UCHU

MIGUU YA NYOKA

Willy alipowasili kwa Col. Thomas Rwivanga, alimkuta anamsubiri. willy alikuwa amemweleza kuwa angekuwa anaendesha gari la Msalaba Mwekundu na angekuja peke yake bila  Vicent. Col. Rwivanga alikuwa amemweleza njia ya kupita mpaka huko nyumbani kwake, Kimihurura.

Col. Rwivanga aliposikia mwungurumo wa gari alitoka nje na kwenda kumpokea Willy.

"Habari yako?", Col. Rwivanga alimsalimia Willy huku akimpa mkono.

"Safi, na wewe?", Willy alimjibu.

"Safi kabisa, nafurahi sana kuonana na wewe, Mzee Musoke amenieleza habari zako, nami nilikuwa na shauku kubwa ya kukutana nawe. Karibu ndani", Col. Rwivanga alimkaribisha Willy.

"Asante sana, nimekaribia", Willy alijibu huku akiingia ndani na kuketi.

"Nikupe kinywaji gani?|".

"Klabu soda inatosha", Willy alijibu.

Col. Rwivanga alileta Klabu soda mbili na kuzifungua, wakaanza kunywa.

"Ehee, habari ya maisha?", Col. Rwivanga aliuliza.

"Safi, naamini Mzee Musoke amekueleza kwanini niko hapa".

"Ndio amenieleza".

"Imebidi nikuone mapema maana kuna jambo lililotokea ambalo linaonyesha kuwa katika uongozi wenu kuna mtu aliyejuwa kuwa mimi nimo ndeani ya ile ndege iliyotunguliwa leo asubuhi, akiwa na nia ya kuniua, bahati nzuri sikuwemo ila nilitakiwa kuwemo kwenye ndege hiyo. Na ninafikiri yeyote yule aliyeagiza hiyo ndege itunguliwe anaamini kuwa mimi sasa ni marehemu", Willy alimweleza Col. Rwivanga ambaye wakati huo alikuwa akimwangalia kwa mshangao mkubwa.

"Hivi swala unaloijia hapa ni nyeti kiasi hicho, mpaka wanataka kukuua! Mimi Mzee Musoke aliponieleza, sikutegemea kama kunaweza kuwa na hatari yoyote, maana wewe unakuja kutathimini tu hali ya mambo yalivyotokea mpaka kufikia watu wengi namna ile kuuawa. Lakini sasa inaonekana kuja kwako kumetia watu wasiwasi na wameamua kukumaliza kabisa hata hujaanza huo uchunguzi. Ndugu Gamba hii inaonekana kuna jambo kubwa ambalo hata sisi hatulifahamu. Hii ni hatari na ni hatari kubwa", Col. Rwivanga alijibu.

"Je, unaweza kujuwa ni nani au ni vipi ile ndege ilitunguliwa?, Huenda tukaanzia hapo ndipo tutajuwa hasa ni nani anahusika na kwa sababu gani?", willy aliuliza.

"Taarifa niliyopata kuhusu tukio hilo kwenye kikao cha makamanda wa jeshi, ambayo imetolewa na Col. Gatabazi, ambaye ndiye mkuu wa utawala jeshini, inasema ndege hiyo ilipoitwa kwenye rada ijitambulishe haikufanya hivyo. Kwa hiyo Luteni Silasi Biniga, ambaye ndiye anaongoza wanajeshi wanaolinda uwanja alimtaarifu Meja Juvenal Mukama, Mkuu wa Kikosi cha Mizinga kinacholinda mji huu, ambaye alitoa amri kuwa kama inakaribia kutua na bado haitoi taarifa yoyote itunguliwe. Na ndivyo ilivyofanyika. Baada ya kujuwa kuwa ilikuwa ndege ya kukodi ya kampuni ya kukodisha ndege ya Kitanzania, habari zilipelekwa Dar es Salaam, na habari tulizopata toka Wizara ya mambo ya Nje ya Tanzania ni kwamba ndege hiyo ilikuwa imekodiwa na mtu mmoja kwa jina la Juma Omari aliyejitambulisha kama mwandishi wa habari na masuala yote ya kupata vibali vya kutua alifanya mwenyewe. Hivyo, serikali ya Tanzania inaunga mkono kutunguliwa kwa ndege hiyo ambayo imeingia anga ya watu bila kibali wala kujitambulisha na huku rubani na kampuni hiyo ikijuwa hali ya hatari iliyomo nchini Rwanda. Taarifa hiyo tumeipata jioni hii na serikali ya Tanzania imezidi kusema itaichukulia hatua kampuni hiyo ya ndege kwani inaweza kuwa inatumiwa na maadui wa Rwanda na kuweza kuleta uhusiano mbaya kati ya nchi zetu rafiki", Col. Rwivanga alieleza na ukawa ni wakati wa Willy kushangazwa na maelezo hayo.

"Rafiki yangu, hapa kuna jambo kubwa maana sababu ya kutunguliwa ndege hii ni moja tu, ambayo ni kutaka kuniua mimi. Lakini sasa maelezo ya makamanda wenu. Col. Gatabazi na maelezo kutoka Dar es Salaam, yamenichanganya kabisa na nahisi kuna kitu kikubwa tusichokijua", Willy alijibu.

"Sasa tufanye nini?", Col. Rwivanga alimwuliza.

"Kwanza, nataka aliyetaka kuniua aendelee kufikiri kwamba ameniua. Pili, huenda huyu Lt. Silasi Biniga anaweza akawa na habari zinazoweza kutusaidia kufumbua hiki kitendawili hivyo anafaa kuonwa na kuulizwa", Willy alijibu.

"Basi niache huyu mimi nitamwuliza", Col. Rwivanga alijibu.

"Hapana, niachie mimi, swala hili linaweza kuwa vilevile linaugusa uongozi wenu. Mimi nikiwa mtu baki naweza kupata ukweli bila kuleta kasheshe sasa hivi. Ni lazima tujitahidi tujue undani wa jambo hili maana ni zito. Naomba tu unieleze huyu Luteni Biniga anakaa wapi nami nitaenda kumwona", Willy alijibu.

"Inaweza kuwa hatari kwako, unajuwa hawa watu ni wanajeshi safi", Col. Rwivanga alimwasa Willy.

"Usijali, hatari ndio jina la kazi yangu", Willy alijibu.

Wote wakacheka, maana Musoke alikwishampa Col. Rwivanga maelezo kamilifu kuhusu Willy na uwezo wake.

"Sawa, huyu Luteni Biniga anakaa barabara ya tatu tu kutoka hapa kwangu, sehemu hiihii ya Kamihurura". Kisha akamweleza mtaa na nyumba ilipo.

"Sasa hivi naanza kushangaa, wakati wanajeshi wa cheo chake wengi bado wako kambini na wengine wako huko Ndera ambako ndiko kuna nyumba za maofisa wa ngazi ya chini yeye anakaa sehemu ambayo wanakaa maofisa wa ngazi za juu. Sijui huenda ikawa tu bahati yake", Col. Rwivanga alisema kama vile anajisemea mwenyewe.

"Nafikiri nikionana naye nitajua. Naona niende kama saa tatu hivi. Nitaacha gari hapa na kwenda kwa miguu", Willy alisema.

"Uamzi wako. Kwa vile bado kuna muda mpaka saa tatu ngoja nitengeneze chakula kidogo", Col. Rwivanga alieleza.


"Na mimi nitakusaidia kupika, kupika ni moja ya starehe zangu", Willy alieleza huku wakiinuka kuelekea jikoni.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru