UCHU

MIGUU YA NYOKA

III

Col. Gatabazi alikuwa kati ya watu wa kwanza kufika kwa Luteni Silas Biniga, maana alikuwa akiishi nyumba ya nne tu kutoka pale. Alipofika hakuamini macho na akili yake ilishindwa kukubali. Watu wote hawa waliouawa walikuwa watu makini katika kundi lake, watu ambao alijua ndio wangemsaidia kuchukua madaraka muda utakapofika. Hili jambo lilimshitua sana. Watu wote hawa walikuwa askari shupavu, jasiri na waliojuwa kazi yao vizuri.

Yeyote yule aliyefanya kitendo hicho hakuwa mtu wa kawaida na kama ni kikundi, hakikuwa kikundi cha kawaida. Hawa watu watatu walikuwa na uwezo wa kuangamiza kikosi kizima cha jeshi la maadui lakini leo wameuawa kirahisi na wote kwa pamoja! Suala hili lilimshitua sana Col. Gatabazi, akaingiwa na woga na wasiwasi.

Gari la jeshi lenye king'ola, lilikuwa tayari limefika pale likiwa na askari wa doria wa sehemu zile, askari hao walifika mara baada ya kusikia milio ya risasi.

"Vipi hamjaona au kukutana na mtu au watu wowote waliofanya kitendo hiki?", Col. Gatabazi aliwauliza wale askari wa doria kwa ghadhabu.

"Hapana afande, kote hapa ni shwari", mmoja wapo alijibu.

"Haiwezekani kuwa shwari wakati maafisa wanaotegemewa kama hawa wameuawa hovyohovyo hivi", Col. Gatabazi alieleza tena kwa ukali.

"Huenda wameuana wao wenyewe afande", askari wa pili wa doria alijibu.

Col. Gatabazi alimwangalia kwa jicho baya mpaka yule askari akarudi hatua moja nyuma.

"Chukueni hizi maiti pelekeni hospitali na poteeni hapa mara moja", Col. Gatabazi aliamrisha mara moja.

Col. Gatabazi alirudi nyumbani kwake ili apige simu Ufaransa. Alipofungua mlango wa mbele aliukuta uko wazi. Alishituka, akatoa bastola yake tayari kukabiliana na lolote ambalo lingetokea mbele yake. Alifungua mlango kwa ghafla huku bastola yake ikiwa tayari tayari.

"Vipi! mbona wasiwasi?", Bibiane alimuuliza huku akiweka mguu mmoja juu ya mwingine pale sebuleni alipokuwa ameketi.

"Hujui kumetokea mauaji mabaya sana usiku huu na vijana wetu watatu wameuawa?", Col. Gatabazi alihoji huku akirejesha bastola yake kwenye mkoba wake na macho yake yakiangalia mapaja ya Bibiane ambayo yalikuwa yameachwa wazi kwa kitendo chake cha kuweka miguu juu ya mwingine na kufanya nguo yake iliyokuwa fupi na ya kubana kuyaacha wazi.

Bibiane Habyarimana alikuwa mtoto wa Kinyarwanda ambaye baba yake alikuwa Mhutu na Mama yake chotara wa Kitutsi na Kifarasa. Alikuwa msichana aliyeumbika kwa sura na mrembo katika warembo. Alikuwa na urefu wa futi tano na inchi nane, hivyo, alikuwa mwanamke na urefu wa kutosha. Alikuwa na nywele ndefu za singa, macho makubwa ya blue, mashavu ya kumimina, pua ya kuchonga, midomo ya tasi, meno meupe yaliyopangika na kuacha mwanya kwenye safu ya juu. Hakika, alikuwa kapendelewa na muumbaji. Mwili wake mzima ulikuwa na muundo wa nyigu, juu mwembamba chini kajaa, akimalizia na miguu minene ivutiayo macho.

Ilimchukua Col. Gatabazi muda mrefu kupata la kusema maana kila alipoonana na msichana huyu alijikuta ulimi wake unakuwa mzito, anashindwa hata kusema. Mara nyingi alipatwa na kigugumizi kwani moyo ulimwenda mbio.

"Aliyewaua mimi nimemwona", Bibiane alieleza bila wasiwasi utafikiri alikuwa anazungumza kitu cha kawaida tu.

"Unasemaje?", Col. Gatabazi alimuuliza kwa mshangao.

"Aliyewaua nimemuona mimi. Nilikuwepo alipofika pale kwa Luteni Biniga", Bibiane alijibu tena kwa utulivu, kisha akasema, "Hamna hata kinywaji humu ndani". Kila wakati Col. Gatabazi alishangazwa na tabia ya huyu binti.

"Kinywaji kipo, huenda kweli tunakihitaji maana sasa wewe unazidi kunichanganya", Col. Gatabazi alisema na kuelekea kwenye kabati la vinywaji akatoa chupa ya whisky na gini, akaleta barafu na glasi mbili.

"Utakunywa nini?".

"Whisky niwekee barafu tu usiiharifu na maji".

"Sawa mama, ehee unamaje eti ulikuwepo kwa Luteni Biniga?", Col. Gatabazi aliuliza kwa shauku ya kutaka kujua.

Bibiane alimweleza kwa kirefu yaliyotokea pale kwa Luteni Biniga na kumalizia, "Watakati natoka ndani walikuwa wakimwuliza maswali pale nje, awaeleze yeye ni nani. Sikuwa na wasiwasi maana nilijuwa yule kaisha. Mbele ya wale wanaume hakuna ambaye angefanya kitu. Niliposikia risasi zinalia ile ya kwanza nilijuwa kauawa, lakini niliposikia milio ya risasi inazidi nikawa na wasiwasi nikarudi haraka kuchungulia na nikaona uliyoyaona, lakini mimi nilikuwa na bahati ya kumwona akiruka ukuta upande ule mwingine, akapotelea gizani. Yule ni mwanaume wa shoka na hapa kazi ipo, sina shaka yule ni Willy Gamba kama Jean alivyomwelezea. Hivyo, umeshindwa mtihani wako wa kwanza huyu mtu hakufa ndani ya ile ndege mliyoitungua. Fanya utafiti, utakuta amekuja na ndege nyingine, kakuzidi maarifa, tayari alishajuwa ni Luteni Silas Biniga aliyeamrisha ile ndege kupigwa. Mtu huyu ni hatari, mbona ni hatari sana! Kazi kwako Gatabazi. Kama unataka Uras kwanza inakubidi huyu mtu ummalize. Hizi habari zitamsikitisha sana Jean, wewe unajua.

"Usipommaliza haraka basi ujuwe wewe umekwisha kwani atakuumbua na RPF watakumaliza na utakuwa umewaangamiza Wahutu", Bibiane alimalizia na tabasamu la mauti.

Woga ulimwingia Col. Gatabazi maana naye alihisi kuwa huenda yule alikuwa Willy Gamba. Rwanda hakukuwa na mtu mwenye uwezo kama huo. Jean alimweleza kwa kirefu uwezo wa huyo Willy Gamba na sasa aliudhihilisha. Vilevile, alijuwa Jean angekasirishwa sana kuona huyu mtu amejipenyeza mpaka kuleta maafa makubwa hivi. 

Mtu wa kuweza kumsaidia kumweleza Jean mpaka amwelewe na kumsaidia katika mapambano na mtu huyu alikuwa ni Bibiane. Ingawa alikuwa akimtamani sana Bibiane, lakini alikuwa mwangalifu sana asimguse maana alijuwa siku moja angeweza kumtumia.

Bibiane alikuwa karibu sana na Jean alikuwa mpenzi wake lakini vilevile Bibiane alikuwa mhitimu wa fani ya upelelezi na usalama na akiwa amesomeshwa kwa msaada wa Jean. Jean alikuwa akifanya mambo yake kwa ufasaha. Alihitaji kuwa na mtu Afrika Mashariki na Kati ambaye angeangalia mambo yake bila kuhisiwa. Pamoja na kuwa alikuwa ametumbukia katika lindi la mapenzi na Bibiane, lakini kwa upande mkubwa alimtumia Bibiane kufanikisha mambo yake yaliyokuwa yakimletea maslahi. 

Sababu hizi ndizo zilizomfanya Jean amugharamie Bibiane mafunzo ya hali ya juu ya upeleelezi na kweli msichana huyu alifuzu vizuri na alikuwa mjuzi. Idara ya upelelezi na usalama ya Ufaransa inayoshughulikia usalama wa nje (DGSE) ilimuongezea ujuzi msichana huyu na mara nyingi walimtumia katika kazi zake.

Ni huyu msichana, kwa kutumwa na DGSE, alikisambaratisha kikundi cha wanajeshi waliotaka kuipindua serikali ya Hassan Gouled wa Djibouti na kufanya wakamatwe, kwani siri zao zote alitoa wa serikali kupitia DGSE mpaka leo haikujulikana jinsi alivyoweza kupata ushahidi huo ambao hata kikundi hicho cha wanajeshi kilibaki kimepigwa na butwaa. Msaada huo wa Bibiane kwa DGSE ulimwongezea Jean uhusiano wa karibu. 

Hivyo hata Bibiane alitumia idara hiyo kwa kumsaidia katika mambo yake. Ni Bibiane aliyekuwa kiungo kikubwa kati ya Jean na familia ya Rais. Ingawaje na yeye aliitwa Bibiane Habyarimana hakuwa na uko na Rais kwani familia za Kinyarwanda hutumia jina lake na siyo jina la ukoo kama jamii zingine.

vilevile, msichana huyu ndiye aliyekuwa kiungo kikubwa na wakubwa wengine wa serikali katika Afrika. Kutokana na umbile na sura yake ya kuvutia, ambayo kila siku ilimuonesha kuwa msichana mdogo asiyezidi umri wa miaka kumi na minane, hakuna aliyeweza kumuhisi kama mmoja ya watu hatari waliokuwa kiungo cha uhaini na ugaidi kati ya wakuu wa serikali, wafanyabiashara na magaidi wa Ulaya. Inasemekana wakati wa mkutano wa amani uliofanyika mjini Arusha, Tanzania, Bibiane alikuwapo kama mkalimani.

Baada ya mkutano huo, rais alimpa nafasi aondoke nae kwenye ndege yake, kwani alikuja kama mkalimani wake lakini Bibiane alikataa na kuondoka na Jean kwa barabara kupitia Nairobi, nchini Kenya. Inasemekana alijua nini kingetokea, kwani yeye aliingia kwa ndege ya jeshi la Ufaransa akitokea Nairobi, mara tu baada ya marais kuuawa tarehe 6 aprili Bibiane alisaidia kumchukua mke wa rais na familia yake ya watu kumi na watano na kuwapeleka Ufaransa.

Pia. Inasemekana. Kwa kusaidiana na Jean aliwawezesha Protais Naimana na Feldinand Zigilanyilazo kuwapatia visa ya kusafiria na kuwawezesha kwenda Ulaya. Hivyo. yote hii inaweza kukuonyesha jinsi gani msichana huyu mwenye umri wa miaka ishirini na saba tu alivyoweza kufanya mambo makubwa. Alikuwa msichana hatari sana.

Lazima tumweleze Jean hali halisi", Col. Gatabazo alimweleza Bibiane.

"Piga simu!".

"Sawa. Lakini uzungumze nae kwanza".

"Sawa!", Bibiane alijibu. Alimwangalia Col. Gatabazi. Akaona kuwa ameingiwa na woga. Bibiane aliwaponda sana wanaume walioonekana waoga. Kwa mara ya kwanza alimponda Col. Gatabazi, aliwapenda sana watu jasiri mwanaume yeyote shupavu aliifanya damu yake ichemke na kuchochea tamaa zake za mwili. Lakini mwanaume mwoga hata awe mzuri na sifa aina gani alimtia baridi. Mara hii alihisi baridi na kumchukia Col. Gatabazo mawazo yake yalitembea na kumfikiria Jean. Ile kumfikiria tu alihisi damu yake ikichemka. Kwake Jean ndiye alikuwa mfano wa mwanaume ampendaye, jasiri, shupavu anayepata kile anachokitaka hata iwe kwa gharama gani, hata ikibidi kuhatarisha maisha yake.

Ndivyo Jean alivyokuwa. Bibiane alimpenda Jean kikwelikweli. Ingawa Jean alikuwa mzungu, lakini alikuwa mzungu wa aina yake. Alijuwa kupenda na alijuwa jinsi ya kumfurahisha mwanamke mpaka kumaliza haja zake za kimwili. Lakini zaidi ya yote alimpenda kwa ujasiri na ushupavu wake katika mambo yake.  Iwe biashara, iwe siasa yeye alikuwa ndie bingwa wa mchezo. 

Alifikiria jinsi watu wenye vyeo vikubwa, wakuu wa nchi, matajiri walivyo yeyuka kama barafu mbele ya Jean kila alipopambana nao. Kila siku ndiye aliyetokea kuwa mshindi. Hata rais alipojaribu kumgeuka na kukabiliana na mambo kinyume na matakwa yake, Jean aliibuka mshindi na rais akapoteza maisha. Hata hali ya sasa ya Rwanda, kuwepo RPF, ilikuwa kata ya mbinu zake. Na Bibiane aliamini kabisa kuwa hii ilikuwa ni mipango yake ili baadae aiondoe serikali ya RPF na kumuweka mtu wake Col. Gatabazi. Mwanzo Bibiane alirudi kwa Col. Gatabazi.

Alimfikiria na kisha akatambua mtu kama yeye ndiye angewafaa yeye na Jean, mtu mwoga, mtu anaependa fedha, mtu ambaye anafanya kile ambacho angeambiwa. Kiongozi kama viongozi wengine wa Afrika, mtu anayejifikiria yeye na wala sio nchi au watu wake, mtu mbinafsi, kama walivyo watawala wengi wa kiafrika, Col. Gatabazi alifaa sana kutawala Rwanda.

"Njoo Jean yupo kwenye simu," Col. Gatabazi alimshtua Bibiane kutoka kwenye lindi la mawazo.

"Oh asante sana"" alijibu.

"Mpenzi hujambo?" Bibiane alimsalimia Jean.

"Sijambo, pole na matatizo huko," Jean alijibu.

"Col. amekueleza?"

"Amesema wewe ndiye utanipa safi!"

"Una maana sikupagi safi?"

"Wacha masihara huu si wakati wake. Hebu nieleze imekuwaje?"

"Huwenda na mimi ningekuwepo ningekuwa nimekufa," Bibiane alijibu.

"Sawa tu hiyo ingekuwa kifo kazini," Jean alijibu kwa sauti kavu.

Mara Bibiane akasikia damu yake inasisimka kwani alitaka mwanamume kama huyu asiye na huruma. Huyu ndiye aliyekuwa mwanamume wa kiwango chake.

"Yaani ningekufa asingejali."

"Bila shaka nigejali, lakini kama ungekufa katika mstari wa kazi ni vizuri zaidi kuliko kufa kibudu," Jean alijibu na kuendelea, "Hebu nipe imekuwaje".

Bibiane alichukuwa muda kumwelezea jinsi mambo yalivyotokea.

"Yaani huyu Willy Gamba umemuona kwa macho yako?.

"Ndiyo kwanza sikumtilia maanani sana, nilishtuka kuwa ni yeye baada ya kazi aliyokuwa ameifanya. Mwanzoni nilifikiri ni ka-Inyezi kalikopata fununu ambako vijana walikuwa tayari kushughulika," Bibiane alijibu

"Lazma umsaidie Col. Gatabazi kummaliza huyu mtu, Na mimi nitafanya mipango ya kukupeni msaada wa watu wenye ujuzi wa juu wawasaidie kumuondoa huyu funza anayetaka kula nyama yetu," Jean alijibu.

"Ukisema wewe sisi tutatekeleza, tunaomba hua msaada wako haraka maana hata siye tuna wasiwasi ," Bibiane alijibu.

"Usiwe na wasiwasi, unajua watu kama huyo Willy Gamba ndio nawataka mimi,"

"Najua Jean, wewe tena! Bwana nakuwaza, nataka nije huko unikumbatie, najua huwezi kuja huku sasa!. Bibiane alijibu kwa sauti ya mahaba.

"Baada ya kazi hiyo ya Willy Gamba tuonane Nairobi hata mimi nakutamuni sana," Jean alijibu.

"Haya kazi kwanza."

"Halafu kama kazi," Jean alimalizia na kumuomba Col. Gatabazi tena.

"Kwaheri mpenzi!"

"Kwaheri Bibiane. Col. Gatabazi atakupa mipango yote," Jean alimalizia.

 Jean alipozungumza na Col. Gatabazi alimweleza mipango yake ya kummaliza Willy ambayo ilikuwa ikiendelea kichwani mwake.

"Nafikiri mawazo yako ni sahihi tutafanya hivyo. Asubuhi nitawasiliana na wewe," Col. Gatabazi alijibu.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru