UCHU  
 KAZI IMEANZA

II

Willy alitua kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza mnamo saa mbili na nusu za asubuhi. Asubuhi kabla hajaondoka nyumbani alimpigia simu rafiki yake mmoja ambaye alikuwa na wadhifa wa juu ndani ya Chama cha Msalaba Mwekundu na kumwomba msaada kati ya ndege zao zilizokuwa Mwanza moja impeleke Kigali. Willy aliwahi kukisaidia sana Chama hiki, na huyu rafiki yake aliona bahati sana kupata fursa kama hii ili nae alipe angalau fadhila kidogo za Willy kwa yote aliyowahi kuwatendea.

"Bila shaka Willy, sasa hivi nitapiga simu Mwanza na hiyo saa mbili na nusu unayotegemea kufika Mwanza utakuta ndege ndogo ya injini mbili aina ya Cessina yenye namba MMT 3 ikikusubiri. Sisi tunaruhusiwa bila matatizo kutua Kigali kutokana na hali ilivyo Wilayani Ngara. Hivyo, huna haja ya kuhangaika kupata kibali cha kutua, hicho sisi tunacho na utakuta maofisa wetu pale Mwanza wameshawasiliana na Kigali", yule rafiki yake Willy alieleza.

"Nitafurahi sana, na kama vilevile mtawaeleza kuwa mimi ni afisa wenu", Willy aliongezea.

"Bila shaka", rafiki yake alijibu huku akicheka maana alijua Willy haendi Kigali bure.

Kwa hiyo, Willy alipotelemka ndani ya ndege ya kukodi ya Tanzanair alikuta ndege ya Chama cha Msalana Mwekundu iko tayari.

"Ina maana mimi sasa nitarudia hapa?", rubani wa Tanzanair alimuulizia alipomwona anashuka na mfuko wake.

"Ngoja kidogo", Willy alimjibu.

Willy alikwenda mpaka kwenye ile ndege na kumkuta rubani na ofisa mmoja wa Msalaba Mwekundu wakimsubiri Willy.

"Karibu mzee", wote wawili walitamka kwa pamoja Willy akawapa mikono kuwasalimia.

"Asanteni sana", alijibu.

"Sisi tuko tayari, ila tu tunaomba uende na ndugu yetu mmoja ambaye anaenda huko vilevile kikazi", yule afisa alimwambia willy.

Willy alimwangalia yule jamaa, na kumwona ni wa makamu yake na wa umbo lake.

"Sawa, lakini ningeomba aje na ile ndege ndogo ambayo nimekuja nayo ili rubani awe na mtu wa kuzungumza nae, maana hiyo nayo inakuja Kigali, ila kwa sababu lazima ijaze mafuta na kukaguliwa kidogo ndio sababu imebidi mimi nikifika tu hapa nipate ndege nyingine kwa vile nina miadi maalumu ya kiserikali pale uwanja wa Kigali na mtu ambaye ataondoka saa moja kuanzia sasa", Willy alieleza.

"Basi, vizuri sana. Je, ndege yako ina vibali vyote vya kutua?", yule ofisa aliuliza maana alijua jinsi hali ilivyokuwa uwanjani pale Kigali.

"Hamna taabu, kila kitu kipo", Willy alijibu, kisha akaenda kwa rubani wa ndege yake.

"Sasa ukishajaza mafuta utakuja na yule bwana pale, naye anakuja Kigali. Ukishamshusha tu basi wewe urudi", Willy alimweleza.

Yule rubani alishangaa kwanini wasitumie ndege moja badala ya ndege mbili. Lakini kwa vile haikuwa shughuli yake na kwa vile alikuwa ameagizwa kwenda mpaka Kigali aliamua kubaki ameshangaa lakini atekeleze wajibu wake.

"Sawa mzee", yule rubani alimjibu huku sauti ikionyesha mshangao. Willy alitoa dola mia za kimarekani, akampa.

Tabasamu safi likaonekana usoni mwa rubani.

"Asante sana mzee", alijibu tena na kupeana mikono ya kuagana. Willy alikwenda kwenye ndege, na rubani wa Chama cha Msalaba Mwekundu akaiondoa ndege kuelekea Kigali ikiwa yapata saa tatu kasoro robo. saa za asubuhi. 


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru