la mahaba.

Willy alimgeuza na kuanza kumbusu tena.

"Inatosha kwa sasa. Ngoja kwanza nikakuwekee maji uoge, halafu utakuta chakula tayari ndipo unieleze kwanini umechelewa kuja nyumbani", Pepe alieleza.

"Nakwambia kuoa kutamu, najisikia kama mtoto wa miaka mitatu, nilivyokuwa nafanyiwa na Mama Willy", Willy alijibu kwa dhati kabisa kwani kila aliporudi nyumbani Pepe alimfanya ajisikie kama mtoto, na hivyo kusikia raha isiyo kifani.

Baada ya kuoga na kula, huku wakizungumza mambo yao ya kawaida Willy alifikiria jinsi ya kuanza kumweleza Pepe juu ya safari yake.

Ni mpaka walipokwenda kulala ndipo Pepe alipotoa wasiwasi wake. Wakiwa wameingia kitandani na kujifunika shuka, Pepe alijilaza juu ya kifua cha Willy na kuuliza.

"Chifu keshanieleza huenda ukasafiri kesho, mbona husemi?".

"Mara moja Willy alimfikiria Chifu ambavyo alijaribu kumsaidia ili asipate tatizo lolote kuhusu masuala ya nyumbani.

"Nilikuwa najishauri nitaanzaje kukueleza".

"Unaenda kesho lakini", Pepe aliuliza kwa sauti kali kidogo.

"Ndio alfajiri", Willy alijibu kwa unyonge.

"Sawa", Pepe alijibu.

"Sawa ya ukweli au ya hasira?".

"Sawa ya kikwelikweli, naelewa. Naelewa ya kwamba mpaka umekubali kuondoka uniache, kweli ni lazima uende, nami yafaa nikubaliane nawe. Willy nataka uelewa kitu kimoja, najuwa unavyonipenda, na unajuwa ninavyokupenda kwa hiyo uamzi wako ndio uamzi wangu, najuwa lingekuwa jambo la hivihivi tu usingekubali na Chifu asingejaribu kama alivyojaribu kunisihi nikueleze. Nimeelewa. Willy, nakupenda Willy, nakupenda sana", Pepe alisema na kuanza kububujikwa na machozi ambayo yalianguka kifuani kwa Willy.

Kwa mara ya kwanza maishani mwake, Willy naye machozi ya mapenzi yalimtoka. Mara mtoto tumboni kwa Pepe alicheza na mara hii kwa fujo sana, na kwa vile walikuwa wamekumbatiana ndani ya shuka Willy naye alimhisi.

Kitendo hiki cha mtoto kiliwatoa kwenye haya mawazo yao ya majonzi ya kuachana kwa muda na kuwarudisha katika hali yao ya furaha ya kawaida".

"Mtoto hataki tuwe na majonzi", Willy alimnong'oneza mkewe.

"Haswa", Pepe alijibu na kumkumbatia kwa kujibana kabisa kwenye mwili wa mumewe na kuweka mguu wake juu ya mapaja yake.

ITAENDELEA 0784296253Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru