UCHU

MIGUU YA NYOKA

IV

Simu ilipolia ilimshitua sana JKS, maana alikuwa tayari amelala na ilikuwa yapata saa sita za usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

"Hallo", JKS aliita.

"Jean".

Mara moja usingizi ulikwisha.

"Ehe, salama huko?", JKS alijibu kwa shauku maana tokea alipopewa taarifa kuwa Willy Gamba alikuwa ameuawa basi roho yake ilikuwa imetulia kabisa.

"Mambo siyo mazuri, rafiki yako hakufa na kaibuka na mambo mapya", kisha akamweleza yote yaliyotokea Kigali.

"Basi huyu ana miguu ya nyuka", JKS alijibu huku sauti yake ikionyesha wasiwasi.

Si wewe mwenyewe ulisema ni mtu hatari, na huu mchezo anaujuwa, sasa basi kazi imefika na inabidi sasa iwe kazi hasa, maana wakati wote tumekuwa tukimchezea", Jean alijibu.

"Sasa mimi nitakusaidia vipi?", JKS aliuliza.

"Utanisaidia mimi au utajisaidia vipi?, unasema kana kwamba wewe haumo kwenye huu mchezo! mchezo huu ni hatari kwako kuliko mimi maana huyu mtu akigundua kuwa wewe umekuwa mmoja wa watu ambao wamekuwa wakiuhujumu mwelekeo wa nchi yako kuhusu suala hili la Rwanda na masuala mengine basi ujuwe umeisha na urais wa Tanzania utauangalia kwenye ndoto zako tu. Kwa hiyo mtu huyu ni hatari kwako kuliko kwangu, hivyo ni kwa faida yako auawe mara moja!!", Jean alimwasa JKS.

"Tufanye nini sasa?", JKS alijibu kwa sauti ya woga.

"Kati ya vijana wetu wazuri na mahiri na wale vijana walioko Arusha ni wazuri sana. Hao ndio saizi ya huyu Gamba kutokana na uzoefu walionao na ujuzi pia ambao wanao. Kwa hiyo. Nataka wote wanne na kiongozi wao, Xavier Nkubana, waende wakaimalize hii kazi. Sasa ninachotaka ufanye ni kuwatafutia pasi mpya za kitanzania waonekane ni Watutsi ambao zamani walikimbilia Tanzania na sasa wanakwenda kuangalia hali ilivyo. Siku zote walikuwa wakifanyakazi yao kwa siri na hakuna atakayewashitukia. Hivyo watafutie hizo pasi na usafiri. Uhakikishe kesho wako Kigali. Wakifika Kigali wawasiliane na Col. Gatabazi atawapa maelekezo ya kufanya. Lazima tusishindwe juu ya jambo hili", Jean alisisitiza.

"Hilo ulilosema hesabu limefanyika, nitatumia nguvu za dola kuhakikisha kesho wako Kigali mapema kabisa. Nkubana amenipigia simu leo na kusema vijana wanasikia kuchoka kukaa tu bila kazi. Hivyo, nikiwaeleza kuwa wanarudi Kigali kwa kazi ngumu, watafurahi sana", JKS alijibu.

"Hiyo safi, basi fanya hivyo na wakishafika nipe taarifa. Hata hivyo, Col. Gatabazi atanipa taarifa, wakiondoka tu mpigie simu Col. Gatabazi", Jean alimalizia na kukata simu.

Saa ileile JKS alipiga simu Arusha ambako ndiko Xavier Nkubana na wenzake walikuwa wakikaa. Tokea kifo cha Rais wa Rwanda, wao walibaki Tanzania kama wakimbizi na JKS aliwafanyia mipango yote. Hakuna mtu hata mmoja aliyewahisi kwa ubaya, walikuwa wakiishi kwa starehe na kifahari, kama kawaida ya wageni katika Tanzania.

Tanzania ni nchi ya namna ya kipekee kwani wageni ndio wanastarehe kuliko wenyeji. Kwa mtu mgeni kuishi kifahari ilikuwa ni sawa, lakini Mtanzania akitokea kuishi hivyo basi watu humhisi kuwa si mtu mwaminifu na husumbuliwa mara kwa mara na vyombo vya dola mpaka imewafikisha watanzania mahala ambapo hata kama wana uwezo huishi kwa kujibana kwa kuogopa kubuguziwa. Lakini mgeni hata akiishi kifahari vipi alionekana ni sawa na hakuna chombo cha dola ambacho kingeweza kumgusa, na vilevile wananchi hubaki kumsifia kwa ufahari wake.

Hivyo, Nkubana na wenzake waliishi Arusha kwa raha mstarehe wakiwa wameifanya Arusha kama sehemu yao ya kufanyia mipango ya kuihujumu serikali ya RPF. Kusema kweli hawa jamaa walikuwa wauaji katili sana, na si kweli kuwa walikuwa wamebaki Tanzania wakati wa kifo cha Rais, ila walikuwa miongoni mwa watu walioongoza mauaji ya Watutsi. Inasemekana mmoja kati yao, Felician Nzirorera, ndiye aliyekuwa akitangaza na kuchochea watu kwa kutumia radio ya RPLM iliyokuwa ikimilikiwa na Wahutu wenye siasa kali. Radio Televisheni Libre Des Milles Collines (RTLM), iliyokuwa radio ya uchochezi, na mauaji yalipoanza wengi wa watangazaji wake walijiunga katika mauaji na wakubwa wao kukimbilia nje baada ya kuchochea mauaji.

Lakini Nzirorera aliendelea kwa muda mrefu akiwa anatangaza kwa kuhama na stesheni yake ya redio kwenye gari akiwachochea Wahutu kuendelea kuwauwa Watutsi. Na ni mtu huyu pamoja na wenzake aliyekuwa akila starehe hapo mjini Arusha akiendesha magari ya fahari badala ya kuwa amekamatwa kungojea mahakama maalumu ya wauaji hapo Arusha. Kama si JKS kuwasaidia na kuwapa sifa tofauti kuwa wao walikuwa ni maafisa safi wa serikali waliojikuta kwenye mapambano ambayo hawakuwa washiriki, leo hii wangekuwa kati ya watu waliokuwa wakitafutwa na mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Rwanda.

Simu ililia chumbani mwa Nkubana, bahati nzuri alikuwa ndio kwanza amerudi toka hoteli Sabasaba kwenye disko ambako alijipatia msichana wa kustarehe naye usiku huo. Simu ilipolia Nkubana alimwacha yule msichana sebuleni na kwenda kuchukua simu chumbani.

"Hello, Xavier".

"JKS".

"Shikamoo, vipi kulikoni".

"Sikiliza kwa makini".

JKS alimweleza yote kuhusu ambavyo yeye na wenzake walikuwa wakitakiwa kwenda Rwanda kumsaidia Bibiane na Col. Gatabazi kummaliza Willy Gamba.

"Hiyo safi sana, tulikuwa tunakaa hapa, tunalewa na kustarehe tu na wanawake maana hatukuwa na kazi. Sisi tuko tayari hata sasa", Nkubana alijibu.

JKS alimweleza mipango yote na jinsi ambavyo wangesafiri mpaka Kigali.

"Hakika mzee, wewe hushindwi kitu. Kweli madaraka ukijuwa kuyatumia ni matamu sana maana kila kitu kinawezekana, sijui bila wewe tungefanya nini. Asante sana. nitawaeleza wenzangu. Hivyo, saa mbili asubuhi tutakuwa tayari. Na hesabu hiyo kazi huko Kigali imeisha maana tuna uchu na damu", Nkubana alijibu kwa majidai.

"Asante na kwa heri".

Nkubana alikuwa amewaacha wenzake kwenye disko. Aliporudi sabuleni alimkuta yule msichana amelala kwenye kiti.

"We, amka turudi kwenye disko".

"Kwanini, mimi nataka kulala, nimechoka".

""Kwani umekuja kulala hapa, kulala ni nyumbani kwako, hapa uko kazini, kazi ya kunistarehesha mimi, kwa vile nasikia nataka kucheza disko tena, utanifuata".

Yule msichana akiwa anashangaa, Nkubana alimuinua na wakaelekea kwenye gari ili kurudi disko sabasaba.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU