UCHUKAZI IMEANZA

Baada ya kuzungumza na Phillipe JKS alimpigia simu ofisa mmoja wa usalama aliyekuwa anashughulikia maswala ya uchukuzi wa abiria. JKS ndiye aliyemsaidia sana ofisa huyu kupanda hadi kufikia ofisa usalama mwandamizi.

"Mulamba", JKS aliita baada ya simu kupokelewa.

"Ndiyo, nani mwenzangu?".

"Pole kwa kukuamsha, naona ulikuwa bado umelala, huyu ni JKS".

Mulamba mara moja usingizi ulimtoka na kuinuka kabisa kitandani na kuketi kwenye ncha ya kitanda.

"Ndiyo mzee, hapana nilikuwa nimeamka ila bado nilikuwa najinyooshanyoosha tu kwani jana nilichelewa kulala", alimjibu kwa woga. Ile sauti ya woga ilimfurahisha JKS maana alipenda na kufurahia kutetemekewa.

"Hamna neno, sasa sikiliza, hii ni amri toka juu kuliko hata mimi. Si unamjuwa Willy Gamba?".

"Ndiyo mzee, nani asiyemjua katika fani yetu hii", Mulamba alijibu.

"Amepewa kazi toka ngazi za juu, na jana alienda Arusha na ndege za Shirika la Ndege Tanzania. Kwa vile sasa hayuko tena kwenye ajira ya serikali, hii kazi amepewa nje ya mipango ya kiserikali maana ni kazi nyeti na serikali haitaki itambulike kuwa inahusika. Ila alitakiwa ajulikane yuko wapi kila wakati, lakini toka jana jioni hajulikani aliko. Sasa imeamriwa tutumie ofisi yako tujuwe yuko wapi na ripoti hiyo isiende kwa mtu yeyote ila mimi", JKS alimaliza.

"Hilo nitalifanya sasa hivi mzee, ila nataka kujua alikuwa anatarajia kwenda wapi baada ya kutoka Arusha?", Mulamba aliuliza.

"Baada ya kutoka Arusha alitakiwa kurudi hapa Dar es Salaam, halafu anende Kigali. Kuna ndege ya asubuhi sana ya ATC toka Kilimanjaro ambayo itaondoka saa moja, kama yumo nipe habari, kama hayumo tafiti ujuwe anakuja Dar es Salaam na usafiri gani, nipate habari haraka. Angalia usafiri wote mabasi, malori na kadhalika.

"Usiwe na wasiwasi mzee, nitakujulisha baada ya saa chache, tutampata tu. Tukimpata tumfanyeje?".

"Usifanye chochote, wewe eleza tu yuko wapi".

"Haya, asante".

"Kwa heri", JKS alikata simu.

Baada ya kukata simu ya Mulamba, JKS alipiga simu Paris kwa Jean na kumweleza mambo yaliyotokea Arusha na hadhari aliyokuwa amechukuwa tayari. Jean, akiwa bado na usingizi kwani Paris ilikuwa yapata saa kumi na nusu za asubuhi, tulikuwa tunapishana saa mbili.

"Nataka utakaponipigia tena simu unieleze kuwa tayari keshauawa, vinginevyo usinipigie simu mpaka utakapofanikiwa kazi hiyo. Natuma pesa leo asubuhi kupitia kwa yule rafiki yangu mwenye kampuni ya kitalii ya Concord Tours zikusaidie kukamilisha kazi. Vilevile nitawapigia simu na marafiki zangu wengine huko Afrika Mashariki wakupe msaada wowote utakaohitaji", Jean alimalizia na kukata simu bila bila kumsubiri JKS ajibu.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yake JKS alisikia woga. Alizijua nguvu za Jean na akajuwa itabidi atimize hii kazi, vinginevyo mambo yangeweza kumgeukia. Alifikiria jinsi Jean alivyokuwa amemwahidi kumsaidia kuunyakuwa urais wa Tanzania na alikuwa anaujuwa uwezo wa Jean kuifanikisha azma yake hiyo. Na dhamira ya JKS kuwa Rais ilizidi vitu vingine vyote, lakini leo huyu Willy Gamba angeweza kumfanya akose nafasi hii. Asubuhi hii alisikia jasho la baridi likimtiririka mgongoni na kujisemea kwa sauti. "Kwa kila hali lazima aondoke".

Bila kujua amesema kwa sauti kubwa mke wake aliyekuwa amelala bado alishtuka na kuuliza. "Unasemaje?".

"Hapana, sijasema kitu", JKS alijibu.

Mke wake alimjua sana. Hivyo, akanyamaza lakini alijuwa mzee alikuwa anasumbuliwa na kitu fulani. 

ITAENDELEA 0784296253   

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru